3/21/2005

TUNAJIGAWIA KAZI

Binadamu tusipofanya kazi kwa kujiwagia au kugawana kazi kama siafu au mchwa, tunaweza kujikuta wote tunafanya kazi moja. Kwahiyo katika nchi wote tukiwa waimba mapambio na nyimbo za chipukizi za kusifu watawala mapambia na nyimbo hizo vitakuwa ni kelele. Jamani, wote msijiunge na kwaya au chipukizi. Wengine mkikimbia mchakamchaka msiibe. Tukiimba wote hatutasikilizana. Wengine waimbe, wangine wasikilize, wengine waongee, wengine waandike, wengine wapime, wengine wakosoe, wengine wapinge, wengine watazama tu...
Kwa mfano, kuna wanaosifia jinsi Tanzania "inavyokwenda mbele." Soma gazeti la uhuru na sikiliza hotuba za viongozi kama unataka kusikia jinsi Tanzania inaelekea kukamilisha Dira ya Kitaifa Ya Maendeleo ya 2020. Waombe watu wanaowandikia hotuba zao wawe wanakutumia nakala za hotuba zao. Kwahiyo viongozi hawa na gazeti kama Uhuru wanafanya kazi nzuri ya kusifu. Sasa kuna wengine kazi yao sio kusifu bali kuzungumzia ile asilimia nyingine ambayo watawala na wanasiasa huwa hawasemi. Kawaida wanatuambia mambo yanayowahakikishia nafasi walizonazo. Ile asilimia wasiyotaka ujue, pale wanapotaka uamini kabisa kuwa nchi yako inakwenda mbele kwa kasi, inatolewa na wengine. Hawa wanaifurahia sana kazi hiyo na inapokuwa mshale wa moto kuwaingia wale wanaoamini wimbo wa "Tanzania inapiga hatua za maendeleo" ndio wanafurahi zaidi maana ndio moja ya kazi zao. Watu hawa lazima tuwachome kwa mshale wa moto. Pambio la Tanzania kuendelea limewaingia katika nafasi zao kiasi ambacho wakisikia mtu anasema kuwa Watanzania wana haki ya kuwa daraja la juu zaidi ya walipo wanaona kama vile wametukanwa. Inakuwa ni kinyume na imani waliyojengewa. Mbaya zaidi ni pale mtu huyo huyo anakuwa anapata mishale unapoongelea sio siasa tu bali dini. Anapata tabu sana. Anapata ghadhabu. Hajui afanye nini. Anaandamwa hadi kwenye imani ya nafsini mwake. Inavunjwavunjwa. Teolojia yake inahojiwa. Inarushwa huku na kule. Kitabu chake anakuta kumbe wala hakijui sawasawa. Anashtuka pia kujua kuwa hatuogopi kuwasema viongozi wake wa dini kuwa ni waongo. Au wanakandamiza wanawake. Kama ni mkatoliki unamuuliza, "Kuna kosa gani mwanamke akiwa Padri?" Mtazame atakavyojilambala mdomo. Kama ni muislamu mwambie, "Kurani inasema mwanamke akikosea una mambo matatu ya kufanya: 1.kataa kulala naye kitanda kimoja 2. muonye 3. mpige." Hiyo namba tatu ndio ninaipenda sana. Muulize, "Je mwanaume akikosea kwenye uislamu anafanywe nini?"
Nimeamua kuwa nitaanza kutafuta kipaji cha kusifia. Ingawa kipaji hiki sikipendi sana, nitakitafuta ili niridhishe kila upande.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com