WEWE MWANAMKE MWANAHARAKATI
Katika waraka wa awali (kabla ya huu) nilianza kuongelea vyombo vya habari, nikarukia mengine. Kuna raha wakati fulani kuandika tu bila kujua hasa unakwenda wapi na utaishia wapi. Waraka uliopita nilikuwa naongelea wanaharakati wanaotaka kubadili nchi kabla hawajabadili mtu mmoja mtaani kwao.
Hii inanikumbusha wanaharakati wanawake wanaounda vyama, mitandao, na kufanya mikutano na makongamano ili kuondoa udhalimu wa mfumo dume. Wanaharakati hawa wanaisukuma sirikali ili iweke mazingira ya kisheria na kisera ambayo yatatoa nafasi sawa kwa wanawake na wanaume. Wanawake hawa wanaharakati wanawashauri, wanawahimiza, na kuwaunga mkono wanawake wenzao wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Swali kubwa hapa ni hili: ni kitu gani kinawafanya wanaharakati hawa wagombee haki za kisiasa na kiuchumi lakini sio za kidini na kiimani? Wanawezaje kuitaka sirikali kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa nafasi sawa katika jamii lakini hawataki dini zao kutoa nafasi hiyo sawa? Unakuwa mwanaharakati wa jinsia na wakati huo huo dini yako ni Ukatoliki wa Roma ambao haumpia mwanamke huyo unayemtetea haki sawa? Kwanini unataka wanawake wawe viongozi kwenye shughuli za siasa, uchumi, na utawala ila sio kwenye dini? Ni lini wanawake watakuwa mapapa na maaskofu? Ni lini wataruhusiwa kuhubiri mbele ya umma wa wakatoliki au waislamu? Ni lini tutawaona wakiwa kwenye uongozi wa juu wa Bakwata au jimbo? Kama hawana haki ya kuwa na uongozi kwenye mambo ya maana kama ya mungu, kwanini wawe na uwezo wa kuongoza kwenye mambo ya kibinadamu? Kwanini sirikali inayoongozwa na wanadamu iwape haki sawa wakati dini inayoongozwa na mungu (kwa mujibu wa wafuasi wa dini yenyewe) haiwapi hizo haki? Je wanadamu tukisema kuwa mfumo dume ni mfumo tunaoiga toka kwa mungu tutakuwa tumekosea? Kama mungu hataki waongoze mambo yake au wahubiri juu yake, kwanini sisi tuwachague? Kama mwanamke hawezi kuwa kiongozi wa juu wa wakristo au waislamu, kwanini apewe uongozi wa juu wa nchi? Kama mungu hataki wanawake wawe mashehe, maimamu, mapadri, maaskofu, n.k. kwanini sisi tung'ang'anie kuwa na viongozi wanawake?
Haki ya mwanamke inayodaiwa kwenye ulingo wa siasa ni haki hiyo hiyo ambayo inapaswa kudaiwa katika dini zinazoongozwa na wanaume wanaojichukulia kuwa ni bora zaidi.
Mwanaharakati yeyote wa jinsia, awe mwanaume au mwanamke, lazima apambane na mfumo dume ulioundiwa mistari ya unabii ili kumbagua, kumdhalilisha, na kumkandamiza mwanamke.
0 Maoni Yako:
Post a Comment
<< Home