WAMISIONARI HAWAKUELEWA WAAFRIKA
Wamisionari walipofika Afrika walitakiwa kwanza wakae chini waelimishwe. Hakutuelewa hata kidogo. Tatizo lao kubwa lilikuwa ni wanatumia tamaduni zao kama kipimo cha ukweli, ustaarabu, na ubinadamu. Kutokana na kutumia tamaduni zao karibu kila jambo toka katika tamaduni zetu lilionekana kuwa ni la kishenzi. Wakatuita wapagani. Wakasema mungu wa kweli hatumjui wao ndio wanamjua. Wakatuambia tumfuate huyo mungu wanayemwabudu wao. Laiti wangejishusha na kuamua kujifunza tamaduni zetu, falsafa, na mantiki zake, toka kwetu.
Kwa mfano walidhani kuwa Waafrika wote wanaabudu miungu wengi. Waliposikia tunasema kuwa kuna mungu wa uzazi, mungu wa mvua, mungu wa mazao, mungu wa maji, mungu wa jua, n.k. wakadhani tuna miungu kibao, pengine isiyohesabika. Kumbe Waafrika wengi tunaposema mungu wa hiki na mungu wa kile tunamzungumzia mungu mmoja. Mungu ni mmoja ila sifa na kazi zake ni nyingi. Tunaamini kuwa nguvu tunayoiita mungu ni vigumu sana kuielewa kwa fikra za kibinadamu. Hatuwezi kabisa kuielewa nguvu hii kwa kufikiria tu na kuunda taswira fulani kichwani huku nguvu yenyewe hatujaiona kwa macho. Kutokana na ugumu huu, Mwafrika anajaribu kumwelewa mungu kupitia kazi zake mbalimbali kama vile uumbaji (hapo ndio unakutana na mungu wa maji, uzazi, mazao, mito, n.k.) Tuliamini kuwa yeye ndiye anatupa maji. Kutokana na kazi yake hiyo tunamwita mungu wa maji. Yeye ndiye katupa mbegu, hapo tukamwita mungu wa mazao. Lakini ni mungu huyo huyo mmoja. Kwahiyo mungu kwetu ni muumbaji na kazi zake za uumbaji tunaziona na hapo ndipo tunamwona yeye. Kwahiyo Waafrika tunamjua mungu kupitia kazi zake mbalimbali, lakini mungu huyo ni mmoja.
Wamisionari waliposikia kuwa tuna mungu wa maji, na uzazi, na mavuno walituambia tuachane na imani hizo maana kuamini mungu zaidi ya mmoja ni kinyume na amri yake. Wakadai kuwa huko ni kuvunja amri ya kwanza. Ajabu ni kuwa baada ya kutuambia tuachane na mungu wa maji, mungu wa uzazi, na mungu wa mazao walitupa mungu baba, mungu mwana, mungu roho mtakatifu wakatuambia kuwa huyo ni mmoja. Kama falsafa yetu ya mungu wa uzazi, mungu wa maji, na mungu wa mazao, haimaanishi mungu mmoja, iweje mungu baba, mungu mwana, mungu roho mtakatifu awe ni mungu mmoja? Halafu tulipofungua kitabu cha Mwanzo katika biblia tukakuta inasema: "Na tuumbe mtu kwa mfano wetu." Inakuwaje mungu mmoja anasema "... kwa mfano wetu?" Wetu wangapi? Mmoja? Waulize swali hili wafuasi wao. Ninajua watakavyokujibu,
Ukiwavalia njuga suala la mungu baba, mungu mwana, na mungu roho mtakatifu kuwa mmoja (lakini mungu wa uzazi, mazao, na maji sio mungu mmoja) watakuambia kuwa hiyo ni siri. Ni fumbo. Wanaita fumbo la utatu. Kwa ufupi, wamisionari walikuwa na uelewa finyu sana na dharau. Kazi tulionayo sasa ni kuelimisha wale walioamua kufuata falsafa, na teolojia zao.
0 Maoni Yako:
Post a Comment
<< Home