3/23/2005

WAKOLONI NA JINA LANGU JIPYA

Rafiki yangu mmoja kanikumbusha jina langu jipya nililopewa na Mloyi katika maandalizi ya kurudisha tawala za kikoloni barani Afrika. Jina hilo ni: Nesto McChair. Unaona karibu linafanana na Ndesanjo Macha. Kuna ukaribu fulani.

Maandalizi ya kurudisha tawala za kikoloni yanaendelea vizuri. Tenda ya ujenzi wa kiwanda cha dawa za kujichubua imeshatangazwa na sirikali ya Tanzania. Tayari tumeshapata washauri kuhusu kujichubua toka (zamani iliitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) Jamhuri ya Kidemokrasia Iliyo Katika Vita Vya Wenyewe kwa Wenyewe ya Kongo. Pia sirikali imeamua kuwa itamchagua mwanamuziki Maiko Jakisoni kuwa waziri wa nchi wa masuala ya kuondoa nuksi ya rangi nyeusi. Kumbuka shetani rangi yake ni nyeusi, na kamwe binadamu mwenye akili zake hawezi kukubali kuwa na rangi moja na shetani.

Halafu ule mradi wa kuandika biblia upya ili kuweka habari za mashirika yanayofanya kazi inayoendana na ule mfano wa Yesu wa Msamaria Mwema, yaani Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani unaendelea vizuri. Pia ili majina ya nabii Musa wa zama hizi, Tony Blair, anayetaka kuwakomboa wana wa Israeli huko Zimbabwe toka katika mikono ya Farao Mugabe yaingia kwenye kitabu hiki kitakatifu. Pia jina la Joji Kichaka ambaye ni Musa wa karne hii anayewasaidia Wairaki kuelekea kwenye zama za asali. Mradi huu unaenda polepole kutokana na ukweli kuwa aya zinashushwa taratibu sana. Sijui ni tatizo la mitambo ya mawasiliano au ni nini.

Kabla sijasahau, ile barabara mliyoiita Barabara ya Nyerere tuko mbioni kuibadili jina. Lazima Nyerere tumwondoe kwenye historia yetu kwa jinsi "alivyotulostisha." Kimbelembele chake cha kugombea uhuru kimetuletea umasikini mtupu. Napandwa na hasira. Siwezi kuendelea kuandika. Ngoja nilie kwanza halafu nitafute picha yake niliyonayo niichanechane. Na nikisikia mtu anasema, "Ujamaa ni kujitegemea ndio njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru" huyo mtu ajue tutakosana. Zitakunjwa. Ama zangu, ama zake. Ngoja nikanywe maji nipunguze ghadhabu niliyonayo dhidi ya Maumau, Nkrumah, Neto, Toure, n.k. kwa kimbelembele chao cha kudai uhuru.
Tazama Mwalimu Nyerere alivyotufanya tukawa tunakimbia mchakamchaka huku tukiimba Kaburu matata iya! Tulikuwa na nyimbo kibao za kuwasakama na kuwabeza makaburu. Sasa hivi majuzi tumekuja kujua kuwa kumbe ni watu wazuri sana. Tena wacha mungu. Halafu hawana kinyongo na sisi hata kidogo. Nadhani wanafuata mafundisho ya biblia yasemayo, "Samehe hata mara saba u sabini." Wamatusamehe na kuamua kuja nchini kwetu kutusaidia kuchimba madini ya Tanzanite kwa faida yetu!

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com