11/30/2005

Mrisho: Mwafrika ni Kama Kituko!

Msanii wa nguvu na rafiki yangu wa karibu, Mrisho Mwana wa Mpoto, wa kundi la Parapanda, ambaye niliwahi kuandika habari kuhusu harusi yake ambapo "shampeni" ilikuwa ni maji ya madafu (bonyeza hapa uisome) kaandika ujumbe ambao umenichekesha ingawa aliyosema sio utani. Anasema kuwa Waafrika ni kama kituko vile. Usome. Naubandika hapa chini:
"Mwafrika nikama kituko maana wanaomba Funding kwa wazungu ili wajadili matatizo yao na jinsi ya kujikomboa toka utumwani sasa icho si kituko yaani mtu akupe pesa ili umjadili yeye alafu unachekelea. Huwezi kubisha .....(hapa Mrisho kataja jina la mtu ambalo nimelitoa)... Maana juzi tu tulikuwa zanzibar kujadili ujinga wetu mbele yao huku wakitulipa pesa na kulala sehemu nzuri huku tukiomba siku ziongezwe hata bila posho."

All the Best
Mrisho Mpoto
********************
Huyo ni Mrisho Mpoto, wewe unasemaje kuhusu kuomba fedha kwa wazungu ili tujadili jinsi ya kujikwamua toka kwenye makucha yao ya uchumi, fikra, siasa, na utamaduni tegemezi?

Vyombo vya Habari au Vyombo vya Uongo?

NYONGEZA!!!!!: Nilipoandika habari hiyo hapo chini mapema leo sikuelezea jambo fulani muhimu sana. Ni kwamba serikali ya Marekani imetoa hela kwa kampuni ya Lincoln Group. Kampuni hii inachukua "habari" zilizoandikwa na wanajeshi wa Marekani kisha inazitafsiri kwa Kiarabu kisha inalipa magazeti ya Iraki ili iyachapishe kwa majina tofauti na yale ya askari wa Marekani walioandika. Na huu ndio uhuru, na hii ndio demokrasia ambayo Marekani inataka kusambaza duniani!
*******************************
Nina tabia ya kuviita vyombo vya habari, "vyombo vya uongo." Usidhani kuwa sina sababu za msingi. Sasa huu ni mfano mmoja. Kampuni iitwayo Lincoln Group imekuwa ikilipa wafanyakazi wake ili wajifanye kuwa ni waandishi wa habari na kuandika habari katika magazeti ya nchini Iraki. Habari hizo nia yake ni kuhadaa akili za Wairaki ili waamini kuwa Marekani ni mkombozi wao na sio mwizi wa mali yao ya asili. Yaani wanachofanya hawa jamaa ambao wanalipwa na serikali ya Marekani ni kupandikiza uzushi kwenye magazeti. Bonyeza hapa usome habari yenyewe.

Mwalimu Alikuwa ana uwezo wa kuona kuleeeeee...

Kituo cha Kusini kina mradi wa tovuti ya kumbukumbu ya Mwalimu. Baadhi ya hotuba zake zinapatikana kwenye tovuti hiyo. Nimemaliza kuzisoma. Mwalimu alikuwa ana namna yake fulani ya kufikiria...ila katika yote ni ule uwezo wake wa kuona mbele kuleeeeeeeeee....wakati wa-twawala wengi tulionao hata leo hawaioni (sembuse kesho). Bonyeza hapa uzisome.

11/27/2005

Kibaki: Mavi ya Kuku Nyie!

Macharia Gaitho wa Daily Nation la Kenya anasema kuwa siku moja baada ya kambi ya Ndizi (iliyokuwa ikiunga mkono katiba mpya ya Kenya) na kambi ya Machungwa (iliyokuwa ikiipinga katiba hiyo) kufanya mkutano katika jiji la Nairobi, alipelekewa ujumbe wa maandishi wa simu ukisema kuwa shirika la uongo la CNN lilikuwa na masikitiko makubwa kwani lilikosa habari ya kutangaza kuhusu Kenya. Maana ya ujumbe huu ni kuwa kwakuwa shirika hilo hupenda kutangaza habari za vita na maaa zaidi ya zile za maendeleo na furaha, hakukuwa na habari nzuri maana walidhani kuwa siku kambi hizo mbili zilipofanya mkutano jijini Nairobi, lazima zingepigwa. Wapi.
Mashirika haya ya uongo yanapenda sana maafa. Tazama Liberia. Nchi hii wakati ikiwa kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe, vyombo vya habari vilijaa habari kuhusu nchi hiyo. Lakini hivi majuzi baada ya kufanya uchaguzi ambao ni kati ya chaguzi za amani ya juu kabisa duniani, hakuna vyombo vya habari vinavyotuambia habari hiyo. Katika uchaguzi huo wamemchagua Mama Ellen Johnson-Sirleaf kuwa Rais. Mwanamama huyu amemshinda mwanasoka wa zamani George Weah. Ingawa yeye ni rais wa kwanza mwanamke Afrika, yeye sio mwanamke wa kwanza kuongoza nchi barani Afrika. Malkia Zauditu wa Ethiopia aliongoza nchi hiyo toka 1916 hadi 1930. Pia mwanamama Ruth Perry aliwahi kuwa kiongozi wa nchi (sio rais) wa Liberia baada ya kuangushwa kwa Sajenti Samuel Doe na kufa kwa Rais Amos Sawyer. Perry alikuwa ni mwenyekiti wa Baraza la Taifa toka 1996 hadi 1997 alipomwachia madaraka mwizi na muuaji Charles Taylor baada ya "kushinda" uchaguzi.
Sielewi kwanini nimepitia njia ndefu namna hiyo hadi kufikia kwenye jambo nililotaka kusema. Niliyoandika hapo juu na ninayoandika hapa sasa hivi hayana uhusiano wa moja kwa moja. Nilifungua ukurasa huu ili niandike kuhusu Kibaki lakini mawazo mengine yakanijia. Sasa niko kwa Kibaki.
Nadhani Kibaki alipokuwa mdogo alikuwa ni matata sana kwa matani. Akina Moi nadhani walikuwa hawafungui mdomo kwa matani. Basi wakati wa kampeni zake za kutaka wananchi waunge mkono katiba iliyokuwa imfanye kuwa mfalme, aliwaita wale wanaoipinga kuwa ni wapumbavu. Ila kali kabisa ni pale aliposema kuwa wao ni "mavi ya kuku." Sijui huwa anatumia mdomo huu huu unaoshusha haya matani kula chakula na pia kusali au ana mdomo mwingine?

11/25/2005

Blogu ya Mpya: Che Mponda na Materu

Kuna blogu mpya ya ndugu Materu iitwayo Fikra Thabiti. Ili umsome bonyeza hapa. Pia aliyekuwa mwandishi wa gazeti la Daily News kwa muda mrefu, Chemi Che Mponda, kaanzisha blogu ya Kiswahili. Kutokana na shughuli utaona hajaweka mapya kwa muda ila anasema ataivalia njuga karibuni. Che Mponda, zaidi ya kuwa mwandishi wa habari, ni muigizaji wa filamu na michezo ya kuigiza. Ameshiriki kwenye filamu ya Tusamahe na Maangamizi. Bonyeza hapa usome blogu ya Chemi. Bonyeza hapa utembelee tovuti yake yenye habari zaidi kuhusu fiamu na michezo ya kuigiza aliyoshiriki.

11/24/2005

Al Jazeera Wamwambia Joji Kichaka: Usitupige Mabomu

Gazeti la Uingereza la Daily Mirror limetoboa kisa hiki: eti Joji Kichaka alitaka kupiga mabomu kituo cha luninga anachokichukia kupita kiasi cha Al Jazeera. Bonyeza hapa usome kisanga chenyewe. Sasa wafanyakazi wa Al Jazeera wameanzisha blogu kumtaka Kichaka asiwapige mabomu. Hata hivyo wamemwambia kuwa hawatishiki. Bonyeza hapa utembelee blogu yao.

Tunaotetea Utamaduni wa Mwafrika Tutembee Uchi?

Nilisema ninavuta pumzi nizungumze kuhusu utamaduni. Utaona kuna wasomaji wameacha maoni wakishutumu wale tunaopinga tabia ya kudharau utamaduni wetu na kukimbilia wa wengine. Wameuliza eti mbona tunavaa viatu na nguo? Mmoja kasema kama tunatetea utamaduni kwanini tusirudi enzi za kuvaa ngozi? Wasomaji hawa nadhani hawafahamu kuwa jamii mbalimbali Afrika zilikuwa tayari zina viwanda vya nguo wakati weupe wakiwa wanaishi mapangoni na kula nyama za watu! Niliwahi kuandika makala nikizungumzia mada hii ya kuvaa nguo/viatu na kutetea utamaduni. Kichwa chake kilikuwa: Kama Unapenda Utamaduni Mbona Unavaa Nguo? Hapo chini nimeweka vipande kadhaa toka kwenye makala hyo. Ila unaweza kusoma makala nzima kwa kubonyeza hapa.
*********************************************
Vipande vyenyewe hivi hapa:

"Mara nyingi mtu unapozungumzia utamaduni wa Mtanzania au Mwafrika, inachukuliwa kuwa unazungumzia tu mambo ya kale. Kwa watu wengi utamaduni na ukale ni kitu kimoja. Watu wanaoamini hivyo huchulia kuwa utamaduni ni kitu cha zamani sana. Kitu kikuukuu. Kimezeeka. Kimetoka kwa mababu na mababu. Kwa maana hii watu wa leo tunarithi utamaduni tulioachiwa na mababu ila sisi haturithishi kizazi kijacho utamaduni mpya (unaotokana na kizazi chetu) bali ule tuliopokea toka kwa waliotutangulia.

Ukikutana na watu wanaofikiri kuwa utamaduni ni ukale kuna swali moja linalochekesha sana ambalo lazima wakuulize huku wakikutolea macho kama vile unafanya uhaini kutetea utamaduni wako: Kama unapenda utamaduni wa Mwafrika kwanini unavaa nguo? Kwanini unavaa viatu?"
****************************************
"Ukidhani kuwa ninaposema tupende utamaduni wetu ninamaanisha kuwa tufanye yote yaliyofanywa na mababu zetu utakuwa umefanya kosa kubwa sana. Kwani mababu zetu walikuwa ni miungu? Kwanini tuchukue kila walichofanya kama vile walikuwa hawana mapungufu? Mababu zetu ni binadamu kama sisi. Walikuwa na mazuri na mabaya pia. Je tukubali kukeketa wanawake maana ni urithi wetu? Hakuna sababu yoyote ya msingi ya kuendelea kukeketa wanawake hata kama tendo hili lilifanywa na mababu zetu."
**************************************************
"Kuna jambo linalonishangaza ninapokutana na wale wanaoniuliza, “Kama unatetea utamaduni mbona unavaa nguo?” Kwanini wanapozungumzia utamaduni wa watu weupe hawarudi nyuma na kuganda kwenye historia. Wanachukulia kuwa wanayofanya leo hii watu weupe ndio utamaduni wao, ila sisi Waafrika utamaduni wetu ni yale tuliyofanya wakati tukiwa tunatembea uchi. Utamaduni wa watu weupe ni yanayofanywa leo na wa kwetu ni yake ya zamani. Ni kitu gani kinachofanya kuvaa nguo kuwe ni utamaduni wa watu weupe ila sio Waafrika?

Mtazamo huu unaashiria kuwa kuna watu hawategemei Waafrika twende mbele maana itakuwa kinyume na utamaduni wetu! Mtazamo mbovu sana huu. Mbona hata hao watu weupe kuna kipindi katika historia yao ambacho waliishi mapangoni, walitembea uchi, walikula nyama mbichi, walikula nyama za watu, waliua wachawi hadharani, n.k. Watu wengi hawafahamu historia hii maana shuleni tunafundishwa historia yetu toka tukiwa tunatumia zana za mawe, tukiishi na kuchora picha mapangoni ila historia ya watu weupe inaanzia zama za mapinduzi ya viwanda. Kutokana na hili, watu wengi wanaona kuwa utamaduni wa mtu mweupe ni mambo ya kileo."
***************************************
"Hakuna jamii yoyote isiyokua, isiyobadilika, isiyochukua mapya, isiyotupa ya zamani, na isiyohifadhi yale ya zamani yanayofaa. Nipe mfano wa jamii kama hiyo. Hoja hii ndio ambayo inawapa tabu wanaotetea ukeketaji wa wanawake kwa madai kuwa ni utamaduni. Kwa uelewa wa zama zile za mababu, tendo hili lilionekana kuwa ni sahihi. Ila kwa uelewa wa mazingira tunayoishi leo tendo hili linaonekana kuwa sio sahihi."

11/23/2005

Kama Kuna Siku Mabata Yanaipata...

Kama kuna siku mabata hapa duniani yanapata ni hapo kesho. Kama kuna siku bata wanaliwa kwa wingi hapa duniani ni hapo kesho Wamarekani wanaposherehekea sikukuu ya "thanksgiving." Kesho ni siku ya kula bata kama vile sijui nini...nchi nzima itakula bata kwa mlo wa mchana. Bonyeza hapa usome kuhusu sikukuu hiyo.
**************************************************
Halafu: Navuta pumzi kisha niongelee mambo kadhaa ambayo wasomaji waliotoa maoni wamezungumzia hasa suala la utamaduni na kuiga.

Kenya: Wa Rangi ya Machungwa Washinda Lakini...

Waliopiga kura kuitakaa katiba iliyokuwa imfanye rais wa Kenya kuwa kama mfalume wameshinda. Ila Rais wa Kenya, Mzee Mwai Kibaki amesema kuwa Wakenya wanapaswa kujua kuwa Kenya tayari ina katiba ambayo imekuwa ikitumika siku zote!
Umeelewa undani wa kauli yake hiyo?

11/21/2005

Kura ya Maoni Kenya: Wana Machungwa Wanaongoza

Wapiga kura wa upande wa machunga ambao unakataa katiba mpya inayomlimbikizia Rais madaraka wanaongoza. Wanaounga mkono katiba hiyo (wanaotumia alama ya ndizi) wanaongozwa na Rais Kibaki ambaye wakati akiwa nje ya madaraka alitaka Kenya iwe na katiba ambayo haitampa mtu mmoja madaraka makubwa. Lakini alipoingia madarakani...au kwenye utamu kama mnavyojua...anataka alimbikiziwe madaraka kama vile yeye ni Mungu. Wanaosema "Hapana" wanaongoza kwa asilimia 56.

Blogu ya Sauti za Dunia Yashinda!

Ule mchuano wa blogu bora katika katika vigezo na lugha mbalimbali (Kiswahili hakimo!) umemalizika. Na kwa upande wa blogu za kiinglishi (kiingereza) blogu ya Mradi wa Sauti za Dunia imeshinda. Shukrani zinakwenda kwa waliopiga kura. Bonyeza hapa uone tangazo la ushindi huo. Bonyeza hapa uone blogu zote zilizoshinda.

11/20/2005

Kizazi cha Watumwa Wapya!

Mjadala kuhusu muziki wa "kizazi kipya" umepamba moto. Jeff na Ramadhani wameuanzisha. Na wasomaji wao wameudaka. Maswali kadhaa bado yanaelea hewani. Hivi "kizazi kipya" ndio akina nani? Na Bongo Flava ndio nini hasa?
Ukitazama kizazi tunachokiita kipya. Ukaangalia tabia, mwenendo, fikra, na njozi zake utakubaliana nami (kama huwa unapenda kuita beleshi kuwa ni beleshi) kuwa jina sahihi la "kizazi kipya" ni "watumwa wapya."
Watumwa wa zamani walidakwa kifikra, kitamaduni, na kiroho katika wimbi la ukoloni, safari za “wavumbuzi,” na kazi za wasambaza "ustaarabu" (wamisionari). Leo hii wimbi linalokumba kizazi kipya cha watumwa wapya ni wimbi la utandawizi. Utandawizi ndio ukoloni mpya. Wimbi hili linasukumwa na falsafa na itikadi za soko na ulaji. Soko lenyewe sio soko kama la Kariakoo au Kiboriloni. Nitamwachia Nkya wa Pambazuko achambue zaidi juu ya hii dhana ya soko. Kwa kifupi dhana ya soko katika ubepari haina maana mahali pa kuuza na kununua. Na ninaposema ulaji simaanishi ulaji kama ule wa kula ugali na kisamvu. Kwa kilugha chao wanaita "consumerism." Katiba ubepari dubwana hili ulaji (consumerism) ndio ibada.
Zamani zile waliotutangulia walitekwa kwa njia mbalimbali, baadhi zikiwa za kinyama (viboko, bundiki, vifungo), nyingine vitisho (utakwenda motoni usipoamini dini yetu), elimu, n.k. Leo hii mabwana wa utumwa wala hawana haja ya kuja na viboko na au kutuma watu wao na biblia na kurani kutuhadaa tukatae tamaduni zetu. Mazingira yamebadilika na mbinu zimebadilika. Lakini pia ziko nyingine zimebaki vile vile au kubadilika kidogo. Vitukuu wa wale waliotia minyororo fikra za mababu zetu ndio hivi sasa wanakaza pingu katika akili za hawa tunaowaita "kizazi kipya." Wanatumia tamaduni maarufu (kilugha chao wanaita pop culture) na vyombo vya uongo kama MTV. Wanatumia picha za wanamuziki wakiwa wamevaa nguo za aina fulani kuwafanya watumwa wapya wadhani kuwa ili wawe wanamuziki wakubwa wanapaswa kuvaa nguo kama hizo, mikufu, na pia kuwa na majina kama Crazy G na hata kubadili namna ya kutembea. Wanatumia majarida. Wanatumia filamu na muziki. Wanatumia redio za FM na Ma-DJ ambao ndio vinara wa utumwa mpya. Wanatumia vipindi vya luninga kama Big Brother. Wanatumia mashindano kama Miss Tanzania. Wanatumia mikufu ya dhahabu (mingine ikiwa ni ya msalaba). Wanatumia mapicha makubwa ya ukutani ya watu kama akina 50 Cent.
Unajua wengi tunaona utamaduni kuwa ni kitu cha mchezo mchezo. Hasa tunapodhani kuwa utamaduni ni ngoma za kukata kiuno, vinyago vya wamakonde, ngonjera, na nguo za batiki. Utamaduni ni rasilimali. Watu wakizimikia utamaduni wako watazimikia pia na bidhaa zako (hadi bendera ya nchi yako wataivaa). Unakuta kuna nchi zinatambua hili na zinafanya kila liwezekanalo kulinda utamaduni wao. Wanatumia sera, sheria, elimu, n.k. kutimiza azma hiyo. Nchi kama Ufaransa zina idadi maalumu ya sinema za Marekani zinazoruhusiwa kuonyeshwa katika majumba ya sinema nchini humo. Nia yake ni kulinda soko la watengeneza sinema wa ndani. Sheria ya mambo ya Intaneti Ufaransa inasema kuwa tovuti yoyote ile ya Ufaransa lazima iwe na lugha ya Kifaransa. Inaweza kuwa kwa Kiingereza au Kijerumani lakini lazima kuwe na toleo la Kifaransa.
Lakini pia utamaduni unaweza kuwa mpambano. Ni mpambano wa mitazamo. Mfano mzuri wa hili ni ugaidi. Ugaidi una sura nyingi. Upande mmoja wa sura ya ugaidi ni utamaduni. Unaweza kutazama ugaidi kama mgongano wa mitazamo ya kitamaduni kuhusu demokrasia, wema, ubaya, historia, n.k.
Nirudi kwenye hoja ya msingi. Wakati tunapotazama kundi tunaloliita "kizazi kipya," mimi ninachoona ni kizazi cha watumwa wapya. Tena watumwa kwa maana mbili. Kwanza, watumwa wa kifikra na kitamaduni. Pili, watumwa kiuchumi, kwa maana ya kuwa katika nchi yao bila uwezo wa kumiliki njia kuu za uchumi au kuwa na uwezo wa kutoa maamuzi makuu kuhusu uendeshwaji wa nchi.
Wa-twawala wanapenda sana kizazi hiki kinapotumia muda mwingi "kujirusha" na Bongo Flava au kuketi mbele ya luninga wakitazama Big Brother wakati nchi keki ya nchi inamalizwa. Kwa akili za kizazi hiki cha watumwa wapya, kitendo cha kuwa na luninga zinazoonyesha Big Brother, redio za FM za kupiga miziki yao, luninga za kuonyesha video zao, na majengo marefu marefu yanayojengwa mjini ambayo wanayatumia katika kutengeneza video zao za muziki, bila kusahau hoteli za kifahari ambazo nazo wanazitumia kutengeneza video hizo...mambo haya kwao ni alama ya maendeleo makubwa ya nchi. Na nchi kwao huwa ni mjini.


11/19/2005

Nitablogu Toka Uingereza Mwezi Ujao

Kama kuna mtu ana mpango wa kujilipua ndani ya treni au mabasi pale London kwa Malikia Lizabeti, namshauri asithubutu kufanya hivyo mwezi ujao. Mwezi ujao nitakuwa yaliyo makao makuu ya shirika la habari la Reuters, Canary Wharf, London. Nitakuwa hapo kwenye mkutano wa pili wa kila mwaka wa Mradi wa Sauti za Dunia. Mradi wa Sauti za dunia uko chini ya Kituo cha Berkman cha Intaneti na Jamii katika chuo kikuu cha Harvard. Habari zaidi kuhusu mradi wa Sauti za Dunia ulivyoanza na pia kuhusu mkutano wa London mwezi ujao na watu wanaohudhuria, bonyeza hapa. Utaona kuwa kati ya wanaohudhuria ni wanablogu wawili mahiri wa Kenya, Kenyan Pundit na Mshairi. Mshairi huandika habari kuhusu wanablogu wanawake wa Afrika kila jumatatu katika blogu ya Sauti za Dunia.
Kwahiyo wasomaji wangu, ndugu, na marafiki wa Uingereza, tuwasiliane ili tuweze kunywa chai na kupiga gumzo (Masawe, Maruma, Kibwana, Mgosi, Theodore, Freddy, Neema (JALO!!!) ...mpo?).

Blogu mpya toka Tanzania ya Kiswahili na Kiingereza

Ndugu Chris Bwalya yuko Arusha. Anablogu kwa Kiswahili na Kiingereza. Bonyeza hapa umsome. Blogu yake haipokei maoni. Nadhani atabadili ili kuruhusu watu kutoa maoni. Nadhani kutakuwa na mijadala mikali kutokana na masuala ambayo anazungumzia. Anaandika, pamoja na mambo mengine, kuhusu ukristo, biblia, yesu, n.k.

Muziki wa Watumwa Wapya?

Ramadhani Msangi ambaye hivi karibu alianza kututaka tuanze kuzungumza badala ya kusema, ameendeleza mjadala ambao Jeff Msangi aliuzungumzia na kuzua cheche. Kwanza aliandika haya, mjadala ukaendelea hapa na hapa.
Hebu bonyeza hapa uende kwa Ndugu Msangi umsome. Kisha soma maoni motomoto ya wasomaji na pia ongeza yako.
****************************************************
Wakati huo huo....
Mapema leo wakati nikiipitia blogu mpya ya ndugu Nyembo nilikutana na hoja yake ya agano jipya na la kale. Agano la Kale ndio lile ambalo tumeambiwa kuwa hakuna anayejua liko wapi...yaani mkataba wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Nimependa aliposema haya, "Kuipaka rangi Manowari si njia sahihi ya kuzuia maji kupenya..."

Pigia Kura Mradi wa Sauti za Dunia (Global Voices)

Tarehe 20 mwezi huu ndio mwisho wa kupigia kura blogu bora kwa ajili ya Tuzo ya Blogu Bora. Mradi wa Sauti za Dunia (Global Voices) ni miongoni mwa blogu zilizo katika mchuano huo kwa upande wa lugha ya Kiingereza. Bonyeza hapa uwapigie kura. Ukifika hapo tafuta lilipo kundi la blogu za kiingereza. Piga kura yako.
Mradi wa Sauti za Dunia umetoa nafasi kila wiki kwa ajili ya muhtasari wa blogu za Kiswahili. Kulikuwa na uwezekano wa kuweka eneo ambalo wanablogu wa Kiswahili wangekuwa na ukurasa wao katika blogu ya mradi huo ila kukawa na hoja kuwa ukifanya hivyo itabidi utoe ukurasa kwa kila lugha. Kwa kifupi, mradi huu unaheshimu mno kazi zinazofanywa na wanablogu wa Kiswahili. Na kazi hiyo ni kuondoa ukoloni mamboleo mtandaoni na kupanua wigo wa lugha zinatotumika katika mijadala kwenye Intaneti. Sababu hii ndio inanifanya kuwataka mupige kura zenu kwa ajili ya Sauti za Dunia. Basi bonyeza hapa. Kura inachukua nusu dakika.

11/18/2005

Mwanablogu Mwingine Aingia Uwanjani

Bwana Nyembo kajiuliza kwanini naye asiamue kuwa na blogu yake ili kutoa mawazo yake mtandaoni? Huyu ni mwabablogu mpya wa Kiswahili. Kanifurahisha mahali fulani ambapo kabadili msemo wa Kiswahili usemao "Asiyekubali kushindwa sio mshindani." Yeye anasema kuwa kule Zanzibar, "Asiyekubali kushindwa ni shujaa!" Bonyeza hapa usome blogu yake na kumkaribisha.

11/16/2005

Kenya: Sakata la Kura ya Maoni

Kundi moja linalojiita vuguvugu la Njano lilikwenda mahakamani likitaka zoezi la kupiga kura ya maoni ya "ndiyo" au "hapana" kuhusu katiba mpya nchini Kenya lisimamishwe. Kundi hili lilidai kuwa bunge lilipounda sheria ya kutengeneza katiba mpya lilijichukulia mamlaka ambayo yako mikononi mwa wananchi. Pia likadai kuwa tume ya uchaguzi ya Kenya haina haki kisheria kusimamia zoezi hilo maana tume hii imepewa wajibu wa kusimamia uchaguzi wa wabunge na rais na sio kura ya maoni kuhusu katiba. Wanasheria wa kundi hili walidai kuwa kesi hii pengine ni kesi ya pili kwa ukubwa nchini Kenya ukiachilia mbali ile ya shujaa Dedan Kimathi. Jana Mahakama Kuu nchini Kenya imeamua kuwa zoezi hilo litaendelea. Bonyeza hapa usome habari hiyo.
Wakati huo huo jamaa wa Kenya National Commission of Human Rights ambao wanafuatilia kwa karibu kampeni za kura hii ya maoni, wana "orodha ya aibu" katika tovuti yao. Orodha hii inaonyesha matumizi mabovu ya mali ya umma na kauli za uchochezi toka kwa waongo na wezi wanaojiita wanasiasa nchini humo. Bonyeza hapa utazame orodha hiyo.




11/14/2005

Mafisadi wale wale, Chama kile kile, uozo ule ule...

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinafanya kampeni kwa kutumia barua pepe. Nimefurahi kujua hili maana haya ndio kati ya mambo ninayotazama kwa karibu (kwasababu za kitaaluma). Ninaamanisha matumizi ya zana mpya za mawasiliano katika kampeni za urais na ubunge.

Kuna mistari ambayo iko katika barua pepe yao ambayo nimeona niwagawieni kidogo (iwapo hujapata barua pepe hiyo). Nabandika hapo chini mistari hiyo:

Maendeleo ya Kweli
hayawezi kuletwana
Mafisadi wale wale
wa Chama kile kile
chenye Uoza ule ule
Wakiendeleza yale yale
eti kwa Kasi mpya,
Nguvu mpya
na Ari mpya.

11/13/2005

Kukataa Kutawaliwa na Wezi ni Wajibu wa Kikatiba na Kiroho

Naendeleza mjadala nilioandika jana ulioitwa: Tatizo ni Wa-twawala au Watawaliwa? Kama hukuusoma bonyeza hapa uusome kisha urudi hapa ndipo uendelee.
*********************************
Kenya itazameni. Kuna masomo chungu nzima pale. Unaona tunavyoonyeshwa kuwa kuna uwezekano kuwa wapinzani na wa-twawala hawana tofauti zaidi ya kuwa upande mmoja uko madarakani na upande mwingine unataka kuyachukua. Wapinzani watapinga mambo yote yanayofanywa na walioko madarakani. Lakini wakiingia madarakani watayafanya yote waliyokuwa wakiyapinga na hata mabaya zaidi. Na wale waliokuwa madarakani wataanza kupinga mambo ambayo nao walipokuwa madarakani waliyafanya. Kumbuka Kaunda alivyotiwa ndani na sheria ambayo alikuwa yeye mwenyewe akiitumia. Akadai kuwa sheria ya kutia watu kizuizini ni kinyume na haki za binadamu. Yaani haki hizo anaziona pale yeye ndiye anapokuwa anakandamizwa.
Pale Kenya waliokuwa wakiiunga mkono katiba wakati wakiwa wapinzani, wameikataa walipoingia madarakani. Waliokuwa wakiikataa wakati wakiwa madarakani sasa wanaikubali. Yote hii ni mchezo wa kuhadaa wananchi kwa nia ya kushika madaraka. Midomo ya wanasiasa ni bomba la uongo. Jana niligusia suala la wanasiasa wanaohama vyama vyao baada ya kutochaguliwa kugombea uongozi wakidai kuwa vyama hivyo havifai. Vyama wanavyohamia vikija kuacha kuwapa nafasi za kugombea uongozi wataondoka wakidai kuwa navyo havifai. Wewe mtu umekuwa kwenye chama toka ukiwa kijana, leo hii umezeeka unakuja kudai eti chama hicho hakifai kuongoza. Na unasema hayo mara tu baada ya kuchujwa kwenye kura ya maoni.
Au tazama kiongozi wa chama fulani anayelalamika juu ya viongozi wasiotaka kuachia madaraka au marais wanaobadili katiba ili waendelee kuwa madarakani wakati yeye mwenyewe hayo madaraka ndani ya chama chake hajayaachia. Ni nini kinakufanya wewe uwe na haki ya kuwa mwenyekiti wa kudumu wa chama chako (au cheo kingine cha "maisha" ndani ya chama chako) na wakati mwingine mgombea urais wa maisha, lakini mpinzani wako hana haki ya kung'ang'ania madaraka?
Jana nilisema kuwa tabaka la wa-twawala limefanikiwa kutufanya tuamini kuwa huu mfumo wa ulaji na ukandamizaji wanaouita "demokrasia" ndio njia pekee ambayo binadamu wanaweza kutumia kujenga taifa. Tazama bunge la Kenya kwa dakika chache. Bunge hili ni upenyo wa kujitajirisha na kuipora nchi. Mwezi uliopita bunge nchini Kenya kwa dakika 30 liliruhusu wizara 18 kuchukua zaidi ya shilingi za Kenya bilioni 100 toka kwenye mfuko maalum. Kwa nusu saa shilingi bilioni 100 za nchi masikini kama Kenya zimeyeyuka. Kura hiyo ilipitishwa na wabunge wangapi unajua? 22!
Sisi wananchi wa kawaida, tabaka la waliwao, tuna uwezo wa kukataa kunyonywa na kudanganywa. Tuna wajibu wa kikatiba na hata kiroho (kama unaamini kuna kitu kama roho) kukataa kuwa chini ya hili tabaka dogo la wezi na wauza nchi. Kuna sababu za kutotimiza wajibu huu?

11/12/2005

Weusi tumetoka Milima ya Mbalamwezi

Lile kundi la Midnite ambalo nimelitaja mapema leo (bonyeza hapa usome nilipowataja) linaendelea kutumbuiza pembeni yangu. Ule wimbo wanaosema: "Ishi maisha upendayo, pena maisha unayoishi" kuna mahali wanasema,"Watu weusi ni Wakushi tuliotoka milima ya mbalamwezi...mlima Kilimanjaro, mlima Ruwenzori, mlima Kibo..."
Tafadhali usiache kusoma niliyoandika hapo chini nikijadili kuhusu watawaliwa na wa-twawala.

TATIZO NI WA-TWAWALA AU WATAWALIWA?

Tatizo kubwa kabisa Tanzania na pengine bara zima la Afrika watu wengi hudhani kuwa ni wa-twawala. Hapana. Tatizo namba moja ni watawaliwa. Wao ndio tatizo kubwa kuliko wanaowatawala. Watawaliwa ni wengi lakini wanakubali kunyonywa na kudanganywa na kundi dogo la watu fulani (wengi wakiwa ni wanaume).
Lakini kundi hili dogo nalo linajua kuwa udogo wake unaweza kuwatia hatarini kwahiyo linaunda vyombo kama polisi, magereza, sheria, mahakama, n.k. Vyombo vyote hivi kazi yake ni kuwalinda. Unadhani kazi ya FFU ni nini? Kazi yake ni kuzuia wananchi kuamka na kuleta mabadiliko. Wananchi wakitaka kutoa madai hadharani au kwenda kuwafuata huko wanakokaa, FFU kazi yao ni kuzuia.
Kila siku polisi wanakamata watawaliwa kwa madai ya uvunjaji sheria lakini huoni hata siku moja polisi hao wakikamata au kupiga mabomu ya machozi watawala. Ina maana kuwa watawala Tanzania au Afrika hawaibi? Hawaui? Hawavunji sheria? Au sheria huwa zinavunjwa na watawaliwa tu? Watawala wakivunja sheria ni sawa. Watawala wetu wanaiba. Wanaua. Wanatesa. Wanatumia vyombo nilivyokutajia.
Kama wahalifu halisi walikuwa ndio wanakamatwa, watawala wengi walioko madarakani wangetakiwa kuwa jela kwa miaka mingi sana.
Kundi hili dogo linapotumia vyombo vta dola kuwaweka ninyi mlio wengi chini ya himaya yake, wanatumia mfumo wa elimu na vyombo vya habari kukuhadaa uamini kuwa bila wao jamii haitakalika. Wanakufanya udhani kuwa maendeleo yako wao ndio watayaleta. Unakutana nao wakati wa kampeni wanasema kuwa watawaleteeni shule, maji, elimu, n.k. Ahadi zinazotolewa na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi zingekuwa zinatekelezwa, Tanzania ingekuwa nchi ya kuigwa na dunia nzima.
Kukiwa na jamii ambayo inadhani kuwa maendeleo atayaleta mtu mmoja ambaye kazi yake mwaka mzima sio kuzalisha kitu bali kujaribu kukushawishi umpe kura, jamii hiyo inapaswa kuzinduka mapema.
Wa-twawala wakishatupata hapo kwenye imani kuwa bila mfumo wa utawala ambao unawapa wao (wachache) nguvu kubwa zaidi yetu (tulio wengi) nchi haitapata maendeleo, wanatukamata kwenye imani nyingine potofu. Imani hiyo ni kuwa bila polisi, magereza, mahakama, sheria, wanajeshi, n.k. jamii haitakalika. Watu watauana na kuibiana.
Kama ni kweli kuwa polisi, mahakama, magereza n.k. kazi yake ni kujenga jamii isiyo na uhalifu, basi nchi zenye polisi wengi na wenye dhana za kisasa kama Marekani, mfumo wa mahakama uliokomaa, magereza yenye ulinzi mkali zingekuwa hazina uhalifu. Pengine unaweza kudhani nimepungukiwa nikisema kuwa kazi ya polisi sio kuondoa uhalifu na kuhakikisha jamii inaishi kwa amani. Nadhani unapaswa uokoke kwanza ndipo ukubaliana nami. Kuokoka kwenyewe sio kama kwa Askofu Kakobe. Kuokoka kwa tofauti.
Usiniambie kuwa na mahakama unadhani kazi yake ni kutoa haki. Kazi yake ni kulinda haki ya mwenye nacho dhidi ya asiyenacho. Haki ya wa-twawala dhidi ya watawaliwa. Niambie, kuna wa-twawala magerezani? Kuna wenye nacho magerezani? Magerezani wengi ni wale wenzetu wenye kuvaa malapa. Je ina maana kuwa wavunja sheria ni watawaliwa tu? Kama unafikiria kama mimi utakubaliana nami kuwa walioko mahakamani, polisi, wanaopitisha hizo sheria pengine ndio walitakiwa kujaza magereza kama haki ingekuwa inatendeka.
Kundi hili dogo la wa-twawala limefanikiwa kwenye jambo moja kubwa sana. Wameweza kutufanya tuamini kuwa hata kama hatuwataki hakuna njia ya kuwaondoa kwenye usukani. Wanatumia sheria kadhaa kutisha watu kuandika maoni yao kama haya ninayoandika hapa. Sheria hizo zinawapa nguvu za kutia watu ndani wanaoelimisha umma juu ya mfumo wa kibabiloni unaonyoya damu ya watawaliwa. Wanaweka sheria ambazo inakuwa vigumu wewe kuungana na wenzako ii kuwaondoa kwenye usukani.
Napenda kukuhakikishia kuwa mfumo huu wa kibabiloni, mfumo wa kihaini unaoneemesha tabaka la wa-twawala huku maelfu ya wananchi wakiwateseka kwa tabu na umasikini uliokithiri, unaweza kuondolewa kwa sayansi ndogo sana. Sio tu unaweza kung'olewa, bali unapaswa kung'olewa.
Usiutii.
Usiutii.
Usiutii.

Rege, katiba ya Kenya, wanasiasa wanavyotuchezea

Siku hizi nimekuwa nyuma sana katika masuala ya muziki wa hisia, Rege. Siwezi kuamini kuwa sikuwa nawafahamu jamaa wa Midnite. Jamaa mmoja alinisikilisha muziki wao hivi majuzi. Nimewafia kabisa. Nalala na kuamka nikiwasikiliza. Kwanza muimbaji wao ana sauti ya pekee sana. Na anajua jinsi ya kuitumua sauti yake. Ukiachilia mbali sauti, ujumbe wa nyimbo za Midnite unanigusa sana. Dakika hii wanaimba wimbo mmoja wanasema:
Penda maisha unayoishi
Ishi maisha unayoyapenda.
Wimbo mwingine unaonimaliza ni ule ambao anazungumzia luninga kuwa ni chombo cha uongo. Anatumia mchezo wa maneno ambao Marasta wanapenda kuutumia kutoa ujumbe wao. Kwa mfano, "television" anasema ni "tell a lie vision." Ni mchezo huu wa maneno ambao aliutumia Peter Tosh alipokuwa akiuita mfumo wa siasa na utamaduni wa kibabiloni "shit-stem" kutokana na neno la kiingereza "system." Bonyeza hapa kwenda tovuti ya Midnite.
Tuachane na Midnite. Sijui kama unafuatilia kampeni za kura ya maoni kuhusu katiba kule Kenya. Nadhani zoezi hili kwa ujumla linatufunza mengi kuhusu uundaji wa katiba ya watu na pia kutuonyesha wanasiasa wanavyotuchezea. Utaona kuwa wale wanasiasa waliokuwa wakiipinga katiba mpya wakati wakiwa madarakani, ndio hao wanaoiunga mkono sasa wakiwa nje ya madaraka. Na wale waliokuwa wakiiunga mkono wakati wakiwa nje ya mduara wa ulaji, sasa wanaipinga kwakuwa ulaji wao utakuwa mashakani. Haya ni mafunzo ya bure lakini wakati mwingine huwa yanatupita.
Umeona hata Tanzania wale wanasiasa ambao wamekosa nafasi za kugombea ubunge kwenye vyama vyao wamehamia vyama vingine wakidai kuwa vyama vyao vya zamani havifai. Wamekuwemo kwenye vyama hivyo hadi dakika ya mwisho (walipokosa nafasi za kugombea) ndio wakagundua kuwa vyama hivyo si lolote/chochote? Wengine wamekuwa wanachama wa vyama vyao vya zamani karibu maisha yao yote. Kama miaka yote hiyo walishindwa kuona ukweli ambao wengine tumekuwa tunauona kila siku, ni vipi tunaweza kuwaamini kuwa wanaweza kuwa viongozi wazuri. Kama inachukua miaka mingi namna hiyo kuona jambo la wazi namna hiyo, kwanini tuwape dhamana ya kutuongoza? Tusipojenga utamaduni wa kuwauliza maswali magumu wanasiasa kama hawa watakuwa wanatuchezea kama wanasesere. Watatuchezea na baadaye wakishalewa madaraka tukiwauliza maswali magumu wataanza kutumia watwana wao (polisi/wanajeshi) kututia vilema, kutuunga na hata kutuua.
Kuhusu kura ya maoni kule Kenya, mwanablogu Kenya Pundit anafuatilia kwa karibu sana zoezi hili. Bonyeza hapa umsome.

11/10/2005

Yanayotokea Ethiopia je?

Sijui kama wandugu mnafuatilia yanayotokea kule Ethiopia. Bara letu litavuja damu hadi lini? Kumbuka Mwizi Mkuu, samahani, Waziri Mkuu wa Ethiopia alikuwa ni miongoni mwa wa-twawala wa Afrika waliokaribisha kule Usoti kupiga picha za pamoja na wa-twawala wa Kundi la Nchi Nane (G8). Mkapa naye alikuwemo. Eti hawa ndio wa-twawala toka Afrika vipenzi vya akina Joji Kichaka na timu yake. Bonyeza hapa usome kwa kina wanablogu wanavyotupasha maafa yanayotokana na maguvu ya dola.

11/07/2005

Ewe mwanamuziki wa Tanzania...wewe ni balozi wa nchi yako

Niliweka barua toka kwa msanii Ferdinando Paul. Pia niliweka beti alizoandika. Bonyeza hapa utasoma barua yake ni beti yake. Sasa ametokea msomaji amempa changamoto kupitia sehemu ya maoni. Changamoto hiyo naiweka hapo chini:
Msanii jina Ferdinando Paul, unatoa HI, msanii wa ku-RAP, unasema ..... mambo TIGHT, ....unatoa VESI, mh... makubwa. Huyo ndo msanii wa Tanzania, kioo cha kuendeleza na siyo kupotosha jamii, balozi wa nchi popote duniani. Kitu kidogo tu, iweje U-rap? wakati tuna makabila zaidi ya 120 nchini yenye utajiri wa sanaa mbalimbali na ya hali ya juu, na huko ulikonuukuu rap pia wanalijua hilo. Sasa ukienda nje na ukacheza rap utadai kupiga muziki wa Tanzania au. Maisha Dasalama siyo jehanamu, wapi ni peponi? Arusha, Mza, Tanga, eh.. au unalinganisha na wapi?. Nadhani Dar siyo mahala pa rap ila pa mahadhi ya madogoli, sindimba, bhughobhoghobho, mdumange, n.k. Pia ni kwa wale waliyeko hapo na si kwingineko kwa mwili, akili na fikra zao. Hivi hi, mambo tight na vesi ndiyo nini? ... msanii, balozi wa nchi!!!!!. Hongera Kingwendu, Saida Karoli .....
*********************************
Changamoto hii inanipeleka kwenye mjadala mzito alioanzisha Jeff Msangi. Kwanza aliandika makala ambao ukibonyeza hapa utaisoma. Alipoandika makala hiyo mjadala ukaanza. Bonyeza hapa uusome. Mjadala haukuishia hapo. Uliendelea. Bonyeza hapa usome muendelezo wa mjadala huo.

Jimbo la Rais Si Nchi Nzima?

Mtumishi wa sirikali kaniandikia waraka huu ambao unaonyesha matatizo yaliyoko katika mfumo wetu wa wizi wa kura (ambao tunauita mfumo wa uchaguzi). Barua yake hiyo hapo chini:

Mimi ni mtumishi wa Umma. Eneo langu la kazi ni kanda ya magharibi yenye mikoa ya Kigoma na Tabora. Tume ilitangaza kuwa kama italazimu watu wawe wamebadili vituo vyao mwisho mwezi Julai. Ghafla imezuka kazi inayonitaka kuja Kigoma kwa wiki kadhaa. Nimechukua kadi yangu ya kupiga kura. Kwa tafakuri tu ya kawaida nikajua sitaweza kuchagua wabunge au madiwani nikiwa Kigoma. Nikajua nitachagua Raisi kwa vile yeye jimbo lake la uchaguzi ni Tanzania nzima. Jana Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuwa kama hutakuwa kituoni kwako huruhusiwi kupiga kura hata ya Raisi. Jambo hili limenishangaza na kunisikitisha sana. Iweje uwe ndani ya Taifa lako, ukiwa na haki zote za kupiga kura uzuiwe? La ajabu serikali yenyewe ndio imetutuma huku tuliko na sio kwa mapenzi yetu. Vipi Ndesanjo, wewe utapiga kura? Kama la mbona hujatoa kauli? (Gumzo?)

Hali ya Kisiasa Zanzibar Hainishangazi

Hivi yaliyotokea, yanayotokea na yatakayoendelea kutokea Zanzibar yananishangaza? Hapana. Wa-twawala ndio watunga sheria za uchaguzi, ndio wasimamizi, ndio wanaolala na masanduku ya kura, ndio wenye jeshi na bunduki na mabomu ya machozi, ndio walioshika utamu. Wameuonja utamu kwanini wasichonge mzinga?
Halafu tazama hawa watu wanaoitwa waangalizi wa uchaguzi. Chama twa-wala na wapinzani husubiri ripoti za waangalizi hawa midomo wazi. Tena wakiwa ni wazungu watu ndio huwasikiliza kwa makini zaidi. Wazungu hawa wakipiga kura kwenye nchi zao sijui ni akina nani huwa wanasimamia uchaguzi wao. Labda mtaniambia kuwa chaguzi zao huwa ni huru na haki kwahiyo hakuna sababu ya kuwa na waangalizi. Joji Kichaka tunajua mwizi wa kura. Uchaguzi wa mwanzo utata ulijitokeza akatangazwa kuwa rais sio kwakuwa kapata kura nyingi za wananchi bali majaji watano kati ta tisa. Majaji hawa watano wa mahakama kuu ndio waliamua kuwa Kichaka eti kashinda.
Nimemtaja Kichaka nikakumbuka kisa hiki. Juzi alikuwa akihudhuria mkutano kule Argentina. Kiboko yake, Hugo Chavez (rais wa Venezuela), ambaye humwita Kichaka gaidi, akaulizwa akikutana na Joji atamwambia nini? Chavez akasema alikuwa amepanga kujificha sehemu kisha amshtue "we!" Kisha amtazame Joji kisigino kikigusa kisogo anapotoka mkuku.
Kuna hili suala la polisi na wanajeshi kujaa barabarani kule Zanzibar. Jambo hili litakushangaza iwapo unadhani kuwa kazi ya vyombo hivi ni kulinda usalama wa wananchi. Wanajeshi na polisi kazi yao ni kulinda usalama wa wa-twawala na jamaa na marafiki zao (yaani matajiri wenzao). Askari ni msukule unaojenga ukuta kati ya wananchi wanaodai haki zao na wa-twawala wezi wenye kiburi na dharau. Baadhi ya askari hawa wanaobeba bendera nyekundu na mitutu ni wale wanaoishi kwenye nyumba za mabati. Huwezi amini. Wanawapiga binadamu wenzao na hata vikongwe kisa eti wanatiii amri. Fela akaimba, "Zombie oooh, Zombie" (Msukule ooh, Msukule). Akaendelea kuimba:
Zombie nah go go unless you tell him to go
Zombie nah go stop unless you tell him to stop
(Msukule haendi hadi umwambie nenda
(Msukule hasimami hadi umwambie simama)
Ndio walivyo askari hawa wanaotutia ngeu na vilemwa tunapodai haki na usawa. Eti walinda usalama, usalama gani wanalinda huku wakiwapa majambazi silaha na wakati mwingine wakiwa ndio majambazi? Siku zinavyokwenda usalama nchini unatuaga huku askari hawa wakiendelea kujaza vitambi. Tukijiunga na wenzetu tukitaka kuandamana kama katiba inavyoturuhusu mara ghafla unaona wale askari wa kuanzisha (sio kuzuia) fujo wanakuja. Sijui kwanini huwa hatuwaoni siku za matembezi ya "mshikamano."
Yaliyotokea, yanayotokea, na yatakayoendelea kutokea Zanzibar hayanishangazi. Ukipanda mahindi huvuni ngano bali mahindi. Na wakati wa kuvuna wala haujafika.

Zanzibar: Damu Zaidi Itamwagika?

Mijadala mizito inaendelea mtandaoni kuhusu mchezo wa kura uliofanyika kule Zanzibar. Soma baadhi ya maoni ya wananchi. Nimetumiwa na bwana mmoja aliyeko Florida.

From: Anonymous-234 <zenj@zanzinet.org>
Reply To: zanzinet@zanzinet.org
To: ZANZINET <zanzinet@zanzinet.org>
Subject: Re: [Zanzinet]Hali halisi ya nchi yetuSent:
Wednesday, November 2, 2005 11:39 AM
Hakuna solution yoyote ndugu yangu kwa Zanzibar zaidiya kuchukua picha ya wapalestina na sisi. Hakuna jinsikwa sasa na mipango yote itakayofanyika itaishiakwenye unafiki tu na kubabaishwa na wakoloni wa CCM.Muafaka wa pili haukusaidia na matokeo yake Mkapaameshairubuni AU, SADCC na Afrika mashariki yote iwezekuside nae na kuona Uppinzani ndio wa kulaumiwa.Angalia ripoti zao kuhusu tathmini ya Uchaguzi,wanaipigia debe CCM na kuifanya CUF kuonekana kitukoduniani. Maji yameshamwagika, na kwa mtindo huu hatuponi.Masikini wazee wetu waliishi katika ukoloni na sisitumeendelea na Ukoloni tena thakili kuliko huo hapokabla.Hivi karibuni utasikia kua Chama cha CUFkinaorodheshwa katika vyama vyenye msimamo mkali nahili ndio lengo. Watajidai kuipatia Wizara za uongokatika serikali ya wizi na wakijua kua CUF haitakubalina hapo ndipo watakapozidi kuipaka katika Jumuiya zakimataifa. Yaani hapo pana mbinu za kiaina kutumalizaWazanzibari, na hakuna kitakacholeta watu mezanikatika kweli na haki, ila itakapodhihirika wazi kuasasa ni kweli na nchi haitawaliki. M.Mungu tusaidiekuondokana na udhalimu huu, tutaabaniiiiiiiiiii!
khamis mustapha

<k_falla2000@yahoo.com> wrote: Jamani hivi kweli kumwaga damu ndiyo solution yamatatizo yaliyokuwapo zanzibar, Hatuoni kamatunaongeza matatizo ambayo hatuweza kuya solve milele:Wacha na tuangalie Damu imemwagika miaka 40 nyuma naeffect yake inaoneka mpaka sasa ijapokuwa tumejidahidikutaka kuifuta lakini wapi bado tunaendelea kuathirikanayo.Mtu asifikirie kama mimi ni pro CCM kwa kuandikamaoni yangu hayo ( mimi nataka kama leo CCM iondokemadarakani hata kama kwenye ndoto) lakini nikoconcerned na ile hali halisi tuliyokuwa nayo palenyumbani.Sasa itakuwa busara zaidi tukikaa na kutafutasolution nyengine na siyo umwagaji wa damu bye

BARKE JUWEID <barkejuweid@yahoo.com> wrote: Asalaam Aleikum Wajumbe, Baada ya kuzingatia haya yote yanayoendeleakwetu nimekuja na kupata jibu hili lisemwalo na wanaCCM,nalo ni kuwa WAO WAMEMWAGA DAMU KUIPATA NCHI,KWAHIYO KUITOWA PIA ITABIDI WAITOWE KWA NJIA HIYO HIYO YAKUMWAGA DAMU,SIO KWA NJIA YA VIKARATASI. Kutokana na hayo basi nduguzanguni hata kamatutafanya chaguzi 100 nchi haitopatikana. Serikali wanayo wao,Polisi wao,Jeshilao,tutaipataje kwa njia ya vikaratasi ? Kilichokuwepo sasa ni kuwaunga mkono na lughahiyo hiyo ya umwagaji wa damu. Sisi hatuna polisi,wala jeshi wa kutusaidiakuimwaga hiyo damu,kwahiyo itatubidi tutumie mikonoyetu na uwezo wowote tulionao kujibu lugha hiyo yaumwagaji wa damu kwa kuwasaka mmoja mmoja nakuwapunguza,kila mwezi tunakwenda na mmoja,tukitimizamwaka na 12 tumeshawapeleka nafikiri hii lugha yakumwaga damu itapungua na labda hapo ndio itakuja hiyofikra ya kukaa pamoja sote kama Wazanzibari na kuiokoanchi yetu. Najuwa kutazuka watu humu ukumbini na kupingahaya kwa vizingiti vya dini,lakini haya yanayotokea nayatayofuatia katika nchi yetu haiwezekani kwa namnayoyote kuiokoa. Namalizia hapa kungoja fikra na mawazo yenuwajumbe ili tuendelee kuchangia haya.

11/06/2005

Mfuko Maalumu kwa Watengeneza Filamu

Kama wewe ni mtengeneza filamu au unafahamu watengeneza filamu, shirika la ITVS (Independent Television Service) limetangaza mfuko maalum kwa ajili ya filamu ambazo zitaelimisha Wamarekani kuhusu tamaduni na jamii mbalimbali duniani. Mwisho wa kuomba kudhaminiwa na mfuko huo ni Januari 20 mwaka ujao. Babu Kadja kazi kwako.
Bonyeza hapa kwa taarifa kamili za jinsi ya kuomba.

Maisha Dasalama Magumu Unaweza Kunywa Sumu

Ferdinando Paul ni mmoja wa wasomaji wa makala zangu katika gazeti la Mwananchi. Yeye ni msanii wa muziki wa rapu. Kanitumia zawadi ya beti chache toka kwenye moja ya mashairi yake. Nami nawapeni nyote zawadi hiyo. Kwenye waraka wake anatuambia kuwa maisha Dasalama ni kama jehanamu ya kufa na kupona! Hapo chini ni sehemu ya waraka wake na beti (ameziita "vesi" zenyewe):

Tunakupa hi sana masela wa bongo. Si unajua darisalam maisha magumu mithili ya jehanam ni kufa na kupona yani unaweza ukanywa sumu. Hizi ni baadhi ya vesi zangu. Mimi ni msanii wa kurap nina misongi mingi lakini ndo hivyo mambo tight ngoja nikupe vesi hii kidogo:

Nanuka dhiki
Sina kipato mwendawazimu
nakuwa sina rafiki
ila wafitini na wanafiki
kwa kuwa ni masikini
nimezungukwa na wazindiki
lakini bado naamini
mwenyezi mungu atanibariki
hivyo nakuwa makini
nahangaika riziki popote na simwamini mtu
walimwengu hawaaminiki
na tena hawariziki
nikipendeza wanakuwa wanoko
wanataka nivae kaniki
maisha niwe mshabiki
wakati haiwezekani
mwendawazimu sibadiliki
- Ferdinando Paul

Mwanablogu Mpinga Uislamu Atiwa Ndani

Abdolkarima Seliman ni mwanablogu toka Misri anayefahamika kwa kupinga vikali udhalimu wa serikali ya Misri na pia mapungufu katika dini ya Uislamu. Blogu yake imemtia matatani. Hivi sasa yuko jela na wanaharakati duniani hivi sasa wanaendesha kampeni ya kutaka aachiwe. Baadhi ya wanakampeni hao wanasema kuwa hawakubaliani na mawazo ya Abdolkarim ila wanaamini kuwa ana haki ya kujieleza. Tazama habari yake toka Kamati ya Kulinda Wanablogu kwa kubonyeza hapa. Pia habari yake iko katika blogu ya mradi wa Sauti za Dunia. Bonyeza hapa na hapa. Ukitaka kusoma blogu ya Abdolkarim bonyeza hapa. Ila lazima uwe unafahamu Kiarabu (na kwa taarifa yako Kiarabu sio "Kiislamu" kama baadhi ya watu wasemavyo. Kiarabu ni lugha na Uislamu ni dini ya Waarabu.)

11/04/2005

Demokrasia Bongo ni Chuki, Kutiana Vilema na Mauaji

Nimemaliza kusoma barua ya msomaji ambaye simtaji jina maana hajaniruhusu. Nimeibandika barua yake hapo chini. Nimetoa sentensi mbili za mwanzo wa barua ambazo zilikuwa ni salamu. Vingine vyote nimeviacha. Soma kwa makini anayosema. Kama hupendi kutazama mambo kwa mapana na marefu unaweza kudhani anayosema ni porojo au ndoto za Alinacha (hivi Alinacha aliota nini tena?). Haya, msome huyu bwana:

Kwako ndugu Ndesanjo,
Mada yangu mahsusi katika barua hii ni kuhusu mchakato mzima wa suala la uchaguzi Zanzibar.Nadhani yaliyotokea umeyapata na ikiwa hujayapata nitakupa kwa ufupi tu kwa kukuona wewe ni mwanamapinduzi halisi wa fikra.Ndesanjo tumepata pigo sisi wana demokrasia wa hapa Tanzania na jibu nililolipata ni kuwa hapa Tanzania hakuna demokrasia.Demokrasia ya viongozi wa Bongo ni chuki,kutiana vilema na mauaji.Ukitaka kuyajua haya fuatilia uchaguzi wa Zanzibar.
Ndesanjo, hakuna shaka upinzani umeshinda uchaguzi Zanzibar lakini je nani anaweza kuwakabidhi nchi?Zanzibar ilikuwa kama Iraq kwa muda wa siku nne,watu waliwekwa chini ya ulinzi wa wanajeshi ambao kazi yao ni kulinda mipaka sasa wanatumika kutisha na kuua raia wanaowalinda.Hii ni aibu kwa serikali ya Tanzania,kumbe haitaki kuondolewa madarakani kwa njia ya kura.Sio siri hakuna Mtanzania mwenye akili iliyochujwa ambae anaikubali hii serikali yetu kwani sasa sote tunajua kumbe nchi hii inatawaliwa kijeshi.
Sisi watu wa Tanzania bara tumekata tamaa kabisa ya uchaguzi kwa kuona yale yaliyotokea Zanzibar.Tulikuwa na muamko wa kuiondoa hii serikali ya CCM kwa njia ya kura lakini hili tumeona halitawezekana.Nashangaa sana vikosi vyetu vya majeshi vinakubali kuua na kutesa raia ambao pia ni ndugu zao kwa maslahi ya wachache.Hawa viongozi hawajui kwamba hii mbegu wanayoipanda hivi sasa ni mbaya sana?Hivi binadamu gani atakaekubali kuonewa kila siku?Ipo siku hali ya hapa Tanzania haitatofautiana na Jamhuri ya Congo,Somalia,Iraq na kwingineko ambako huko kote hakukaliki kwa ajili ya viongozi wenye tamaa.
Tunasikitika serikali ya CCM hapa Tanzania imeweza kuwatisha mpaka waangalizi wa uchaguzi wa kutoka nje ya nchi ambao kwa kweli nao wamekubali vitisho vyao na kutoa taarifa za uongo eti kweli uchaguzi ulikuwa huru na haki.Mkapa ndie aliewatisha mpaka wamesahau majukumu ya kazi yao.Ndio hapa nauliza nini maana ya demokrasia?
Tunashukuru tu kuwa Marekani imeona yenyewe na kutamka kuwa uchaguzi wa Zanzibar ni hovyo japo katika hili hatujui nayo itasimamia upande gani kutokana na yenyewe kuwa na sera kama za CCM.Kama kweli wana dhati basi wanaweza kuzuia umwagikaji mkubwa wa damu huku Tanzania kwani Watanzania wameshachoka na ubabe wa CCM.
Ndesanjo muda haunitoshi tu wewe si unajua haya maisha ya Bongo nimejinyima kula ili nikuandikie wewe hii barua huku kutuma Email ni shilingi 500/=
Mtiifu.
X.

11/02/2005

Shujaa Rosa Parks Azikwa Leo

Mwanamama shujaa Rosa Parks, aliyekataa kumpisha mtu mweupe kiti ndani ya basi enzi za ubaguzi wa waziwazi (maana ubaguzi wa chinichini unaendelea) nchini Marekani, amezikwa leo. Bonyeza hapa kuhusu mazishi ya mwanamama Parks aliyekuwa na miaka 92. Bonyeza hapa na hapa kusoma historia yake.

"Lile Jani" ni halali kwa watu wazima huko Denver

Kama una miaka 21 na unaishi huko Denver, Marekani, basi ukikamatwa na polisi na kipisi au msokoto wa "lile jani" hakuna noma. Bonyeza hapa usome wapiga kura walivyoamua.

11/01/2005

Je Blogu Zinaidharau Afrika?

Ethan Zuckerman kazua mjadala mkali. Siku zinavyokwenda unapamba moto. Anasema kuwa blogu, kama vilivyo vyombo vikubwa vya habari havipendi kuandika mambo yanayohusu Afrika. Anasema blogu zinapenda kuandika zaidi mambo kuhusu teknolojia. Ametoa mifano miwili toka blogu ya Boing Boing. Ili upate uhondo wenyewe bonyeza hapa. Ukishasoma aliyoandika, soma na maoni ya wasomaji wake (hapo ndio kuna uhondo hasa).

Hongera Anna na jamaa wengine wa Open Cafe

Afadhali nichelewe kutoa pongezi kuliko kutotoa pongeza kabisa. Rafiki yangu Anna na wanaharakati wenzake wa programu huria wa shirika la Open Cafe la Afrika Kusini walitimiza mwaka mmoja tarehe 21 mwezi jana. Hongereni sana. Bonyeza hapa uone tovuti yao na miradi wanayoshughulika nayo. Pia tazama mradi wao uitwao ArtMarketOnline. Na blogu yao ya Szavanna na OpenCafe. Open Cafe imeundwa na wanaharakati wanaoendeleza matumizi ya programu huria barani Afrika.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com