11/07/2005

Hali ya Kisiasa Zanzibar Hainishangazi

Hivi yaliyotokea, yanayotokea na yatakayoendelea kutokea Zanzibar yananishangaza? Hapana. Wa-twawala ndio watunga sheria za uchaguzi, ndio wasimamizi, ndio wanaolala na masanduku ya kura, ndio wenye jeshi na bunduki na mabomu ya machozi, ndio walioshika utamu. Wameuonja utamu kwanini wasichonge mzinga?
Halafu tazama hawa watu wanaoitwa waangalizi wa uchaguzi. Chama twa-wala na wapinzani husubiri ripoti za waangalizi hawa midomo wazi. Tena wakiwa ni wazungu watu ndio huwasikiliza kwa makini zaidi. Wazungu hawa wakipiga kura kwenye nchi zao sijui ni akina nani huwa wanasimamia uchaguzi wao. Labda mtaniambia kuwa chaguzi zao huwa ni huru na haki kwahiyo hakuna sababu ya kuwa na waangalizi. Joji Kichaka tunajua mwizi wa kura. Uchaguzi wa mwanzo utata ulijitokeza akatangazwa kuwa rais sio kwakuwa kapata kura nyingi za wananchi bali majaji watano kati ta tisa. Majaji hawa watano wa mahakama kuu ndio waliamua kuwa Kichaka eti kashinda.
Nimemtaja Kichaka nikakumbuka kisa hiki. Juzi alikuwa akihudhuria mkutano kule Argentina. Kiboko yake, Hugo Chavez (rais wa Venezuela), ambaye humwita Kichaka gaidi, akaulizwa akikutana na Joji atamwambia nini? Chavez akasema alikuwa amepanga kujificha sehemu kisha amshtue "we!" Kisha amtazame Joji kisigino kikigusa kisogo anapotoka mkuku.
Kuna hili suala la polisi na wanajeshi kujaa barabarani kule Zanzibar. Jambo hili litakushangaza iwapo unadhani kuwa kazi ya vyombo hivi ni kulinda usalama wa wananchi. Wanajeshi na polisi kazi yao ni kulinda usalama wa wa-twawala na jamaa na marafiki zao (yaani matajiri wenzao). Askari ni msukule unaojenga ukuta kati ya wananchi wanaodai haki zao na wa-twawala wezi wenye kiburi na dharau. Baadhi ya askari hawa wanaobeba bendera nyekundu na mitutu ni wale wanaoishi kwenye nyumba za mabati. Huwezi amini. Wanawapiga binadamu wenzao na hata vikongwe kisa eti wanatiii amri. Fela akaimba, "Zombie oooh, Zombie" (Msukule ooh, Msukule). Akaendelea kuimba:
Zombie nah go go unless you tell him to go
Zombie nah go stop unless you tell him to stop
(Msukule haendi hadi umwambie nenda
(Msukule hasimami hadi umwambie simama)
Ndio walivyo askari hawa wanaotutia ngeu na vilemwa tunapodai haki na usawa. Eti walinda usalama, usalama gani wanalinda huku wakiwapa majambazi silaha na wakati mwingine wakiwa ndio majambazi? Siku zinavyokwenda usalama nchini unatuaga huku askari hawa wakiendelea kujaza vitambi. Tukijiunga na wenzetu tukitaka kuandamana kama katiba inavyoturuhusu mara ghafla unaona wale askari wa kuanzisha (sio kuzuia) fujo wanakuja. Sijui kwanini huwa hatuwaoni siku za matembezi ya "mshikamano."
Yaliyotokea, yanayotokea, na yatakayoendelea kutokea Zanzibar hayanishangazi. Ukipanda mahindi huvuni ngano bali mahindi. Na wakati wa kuvuna wala haujafika.

2 Maoni Yako:

At 11/07/2005 08:54:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

Mbona una ugomvi na vitambi vya maaskari Ndesanjo? Kitambi ni sehemu ya sare siku hizi. Usipokuwa nacho unafukuzwa kazi.

 
At 11/07/2005 01:23:00 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Nakubaliana na wewe Ndesanjo,wanaoshangaa ni kwamba wanaweka pazia jeusi mbele yao wakati giza totoro limetanda mbele yao.Hatutakiwi kushangaa,tunatakiwa kusimama na kuchonga mitego.

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com