Demokrasia Bongo ni Chuki, Kutiana Vilema na Mauaji
Nimemaliza kusoma barua ya msomaji ambaye simtaji jina maana hajaniruhusu. Nimeibandika barua yake hapo chini. Nimetoa sentensi mbili za mwanzo wa barua ambazo zilikuwa ni salamu. Vingine vyote nimeviacha. Soma kwa makini anayosema. Kama hupendi kutazama mambo kwa mapana na marefu unaweza kudhani anayosema ni porojo au ndoto za Alinacha (hivi Alinacha aliota nini tena?). Haya, msome huyu bwana:
Kwako ndugu Ndesanjo,
Mada yangu mahsusi katika barua hii ni kuhusu mchakato mzima wa suala la uchaguzi Zanzibar.Nadhani yaliyotokea umeyapata na ikiwa hujayapata nitakupa kwa ufupi tu kwa kukuona wewe ni mwanamapinduzi halisi wa fikra.Ndesanjo tumepata pigo sisi wana demokrasia wa hapa Tanzania na jibu nililolipata ni kuwa hapa Tanzania hakuna demokrasia.Demokrasia ya viongozi wa Bongo ni chuki,kutiana vilema na mauaji.Ukitaka kuyajua haya fuatilia uchaguzi wa Zanzibar.
Ndesanjo, hakuna shaka upinzani umeshinda uchaguzi Zanzibar lakini je nani anaweza kuwakabidhi nchi?Zanzibar ilikuwa kama Iraq kwa muda wa siku nne,watu waliwekwa chini ya ulinzi wa wanajeshi ambao kazi yao ni kulinda mipaka sasa wanatumika kutisha na kuua raia wanaowalinda.Hii ni aibu kwa serikali ya Tanzania,kumbe haitaki kuondolewa madarakani kwa njia ya kura.Sio siri hakuna Mtanzania mwenye akili iliyochujwa ambae anaikubali hii serikali yetu kwani sasa sote tunajua kumbe nchi hii inatawaliwa kijeshi.
Sisi watu wa Tanzania bara tumekata tamaa kabisa ya uchaguzi kwa kuona yale yaliyotokea Zanzibar.Tulikuwa na muamko wa kuiondoa hii serikali ya CCM kwa njia ya kura lakini hili tumeona halitawezekana.Nashangaa sana vikosi vyetu vya majeshi vinakubali kuua na kutesa raia ambao pia ni ndugu zao kwa maslahi ya wachache.Hawa viongozi hawajui kwamba hii mbegu wanayoipanda hivi sasa ni mbaya sana?Hivi binadamu gani atakaekubali kuonewa kila siku?Ipo siku hali ya hapa Tanzania haitatofautiana na Jamhuri ya Congo,Somalia,Iraq na kwingineko ambako huko kote hakukaliki kwa ajili ya viongozi wenye tamaa.
Tunasikitika serikali ya CCM hapa Tanzania imeweza kuwatisha mpaka waangalizi wa uchaguzi wa kutoka nje ya nchi ambao kwa kweli nao wamekubali vitisho vyao na kutoa taarifa za uongo eti kweli uchaguzi ulikuwa huru na haki.Mkapa ndie aliewatisha mpaka wamesahau majukumu ya kazi yao.Ndio hapa nauliza nini maana ya demokrasia?
Tunashukuru tu kuwa Marekani imeona yenyewe na kutamka kuwa uchaguzi wa Zanzibar ni hovyo japo katika hili hatujui nayo itasimamia upande gani kutokana na yenyewe kuwa na sera kama za CCM.Kama kweli wana dhati basi wanaweza kuzuia umwagikaji mkubwa wa damu huku Tanzania kwani Watanzania wameshachoka na ubabe wa CCM.
Ndesanjo muda haunitoshi tu wewe si unajua haya maisha ya Bongo nimejinyima kula ili nikuandikie wewe hii barua huku kutuma Email ni shilingi 500/=
Mtiifu.
X.
4 Maoni Yako:
Ndesanjo, nadhani hoja yako ya msomaji huyo hapo yapaswa kutanuliwa na kupewa kipaumbele. Vyombo vya habari vya Tanzania vilikalia ukweli na vyombo vya kimataifa vikaanika wazi. Bado kuna wakati wa kupigania haki ya wanyonge katika Tanzania kutokana na kukosekana wenye malengo ya kuipigania.
Hakuna haki hakuna haki kabisa kututawala kwa njia ya wizi au udanganyifu. Hakuna haki ya kutumia nguvu zetu wenyewe kufanikisha matakwa ya wachache. Sasa nakumbuka, namkumbuka Marehemu, Kalikawe na Wimbo wake wa Mv Bukoba, alisema, "usitumie cheo chako kama daraja la matwakwa yako, utasababisha ajali kama ya MV Bukoba."
Mtakumbuka Meli ile ilipelekwa majini huku ikifahamika kuwa mbovu. Inajulikana kuwa CCM Zanzibar haipendwi na pia haijafanya vile inavyojinasibu lakini kwa nini itumie askari kuua ili ichaguliwe? Huo ndio utawala wa aina gani, tuambie tujue moja kuwa Tanzania inatawaliwa kijeshi, wakati wa kusema haya ni sasa na ninajua Blogu zipo nyingi sasa na zaweza kuwa cheche za ujumbe huu wa haki za raia.
Kwa kweli Zanzibar imetia aibu. Ni aibu tena ni aibu. Hakuna cha kuongeza zaidi ya hapo. Matatizo yote huanzia hapa. Angalia yanayotokea Ethiopia leo kwa uchaguzi uliofanyika Mei. Ni huo udanganyifu. Waangalizi wanaoojiita wa kimataifa ni upuuzi mtupu. Hata kama hawakutishwa na Mkapa. Hivi unatarajia waangalizi toka SADC wasihalalishe uchaguzi wa nchi nyingine ya SADC? Utakuta nchi zao nazo zinadanganya katika chaguzi. Hakuna namna ambayo watasema uchaguzi wa nchi nyingine ya SADC si huru na haki. Mkapa alisema kwamba kuwepo kwa wanajeshi Zanzibar si ajabu akalinganisha na IRAQ! kweli unalinganisha Zanzibar na Iraq? Jamani tunaelekea wapi? Hayo aliyosema msomaji wako kuhusu Somalia, DRC na kwingineko hawakupenda yatokee. Sisi tunayasoma kama historia. Lakini huwa na mwanzo. Mwanzo ndio huo unaotakiwa kuanzishwa Tanzania.
Mie niko mbali na nyumbani, lakini hapa nilipo nimekamata gazeti la Guardian Weekly, kuna habari za uchaguzi wa Zanzibar... maoni yao ni kuwa uchaguzi ulikuwa ni wa kibabe, kwa kadiri nilivyofuatilia vyombo vya nyumbani... ubabe ulitendeka.
vyama tawala vinaogopa mabadiliko lakini mantiki inatuambia mabadiliko yote huwa si mabaya... kuna watu wenye uwezo wa kutawala ambao si kutoka chama tawala...
Congress ya India iliogopa mabadiliko... Kina Indira wakapigwa risasi nk. Lakini BJP ilivyochukua nchi mambo yakaendelea bila ya shaka... CCM wasiogope kukubali mabadiliko.. kama CUF wameshinda kihalali.
Unapoanza kufunga kifungo kwenye tundu lisilo lake, shati haiwezi kupendeza mpaka ufungue vyote na kuanza upya... DRC walianza vibaya, sisi tunao uwezo wa kuanza vyema
Kaka TUNASEMA sana na wala HATUZUNGUMZI ndio maana.............. nitakueleza kwanini karibuni
Post a Comment
<< Home