11/24/2005

Tunaotetea Utamaduni wa Mwafrika Tutembee Uchi?

Nilisema ninavuta pumzi nizungumze kuhusu utamaduni. Utaona kuna wasomaji wameacha maoni wakishutumu wale tunaopinga tabia ya kudharau utamaduni wetu na kukimbilia wa wengine. Wameuliza eti mbona tunavaa viatu na nguo? Mmoja kasema kama tunatetea utamaduni kwanini tusirudi enzi za kuvaa ngozi? Wasomaji hawa nadhani hawafahamu kuwa jamii mbalimbali Afrika zilikuwa tayari zina viwanda vya nguo wakati weupe wakiwa wanaishi mapangoni na kula nyama za watu! Niliwahi kuandika makala nikizungumzia mada hii ya kuvaa nguo/viatu na kutetea utamaduni. Kichwa chake kilikuwa: Kama Unapenda Utamaduni Mbona Unavaa Nguo? Hapo chini nimeweka vipande kadhaa toka kwenye makala hyo. Ila unaweza kusoma makala nzima kwa kubonyeza hapa.
*********************************************
Vipande vyenyewe hivi hapa:

"Mara nyingi mtu unapozungumzia utamaduni wa Mtanzania au Mwafrika, inachukuliwa kuwa unazungumzia tu mambo ya kale. Kwa watu wengi utamaduni na ukale ni kitu kimoja. Watu wanaoamini hivyo huchulia kuwa utamaduni ni kitu cha zamani sana. Kitu kikuukuu. Kimezeeka. Kimetoka kwa mababu na mababu. Kwa maana hii watu wa leo tunarithi utamaduni tulioachiwa na mababu ila sisi haturithishi kizazi kijacho utamaduni mpya (unaotokana na kizazi chetu) bali ule tuliopokea toka kwa waliotutangulia.

Ukikutana na watu wanaofikiri kuwa utamaduni ni ukale kuna swali moja linalochekesha sana ambalo lazima wakuulize huku wakikutolea macho kama vile unafanya uhaini kutetea utamaduni wako: Kama unapenda utamaduni wa Mwafrika kwanini unavaa nguo? Kwanini unavaa viatu?"
****************************************
"Ukidhani kuwa ninaposema tupende utamaduni wetu ninamaanisha kuwa tufanye yote yaliyofanywa na mababu zetu utakuwa umefanya kosa kubwa sana. Kwani mababu zetu walikuwa ni miungu? Kwanini tuchukue kila walichofanya kama vile walikuwa hawana mapungufu? Mababu zetu ni binadamu kama sisi. Walikuwa na mazuri na mabaya pia. Je tukubali kukeketa wanawake maana ni urithi wetu? Hakuna sababu yoyote ya msingi ya kuendelea kukeketa wanawake hata kama tendo hili lilifanywa na mababu zetu."
**************************************************
"Kuna jambo linalonishangaza ninapokutana na wale wanaoniuliza, “Kama unatetea utamaduni mbona unavaa nguo?” Kwanini wanapozungumzia utamaduni wa watu weupe hawarudi nyuma na kuganda kwenye historia. Wanachukulia kuwa wanayofanya leo hii watu weupe ndio utamaduni wao, ila sisi Waafrika utamaduni wetu ni yale tuliyofanya wakati tukiwa tunatembea uchi. Utamaduni wa watu weupe ni yanayofanywa leo na wa kwetu ni yake ya zamani. Ni kitu gani kinachofanya kuvaa nguo kuwe ni utamaduni wa watu weupe ila sio Waafrika?

Mtazamo huu unaashiria kuwa kuna watu hawategemei Waafrika twende mbele maana itakuwa kinyume na utamaduni wetu! Mtazamo mbovu sana huu. Mbona hata hao watu weupe kuna kipindi katika historia yao ambacho waliishi mapangoni, walitembea uchi, walikula nyama mbichi, walikula nyama za watu, waliua wachawi hadharani, n.k. Watu wengi hawafahamu historia hii maana shuleni tunafundishwa historia yetu toka tukiwa tunatumia zana za mawe, tukiishi na kuchora picha mapangoni ila historia ya watu weupe inaanzia zama za mapinduzi ya viwanda. Kutokana na hili, watu wengi wanaona kuwa utamaduni wa mtu mweupe ni mambo ya kileo."
***************************************
"Hakuna jamii yoyote isiyokua, isiyobadilika, isiyochukua mapya, isiyotupa ya zamani, na isiyohifadhi yale ya zamani yanayofaa. Nipe mfano wa jamii kama hiyo. Hoja hii ndio ambayo inawapa tabu wanaotetea ukeketaji wa wanawake kwa madai kuwa ni utamaduni. Kwa uelewa wa zama zile za mababu, tendo hili lilionekana kuwa ni sahihi. Ila kwa uelewa wa mazingira tunayoishi leo tendo hili linaonekana kuwa sio sahihi."

4 Maoni Yako:

At 11/24/2005 05:00:00 AM, Blogger mwandani said...

Ay! Kwenda uchi mie siwezi. Baba yangu nimemkuta anavaa nguo, babu yangu alikuwa anavaa nguo na blanketi alikuwa akijitupia shingoni. Hawa ndio walionifunza utamaduni bila kunihubiria.
Hata uchi mtu anavyoutazama pia inategemeana na mazingira ya utamaduni uliokuwepo - context. Kwetu kule ziwa Nyanza akina mama wanakoga sio mbali sana na wanaume, na sisi akina baba tunakoga kwa jumla ziwani - asubuhi na jioni. Mie sikumbuki watu waliokuwa wanajali uchi au kupiga chabo akina mama.Nilipokuwa umasaini kila siku nilikuwa naona matiti ya akina mama yanachungulia nje ya lubega...Haitii shaka.
Hao wanaosema tuvae ngozi... Mswati anavaa ngozi na wake zake mia - katika mazingira yake haina shaka.
Hivi leo tuanze kwenda uchi kisa utamaduni, jama! Utamaduni unabadilika - hakuna utamaduni unaoganda. Utamaduni wa zamani nyumbani kwake makumbusho. Halafu utamaduni unaofanya kazi uko kwenye dhana - mila na desturi.
Mavazi ni kielelezo cha nje tu. Tembea tembea utakutana na watu wenye kuvaa vitenge na vielelezo vyengine vya utamaduni wa mwafrika - lakini wakifungua midomo utasikia kasumba tupu...
Dumisha utamaduni kwa vitendo na kauli. Kwenda uchi??... sijui

 
At 11/24/2005 09:51:00 AM, Blogger Jeff Msangi said...

Ndesanjo na Mwandani,
Nimepumua bila tabu baada ya kusoma hoja zenu.Ahsanteni sana.Huu ndio mtazamo makini na endelevu.Lazima tupende vyetu na tujitahidi kwa hali na mali kuviboresha.Hapa nina maana zikiwemo mila na tamaduni zetu.Na kama katika kuboresha huko itatubidi kuiga kidogo basi tufanye hivyo lakini asili(originality)tuitunze na kuienzi.Tunapokubali kumezwa na tamaduni zingine tunajichimbia makaburi.Tunazitendea visivyo asili zetu.Sijui kama nimeeleweka hapa,kidogo napata hasira na hawa watu wanaotamani tubakie mitini!

 
At 11/25/2005 12:35:00 AM, Blogger mloyi said...

Wapinzani kazi yao ni kupinga tuuuuu... bila kumalizia ile u! Inaonyesha jinsi ukoloni na vyombo vyake vilivyofanikiwa kujiimarisha kwenye akili zetu!
Leo hatustahili kuvaa nguo sababu babu zetu hawakuvaa nguo!!!! aliyesema hili hana mishipa ya aibu! anadharau isiyovumilika kwa utu wa mwafrika. Kila kitu cha mwafrika yeye anatunga uongo wa kukikashifu. Alianza tulikuwa tunavaa magome ya miti, tukalikubali hilo, akaendelea tulikuwa tunavaa ngozi za wanyama bila kuangalia sayansi iliyokuwa inatumika kutayarisha mavazi hayo. Sasa anataka kututukana kwa hili. Waambie wasome kitabu cha R.A Rogers "from superman to man" kitafaa kuufyatua ubongo wao na kujifikiria vizuri!
Wajue wazungu hawakutukuta sisi tunalala nje, tulikuwa na vijiji vyetu tayari, Nguo zilikuwepo kwa wote, chakula hakikuwa shida, magonjwa yaliyokuwepo(jua mengi yameletwa na hao wanaowasifia kuliko tsunami) yalikuwa na tiba zake. Watumbie nini tulikosa.
Mjadala mzuri.

 
At 11/28/2005 04:09:00 PM, Anonymous Anonymous said...

yaani huu mjadala nimeanzisha ni mzuri ndo mambo kama haya mnapaswa kuongelea ya kuelimishana ni wapi tunatokea na sio gumzo tuu kulalama tuu hauoni sasa mnaelekeza watu shule na sio kuwaambia utamaduni kila saa waelewesheni ni wapi walianza na kwamba wao si watumwa kabisa.

nampaka hapo tulipofika yani mambo yanawiana sasa na si kumnyima mtu uhuru wake kabisa.

blogu zilikuwa zinafikia mahali zinaanza kuchosha ni vizuri kuanza kuchangamsha watu.

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com