Kizazi cha Watumwa Wapya!
Mjadala kuhusu muziki wa "kizazi kipya" umepamba moto. Jeff na Ramadhani wameuanzisha. Na wasomaji wao wameudaka. Maswali kadhaa bado yanaelea hewani. Hivi "kizazi kipya" ndio akina nani? Na Bongo Flava ndio nini hasa?
Ukitazama kizazi tunachokiita kipya. Ukaangalia tabia, mwenendo, fikra, na njozi zake utakubaliana nami (kama huwa unapenda kuita beleshi kuwa ni beleshi) kuwa jina sahihi la "kizazi kipya" ni "watumwa wapya."
Watumwa wa zamani walidakwa kifikra, kitamaduni, na kiroho katika wimbi la ukoloni, safari za “wavumbuzi,” na kazi za wasambaza "ustaarabu" (wamisionari). Leo hii wimbi linalokumba kizazi kipya cha watumwa wapya ni wimbi la utandawizi. Utandawizi ndio ukoloni mpya. Wimbi hili linasukumwa na falsafa na itikadi za soko na ulaji. Soko lenyewe sio soko kama la Kariakoo au Kiboriloni. Nitamwachia Nkya wa Pambazuko achambue zaidi juu ya hii dhana ya soko. Kwa kifupi dhana ya soko katika ubepari haina maana mahali pa kuuza na kununua. Na ninaposema ulaji simaanishi ulaji kama ule wa kula ugali na kisamvu. Kwa kilugha chao wanaita "consumerism." Katiba ubepari dubwana hili ulaji (consumerism) ndio ibada.
Zamani zile waliotutangulia walitekwa kwa njia mbalimbali, baadhi zikiwa za kinyama (viboko, bundiki, vifungo), nyingine vitisho (utakwenda motoni usipoamini dini yetu), elimu, n.k. Leo hii mabwana wa utumwa wala hawana haja ya kuja na viboko na au kutuma watu wao na biblia na kurani kutuhadaa tukatae tamaduni zetu. Mazingira yamebadilika na mbinu zimebadilika. Lakini pia ziko nyingine zimebaki vile vile au kubadilika kidogo. Vitukuu wa wale waliotia minyororo fikra za mababu zetu ndio hivi sasa wanakaza pingu katika akili za hawa tunaowaita "kizazi kipya." Wanatumia tamaduni maarufu (kilugha chao wanaita pop culture) na vyombo vya uongo kama MTV. Wanatumia picha za wanamuziki wakiwa wamevaa nguo za aina fulani kuwafanya watumwa wapya wadhani kuwa ili wawe wanamuziki wakubwa wanapaswa kuvaa nguo kama hizo, mikufu, na pia kuwa na majina kama Crazy G na hata kubadili namna ya kutembea. Wanatumia majarida. Wanatumia filamu na muziki. Wanatumia redio za FM na Ma-DJ ambao ndio vinara wa utumwa mpya. Wanatumia vipindi vya luninga kama Big Brother. Wanatumia mashindano kama Miss Tanzania. Wanatumia mikufu ya dhahabu (mingine ikiwa ni ya msalaba). Wanatumia mapicha makubwa ya ukutani ya watu kama akina 50 Cent.
Unajua wengi tunaona utamaduni kuwa ni kitu cha mchezo mchezo. Hasa tunapodhani kuwa utamaduni ni ngoma za kukata kiuno, vinyago vya wamakonde, ngonjera, na nguo za batiki. Utamaduni ni rasilimali. Watu wakizimikia utamaduni wako watazimikia pia na bidhaa zako (hadi bendera ya nchi yako wataivaa). Unakuta kuna nchi zinatambua hili na zinafanya kila liwezekanalo kulinda utamaduni wao. Wanatumia sera, sheria, elimu, n.k. kutimiza azma hiyo. Nchi kama Ufaransa zina idadi maalumu ya sinema za Marekani zinazoruhusiwa kuonyeshwa katika majumba ya sinema nchini humo. Nia yake ni kulinda soko la watengeneza sinema wa ndani. Sheria ya mambo ya Intaneti Ufaransa inasema kuwa tovuti yoyote ile ya Ufaransa lazima iwe na lugha ya Kifaransa. Inaweza kuwa kwa Kiingereza au Kijerumani lakini lazima kuwe na toleo la Kifaransa.
Lakini pia utamaduni unaweza kuwa mpambano. Ni mpambano wa mitazamo. Mfano mzuri wa hili ni ugaidi. Ugaidi una sura nyingi. Upande mmoja wa sura ya ugaidi ni utamaduni. Unaweza kutazama ugaidi kama mgongano wa mitazamo ya kitamaduni kuhusu demokrasia, wema, ubaya, historia, n.k.
Nirudi kwenye hoja ya msingi. Wakati tunapotazama kundi tunaloliita "kizazi kipya," mimi ninachoona ni kizazi cha watumwa wapya. Tena watumwa kwa maana mbili. Kwanza, watumwa wa kifikra na kitamaduni. Pili, watumwa kiuchumi, kwa maana ya kuwa katika nchi yao bila uwezo wa kumiliki njia kuu za uchumi au kuwa na uwezo wa kutoa maamuzi makuu kuhusu uendeshwaji wa nchi.
Wa-twawala wanapenda sana kizazi hiki kinapotumia muda mwingi "kujirusha" na Bongo Flava au kuketi mbele ya luninga wakitazama Big Brother wakati nchi keki ya nchi inamalizwa. Kwa akili za kizazi hiki cha watumwa wapya, kitendo cha kuwa na luninga zinazoonyesha Big Brother, redio za FM za kupiga miziki yao, luninga za kuonyesha video zao, na majengo marefu marefu yanayojengwa mjini ambayo wanayatumia katika kutengeneza video zao za muziki, bila kusahau hoteli za kifahari ambazo nazo wanazitumia kutengeneza video hizo...mambo haya kwao ni alama ya maendeleo makubwa ya nchi. Na nchi kwao huwa ni mjini.
9 Maoni Yako:
Kukata mti unaong'oa mizizi siyo uchanje matawi, kuzuia kujikwaa unang'oa kisiki siyo kusawasisha ardhi ya pale ulipoangukia, kuondokana na huo ulimbukeni ni ............
Ukichunguza utaona hao vijana wanaonewa. Labda wengi wao hawajatoka hata nje ya mipaka ya mikoa yao, sasa 50 Cent walimfahamu vipi? Tatizo ni hivyo vyombo vya habari, magazeti, redio na luninga ...... ambazo ni silaha kali za maangamizi kuliko zote duniani. Vyombo vya habari hushambulia akili ya mtu ashindwe kuona, kusikia, kufikiri na kutafakari. Dr Remmy Ongara aliwahi kuhoji "Nimezunguka sana duniani, mbona huko nje sijasikia redio na maluninga zikipiga nyimbo za Sikinde, Msondo, n.k."? sisi hapa,Tz, iweje redio zetu zipige nyimbo za nje tena kuliko zetu. Sijui kama alieleweka. Wachache kama Mwalimu alilijua hilo muda mrefu, kwani umesahau enzi zake RTD ilikuwa ikipiga ngoma za nyumbani tu!!!!. RFA nadhani na Clouds (kama sijakosea) nao walianza vizuri, lakini hiki Kirusi cha ulimbukeni na pesa kimewapata, nao siku hizi wanapiga miziki ya nje na hiyo miziki ya Ki-marekani inayoimbwa na Wa-Tz halafu ikapewa jina muziki wa "Kizazi cha Malimbukeni". Tukiachana na hao wanamuziki, hao watangazaji je? kipindi cha Kiswahili redioni - yeye anachomekea maneno ya kiingereza, tena mengi sana, ndiyo fasheni na kuonekana amesoma na ameendelea GDP ngapi sijui. Mdada mtangazaji wa FM redio fulani ya Dar alisema hivi " .... lakini in that case I don't think kwamba......."!!!. Tumekwisha, hawa vijana siyo wasanii, ni watu wanotumika tu kuua utamaduni wetu kwa kupitia vyombo vya habari. Wala hakuna wanachoelewa, kwao wao kuimba kwa kiswahili ni kupiga muziki wa TZ. Wanachoshindwa ni kufahamu ni kuwa muziki hutambulika kwa mirindimo. Alpha Blondy anapoimba rege kwa hatumii kiingereza lakini muziki unabakia ni tu, muziki wa Jamaica. Sasa kijana Tz anaimba rapu ya Kimarekani kwa kiswahili halafu hivyo vyombo vya habari vinaturubuni kuwa huo ni muziki wa kizazi kipya. Tatizo ni hivyo vyombo vya habari ...... wala siyo vijana. Vyombo vyenyewe vichache kuwawajibisha ni wajibu na wakubali kuwa wanafanya jitihada za makusudi kutuuza utumwani......
Ebo!hapa umenigusa sana mheshimiwa Ndesanjo;pamoja na kuwa vyombo vya habari vina mchango wake lakini mimi naliona hili chanzo chake ni kufeli kwa taasisi ya familia.
Kama watoto wetu wangelelewa na wazazi waelewa wasingevutwa sana na hivi vikolombwezo vya utandawazi.Tatizo kwanza wazazi wengi hawajui hata ni nini utandawazi.Sasa watajuaje hata madhara?Hawa waandishi wa habari ndio hao hao watoto wa familia zilizofeli kimaadili.Sasa utarajie watutangazie nini?
Tumewaachia wa-twawala nchi wala hatujali kazi yetu ni kupiga kura na kufuraia kipindi cha kampeni kulipwa hongo.
Sijui nisemeje lakini:
TUMEKWISHA.
@Mti,
Umesema kweli, miziki ni mirindimo na si maneno. Pata picha Hayati Mzee Morris Nyunyusa na ngoma zake angekuwa akiimba kwa kizungu halafu adai kwa nguvu zake zote kwamba yeye anapiga muziki wa kimarekani, je watu wangekubali???
Lazima watoto wa vijiweni wangesema sasa Mzee Morris anazeeka vibaya. Kwa hiyo utambulisho wa muziki ni midundo na si lugha.
Kwani uongo? mzee Nyunyusa hata angeimba kwa lugha ipi bado muziki ungekuwa wa kwetu, sasa hawa vijana wanapiga muziki wa kigeni halafu wanaimba kwa kiswahili na tuauita muziki wetu wa kizazi kipya, ni mazingaombwe haya. Nashauri unafiki uondolewe wauite tu muziki wa kule kwenye asili yake. Kama ni rap/rnb au rmb? ni ya marekani na charanga ni ya latino. Lakini usisahau ni hivyo hivyo vyombo vya habari vimewapa au kulikuza hilo jina la kizazi kipya. Sana sana hizo redio za FM. Kwani umesahau vipindi vya rock-time na charanga time tena vikiendeshwa na watangazaji tulodhania ni mahiri? katika vyombo vya habari za kitanzania? aibu.
mimi ninaona hii ya kuva dhahabu mnazidisha kwani Tanzania haichimbwi dhahabu? sasa iweje watanzania wasivae dhahabu? kwani watanzania kazi yao ni kuwachimbia dhahabu watu wengine tuu ili wavae na sii wenyewe? na mlikuwa wapi wakati vazi la Tanzania likitafutwa? nafikiri ingekuwa vizuri sana mngekuwepo ili mkasaidia na kuweke sheria nini kivalike na nini kisivalike na mtu atapata adhabu gani kwa kuvunja sheria hizi.
Halafu niulize kwani hata hizo siruwili na mashati na gauni na sketa na mavazi ya kitanzania au pia tumeiga tuu sii zamani tulikuwa tunavaa nini sio ngozi kufunika maeneo tuu ili tusibaki huluuuma. basi mimi naona na hili mliongelee kila mtu arudi kuva kijipande cha ngozi pekee.
Mnaongea sana na kuigana tuu mmoja kaanzisha mada kaona imevutia watu wengi basi watu wote mnaiga na kuingilia mada hiyo, aaaah mnachosha na ninyi hebu badilikeni sasa kuweni wabunifu angalieni ni jambi gani lingine halijagusiwa tuzidi kusonga mbele.
Hapo umesema kweli, Dar mtu anavaa suti na tai pamoja na joto lote hilo, hata huo ni utumwa. Kuvaa cheni ruksa, wala hakuna kosa. Iringa/Mbeya/Arusha wakivaa suti itaeleweka. Wenzie ughaibuni wakati wa joto wanavaa kaptula na vimini. Pamoja na hayo tamaduni zote ni za kuiga. Ndiyo maana watu wa bara wanakula pilau. Wameikuta mjini tena ukubwani. Tofauti ni kwamba hawakuchapwa bakora kulazimishwa kuila. Ungejifunza historia muda wote wa masomo yako labda ungekuwa na wazo tofauti. Je, unajua kama babu zako mwanzoni walikuwa wakipewa nguo bure? na wakikutwa hawajavaa wanalambwa bakora??. Je, unajua kuwa babu zako hawakuruhusiwa kujiunga na shule au kutibiwa hospitali hadi abadilishe jina na kuchukua jina la kigeni??. Tamaduni huigwa, lakini unaiga iliyo nzuri kwa manufaa yako na siyo kuiga kwa vile UMELAZIMISHWA au kwa vile unajiona wewe ni DUNI au kwa vile UMEHONGWA pesa kuuwa tamaduni nyingine. Ukigundua hizo tofauti kupitia historia nadhani utakuwa na wazo tofauti. Utandawazi ni kisa cha wewe kuuiga huo muziki na siyo ubora wa sanaa iliyomo ndani yake. Sasa kwanza ujue utandawazi ni nini na nafasi yako katika huo utandawazi.
hata viatu navyo mlivijulia wapi kama sio kuiga pia? kuna kiwanda Tanzania kinaweza kuzalisha viatu kwa ajili ya watanzania wote au inabidi watu wazidi kusibiria mitumba na ndio viatu vya maana, we nenda kimbilia yale maocean sandals au yale mayeboyebo ya Dar kama hujakaanga miguu na sijui nani atakusaidia kuila maana ujue hiyo ni nyama ya mtu na aliyekuwa anakula nyama za watu idd Amin hayupo. mengine mfikirie kabla hamjaongea.
RUKSA WATU KUJIKWATUA hizi zingine ni sheria za kigagula sasa. JAMANI
Mwenzetu unakwenda mbali. Anayevaa kiatu kwa vile ni bora na muafaka kuliko kupekuwa ni tofauti na nayevaa kiatu kwa vile anataka kuonekana yu sawa na hao mabwana wakubwa halafu ndiyo kuendelea. Sasa wewe uko wapi?
Kuna bwana katukumbusha swali alilouliza Remmy Ongala: mbona redio na luninga nchi za weupe hawapigi Msondo Ngoma??
Kama mtoa maoni huyo alivyosema hapo juu, inawezekana hatukumwelewa Remmy. Na swali bado liko pale pale. Ninaona ni sawa kabisa alivyoamua kuita vyombo vya habari (yaani uongo) kuwa ni vyombo vya maangamizi. Na ametukumbusha enzi zile za RTD wakati wa uhai wa Mwalimu. Kulikuwa na vipindi ambavyo hadi leo hii nikivikumbuka nataka kutoa machozi. Tumevifuta na kuweka vipindi vya kuhadaa fikra.
Mtoa maoni mwingine kasema jambo la msingi sana. Kasema kuwa bora kuvaa viatu kwa kuwa ni bora kuvaa viatu kuliko kutembea peku kuliko kuvaa viatu kwakuwa unataka kufanana na watu wengine. Nami naongeza: watu hawa huwa ni wale tunaowaona kwenye filamu za muziki, magazeti kama Ebony, vipindi kama Big Brother, n.k.
Mtoaji mwingine hapo juu kasema kuwa tubadili mada. Ameshutumu kuwa tumekosa ubunifu kwakuwa tumedakia hoja hii ambayo kaanzisha mmoja (na wengine wote tumeishupalia hiyo hiyo). Mimi binafsi sioni ubaya wa kuendeleza hoja hii. Kosa lake ni nini? Kwani hatuna uhuru wa kuzungumzia masuala ambayo yanatugusa? Jeff Msangi kaanzisha hoja, Msangi Mdogo naye akaendeleza, mimi nami ikanikuna. Kuna ubaya gani? Suala hili, hasa kwakuwa linahusu utamaduni, linanikuna mno na nina haki zote za kujadilia mada yoyote ile ninayotaka (iwe imejadiliwa na wengine au ni mpya). Ndio uzuri wa blogu ninaoongelea kila siku. Hakuna mtu anayeweza au mwenye haki ya kutuzuia kujadili chochote tunachotaka. Ila wasomaji pia wana haki, kama mtoa maoni huyu, kutuambia wanayofikiri wao. Kwahiyo, msomaji huyu hajafanya kosa kututaka tujadili jambo jingine. Nami sijafanya kosa kumwambia kuwa tuna haki ya kujadili hoja yoyote ile tunayotak. Kwahiyo mwisho wa mchezo unakuta mabao ni 0-0.
Post a Comment
<< Home