11/13/2005

Kukataa Kutawaliwa na Wezi ni Wajibu wa Kikatiba na Kiroho

Naendeleza mjadala nilioandika jana ulioitwa: Tatizo ni Wa-twawala au Watawaliwa? Kama hukuusoma bonyeza hapa uusome kisha urudi hapa ndipo uendelee.
*********************************
Kenya itazameni. Kuna masomo chungu nzima pale. Unaona tunavyoonyeshwa kuwa kuna uwezekano kuwa wapinzani na wa-twawala hawana tofauti zaidi ya kuwa upande mmoja uko madarakani na upande mwingine unataka kuyachukua. Wapinzani watapinga mambo yote yanayofanywa na walioko madarakani. Lakini wakiingia madarakani watayafanya yote waliyokuwa wakiyapinga na hata mabaya zaidi. Na wale waliokuwa madarakani wataanza kupinga mambo ambayo nao walipokuwa madarakani waliyafanya. Kumbuka Kaunda alivyotiwa ndani na sheria ambayo alikuwa yeye mwenyewe akiitumia. Akadai kuwa sheria ya kutia watu kizuizini ni kinyume na haki za binadamu. Yaani haki hizo anaziona pale yeye ndiye anapokuwa anakandamizwa.
Pale Kenya waliokuwa wakiiunga mkono katiba wakati wakiwa wapinzani, wameikataa walipoingia madarakani. Waliokuwa wakiikataa wakati wakiwa madarakani sasa wanaikubali. Yote hii ni mchezo wa kuhadaa wananchi kwa nia ya kushika madaraka. Midomo ya wanasiasa ni bomba la uongo. Jana niligusia suala la wanasiasa wanaohama vyama vyao baada ya kutochaguliwa kugombea uongozi wakidai kuwa vyama hivyo havifai. Vyama wanavyohamia vikija kuacha kuwapa nafasi za kugombea uongozi wataondoka wakidai kuwa navyo havifai. Wewe mtu umekuwa kwenye chama toka ukiwa kijana, leo hii umezeeka unakuja kudai eti chama hicho hakifai kuongoza. Na unasema hayo mara tu baada ya kuchujwa kwenye kura ya maoni.
Au tazama kiongozi wa chama fulani anayelalamika juu ya viongozi wasiotaka kuachia madaraka au marais wanaobadili katiba ili waendelee kuwa madarakani wakati yeye mwenyewe hayo madaraka ndani ya chama chake hajayaachia. Ni nini kinakufanya wewe uwe na haki ya kuwa mwenyekiti wa kudumu wa chama chako (au cheo kingine cha "maisha" ndani ya chama chako) na wakati mwingine mgombea urais wa maisha, lakini mpinzani wako hana haki ya kung'ang'ania madaraka?
Jana nilisema kuwa tabaka la wa-twawala limefanikiwa kutufanya tuamini kuwa huu mfumo wa ulaji na ukandamizaji wanaouita "demokrasia" ndio njia pekee ambayo binadamu wanaweza kutumia kujenga taifa. Tazama bunge la Kenya kwa dakika chache. Bunge hili ni upenyo wa kujitajirisha na kuipora nchi. Mwezi uliopita bunge nchini Kenya kwa dakika 30 liliruhusu wizara 18 kuchukua zaidi ya shilingi za Kenya bilioni 100 toka kwenye mfuko maalum. Kwa nusu saa shilingi bilioni 100 za nchi masikini kama Kenya zimeyeyuka. Kura hiyo ilipitishwa na wabunge wangapi unajua? 22!
Sisi wananchi wa kawaida, tabaka la waliwao, tuna uwezo wa kukataa kunyonywa na kudanganywa. Tuna wajibu wa kikatiba na hata kiroho (kama unaamini kuna kitu kama roho) kukataa kuwa chini ya hili tabaka dogo la wezi na wauza nchi. Kuna sababu za kutotimiza wajibu huu?

9 Maoni Yako:

At 11/13/2005 04:02:00 PM, Blogger Boniphace Makene said...

Kuna kazi Ndesanjo, maandishi haya yanachoma moyo na hasa ukiangalia mfano huo wa Kenya, inanikumbusha shairi moja katika Karibu Ndani kitabu cha Kezilahabi lisemalo

"Hatumwoni"

 
At 11/15/2005 11:45:00 AM, Blogger Jeff Msangi said...

Ndesanjo,
Uchungu wako ni halali na makini isivyo kawaida.Tutamtambuaje?Hili ndilo suala la kujiuliza wananchi wenzangu.Tuanze sasa

 
At 11/18/2005 01:57:00 AM, Blogger Bwaya said...

Aisee umenichoma moyo kwa maneno makali namna hiyo.Ninafikiri mengi mengi sana sasa hivi. Najisikia kulia kwa jinsi ambavyo siasa zetu za kiswahili zinaendeshwa kiufundi ufundi. Unajua nini, nimefikiri sana, nani sasa wa kumwamini kati ya mpinzani na hawa "wanaume" wanaoamini kuwa Tanzania ni yao daima dumu? Wakati ninatafakari nani wa kumpa kura yangu, nitamtambuaje "mwanasi-hasa" mwenye kumaanisha ayasemayo, na yule anayeitamani keki tu na si vinginevyo? Isije ikawa nikaona mpinzani ndiye, kumbe ndio balaa kabisa. Nadhani hilo usilisahau unapoendelea na mjadala huu mzito.

 
At 11/18/2005 04:18:00 AM, Blogger Mija Shija Sayi said...

Ndesanjo, tatizo liko kwetu sisi raia, tumeamua kuishi kienyeji bila kutaka kujua haki zetu na wajibu wetu katika maisha yetu. Hatuna ukereketo wa kuisaka katiba ya nchi na kuisoma, kazi hii tumeona ni ya wanasiasa tu na ndio maana hata nchi na maisha yetu kwa ujumla tumewakabidhi wanasiasa. Na wenyewe kwa kulijua hilo ndio maana wanatuchezea mchezo wa kuigiza wakijua tulio wengi hatujui haki zetu, wala nafasi zetu katika nchi, na ndio maana tunakubali kumpiga hadi kumuua kibaka wa shilingi 100, na kumsifia kwa utajiri mtwawala mwenye akaunti ya mamilioni huko Uswis, Au tunambeza na kumdhalilisha Omba-omba Matonya kwa kuikimbia Dodoma kuja Dar kutafuta riziki, lakini wakati huo huo hatuoni kama watwawala wa kibongo nao wanafanya yale yale anayoyafanya Matonya.
Kwa hiyo sisi raia ndio tunawapa kichwa, ni wavivu wa kutaka kujua na ndio maana tunaburuzwa, hata katika Biblia Hosea 4:6 Mungu anasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Ni lazima tubadilike sisi raia halafu watwawala hawatakuwa na nguvu.

 
At 11/18/2005 04:31:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

Mija kwa kweli umenigusa na hili suala la umatonya wa Serikali. Sasa hivi kuna watu wa ajabu sana wanasema eti kwa vile Kikwete alikuwa Waziri wa Mambo ya nchi za nje kwa miaka mingi basi ataweza kupata misaada kibao. Yaani wanafurahia rais ombaomba!!. Tuamke. Kizazi hiki tutimize wajibu wetu au tuutupilie mbali kama anavyosema Fanon.

 
At 11/18/2005 06:32:00 AM, Blogger Mija Shija Sayi said...

@Inkya,
Na omba omba yeyote ni mtumwa kwa mwenye kuombwa (mwenye nacho). Jinsi tunavyomdharau Matonya kwa uombaji wake, ndivyo nchi pokea misaada zinavyodharauliwa na nchi toa misaada.

 
At 11/18/2005 10:24:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

@Mija
Huo ndiyo ukweli. Ukisoma yale aliyosema Mwalimu mwaka 1967 kwamba fedha si msingi wa maendeleo alikuwa akikemea hii misada ya nje. Moja ya hoja zake ni kwamba kuna misaada ya aina mbili; moja ni mkopo ambao ni lazima baadaye ulipwe kwa hivyo unahitaji kuzalisha ili kulipa huo mkopo; pili ni msaada unaotolewa kama sadaka. Huu unakukosesha uhuru. Unaambiwa cha kufanya. Unakuwa mtumwa katika nchi yako mwenyewe. Hivi unajua sasa hivi huwezi kupitisha mpango wowote pale nchini bila kukubaliana na "wahisani"? Ndio utumwa huo. Pesa si msingi wa maendeleo. Zalisha zaidi.

 
At 11/19/2005 08:48:00 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Mfano wa Matonya na uombaji wa wa-twawala wetu ninaupenda sana. Pia Mija umegusia suala la katiba. Nimewahi kukutana na watu wanakaribia kutoana ngeu wakibisha juu ya katiba. Ukiwauliza kama wamewahi kuigusa. Wala sio kuisoma. Hapana, kuigusa tu jalada lake...unakuta hawajawahi hata siku moja. Hivi sasa kuna vilabu vinaanzishwa Tanzania na vijana vinaitwa Jikomboe. Vilabu hivi kati ya mambo wanayofanya ni kujisomea katiba na kuijadili.

Halafu Nkya umesema jambo zuri sana: pesa sio msingi wa maendeleo. Ningependa ulifafanue hili zaidi kimakala siku moja ukiwa na wasaa. Tafadhali.

 
At 11/20/2005 11:28:00 PM, Blogger Indya Nkya said...

@Macha
Nililifafanua hili suala katika makala yangu niliyoandika kwenye gazeti la Rai tarehe 13.10.2005 katika kumbukumbu ya Mwalimu. Niliiweka kwenye blogu. Lakini sikubandika kwenye kona ya makala zangu. Nitaiweka ili watu waisome.

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com