11/12/2005

Rege, katiba ya Kenya, wanasiasa wanavyotuchezea

Siku hizi nimekuwa nyuma sana katika masuala ya muziki wa hisia, Rege. Siwezi kuamini kuwa sikuwa nawafahamu jamaa wa Midnite. Jamaa mmoja alinisikilisha muziki wao hivi majuzi. Nimewafia kabisa. Nalala na kuamka nikiwasikiliza. Kwanza muimbaji wao ana sauti ya pekee sana. Na anajua jinsi ya kuitumua sauti yake. Ukiachilia mbali sauti, ujumbe wa nyimbo za Midnite unanigusa sana. Dakika hii wanaimba wimbo mmoja wanasema:
Penda maisha unayoishi
Ishi maisha unayoyapenda.
Wimbo mwingine unaonimaliza ni ule ambao anazungumzia luninga kuwa ni chombo cha uongo. Anatumia mchezo wa maneno ambao Marasta wanapenda kuutumia kutoa ujumbe wao. Kwa mfano, "television" anasema ni "tell a lie vision." Ni mchezo huu wa maneno ambao aliutumia Peter Tosh alipokuwa akiuita mfumo wa siasa na utamaduni wa kibabiloni "shit-stem" kutokana na neno la kiingereza "system." Bonyeza hapa kwenda tovuti ya Midnite.
Tuachane na Midnite. Sijui kama unafuatilia kampeni za kura ya maoni kuhusu katiba kule Kenya. Nadhani zoezi hili kwa ujumla linatufunza mengi kuhusu uundaji wa katiba ya watu na pia kutuonyesha wanasiasa wanavyotuchezea. Utaona kuwa wale wanasiasa waliokuwa wakiipinga katiba mpya wakati wakiwa madarakani, ndio hao wanaoiunga mkono sasa wakiwa nje ya madaraka. Na wale waliokuwa wakiiunga mkono wakati wakiwa nje ya mduara wa ulaji, sasa wanaipinga kwakuwa ulaji wao utakuwa mashakani. Haya ni mafunzo ya bure lakini wakati mwingine huwa yanatupita.
Umeona hata Tanzania wale wanasiasa ambao wamekosa nafasi za kugombea ubunge kwenye vyama vyao wamehamia vyama vingine wakidai kuwa vyama vyao vya zamani havifai. Wamekuwemo kwenye vyama hivyo hadi dakika ya mwisho (walipokosa nafasi za kugombea) ndio wakagundua kuwa vyama hivyo si lolote/chochote? Wengine wamekuwa wanachama wa vyama vyao vya zamani karibu maisha yao yote. Kama miaka yote hiyo walishindwa kuona ukweli ambao wengine tumekuwa tunauona kila siku, ni vipi tunaweza kuwaamini kuwa wanaweza kuwa viongozi wazuri. Kama inachukua miaka mingi namna hiyo kuona jambo la wazi namna hiyo, kwanini tuwape dhamana ya kutuongoza? Tusipojenga utamaduni wa kuwauliza maswali magumu wanasiasa kama hawa watakuwa wanatuchezea kama wanasesere. Watatuchezea na baadaye wakishalewa madaraka tukiwauliza maswali magumu wataanza kutumia watwana wao (polisi/wanajeshi) kututia vilema, kutuunga na hata kutuua.
Kuhusu kura ya maoni kule Kenya, mwanablogu Kenya Pundit anafuatilia kwa karibu sana zoezi hili. Bonyeza hapa umsome.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com