Jamaa yangu mmoja ananijia na historia yake ya Afrika aliyosoma toka vitabu vya wazungu. Wakati ananiuliza uliza maswali juu ya watawala wa Afrika akinionyesha kuwa analifahamu bara langu, alitaja vita vya pili ya "dunia."
Nikamuuliza, "Vita gani hiyo umeitaja mbona siijui?" Akatoa macho kwa mshangao, "Yaani hujui vita vya pili vya dunia?"
"Sifahamu." Nikamjibu.
"Ni ajabu sana kama hujasoma habari za vita hivyo shuleni."
"Kama vita hivi viko kwenye vitabu vyenu vya historia ni ajabu sana kuwa sivijui maana historia tunayofundishwa Afrika asilimia kubwa ni historia yenu na kidogo tunachojifunza kuhusu Afrika ni ninyi mmetuandikia." Namwambia.
Baada ya hapo alitumia dakika kadhaa kunieleza juu ya vita hivyo. Alipomaliza nikamuuliza, "kwanini unaita vita vya dunia wakati maelezo yako yanaonyesha kuwa ugomvi ulikuwa ni wenu wazungu Ulaya na Marekani?"
Akashtuka kidogo. Akataka kufungua mdomo akaacha. Sasa anaona historia kwa jicho jingine.
Nikachukua nafasi hiyo kumpasha sawasawa. Kuna wakati unachoka kabisa kufundisha watu kila dakika. Ukikutana na nduguzo toka Afrika unakuta wamekwenda shule ila wamedanganywa toka vidudu hadi chuo kikuu, basi inabidi uanze kuwafundisha taratibu. Ukikutana na hawa jamaa zake Karl Peters nao unakuta wanaogelea kwenye uongo uitwao historia.
Kwanini vita vya kwanza na vya pili vya wazungu vinaitwa vya "dunia"? Hawa mabwana wamechukua historia yao na uzoefu wao kuwa ni historia na uzoefu wa dunia. Vita yao wanafanya ni vita vya dunia nzima. Vita vya kwanza na vya pili vya dunia vilijaa unyama usioelezeka. Sasa wanataka tugawane lawama na hatia ya vita hivyo. Vita vile havikuwa vya dunia. Dunia nzima haikuwa inapigana. Kama ni vya dunia, je Tanzania tulikuwa tumegombana na nani katika vita vya kwanza na vya pili? Je Kambodia ilikuwa ikipambana na nani? Je Brazili, Venezuela, Paraguay, n.k.? Kuna watu katika nchi hizi waliopigana katika vita hivyo ila hawakuwa wanatetea maslahi yao, walikuwa wakitetea maslahi ya wazungu, maslahi ya wakoloni. Walikuwa wakipigana kwenye ugomvi wa wazungu. Havikuwa vita vyetu vile, havikuwa vita vya dunia.
Kwahiyo ninakushauri kama nilivyomwambia huyu bwana, usije hata siku moja ukasema vita vya kwanza au vya pili vya "dunia." Kama ni mwanafunzi, usikubali hata kidogo mwalimu akudanganye kwa kukwambia kuwa kuna vita vinaitwa vya dunia. Dunia haijawahi kupigana. Jiulize nini kilikuwa kinagombaniwa, maslahi yalikuwa ya nani, n.k. Jiulize sikukuu za kukukmbuka ushindi wa vita hivi zinafanywa wapi?
Nchi za Ulaya zilikuwa na magomvi yao, sasa wanatumia uongo uitwao historia kufanya kuwa vita vile ni vya dunia nzima...usikubali. Sema vita vya kwanza vya wazungu (au Ulaya) au vita vya pili vya Ulaya na Marekani.
Ndivyo nilivyomwambia jamaa yangu. Nikamuonya.
Wakati tunaagana aliniacha akitikisa kichwa. Aliniuliza, "Hivi nchi yenu ilipata uhuru lini tena?"
Nikamjibu, "Bado tunatafuta uhuru!" Kuna watu wanaamini kabisa, na siwalaumu, kuwa nchi za Afrika ziko huru. Kama unadhani uko huru, utaona vipi minyororo?