Ninapitia vitabu vyangu vya kumbukumbu nilizoandika nikiwa Tanzania. Hii ni sehemu ndogo ya mambo niliyoandika katika pilikapilika za kwenye daladala katika jiji la Dar Es Salaam. Ni kati ya mwaka 1999-2001.
Oya, Shika Mchuma!
Kondakta: Kaa mkao wa pesa.
Abiria: Si tumetosha? Twende basi!
Kondakta: Tunafanya kazi kwa hesabu mama mdogo.
Abiria: Hebu twendeni. Kuna watu huko mbele.
Kondakta: Kama una haraka ungeenda toka juzi. Tuko kazini hapa.
Mpiga debe: Wenye haraka wanaonyesha. Wenye haraka huchukua teksi.
Abiria: Tukichukua teksi mtakula wapi. Hebu acheni dharau. Twendeni, gari si imejaa?
Mpiga debe: Jamani, mchuma haujai. Inayojaa ni ndoo ya maji. Haya, Kariakoo, Kariakoo... gari nyeupe hii.
XXXXXXXXXXXXXXX****XXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Kondakta: Tiketi mbele kama tai. Tiketi mbele jamani. Tiketi sio mzigo wa bangi...mbele kama tai.
XXXXXXXXXXXXXX***XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Kondakta: Manzese wapo?
Abiria: Tupooooo...
Kondakta (akijifanya kuwa hakusikia): Manzese hakuna sio?
Abiria (kwa hamaki): Shushaaaaa...Tupo!
Kondakta (huku akijizuia kucheka): Babu endesha, Manzese hakuna.
Abiria: He, we konda vipi? Tumesema tupo!
XXXXXXXXXXXXX***XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Ni saa tano usiku. Siku ya jumamosi. Kituo cha mabasi Mwenge. Tunaelekea Mbezi Beach.
Abiria: Dereva twende bwana...saa za majeruhi hizi.
Kondakta: Bado vichwa babu. Gari haiendi mswaki hii hata siku moja.
Abiria (amelewa chakari): Nina haraka ya kufumania. Nimeambiwa saa tano na nusu ndio saa ya kumfumania mbaya wangu.
Mara abiria huyu aliyelewa anaanza kutapika.
Abiria 1: Jamani watu wameanza kutapika humu ndani.
Abiria 2: Nipisheni nitoke miye...
Abiria 3: Afadhali niende kwa miguu.
Kondakta: Kuna wagonjwa huku?
Abiria 4: Twendeni. Hamjui ni mambo ya wikiendi haya?
Abiria 5: Pombe za bure hizo.
Kondakta: Kama sio pombe za bure basi ni za mkopo. Shuka bwana mzee. Walevi hawa kwanza huwa hawataki kulipa.
XXXXXXXXXXXXXXXX***XXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Abiria: Kuna nafasi?
Kondakta: Nafasi kwani gesti hapa? Kama unakwenda, twende.
XXXXXXXXXXXXXXX***XXXXXXXXXXXXXXXXXXXX