7/07/2004

Ukimwi na laana toka kwa mungu

Kama ukimwi ni adhabu toka kwa mungu, na malaria nayo ni adhabu? Malaria inaua watu wengi kuliko ukimwi hivi sasa duniani. Ukimwi sio ugonjwa pekee ambao mtu akiupata lazima afariki. Nchi kama Tanzania ina magonjwa mengi sana kama kansa ambayo mtu akipata ni kama ukimwi. Swali ninalotaka kukuuliza ni hili: ni kitu gani kinfanya ukimwi uwe ni adhabu ila sio magonjwa mengine? Na kama ukimwi ni adhabu kutokana na binadamu kuwa na tabia kama za walioishi Sodoma na Gomora, mbona nchi ambazo ukimwi sio tatizo kubwa sana ni zile ambazo hata kwenda kanisani, hekaluni, au msikitini kwa unafiki hawakwendi. Mungu hawamjui hata kidogo. Nchi kama Uholanzi ambako uchangudoa na mapenzi kwa watu wa jinsia moja vimeruhusiwa, idadi ya wenye ukimwi ni ndogo sana.

Kama ukimwi ni adhabu kutokana na uzinzi na uasherati, mbona kuna watu wanaopata ugonjwa huu kutokana na kupewa damu yenye vidudu na sio uzinzi? Na je watoto wanaoambukizwa kutokana na kubakwa? Nchi kama Afrika Kusini kuna imani kuwa mtu mwenye ukimwi akishiriki "tendo la ndoa" na bikira atapona. Hawa watoto wadogo wasio na hatia wanapopata ukimwi wanakuwa wanaadhibiwa kwasababu gani? Kwa makosa ya mababu zao? Inawezekana maana ndivyo Nuhu, ambaye anaheshimiwa sana kwenye Bibilia, alivyofanya. Alikunywa, akalewa, alipochunguliwa na mwanaye Ham, alitoa laana kwa kizazi cha Ham ambacho kilikuwa hakijazaliwa! Mungu wa ajabu kweli huyu. Anaadhibu wasio na hatia. Mbona hawi mfano mzuri? Halfu mungu huyu huyu anakuja kutuambia kuwa ufalme wa mbinguni ni wa watoto.

Mbu wanaweza kuwa wanasaidiana na shetani nini? Si wanatupa malaria???

1 Maoni Yako:

At 7/11/2004 04:44:00 PM, Anonymous Anonymous said...

ukimwi ni adhabu ya mungu. Wanadamu tumezidi.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com