11/30/2004

ENZI ZA JESHINI

Nimekumbuka jeshini! Da! Historia ile sitakaa nisahau. Nakumbuka siku naondoka na Nickson Malisa kuelekea tusikokujua. Kwanza tulipangwa kwenda kule Mgambo, Tanga. Mwanzoni tulitaka kujipeleka…ile kambi ya Arusha inaitwaje tena? Nimeisahau jina. Hata hivyo tukaamua kuelekea Tanga. Lakini tukiwa ndani ya basi tukaamua kwenda Maramba badala ya Mgambo. Tulisikia habari za kutisha kuhusu Mgambo na habari njema kuhusu Maramba. Basi hao tukamua kuchagua kambi wenyewe. Wakati huo tayari tumeshachelewa kuripoti. Tarehe zilishapita siku nyingi. Tukaingia Maramba jioni jioni hivi na vibegi vyetu na makubazi. Nakumbuka tulikuwa tunapenda sana kuvaa soksi za bluu na yale makubazi. Tulipoingia Maramba tuliamua kuwa hakuna haja ya kuripoti. Kuripoti kosa. Soo. Tulikuwa tunatumia mbinu za juu kabisa za kikachero. Ukifika mahali, kaa chini. Tafuta wajuaji. Ongea nao. Chunguza, “Kilitoka wapi, kikaishia wapi.” Hii ilikuwa ndio mbinu yetu ya kwanza.

Na wajuaji ndio akina nani? Wajuaji si wengine bali ni wale wanaolipia siku. Wale ambao hawajaruhusiwa kwenda nyumbani na wenzao kutokana na makosa kama utoro. Hawa ndio tuliwatafuta giza lilipoingia. Tuliingia bweni hadi bweni tukiwatafuta na kuongea nao. Nakumbuka, kama kumbukumbu hainihadai, kuna bwana mmoja ambaye hivi sasa anaishi Kinondoni. Nadhani ni fundi wa elektroniki. Alisoma Chuo cha Ufundi Mbeya. Basi huyu alikuwa ni mmoja wa jamaa waliotupa “picha” halisi. Jamaa poa sana. Usiku huo baada ya kuongea na watu kadhaa, tukaenda pembeni (mimi na Nickson Malisa) na kuanza kuchambua taarifa tulizokusanya. Kabla jimbi hajawika tulishaamua kuwa Maramba sio kambi yetu. Tutakaa hadi kesho yake usiku, kisha tutatoroka.

Sasa swali likaja, kwakuwa tunatoroka na hatutaki kujiandikisha, tutafanya nini siku nzima ili tusishtukiwe?

Wazo hili sijui nani alikuja nalo kati yangu na Nickson. Kesho yake asubuhi wakati jamaa wengine wanaelekea kwenye “kazi za ujenzi wa taifa” sisi tulielekea nje ya ofisi ya mkuu wa kambi! Tulijua kuwa watu wanaongopa sana eneo lile. Afande yeyote akituona pale hawezi kutubugudhi. Lazima atajua kuwa tumeamriwa kusubiri mtu hapo. Basi tulikaa pale hadi saa ya kula. Tukaenda kula. Wakati tunachukua chakula tukashtukiwa. “Sura ngeni hizi.” Tukajitetea ni wageni na tumetakiwa tuonane na mkuu wa kituo na anavyotuona hivyo tukimaliza chakula tunaenda ofisini kwake. Tukala, kisha hao tukarudi kwenye “ofisi” yetu. Tukasimama nje ya ofisi ya mkuu wa kituo tukipiga gumzo na kubishana. Tulikuwa tunapenda kubishana sana enzi zile. Kubishana na kucheka. Na kuzidi watu akili! Hakuna kitu kilichotufurahisha kama kuzidi watu akili. Hasa watu kama maafande.

ITAENDELEA
***************************************++*****************************************
Nabakisha uhondo kwa ajili ya siku nyingine. Njoo nitaendelea. Nitakupa pia na kisa cha kambi ya Ruvu nilipokutana na bwana Obey Nkya amekusanya watu anahubiri ukombozi…Obey, mpaka leo sikumalizi. Sitakaa nisahau pale Ruvu. Mimi na Nickson tulikutazama kisha tukatazamana na kusema, “Huyu jamaa ni nani? Lazima tujuane naye.”

REHEMA NCHIMBI: BARUA TOKA BONDENI

Kuna nasaha nyingine za Rehema Nchimbi: SHIME TUSHIKAMANE. Kongoli hapa ujisomee.

Pia kuna barua toka Amsterdam ambayo nimeifuta kimakosa. Barua hii ni toka kwa bwana Chumi. Nitamuomba atume tena.

MAKALA MPYA: MAPINDUZI YA UMMA...

Makala niliyoahidi tayari nimeiweka hapa ndani. Nenda pale kwenye kona za makala zangu. Kumbuka ni chini ya picha yangu, upande wa kulia, chini ya maneno haya: KONGOLI USOME MAKALA ZANGU. Makala yenyewe inaitwa: Mapinduzi ya Umma Dhidi ya Dhuluma.

MAPINDUZI YATAKUWA BLOGUNI

Yule mshairi mahiri wa hapa Marekani, Gil Scott-Heron, ana shairi liitwalo The Revolution Will Not Be Televised (kongoli hapa ulisome). Sasa sisi wanablogu tunakuja na yetu. Tunasema kuwa MAPINDUZI YATATOKEA BLOGUNI (The revolution Will be Blogged!). Tazama jamaa wa Kona Yangu anavyochanja mbuga na kutimulia vumbi wabunge, wana si-hasa, na wahariri wenye mikono inayotetemeka. Halafu kuna jirani yetu wa Mawazo na Mawaidha. Anakwenda mwendo wa Kimombasa, ambako meli hupita barabarani na nyumba zina gorofa ndani kwa ndani. Yeye tayari ameshamlima "Baba" Moi. Eti "Baba." Ilibaki kidogo tu wangemwita mungu! Unakumbuka kila taarifa ya habari Kenya ilikuwa lazima ianze na habari za "Baba." Mara kakohoa. Mara kalala mchana. Kila jumapili lazima tuambiwe eti kaenda kanisani. Hivi alikuwa anatumia mdomo huo huo kudanganya wananchi kwa kuombea mola au alikuwa ana mdomo mwingine?
Haya, kuna ndugu yetu Mponji wa Furahia Maisha. Anauliza, "Ulaya kunani?" Kaahidi mambo yako jikoni. Epua upesi!
Kuna yule dada yetu Ory Okolloh wa Kenyan Pundit. Anaambaa kwa blogu ya ung'eng'e toka Harvard. Katundika hadharani furaha yake kwa kuona wanablogu wa Kiswahili wanavamia uwanja. Ndio, tumeingia na baraka za mizimu ya mababu. Jamani, mnakumbuka wimbo wa marehemu Kalikawe wa Mizimu? Katika nyimbo alizoandika ule wimbo. Halafu kuna wanablogu Waafrika wengine kama akina Mshairi, Uaridi, Beginsathome, na kadhalika.

SIKU MPENDA UGOMVI RUMSFIELD...

Siku mpenda ugomvi Rumsfield alipomtembelea Saddam Hussein mjini Baghdad na kushikana mkono wa urafiki. Tazama mikono yenye damu ikisalimiana. Bonyeza hapa.

11/29/2004

UTASHAA!

Nimeng'ang'aniwa. Kono la beberu kooni. Buti lake mgongoni. Nahema kwa masikio! Nikiuliza naambiwa, "Ndio 'American Dream' ati! Ulidhani picha za kwenye gazeti la Ebony ndio maisha halisi ya kiwanja cha Joji Dabliyuu Kichaka? Utashaa..."
Basi wakati napambana na beberu, bwanyeye, mchuna nafsi, ngozi, na utu nakushauri kongoli/bonyeza hapa.

11/28/2004

NCHI YA KIPOLISI

Siku hizi najisikia kama vile naishi nchi ya kipolisi. Licha ya kuwa kuna vimulimuli vya polisi na ving'ora kila mahali, sasa hivi madereva wanabanwa kila kona. Barabarani manjagu wamejaa, halafu kuna kamera zinazochukua picha ukivunja sheria ambapo unatumiwa tiketi nyumbani kwa njia ya posta pamoja na uthibitisho wa picha ya gari lako (namba zake) na saa. Zaidi ya hilo hapa Toledo wameanza kutumia helikopta. Jamani! Ukiendesha unakuwa kama vile kuku aliyemwagiwa maji. Kama utatazama kila upande kutafuta askari ujue una kazi ya kuendesha huku ukitazama angani kutafuta iliko helikopta.

Tuache hilo, wanadai wanaimarisha usalama.

Nimeanza kuandika moja ya mradi mkubwa wa JIKOMBOE. Mradi huu umepewa jina: MWAFRIKA AKUTANA NA... Kwahiyo kutakuwa na sehemu mbalimbali kwa mfano: MWAFRIKA AKUTANA NA MUISLAMU, MWAFRIKA AKUTANA NA MKRISTO, n.k. Unaweza kujiuliza, "Kwani muislamu na mkristo sio Waafrika?" Ukiwa na swali hili, jua kuwa JIKOMBOE iko kwa ajili yako. Unaihitaji. Wakati unasubiri jibu lake, uwe ukisikiliza Wimbo wa Ukombozi (Redemption Song) wa Bobu Malya (ndio, Malya...hujui Bobu alikuwa Mchagga ndio maana Wachagga huwaambii kitu kwenye marege??)

Kuna habari nzuri sana kanitumia Nambiza Joseph Tungaraza (mwenzetu anayeishi Australia) kuhusu madhara ya dawa za kujichubua. Nitaipandisha hapa maana iko kwenye misingi ya ukombozi wa fikra. Kuna tatizo kila nikiiweka, lakini nitapatia ufumbuzi karibuni. Nitasonga kwanza ugali kisha nije kujaribu tena. Kwa taarifa yako leo najikata ugali wa nguvu. Ugali na kabichi na karanga. Habari hii ya kujichubua inaendana na dhana ya bwana mmoja toka NIgeria, Chinweizu, anayoiita Negro negrophibia. Yaani chuki ya watu weusi kwao wenyewe (kujichukia kwa watu weusi). Huyu bwana ana kitabu kizuri sana kwa watu wanaofuatilia masuala ya ukombozi wa fikra na elimu ya historia na utamaduni wa Mwafrika. Kinaitwa: THE WEST AND THE REST OF US. Nadhani kinapatikana pale British Council, Dar Es Salaam. Sina uhakika, ninadhani. Lazima ukisome hiki kabla hujaaga dunia!!!!!!

Usisahau kutazama blogu mpya nilizopandisha ikiwemo ile ya mwenzetu toka Kenya ya Mawazo na Mawaidha. Iko hapa. Zile mbili za Watanzania, Kona Yangu na Furahia Maisha, nazo zina mambo mapya. Ninakumbusha kuwa wale wanaotaka kuwa na vyombo vya habari (kuwa na "shihata" yao) kwa njia ya blogu wasisite kuwasiliana nami kama wana maswali. Na pia nimeweka somo la kwanza hapa kwenye blogu kwa wale ambao wanazo na wale ambao wanatengeneza zao kama bwana Kesi kule Kampala. Kesi karibu sana kwenye ulimwengu wa blogu.

11/27/2004

NYERERE NA KISA CHA SIAFU

Azimio Magehema kaniandikia kisa cha siafu alichokitoa Mwalimu Nyerere. Ujumbe wa kisa hiki unaendana na dhana ya kujikomboa. Ukombozi wa fikra hautokei siku moja. Polepole, tutafika. Nakumbuka maneno ambayo Nambiza Joseph Tungaraza alipenda kuyasema tukiwa pale Ilboru, Arusa (Arusa, ndio, usidhani nimekosea!). Alipenda kusema: Daima Mbele, Nyuma Mwiko.
Haya ujumbe alioniandikia Azimio (jina zuri sana hili) huu hapa:

Namnukuu Mwalimu Nyerere aliposema, "Sungura alimuuliza siafu unakwenda wapi, Siafu akajibu KUMUUA TEMBO!!! Sungura kwa mshangao akasema lakini Tembo mkubwa sana mtamuweza?? Siafu akajibu TUTAJARIBU TENA TENA TENA NA TENA..."

MAKALA MPYA: MAMBO YAMEPARAGANYIKA

Nilikuwa natafuta sehemu ya pili ya makala ya Urasta baada ya Azimio Magehema kunikumbusha. Katika tafutatafuta nikakutana na makala ambayo niliiandika miaka mitatu hivi iliyopita. Makala hii itafaa sana kusomwa na Mtanzania aliyeondoka nchini muda mrefu. Hata walioko Tanzania nao itawafaa. Nimeipandisha bila kuipitia kutazama kama kuna mambo yamepitwa na wakati. Wakati huo huo ninaendelea kutafuta sehemu ya pili ya ile ya Urasta. Nenda kwenye kona ya makala zangu kisha bonyeza kwenye makala hii mpya iitwayo: MAMBO YAMEPARAGANYIKA.

11/26/2004

BLOGU NYINGINE YA KISWAHILI HIYOOOOO...

Napenda kutangaza kuwa ulimwengu wa blogu una rafiki mwingine toka Kenya. Naye kama ilivyo JIKOMBOE anasema titi la mama litamu. Anaandika kwa Kiswahili. Anasema kuwa alipata mshawasha wa kuwa na blogu baada ya kutembelea JIKOMBOE. Haya ni maneno toka katika blogu yake:
"Juzi katika pilka pilka zangu za kuchakura mtandao nilikutana na " blogu " moja ya kaka kutoka tanzania , amabayo kwa kifupi ilinifurahisha sana kiasi cha kwamba nikaamua kuanzisha yangu piaSasa najua wapiga domo watasema kuwa nimeaanza kuiiga lakini kwa sasa nitawaacha waseme kwani wanamuziki wengi tayari washatuambia kuhusu wenzetu ambao huongea sana jioni tu - watalala ."
Blogu yake inaitwa : MAWAZO NA MAWAIDHA. Mtembelee hapa.


KAMUSI YA KISWAHILI

Ukitaka unaweza kushiriki katika mradi wa chuo kikuu cha Yale wa kuandika kamusi ya Kiswahili. Mradi huu unahusisha watu toka pande nne za dunia (dunia ni kweli ina pande nne??). Mtu yeyote anaweza kuweka neno, kuhariri, kusahihisha, n,k. Ni kamusi ambayo inaandikwa na kila mtu. Kamusi yenyewe iko hapa.

BABA MOI, BABA MOI, BABA MOI!!!

Mahakama Kuu nchini Kenya imeamua kuwa "Baba" Moi na wenzie (akiwemo mwanaye Philip) lazima watoe ushahidi katika uchunguzi wa kashfa ya Goldenberg. Hukumu hii inafuatia kesi iliyofunguliwa na wanaharakati waliodai kuwa uchunguzi huo lazima usikilize ushahidi toka kwa watu hawa. Mambo kama haya yanapotokea Afrika yananifanya niwe na furaha mwezi mzima. Hii tabia ya kuona kuwa mtu akiwa ameshika cheo cha juu serikalini hatakiwi kuhojiwa, kufikishwa mahakamani au mbele ya tume za uchunguzi inachochea rushwa, wizi, uzembe, na ulaghai. Ni tabia mbovu kabisa isiyohitajika barani kwetu. Tanzania nako lazima tubadili sheria inayozuia, kwa mfano, Rais kufikishwa mahakamani. Ukimpeleka Rais mahakamani unaambiwa, "Huwezi kumshtaki Rais wakati akiwa madarakani." Ukisubiri hadi atoke madarakani kisha ukampeleka mahakamani utaambia, "Sheria inasema kuwa huwezi kumshtaki Rais kwa makosa aliyofanya wakati akiwa madarakani." Jamani!
Mtu mwenye wadhifa kama Rais akiwa haogopi nguvu ya sheria (na jela), ni vipi tutanajenga uaminifu na uwajibikaji? Hakuna haki ya raia yeyote Afrika anayepaswa kuwa juu ya sheria (sio Rais wala Rais mstaafu).
Soma habari hiyo hapa.

KONA YA WANABLOGU WAPYA

Nimeweka ukurasa wa wanablogu wapya. Nimeanza na somo la kwanza. Baadhi ya wanablogu na wale wanaotaka kuanza wamekuwa wakiniuliza maswali mbalimbali. Ukurasa wenyewe uko chini ya makala na hadithi za Freddy Macha. Bonyeza palipoandikwa: Somo La Kwanza. Wenye maswali zaidi wanaweza kuniandikia. Naweza nisijibu haraka. Usiwe na wasiwasi, nitakujibu.
Kuna habari njema za wanablogu wa kiswahili wa Tanzania. Yule mwanadada wa Kenya, Ory Okolloh, anayesoma sheria katika chuo kikuu cha Harvard ameziweka blogu mbili mpya za Watanzania, Kona yangu na Furahia Maisha, ndani ya blogu yake ambaye inapendwa na kusomwa na watu wengi.
Mimi nami nimeongeza blogu nilizokuwa nimeweka hapa. Kona niliyoiita: Blogu za Wana Afrika Mashariki nimeibadili na kuiita Blogu za Waafrika. Nimeongeza blogu kadhaa na nitaendelea kuweka nyingine.

11/25/2004

MWAMKO WA UMMA

Kabla sijaelekea kwenye mazishi ya bata, napenda kuwauliza kama mnafuatilia mwamko wa umma huko Ukraine. Saa moja na dakika nane zilizopita, Mahakama Kuu nchini humo imemzuia anayedaiwa kuiba kura (kama wanavyofanya watawala wa Tanzania) kuchukua madaraka. Soma habari hiyo hapa. Halafu, makala yangu ya wiki hii katika safu la Gumzo ya Wiki, nchini Tanzania inazungumzia juu ya haki na uwezo wa wananchi kuleta mapinduzi. Nitaiweka makala hiyo iitwayo: MIMI NA WEWE TUNA NGUVU KUSHINDA DOLA mara baada ya kutolewa nchini Tanzania. Yanayotokea huko Ukraine ( na yaliyowahi kutokea Jojia, Ufilipino, Indonesia, n.k. ni moja ya vielelezo vya nguvu walizonazo walalanjaa). Ngoja nielekee kwenye bata maana tumbo limeanza kunguruma kwa ubao.

LEO NI KULA BATA HADI WATUTAMBUE!

Leo Marekani nzima ni siku ya kula bata! Ni sikukuu ya thanksgiving hapa Marekani. Maduka kwa siku kadhaa zilizopita yalikuwa yakiuza bata kwa wingi kwa ajili ya siku ya leo. Sikukuu hii ya kula bata, mahindi, na keki ya maboga iitwayo thanksgiving ilianza kusherehekewa rasmi mwaka 1789. Lakini inaaminika kuwa thanksgiving ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1621. Sikukuu hii kama zilivyo sikukuu nyingine kama krisimasi na pasaka, imejengwa juu ya historia ya uongo. Inadaiwa kuwa siku hii ni siku ambayo wavamizi wa nchi hii ya Marekani (kumbuka hii nchi ni ya "Watu wa Kwanza" kama makabila ya wahindi wa asili wanavyopenda kujiita) walikaa kwa upendo na amani wakala chakula na watu wa asili wa nchi hii. Watu wengi wameanza kufundisha watoto wao ukweli wa sikukuu hii na ukweli wa historia ya mauaji ya halaiki, mikataba ya ulaghai, na wizi uliofanywa na wahamiaji waliokuja toka Uingereza. Rafiki yangu, Malaika, ambaye amenipigia simu dakika chache zilizopita kunikaribisha nikale bata anasema kuwa leo asubuhi alikuwa akimfundisha mwanaye juu ya ukweli wa sikukuu hii.

Kwahiyo kama kuna kiyama ya bata basi ni Novemba 25. Malaika anasema alianza kupika toka jana. Siku hii watu hula siku nzima huku wakitembeleana, kujumuika kifamilia, na wengine (hasa wanaume) kutazama mpira wa "miguu" wa Marekani. Huu mchezo wanauita mpira wa miguu (american football) wakati ambapo asilimia 99.99 ya mchezo huu wanatumia mikono! Nashindwa kuwaelewa. Basi Malaika anasema jikoni kwake kumeshehena chakula: bata, viazi vitamu, keki, mboga za majani, soseji, n.k. Anasema kuwa hofu yake ni kuwa mimi sili nyama na eti nisipokula bata leo sijasherehekea thanksgiving. Jamani, nile bata nisile?


Nimemtaja rafiki yangu Mailaika nikakumbuka makala niliyowahi kuandika juu yake iliyokuwa inauliza kama WamarekaniWeusi ni Waafrika. Nitaitafuta na kuipandisha ndani ya blogu. Haya ngoja nielelekee kwa Malaika ingawa sijaamua kama nitashiriki katika ulaji wa bata wa kitaifa au la.

11/24/2004

MNAONIANDIKIA NA MENGINE...

Nawashukuru sana wote wanaoniandikia. Ingawa nina muda kidogo, ninajaribu kuwajibu wote mimi mwenyewe. Situmii mashine kama wengine wanavyodhani. Pamoja na shukrani zangu, nina ombi moja. Sipendi kabisa...narudia, SIPENDI KABISA Watanzania wenzangu wanaponiandikia barua pepe kwa kutumia lugha za watu wengine/wakoloni. Hivi mbona wao hawatumii zetu wanapowasiliana wao kwa wao? Ninaposema "wao" mnajua ninawazungumzia akina nani. Kwa ufupi, mimi lugha ninayoifahamu kwa ufasaha zaidi na kuipenda ni Kiswahili na Kichagga. Hata ndoto huwa napata kwa lugha hizi. Blogu hii iko kwa ajili ya kuendeleza titi la mama yetu: Kiswahili. Iwapo Kiswahili chako ni cha kubabaisha kidogo (kama rafiki zangu wa nchi za jirani ambao huniandikia kwa kiswahili cha hapa na pale na kiingereza...wao nitawasamehe kwa sasa) unaweza kuniandikia kwa hicho kiingereza au lugha yoyote ya kuazima kwa mabeberu ila tafadhali fanya hima, jifunze Kiswahili ili siku za usoni tuwasiliane kwa Kiswahili. Hii ni blogu ya Kiswahili. Mimi nazungumza Kiswahili. Kiingereza nakifahamu kiasi ila sihitaji kukitumia kuwasiliana na watu wangu. Sidhani kuwa kuna ubaya kuzungumza kiingereza. Kwa mfano, ninatumia lugha hii katika shughuli zangu nyingine za kitaaluma. Ninahariri jarida la kiingereza liitwalo Perpectives on Global Development and Technology. Nina blogu ya kiingereza ya masuala ya teknolojia. Sina ugomvi na kiingereza au kifaransa. Mimi mwenyewe ninajilaumu kwanini nilipokuwa shuleni sikusoma kifaransa kwa makini. Pia nina mpango wa kujifunza kiarabu hivi karibuni. Kwahiyo isionekane kuwa mimi ni mtamaduni mwenye siasa kali. Najua tunaishi kwenye dunia ya maingiliano. Watanzania hatutaki kuwa kisiwa. Ila inapokuja katika mawasiliano kati yangu na wewe Mtanzania mwenzangu, hatuhitaji lugha ya kigeni. Nasema haya kwa nia njema ya kujenga na kutunza utu wetu.

Jambo jingine ni kuhusu blogu nyingine mbili za Kiswahili. Ile blogu ya Kona Yangu imeiva kwa habari kuhusu "wawakilishi" wetu (wabunge). Tafadhali ipitie upate undani wa hawa mabwana tunaowapa kura zetu nao wanazifanya kuwa "kula." Mwandishi wa Kona Yangu, Simon Mkina, alikuwa Dodoma wakati wa kikao cha bunge. Bonyeza hapa kwenda Kona Yangu. Mwandishi wa blogu ya pili, Furahia Maisha Yako, Dennis Mponji, kaniambia kuwa alikuwa na mihangaiko ndio maana amekuwa kimya ila hivi sasa yuko mbioni kuweka mambo mapya. Blogu yake iko hapa.

NASAHA ZA REHEMA NCHIMBI: NANI MWIZI NA MPORAJI WETU???

Mwanahistoria, mwalimu wa chuo kikuu cha Dar Es Salaama, mzawa mwenzetu, anayesoma pale kwa Kaburu matata iya, Afrika Kusini, Rehema Nchimbi, kaniandika maneno haya ya kutufikirisha. Hivi ndivyo safari ya kujikomboa inavyoanza. Inaanza kwa kubonyeza hapa.

11/22/2004

MAKALA KUHUSU JOJI DABLIYUU KICHAKA

Makala mpya niliyoahidi kuhusu Joji Dabliyuu Kichaka tayari nimeipandisha bloguni. Nenda kwenye kona ya makala zangu. Inaitwa JOJI KICHAKA NA YESU MNAZARETI. Hii makala iliandikwa kwa ajili ya safu yangu katika gazeti la Mwannanchi, nchini Tanzania.

11/21/2004

FIDELIS TUNGARAZA AHOJI

Watanzania tutajiheshimu lini?
Ufuatao ni waraka wa Mtanzania anayeishi Helsink, Ufini, Fidelis Tungaraza, kufuatia habari za kuuawa kwa Mtanzania mwenzetu, dada yetu, mwanetu, jirani yetu, binadamu mwenzetu, mlalanjaa mwenzetu, shangazi yetu, binamu yetu....
Mtanzania huyu aliuawa kinyama na askari wawili wenye ngozi isiyo na kemikali muhimu sana ya Melanin. Nawaambia askari hawa, "Mbwa mwizi wa machinjioni!" Soma kwa makini utaelewa kwanini blogu hii nimeiita: Jikomboe. Safari yetu ya kujijua na kuthamini utu wetu ni ndefu ila najua kwa nia moja tutafika. Waraka wenyewe huu hapa chini:

Ndugu mhariri wa gazeti, ndugu viongozi wa serikali, na Watanzania wenzangu wengine, Ninatuma ujumbe huu kwa kustushwa, kusikitishwa, na kukasirishwa kutokana habari ya kuuawa kwa mwanamama wa Kitanzania na askari wahuni wa Kiingereza. Nimestushwa, kusikitishwa, na kukasirishwa kwa unyama na mauaji ya Mtanzania mwenzetu. Pia nimestushwa, kusikitishwa, na kukasirishwa na jinsi gazeti hili ambalo linasomwa na wasomaji wa Kiswahili ulimwenguni kote kupitia kwenye tovuti yao kwa jinsi lilivyoandika juu ya mauaji haya ya kinyama ya Mtanzania mwenzetu, hususani kichwa cha habari cha mauaji haya ya kinyama kama kilivyo hapo chini:

Askari Waingereza wadaiwa kuua changudoa D'Salaam


Ndugu Mhariri wa gazeti na viongozi wa serikali niawaombeni mlichukulie suala hili kwa uzito wa kina kwa upande wa kesi ya mauaji, na pia kwa jinsi gazeti hili lilivyochapisha habari hizi kwa kumuita 'changudoa' Mtanzania mwenzetu aliyetendewa ufuska na kuuawa kinyama. Kwa wale wote ambao wamewahi au bado wanaishi nchi za watu weupe tunajua jinsi suala kama hili ambavyo lingekuwa limewekwa katika vyombo vyao vya habari kama ingelikuwa wao ndiyo wametendewa kitendo kama hicho. Suala hili lingelitokea Ulaya, Amerika, Asia, au Uarabuni pengine lingeandikwa 'Askari wanaharamu, wahuni wa Kiingereza wasemekana kuua raia wetu mwanadada mwananchi maskini mnyonge mpole' Kuonyesha tu jinsi wanavyojithamini na kuthaminiana. Ndugu zangu wote tunaohusika na suala hili kwa njia moja au nyingine nawaombeni tulifuatilie suala hili.
Tanzania Nakupenda kwa Wote,
Fidelis Tungaraza, Helsinki, Finland.


Kisa chenyewe hiki hapa toka gazeti la Majira:

Askari Waingereza wadaiwakuua changudoa D'Salaam
*Walitoka Iraki vitani kuja kupumzika
*Yadaiwa walifanya mapenzi ufukweni
Na Kulwa Mzee

WANAJESHI wawili wa Uingereza wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya mauaji. Wanajeshi hao, Nigel David (23) na Brett Richard (20), walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Bi. Pellagia Khaday. Akisoma mashitaka hayo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Patrick Byatao, alidai kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 10 mwaka huu katika ufukwe wa hoteli ya Silver Sands. Inadaiwa Waingereza hao walimuua Bi. Conjesta Ulikaye. Hata hivyo hawakutakiwa kujibu mashitaka hayo kwa sababu Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya mauaji. Habari zilizopatikana mahakamani hapo zinadai kuwa wanajeshi hao walitoka vitani Iraki na walifika nchini kwa ajili ya mapumziko. Inadaiwa wakiwa kwenye ufukwe huo, mmoja wa washitakiwa alifanya mapenzi na changudoa huyo na kumlipa dola 70 (70,000/-) na kumshawishi ili afanye mapenzi pia na mwenzake kwa ahadi ya kumwongezea kitita. Alikubali, lakini haikufahamika walielewana kitu gani na baadaye walionekana washitakiwa wote wawili wanashirikiana kimapenzi na mwanamke huyo. Inadaiwa marehemu alifika katika eneo la tukio kwa ajili ya biashara ya kujiuza akiongozana na mwenzake ambaye alipata Mzungu mwingine. Washitakiwa walirudishwa rumande, upelelezi haujakamilika na kesi itatajwa Novemba 29 mwaka huu.

11/20/2004

Blogu ya Kona Yangu Yarudi na Vipande vya Wabunge

Jana niliizungumzia blogu ya Kona yangu kuwa ilikuwa ni ya kwanza kutupa vipande toka Bungeni Dodoma. Ila nikasema jamaa (Simon Mkina) kawa kimya. Sasa amerudi. Bonyeza hapa usome.

BILL GATES ANAPATA BARUA PEPE NGAPI KWA SIKU?

Unaweza usiamini Bill Gates, bepari anayemiliki Microsoft, anapata barua pepe ngapi kwa siku. Kongoli hapa utajua. Barua pepe anazopata zinaweza kusomwa na raia wote wa nchi za Namibia na Botswana na nyingine kubakia!

11/19/2004

BLOGU TOKA BUNGENI

Mtanzania, Simon Mkina, amekuwa ni mwanablogu wa Bongo wa kwanza kublogu toka bungeni. Blogu yake hii hapa. Amepeleka teknolojia hii kuliko waliko "waheshimiwa." Ila alituacha njiani baada ya kutuma taarifa mara mbili. Sijui nini kimempata. Labda kuna mvua, maana mvua ikinyesha nyumbani kule umeme unakatika, umeme ukikatika hakuna uwezo wa kutumia mtandao wa tarakilishi! Bogu ni nyenzo nzuri sana kwa mtu kama Mkina ambaye anafanya kwenye nyanja ya habari. Tunajua kuwa waandishi wengi wanaandika habari zao kisha zinapitiwa na watu wengine ambao katika kuhariri wanaweza kubadili habari nzima. Na wakati mwingine kuna habari ambazo hazichapwi kabisa hasa zikiwa zimechora makampuni yanayotoa matangazo kwenye gazeti lenyewe au kampuni ambazo wenye gazeti wana hisa au urafiki na wenye kampuni. Au wakati mwingine mhariri anaweza kuona habari ni moto akapata woga kuitoa. Nadhani kwa waliofanya kwenye vyombo vya habari wanaelewa tatizo la habari "kuhaririwa." Sasa kwa teknolojia rahisi na nyepesi ya blogu, watu wa kawaida, sio waandishi tu, tunaweza kuitumia kupashana habari, kuwasiliana, kuelimishana, kukosoa, kuhoji, kupinga, n.k. bila hofu ya kukosa fedha za wenye matangazo, kufukuzwa kazi na mwenye gazeti, kuhaririwa na mhariri mwoga au asiyekupenda, n.k. Blogu inafanya kila mtu kuwa mwanahabari! Unaona, kwa mfano, kwenye blogu hii naweza kusema kuwa VIONGOZI WOTE WA TANZANIA NI WEZI NA WALAGHAI! Wakiniletea za kuleta zaweza kuwaambia, "Ishilieni mbali! Kitoe!" Jambo ambalo siwezi kusema kwa urahisi gazetini! Je wanaweza kuifungia hii blogu????? Waambie wajaribu!

Kwa ujumla teknolojia hii ya mtandao wa tarakilishi inaleta mapinduzi makubwa. Tunakumbuka jinsi Mkapa alivyofungia kile kitabu cha Mwembechai Killings
(bonyeza hapa ukione) lakini muda sio mrefu kikazuka mtandaoni ambapo tunaweza kukisoma na serikali na maguvu yake yote ya dola haiwezi kufanya lolote. Tukio hili, kwa wale tuonaofuatilia mabadiliko makubwa ya kijamii, kisiasa, kitamaduni, na kifikra yanayoletwa na teknolojia hii, liliashiria jambo fulani kubwa sana mbele yetu. Kuna shairi maarufu sana hapa Marekani liitwalo: The Revolution Will Not Be Televised (Mapinduzi Hayataonyeshwa Kwenye Luninga.) Sasa watu wamebadili utabiri huu, wanasema: The Revolution Will be Digitized! Wanasema hivi wakiashiria mapinduzi makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Najaribu kutafsiri hii kwa Kiswahili. Anayeweza anisaidie! Digital kwa Kiswahili sijui ni nini. Nikikosa tafsiri yake nitaitunga. Ndio lugha inavyojengwa na kukua. Lugha haitoki mawinguni. Hatuhitaji kusubiri watu wajenge mnara wa Babeli ili lugha ikue au izaliwe. Lugha hujengwa na sisi wenyewe. Nisaidieni maana yake, kama hakuna tutaanzisha wenyewe.

Sikumbuki nilikuwa nataka kusema nini nilipoanza kuandika hiki kipande. Mkono ulikuwa unaniwasha. Ngoja nirudi kwenye shughuli nyingine niliyokuwa naifanya. Baadaye.


MAKALA IKO NJIANI

Nimeandika makala ya safu yangu ya wiki hii katika gazeti la Mwananchi iitwayo: JOJI KICHAKA NA YESU MNAZARETI. Ninajaribu kutazama madai kuwa Joji Kichaka ni mlokole na kuwa ni mwakilishi wa Yesu hapa Marekani. Madai haya hutolewa na Wakristo wakihafidhina ambao walimpigia kura kwa wingi kwakuwa eti analinda maadili ya Kikristo. Makala hii itakapotoka tu kule Tanzania, nitaiweka hapa. Kwa sasa siwezi kuiweka maana bado haijachapwa. Kumbuka subira yavuta heri. Subiri.

KENYA: URAIA UWILI UKO NJIANI

Naona Wakenya huenda wakaruhusiwa kuwa na uraia uwili. Nimepata habari hii toka kwenye blogu nzuri sana ya Ory Okolloh iitwayo Kenyan Pundit. Nadhani suala la uraia uwili kwa Tanzania ni muhimu sana. Watawala wetu wanapenda sana kutuambia kuwa dunia inakuwa kijiji (dunia-kijiji) na kuwa hizi ni zama za utandawazi. Dhana hizi mbili, utandawazi na dunia-kijiji, zinatulazimisha kukubali kuwa uraia uwili ni jambo ambalo halihitaji mabishano marefu. Kinachohitajika ni mjadala wa kisera na kujifunza toka kwa nchi zenye sheria za uhamiaji zinazoruhusu uraia uwili. Watanzania tunaweza vipi kuishi katika dunia-kijiji kama sheria za nchi yetu zinatubana kuweza kufaidi uraia wa dunia? Bonyeza hapa usome habari hiyo kuhusu Kenya.

11/17/2004

TAZAMA TOVUTI YA KONGOI

Kuna tovuti yenye habari kemkem inayoendeshwa na Mtanzania aliyeko Oslo, Norway, Nasibu Mwanukuzi ambayo inaitwa Kongoi. Itembelea kwa kubonyeza hapa.

Joji Kichaka

Jana usiku nilipata wazo. Wazo lenyewe ni kuwa Rais Joji Kichaka ni madungayembe!
Kama haupo Bongo na ulitoka siku nyingi neno hili litakuacha njia panda. Na haliko kwenye kamusi. Kazi kwako.

Halafu kuna watu wameniuliza eti kwanini napenda kumwita huyu Rais mwizi wa kura Joji Kichaka badala ya jina lake hasa. Napenda kumwita hivyo ili hawa jamaa zake wanaofanya kazi katika yale mashirika ya kijasusi yenye majina yanayoanza na "C" na "F" na kuishia na "I" wasinishtukie! Wakinishtukia nitabadili. Naweza kuanza kumwita Madungayembe.

Na yule gaidi namba moja huwa namwita: Jamaa mwenye madevu anayeishi mapangoni akila tende na halua! Ukitajataja jina lake basi jamaa wa hayo mashirika wanaanza kufuatilia barua pepe zako na kila kitu.

KISWAHILI KWENYE SINEMA YA HOLLYWOOD

Sinema ya PhoneBooth ina sehemu moja ndogo ambayo kuna jamaa anaongea kwa Kiswahili. Nilipoitazama nilibaki kucheka. Maneno yenyewe yanatamkwa na "machinga" wa New York. Anasema, "We niaje unataka kuniharibia biashara?"

11/16/2004

MAJANGILI YA HISTORIA NA URITHI WA WAAFRIKA

Kwa wale wanaofuatilia historia ya wizi wa urithi na mali za Waafrika uliofanywa na majangili, masinzia, na vibaka wa kimataifa wakati wa ukoloni Barani Afrika, kuna habari ya kusisimua. Italia imeamua kurejesha mnara waliouiba zaidi ya miaka 70 iliyopita huko Abisinia/Ethiopia. Bonyeza hapa kwa habari kamili.
Majangili haya yaliyokuwa yamebeba Biblia mkono mmoja huku mkono mwingine ukidokoa na kukandamiza yamekuwa kwa miaka mingi yakikataa kurudisha mali za wizi zilizoibwa wakati "wakitufundisha ustaarabu"!! Washenzi kweli, yaani wanatufundisha ustaarabu kwa huku wakituibia? Nchi ya Ethiopia/Abisinia ambayo ina historia ndefu ya kale na nzito duniani imekuwa ikipiga kampeni kubwa kwa duniani ili urithi wao urejeshwe. Chama kiitwacho The Association for the Return of the Magdala Ethiopian Treasures (AFROMET)kimekuwa mstari wa mbele katika kampeni hii. Kongoli hapa uende kwenye tovuti yao.
Kwa habari zaidi juu ya wizi wa urithi wetu uliofanywa na mabeberu wa Kibabiloni kongoli hapa na hapa na hapa na hapa na hapa na hapa na hapa . Hivi Tanzania Mijerumani na Miingereza ilituibia nini? Lini tutaanza kudai? Wana historia, akina Rehema Nchimbi, tupeni ukweli juu ya hili. Nasikia hata kichwa cha Mkwawa walichorudisha sicho. Kweli??

HATIMAYE...MAKALA YA URASTA!

Hamadi! Nimeipata ile disketa iliyokuwa imehifadhi makala juu ya Urastafari iliyokuwa imeuliziwa na wengi. Makala hii ambayo ilitoka kwenye safu yangu ya gazeti la Mwananchi, nchini Tanzania, iko katika sehemu tatu. Hii ni sehemu ya Kwanza. Basi nenda kwenye kona ya makala zangu, upande wa kuume, chini ya picha yangu, bonyeza juu ya kichwa cha habari cha makala yenyewe. Inaitwa: RASTAFARI: JIWE WALILOLIKATAA WAASHI...

11/15/2004

MAKALA MPYA: JOJI KICHAKA ALIPIGIWA KURA NA MIZIMU YA WATU WA KALE?

Nimepandisha makala mpya niliyoahidi kuitoa inayohusu uchaguzi wa Urais wa Marekani. Nenda kwenye kona ya makala zangu. Inaitwa JOJI KICHAKA ALICHAGULIWA NA MIZIMU?

11/13/2004

DAUDI NA GOLIATHI

Tatizo kubwa la Marekani katika ubeberu wake wa kivita huko Iraki ni kuwa, jeshi la Marekani linajua vita vya jeshi kwa jeshi. Mbinu wanazotumia, silaha walizonazo, mafunzo yao na saikolojia yao kwa ujumla ni kwa ajili ya vita ambavyo adui ni jeshi jingine ambalo wanajua liko wapi, lina silaha gani , n.k. Vita vya mtaani vinavyoendeshwa na watetezi wa Iraki ni tofauti kabisa na vita wanayoweza Wamarekani. Kutokana na sababu hii ndio maana unaona kuwa hakuna siku eti Marekani itaweza kutamka, "Tumeshinda vita." Sasa juzi wamevamia Fallujah kwa mara ya pili. Wanadai eti wameteka mji. Kumbe wakati wakiingia Fallujah, wenzao hao wakatokomea. Sasa wameingia Mosul ambako polisi wamekimbia na kuacha vituo vya polisi. Mkuu wa polisi kafukuzwa kazi baada ya vijana wake kukimbia! Wameongeza pia mashambulizi Baghdad ambapo Wizara ya Elimu imeshambuliwa. Kawaida vita vya namna hii vinakwenda kama Paka na Panya. Wamarekani wakitokea jamaa wanaingia mitini, kisha wanajitokeza baadaye. Hawa jamaa wanajua kuwa sio rahisi kupambana na Marekani ana kwa ana. Kwahiyo wanachofanya ni kuyeyuka na kuibuka. Kuyeyuka na kuibuka. Sasa baadhi ya vikosi vya Marekani vinakwenda Mosul. Wakifika huko jamaa wanayeyuka, wanakwenda pengine. Wanawakimbiza Wamarekani huko na kule. Bonyeza hapa usome habari hiyo. Kwa ufupi tunayoona Iraki ni kama hadithi ya Daudi na Goliathi. Kwa kombeo Marekani atakumbuka yaliyomkuta Vietnam na Somalia.


KWA WAKUBWA TU...

Kisa hiki kiko kwenye mkusanyiko uitwao MAMBO YA NYAKATI ambao unaweza kuupata kwa kubonyeza hapa. Soma kisa hiki kama una umri zaidi ya miaka 18!!!!!!!


MSWAHILI APATA WAZUNGU

Wa kwanza alikutana naye kilabu cha usiku. Akamuuliza, “Umewahi kujaribu mtu mweusi?” Akasema hajawahi. Wakajaribu. Akapenda. Wakajaribu tena na tena na tena hadi alipohamia Columbus akamwacha New York.

Wa pili walikuwa naye darasa moja. Akamuuliza kama amewahi kujaribu watu weusi. Akasema amewahi. Akamuuliza, “Umewahi weusi wa hapa Marekani au weusi toka Afrika ?” Akasema amejaribu weusi wa Marekani. “Basi hujajaribu weusi mpaka ujaribu Mwafrika.”

Huyu naye Wakajaribu. Hadi leo wanaendelea mara moja moja.

Wa tatu walikuwa wanafanya ofisi moja. Walipenda sana kutaniana. Siku moja binti huyo akaja na kipande cha gazeti chenye habari isemayo kuwa weusi wa Afrika wana nanihii kubwa kupita watu wengine duniani. Wazungu ndio wa mwisho. Yao kiduchu kama kidole cha mtoto mchanga. “Ni kweli?” Binti akamuuliza.
“Sijui. Jaribu utajua.”
“Jumatano tusije kazini. Tafuta sababu.” Binti akamwambia.
Wakakubaliana. Ilikuwa ni jumatatu.

Alhamisi alipoamka asubuhi alijua kengele ya mlango ikilia lazima atakuwa mwenye nyumba akilalamika juu ya kelele za mwanamke usiku mzima. Laiti Kibo angejua. Kumbe usiku mzima mwenye nyumba aliweka sikio ukutani akisikiliza kwa furaha isiyo na kifani.

Wa tano alimfanya aamini kuwa weupe zimewaruka. Kabla hajahamia hapa alikuwa anakaa mtaa wa pili, gorofani. Siku moja wakati anashuka chini kuchukua nguo toka chumba cha kusafishia nguo akakutana naye katikati ya ngazi. Akawa anampita, lakini binti akasimama. “Nakuona kila siku unakaa namba ngapi?”
“Niko namba 8.”
“Unaishi mwenyewe?”
“Ndio.” Akamjibu huku akijiuliza kwanini anaulizwa hayo maswali.
“Nakuona kila siku. Huwa nakutazama lakini wewe huna habari.”
Jamaa akatabasamu. Binti akaangusha bomu la silaha za maangamizi ya hisia na uroda.
“Kama hujali twende kwako tukafanye.”

Ndio maana toka siku hiyo Kibo huwa anawaambia marafiki zake, “Wazungu hawana tofauti na wanyama wakati mwingine. Lakini uzuri wako ni kuwa hakuna kiswahili kirefu...mara kimetoka huku kikaishia kule...hiyo hawana.”

Baaadaye akaamua kurudi “nyumbani.” Akaenda kwa Sofia ambaye kahamia hapa Columbus toka Atlanta. Sofia, mtoto wa Kinyakyusa , akaja juu. “ Wewe na hao wazungu wako siku zote hutuoni. Leo imekuwaje? Wamekutema?”
“Unajua dada zetu ninyi hamna mfano.”
“Hebu acha hizo. Kwanza sote tunatafuta dokumenti, huko si kupotezeana muda bure?”

Sofia akakataa katukatu. Hana muda na Wabongo.

SOMA HADITHI NA VISA TOKA KWANGU

Jana niliweka safu ya mashairi yangu. Kumbuka kuwa bado ninaipanua. Leo nimeweka safu ya hadithi, visa, hisia, mikasa, na uzushi toka kwangu. Kona ya Ushairi inaiywa: AYA JUU YA AYA. Kona ya hadithi, mikasa, n.k. inaitwa: MAMBO YA NYAKATI. Nenda upande wa kuume chini ya picha yangu kisha ukongoli upate kusoma.

MAKALA MPYA

Nimeweka makala mpya ambayo niliandika kabla ya kiini macho cha uchaguzi wa Urais hapa Marekani. Nenda kwenye kona ya makala zangu, chini ya picha yangu kisha kongoli uisome. Inaitwa Demokrasia Kiini Macho.

11/12/2004

SOMA MKUSANYIKO WA MASHAIRI YANGU

Nimeanza kuweka safu maalum yenye mkusanyiko wa mashairi yangu: AYA JUU YA AYA. Nimeweka mashairi matatu tayari, ila ninataongeza kadri siku zinavyokwenda. Ninahitaji muda kuchambua mashairi ya kuweka toka katika disketa, vitabu vya kumbukumbu, vipande vya karatasi, risiti, bahasha, n.k. Safu yenyewe iko chini ya picha yangu, chini ya Kitabu cha Wageni. Bonyeza hapo utapelekwa yaliko.

NASAHA FUPI ZA REHEMA REHEMA NCHIMBI: MIZIMU, MAJINI, VINYAMKERA NA UCHAGUZI WA MAREKANI

Mzalendo mwenzetu, mwanahistoria, mwalimu wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam, Rehema Nchimbi, anayesoma nchini Afrika Kusini kaniandikia kunijibu barua pepe yangu niliyomwandikia kumwambia kuwa Rais Joji Kichaka kapigiwa kura na mizimu ya watu wa kale. Kanijibu kwa mtiririko wa nasaha za kifasihi ambazo nimeona tuzisome wote. Naweka nasaha hizo hadharani. Hivi ndivyo alivyonijibu (nami nakubaliana naye):

Ndugu yangu, nashukuru sana kusikia kutoka kwako. Poleni sana na hiyo hali ya Joji kichaka. Ilikuwa ni lazima mizimu impigie kura kwani hata yeye ni mzimu wa hao mizimu yenye makampuni makubwa ambayo yanapora huko Iraq. Hakika muda haukuwa mwafaka kwa Kerry kwani azma yao ya kufilisi Iraq na kujineemesha kwa rasilmali za huko ulikuwa ndiyo kwanza mbichi kabisa. Wanahitaji uongozi wa kichaka ili wafanikishe mambo yao. Hapo hakukuwa na uchaguzi ila kiini macho, lakini kura tayari walikuwa wamezipanga, na ninahakika hata hazikuhesabiwa kwani hawakuwa na haja ya hizo hesabu zenu, wao tayari walikuwa na hesabu zao. Ndiyo hivyo tena, ulimwengu wa utawala wa mashetani, wapiga kura ni mizimu, na mitambo inatawaliwa na majini, na wapambe ni vinyamkela, nk. Binadamu kama nyinyi hamkuwa na nafasi yenu, subirini, safari nyingine kama hayo mashetani yatakuwa yametosheka na yatakuwa tayari kuachia ngazi. Msilalamike kwani hakuna anayewasikia, wote ni mashetani na mizimu yao.
Kila la heri, Mungu awe nawe. Ukombozi daima
rehema

TAZAMA PICHA ZA PWANI YA PEMBE YA NDOVU

Yanayotokea nchi ya Pwani ya Pembe ya Ndovu (Ivory Coast) yanatatanisha. Hujui wa kumwanini. Tuamini serikali ya nchi hiyo au tuamini Wafaransa? Tuamini waasi au tuamini vyombo vya habari? Rafiki yangu toka nchi hiyo aliyeko hapa Marekani kanitumia picha hizi. Anasema kuwa mama yake kamwambia kuwa wazawa wa nchi hiyo wako tayari kufa wakipambana na Wafaransa kutetea heshima na utu wao. Bonyeza hapa utazame picha zenyewe. Bonyeza juu ya kila picha ili kuifanya iwe kubwa. ONYO: BAADHI YA PICHA ZINATISHA KIDOGO.

11/11/2004

MAKALA KUHUSU KUCHAGULIWA KWA JOJI KICHAKA

Wengi wameniuliza juu ya kuchaguliwa kwa kichwa ngumu, mzee wa kibri, Joji Kichaka. Kwa walioko Tanzania, soma gazeti la Mwananchi la jumapili wiki hii katika safu yangu iitwayo: GUMZO LA WIKI. Nimeandika makala iitwayo: NINI KILITOKEA? JE JOJI KICHAKA ALIPIGIWA KURA NA MIZIMU? Kwakuwa makala hii bado haijachapwa gazetini, sitaweza kuiweka hapa ndani kwa sasa. Nitaiweka baada ya kutoka katika safu yangu. Wiki ijayo nitaendeleza makala hiyo kwa uchambuzi wa hoja za wakristo wenye msimamo mkali, waliompigia Joji kura kwa wingi, kuwa Joji anatetea maadili ya kikrsto kwahiyo ni mwakilishi wa Yesu hapa Marekani! Subiri. Kumbuka subira yavuta... Pia makala ya Urasta iliyotoka katika safu yangu ambayo wasomaji wengi wameomba niiweke hapa ndani itapandishwa. Ninatafuta disiketi niliyohifadhi makala hiyo iliyokuwa katika sehemu tatu. Najua iko mahala. Nikiipata tu nitaipandisha.

WARAKA WA FREDDY MACHA TOKA LONDON

Usiwe unakosa waraka wa mwandishi wa siku nyingi, Freddy Macha, anayeishi nchini Uingereza, kila wiki. Bonyeza hapa usome waraka wake wa wiki hii.

BARUA TOKA AMSTERDAM

Mara kwa mara nitakuwa naweka barua toka kwa Watanzania mbalimbali wanaoishi ughaibuni. Bonyeza hapa usome barua toka Amsterdam iliyoandikwa na Cosato Chumi.

UCHAGUZI MARIKANI: HABARI NJEMA!

Kwa wanaomchukia Rais mkaidi mwenye kibri mwiba kura Joji Kichaka, ingawa amechaguliwa tena, kuna sababu ya kufurahia: KWA MUJIBU WA SHERIA, JOJI HATARUHUSIWA KUGOMBEA URAIS WA MAREKANI MAISHA YAKE YOTE! Kwahiyo baada ya miaka minne ndio imetoka!

11/08/2004

UCHAGUZI MARIKANI: HABARI NJEMA!

Ndugu zanguni, baadaye leo au kesho nitaorodhesha sababu kadhaa za kufurahia kuchaguliwa kwa Bush! Kwahiyo usiache kurudi....nashindwa kuorodhesha hivi sasa maana mkono wa Babiloni Mkuu, beberu wahedi umenikamata kabali ya nguvu. Mshikemshike, jumatatu mwanzo wa wiki. Kimbia. Paka na panya...

11/06/2004

UKATAJI VICHWA WATAPAKAA DUNIANI

Kuna kitu kinaitwa Opereseheni Baghdad ambacho kinasambaa duniani kwa kasi: Ukataji vichwa watu wasio na hatia kama njia ya mapambano ya kisiasa.
Sijui ni lini dunia itaiga Operesheni Tanzania: uchomaji moto wa binadamu akiwa hai kwa wizi wa shilingi 3000 au kwa kusingiziwa kuwa kibaka
. Yahoo !wana hii habari ya ukataji kichwa. Nimeisoma dakika chache zilizopita. Ipate hapa.

MIZIMU ILIMPIGIA KURA JOJI KICHAKA?

Moja ya masuala ninayofanya siku hizi katika uwanja wa taaluma ni kusoma na kufuatilia kwa karibu mabadiliko makubwa ya kitamaduni, kiuchumi, kimahusiano, kisiasa, kisheria, na kisera yanayoletwa na mapinduzi ya tarakilishi na mtandao wa tarakilishi. Kwahiyo moja ya mambo ambayo nilikuwa nafuatilia kwenye uchaguzi uliomalizika hivi karibuni ilikuwa ni matumizi ya teknolojia hii mpya katika ujenzi wa demokrasia. Kwa mfano, nilikuwa ninatafiti jinsi ambavyo shirika la America Coming Together na The League of Pissed Off Voters wanavyotumia tarakilishi za mezani na mkononi, simu za mkono, na tovuti katika kampeni na harakati. Lakini jambo jingine nililokuwa nalitazama kwa makini lilikuwa ni upigaji wa kura-pepe (e-voting). Moja ya maswali ambayo watu wengi wamekuwa nayo ni hili: Unapobonyeza tarakilishi yako kumpigia mgombea wako kura, utajuaje kuwa tarakilishi hiyo imeorodhesha kura yako? Utajuaje kuwa kura yako imekwenda kwa uliyemtaka? Utajuaje kuwa waliotengeneza mashine hizo hawana chama wanachokipenda kwahiyo wameunda tarakilishi zao ili kura ziende kwa wanayempenda? Tuamini kwa kiasi gani upigaji kura kwa tarakilishi?

Katika kituo 1B eneo la Gahanna hapa Ohio, tarakilishi zilimpa Joji Kichaka kura 3,893 kabla hata wapiga kura hawajapiga kura hata moja. Mwishowe ikawa kuwa kura zilizopigwa kituoni hapo zilikuwa nyingi kuliko idadi halisi ya wapiga kura. Kulikuwa na wapiga kura 638, Joji Kichaka alipata kura kwa ujumla kura 4,258!
Soma habari zaidi hapa. Kumbuka kuwa kamnpuni iliyotengeneza tarakilishi za kupigia kura hapa Ohio, Diebold, imekuwa ikichangia fedha chama cha Republican na wakuu wa kampuni hii wamekuwa wakiitwa kwenye tafrija za chama hiki na chai za ikulu!

UCHAGUZI WA MARIKANI UNGEKUWA WA DUNIA NZIMA...

Kuna baadhi ya watu wanasema, kwa kejeli, kuwa Rais wa Marikani angechaguliwa kwa kura za dunia nzima maana maamuzi yake yanaathiri dunia nzima. Kwa mujibu wa GlobalVote matokeo ya kura za watu wasio Wamarikani yanaonyesha kuwa Waafrika hawampendi kabisa Joji Kichaka. Bonyeza hapa uone matokeo ya wapiga kura ambao sio Wamarekani. Ingawa inaonyesha kuwa Waafrika wengi wanampenda John Kerry, haina maana kuwa wanaelewa Kerry anasimamia masuala gani. Muhimu ni kuwa Kerry sio Joji Kichaka.

11/05/2004

UCHAGUZI WA MARIKANI: DUNIA YAOMBWA MSAMAHA!

Asilimia 49 ya Wamarekani ambao hawakumpigia kura Rais Joji Kichaka (yaani Wamarekani wanaomchukia!) wanaomba dunia msamaha kwa kushindwa kumg'oa madarakani Rais mpenda vita na mafuta. Je tuwasamehe? Kongoli hapa uone waomba msamaha.

11/04/2004

NCHI IMETEKWA!

Marekani imetekwa na mahafidhina.
Babiloni inawaka moto. Tumbo la jitu halikaliki.
Waliberali wanafunika nyuso, wanaona haya.
Miaka minne ya Joji Kichaka!
Sitaweza.
Nakumbuka wimbo wa Remmi: Narudi nyumbani nikale ugali...

Miaka minne ya Kerry nayo nisingeipenda, ila huyu mhafidhina wahedi, mpenda vita, ubabe, "kibri" na laghai ananitisha sana. Ndio, ananitisha kuliko akina Osama Bin Laden 100!
Lakini kama nilivyosema jana, niacheni kwanza nipumue na kutafakari.

MTU MWEUSI PEKEE KWENYE SENETI YA MAREKANI

Familia ya Obama, seneta pekee mweusi aliyechaguliwa mwaka huu, nchini Kenya imefurahishwa sana na ushindi wake. Bibi yake, Sarah Hussein Obama, na nduguze wengine, hawakulala usiku wakisubiri matokeo ya uchaguzi wa Marekani wakiwa makwao huko Nyanza, nchini Kenya. Soma habari zaidi toka BBC kwa kukongoli hapa.

MKUTANO MKUBWA JUU YA BLOGU

Mwezi ujao kuna mkutano mkubwa wa wanablogu na wana teknolojia ya zana za kisasa za habari na mawasiliano. Bonyeza hapa kupata habari zaidi juu ya mkutano huu na nyingine zinazohusiana na blogu, tovuti, mtandao wa tarakilishi, n.k.

11/03/2004

NIACHENI KWANZA NIPUMUE

Naombeni mnipe muda wa kupumua, kula, kulala, na kutafakari. Kwanza nataka kuhakikisha kuwa niko macho. Sijalala na wala sioti. Nasikia kuwa Joji Kichaka kawa tena rais wa Marikani. Kashinda kura za umma na kura za chuo cha kura. Ataongoza kwa miaka mingine minne. Hapana, nipe muda kidogo. Sina la kusema zaidi kwa sasa. Kuna wanaohamia Canada. Kuna wanaolia. Kuna wanaocheka. Nifunge virago kurudi kijijini Moshi? Kuishi miaka minne ndani ya serikali na bunge la kihafidhina sio mchezo jamani. Hapana, nipe muda. Ngoja nikasafishe uso isije ikawa ninaota au labda luninga yangu inanichezea shere!

11/02/2004

MJADALA WA NDEGE YA RAIS

Mjadala kuhusu ununuzi wa ndege ya Rais wa nchi yangu fukara niipendayo ya Tanzania umepamba moto. Soma baadhi ya mawazo ya wenye nchi wenye:

Maoni ya Joe Nambiza Tungaraza:
Ndugu Wananchi,

Kwanza kabisa naunga mkono maoni ya bwana Ndesanjo Macha juu ya usafiri wa mheshimiwa Rais Mkapa, kwamba wajumbe wa baraza la wachawi kutoka makabila mia mbili na hamsini na saba ya Tanzania washirikiane kutengeneza ungo au fisi wa kusafiria vilivyo na mwendo kasi maradufu zaidi ya ndege za kisasa za magharibi. Kwa maoni zaidi tembelea blogu ya Macha : http://jikomboe.blogspot.com

Pili, baada ya masihara ya hapo juu, mjadala huu wa ndege ya rais umeamsha hisia kali miongoni mwetu watanzania hata wengine wengi tulioko ughaibuni tukakiri kuwa asilani hatuwezi kurejea Tanzania ikiwa mfumo wa sasa na serikali hii vitaendelea kutawala!

Wengi wetu tuna hasira kali na nchi yetu iliyotuangusha na kuzidi kutuangusha hadi hivi sasa. Kuanzia masuala ya mishahara ya Walimu; ada za shule; umeme usiotabirika; kufa kwa huduma za halmashauri ya Jiji; kuporomoka kwa huduma za afya ya msingi; utamaduni wa ufujaji na rushwa kwa wafanyakazi na viongozi wa serikali yetu; uwekaji rehani wa mali ya mtanzania katika jina la ubinafsifishaji na soko huria na kadhalika.
Kuwa na hisia kali ni jambo zuri tu kwani nchi yoyote iliyoendelea au mfumo wowote uliowahi kufanya kazi vyema ulijengwa na wale wenye hisia zenye mrengo mkali.

Bwana Abubakar umetoa ushauri mzuri tu kwamba kama tunataka kufanya madiliko basi na tuanze kusaidia au kurejea nyumbani na kutoa mchango wetu moja kwa moja kwani nguvukazi yetu inahitajika. Ikesha Dan umetushauri tugombee udiwani au ukatibu kata , yaani tuwe pale kwenye ‘grass root level’

Pengine muhimu tukumbuke sababu zilizowafanya wengi waishi ughaibuni. Kama mito inavyofuata mikondo basi sisi binadamu pia tunafuata mikondo inayopelekea kwenye matumaini na uwepesi wa maisha. Hakuna mtu anayeweza kusema hii si kweli. Wengi wetu tunaipenda nchi yetu lakini nchi yetu haina vibarua vya kutosha ambavyo vinaweza kumpa kila mmoja wetu ridhaa wakati wakitoa mchango wenye manufaa kwa taifa.
(Self-actualization - being rewarded for a meaningful contribution in a meaningful career..).
A burnt child dreads fire. Hivyo, si rahisi kwa yeyote kurejea nyumbani na kuingia kwenye siasa ili alete mabadiliko bila kuzingatia sababu zilizomtowa huko nyumbani. Pengine ni vizuri kangalia uwezekano wa kusaidia Tanganyika yetu hapo hapo uliko. Kwani bila mkataba maalum, wengi wetu tumechukua kazi ya ustawi wa jamii kutoka serikalini, na kila mara bila ya shaka tumefika Western Union kutuma fedha kwa wadogo zetu au wazazi waliostaafu.

Katika misingi hiyo hiyo naamini kuna uwezekano kuleta tena matumaini ikiwa tutachangia katika elimu na afya kama watu wa magharibi wanavyofanya na WorldVision au Oxfarm lakini katika vyombo vyetu wenyewe Watanganyika. Na wale wanaoweza kuandika na waandike kukosoa na kuelimishana, ikiwa unafundisha vyuoni huku ulaya basi toa muda kidogo kuchangia mada huko vyuoni Tanzania au muda wa likizo yako katika masemina pale mlimani na kadhalika.

Pia la muhimu tusisahau kuwa PROUD kama waafrika hata kama IMF wangesema nini. Kumbuka hakuna mtu mweupe aliyegawanyika kimawazo kuhusu nafasi yake hapa ulimwenguni. They are convinced that they deserve what they have, whatever the costs.

Mwisho, hivi ni kweli? eti nasikia wanataka kununua helikopta mpya ya rais kwani daraja linaloelekea Nachingwea limevunjika hivyo Mkapa akitaka kumtembelea Mama yake anaogopa kupita kwenye matope!

Wasalaam,

Joe Tungaraza


MAONI YA NYANGU R. MEGHJI:
Jamani,
Sidhani kama kuwa maskini kuna maana usile chakula kizuri au kulala pazuri. Kama nikiomba msaada kutoka kwa jirani yangu kwa ajili ya kununua chakula lakini halafu badala yake nikanunua TV, ina maana yule mtu anidai pesa zake au akasirike? Je kama nimepata njia nyingine ya kupata chakula na nikaitumia ile pesa kununua kifaa kingine?
Nafikiri kutusaidia haina maana watusaidie hata kufikiri. Ninaamini uamuzi wa kununua ndege(asset) ulifikia baada ya "vichwa" kukaa na kutafakari. Hata tuliponunua rada inayoweza kutumika na jeshi pia, watu walipiga kelele kwamba hatukuhitaji teknolojia ya kiasi hicho sasa.
Lakini swali linabaki, ni mara ngapi katika maisha yako unanunua ndege au rada? Naamini hata kama ni maskini, unaponunua kitu basi jitahidi kiwe kizuri na kinachodumu. Ndege za Gulfstream zinajulikana kwa "fuel economy" na ubora.
Baadaye tutaulizwa kwa nini unaendesha gari au kuwa mobile wakati asilimiaa 90 ya nchi hawawezi kuwa navyo. Tungenunua basikeli kwa hela za magari tuliyonayo kila mtu Tanzania angeendesha basikeli...
Wasalaam,
Nyangu.Nyangu R. Meghji

MAONI YA ABUBAKAR FARAJI:

Asaalam ALeykum All!
Laila rais alikuwa na ndege ambayo sasa vipuri nvyake havipatikani maana the company who made it are long out of business....but besides that
Tuna watu wengi wana njaa Tanzania, hawana nyimba bora na mambo mengine mengi ...so does this means Rais asitembelee Benz or a decent Car because the money could be better placed else-where....lets be pragmatic and not over-simplify issues....things are far more complex than many critics would have us think....
Its easy to criticise but all of us Tanzanians living abroad especially or even at home have an opportunity to contribute to this debate in many ways but honestly what have we all done in the last year or six months to contribute to our country.....yet we point the fingers of criticism.....lets suggest some solutions we can come together even on this forum put up some suggestions... they may be totally ignored or one or two will be taken onboard...and we will have contributed positively instead of just criticising.....its our country we are criticising so it is our responsibility...

MAONI YA LAILA WAZIRI:
Habari zenu jamani!!?
Maoni yenu nimeyasoma, ni kweli rais anahitaji kuwa na usafiri wake binafsi kama marais wa nchi nyingine waliokuwa nazo. Lakini ununuzi wa pesa za kiasi kikubwa hivyo ulihitaji fikira za kina.Kama habari zilivyo eleza gharama ya ndege ingeweza kutosheleza elimu ya msingi hapo nyumbani lakini ikaonekana kwamba usafiri wa mtu mmoja ni muhimu kuliko elimu ya msingi ya watoto wengi tu hapa nyumbani. Sio lazima hizo pesa zitumike kama hao wafadhili wanavyosema, matumizi ya kuboresha maisha ya watu wengi yangekubalika zaidi kuliko kuboresha safari za rais peke yake.
SWALI: Kabla ya hiyo ndege rais alikuwa anasafiri vipi? Tatizo lilikuwa nini mpkaka kufikia uamuzi huo?
Kama jibu la swali hili ni kuwa rais has to have his own plane that's a no no.....
Nchi ni kama familia na rais ndio baba( The man)
They say " The man's success is not how much money he has made but what kind of family he has brought"
Baba asijiboreshe bila kujali familia.
Laila Waziri

UCHAGUZI MAREKANI: WANAKABANA KOO

Vyama viwili vikubwa vinavyoendeleza udikteta wa vyama viwili vimekabana koo katika uchaguzi uliofanyika leo hapa Marekani. Dakika chache zilizopita nimerudi toka kujitolea na shirika liitwalo America Coming Together ambapo tulikuwa tunakwenda nyumba hadi nyumba kuhimiza watu kwenda kupiga kura, kuuliza wale ambao wameshapiga kura kama wamekumbana na matatizo yoyote, kutoa usafiri kwa wale wasio na usafiri wa kwenda vituoni, na msaada wa kutunza watoto kwa wale wasio na fedha za kulipa mayaya. Miongoni mwa watu waliojitolea ni Wazanzibar wawili, Mussa na Omari, wanaoishi hapa Toledo.

Toka jua lilipochomoza mahakama zimekuwa zikipokea kesi toka kwa wagombea na vyama mbalimbali vya wananchi. Baadhi ya hukumu zilitolewa alfajiri hata kabla upigaji kura haujaanza. Na kesi nyingine ziko mbioni. Nimeambiwa kuwa kuna mtu kauawa huko Florida, baadhi ya watu wamepigiwa simu na kuambiwa kuwa vituo vya kura vimebadilishwa (walipokwenda kwenye "vituo vipya" walikuta kuwa habari hizo ni za uongo!), huko Michigan makaratasi yamesambazwa yakisema, "Ili uchaguzi uwe huru na haki, siku ya kupiga kura imesogezwa hadi tarehe tatu. Tarehe mbili ni kwa ajili ya wafuasi wa Republican na tarehe 3 ni kwa ajili ya Democrat." Habari hizi ni za uongo maana mwisho wa kupiga kura ilikuwa leo saa moja unusu usiku.

Kwa ufupi kuna kazi. Wafuasi wa John Kerry na wengine wasiompenda Joji Kichaka wanajiandaa kwa maandamano makubwa hapo kesho. Kuna vyama kama November 3, This Time We Are Watching, League of Pissed Off Voters, n.k. vimekuwa vikijiandaa kwa tarehe 3: maandamano, mapambano na polisi, mwamko wa umma, n.k.

Shirika la American Civil Liberties Union lina mradi ambao unatumia camera za mtandao usiwaya ili kurekodi vitisho kwa wapiga kura na unyama wowote wa polisi. Unaweza kubonyeza hapa kutazama video hizo moja kwa moja.. Ukitaka kufuatilia kesi mbalimbali za uchaguzi zilizofunguliwa na shirika hili kongoli hapa. Pia unaweza kubonyeza hapa ili kupata taarifa za moja kwa moja za matokeo kadri kura zinavyohesabiwa. Bonyeza hapa ili uone mlolongo wa matatizo yaliyojitokeza leo hii.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com