11/28/2004

NCHI YA KIPOLISI

Siku hizi najisikia kama vile naishi nchi ya kipolisi. Licha ya kuwa kuna vimulimuli vya polisi na ving'ora kila mahali, sasa hivi madereva wanabanwa kila kona. Barabarani manjagu wamejaa, halafu kuna kamera zinazochukua picha ukivunja sheria ambapo unatumiwa tiketi nyumbani kwa njia ya posta pamoja na uthibitisho wa picha ya gari lako (namba zake) na saa. Zaidi ya hilo hapa Toledo wameanza kutumia helikopta. Jamani! Ukiendesha unakuwa kama vile kuku aliyemwagiwa maji. Kama utatazama kila upande kutafuta askari ujue una kazi ya kuendesha huku ukitazama angani kutafuta iliko helikopta.

Tuache hilo, wanadai wanaimarisha usalama.

Nimeanza kuandika moja ya mradi mkubwa wa JIKOMBOE. Mradi huu umepewa jina: MWAFRIKA AKUTANA NA... Kwahiyo kutakuwa na sehemu mbalimbali kwa mfano: MWAFRIKA AKUTANA NA MUISLAMU, MWAFRIKA AKUTANA NA MKRISTO, n.k. Unaweza kujiuliza, "Kwani muislamu na mkristo sio Waafrika?" Ukiwa na swali hili, jua kuwa JIKOMBOE iko kwa ajili yako. Unaihitaji. Wakati unasubiri jibu lake, uwe ukisikiliza Wimbo wa Ukombozi (Redemption Song) wa Bobu Malya (ndio, Malya...hujui Bobu alikuwa Mchagga ndio maana Wachagga huwaambii kitu kwenye marege??)

Kuna habari nzuri sana kanitumia Nambiza Joseph Tungaraza (mwenzetu anayeishi Australia) kuhusu madhara ya dawa za kujichubua. Nitaipandisha hapa maana iko kwenye misingi ya ukombozi wa fikra. Kuna tatizo kila nikiiweka, lakini nitapatia ufumbuzi karibuni. Nitasonga kwanza ugali kisha nije kujaribu tena. Kwa taarifa yako leo najikata ugali wa nguvu. Ugali na kabichi na karanga. Habari hii ya kujichubua inaendana na dhana ya bwana mmoja toka NIgeria, Chinweizu, anayoiita Negro negrophibia. Yaani chuki ya watu weusi kwao wenyewe (kujichukia kwa watu weusi). Huyu bwana ana kitabu kizuri sana kwa watu wanaofuatilia masuala ya ukombozi wa fikra na elimu ya historia na utamaduni wa Mwafrika. Kinaitwa: THE WEST AND THE REST OF US. Nadhani kinapatikana pale British Council, Dar Es Salaam. Sina uhakika, ninadhani. Lazima ukisome hiki kabla hujaaga dunia!!!!!!

Usisahau kutazama blogu mpya nilizopandisha ikiwemo ile ya mwenzetu toka Kenya ya Mawazo na Mawaidha. Iko hapa. Zile mbili za Watanzania, Kona Yangu na Furahia Maisha, nazo zina mambo mapya. Ninakumbusha kuwa wale wanaotaka kuwa na vyombo vya habari (kuwa na "shihata" yao) kwa njia ya blogu wasisite kuwasiliana nami kama wana maswali. Na pia nimeweka somo la kwanza hapa kwenye blogu kwa wale ambao wanazo na wale ambao wanatengeneza zao kama bwana Kesi kule Kampala. Kesi karibu sana kwenye ulimwengu wa blogu.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com