11/24/2004

MNAONIANDIKIA NA MENGINE...

Nawashukuru sana wote wanaoniandikia. Ingawa nina muda kidogo, ninajaribu kuwajibu wote mimi mwenyewe. Situmii mashine kama wengine wanavyodhani. Pamoja na shukrani zangu, nina ombi moja. Sipendi kabisa...narudia, SIPENDI KABISA Watanzania wenzangu wanaponiandikia barua pepe kwa kutumia lugha za watu wengine/wakoloni. Hivi mbona wao hawatumii zetu wanapowasiliana wao kwa wao? Ninaposema "wao" mnajua ninawazungumzia akina nani. Kwa ufupi, mimi lugha ninayoifahamu kwa ufasaha zaidi na kuipenda ni Kiswahili na Kichagga. Hata ndoto huwa napata kwa lugha hizi. Blogu hii iko kwa ajili ya kuendeleza titi la mama yetu: Kiswahili. Iwapo Kiswahili chako ni cha kubabaisha kidogo (kama rafiki zangu wa nchi za jirani ambao huniandikia kwa kiswahili cha hapa na pale na kiingereza...wao nitawasamehe kwa sasa) unaweza kuniandikia kwa hicho kiingereza au lugha yoyote ya kuazima kwa mabeberu ila tafadhali fanya hima, jifunze Kiswahili ili siku za usoni tuwasiliane kwa Kiswahili. Hii ni blogu ya Kiswahili. Mimi nazungumza Kiswahili. Kiingereza nakifahamu kiasi ila sihitaji kukitumia kuwasiliana na watu wangu. Sidhani kuwa kuna ubaya kuzungumza kiingereza. Kwa mfano, ninatumia lugha hii katika shughuli zangu nyingine za kitaaluma. Ninahariri jarida la kiingereza liitwalo Perpectives on Global Development and Technology. Nina blogu ya kiingereza ya masuala ya teknolojia. Sina ugomvi na kiingereza au kifaransa. Mimi mwenyewe ninajilaumu kwanini nilipokuwa shuleni sikusoma kifaransa kwa makini. Pia nina mpango wa kujifunza kiarabu hivi karibuni. Kwahiyo isionekane kuwa mimi ni mtamaduni mwenye siasa kali. Najua tunaishi kwenye dunia ya maingiliano. Watanzania hatutaki kuwa kisiwa. Ila inapokuja katika mawasiliano kati yangu na wewe Mtanzania mwenzangu, hatuhitaji lugha ya kigeni. Nasema haya kwa nia njema ya kujenga na kutunza utu wetu.

Jambo jingine ni kuhusu blogu nyingine mbili za Kiswahili. Ile blogu ya Kona Yangu imeiva kwa habari kuhusu "wawakilishi" wetu (wabunge). Tafadhali ipitie upate undani wa hawa mabwana tunaowapa kura zetu nao wanazifanya kuwa "kula." Mwandishi wa Kona Yangu, Simon Mkina, alikuwa Dodoma wakati wa kikao cha bunge. Bonyeza hapa kwenda Kona Yangu. Mwandishi wa blogu ya pili, Furahia Maisha Yako, Dennis Mponji, kaniambia kuwa alikuwa na mihangaiko ndio maana amekuwa kimya ila hivi sasa yuko mbioni kuweka mambo mapya. Blogu yake iko hapa.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com