11/19/2004

BLOGU TOKA BUNGENI

Mtanzania, Simon Mkina, amekuwa ni mwanablogu wa Bongo wa kwanza kublogu toka bungeni. Blogu yake hii hapa. Amepeleka teknolojia hii kuliko waliko "waheshimiwa." Ila alituacha njiani baada ya kutuma taarifa mara mbili. Sijui nini kimempata. Labda kuna mvua, maana mvua ikinyesha nyumbani kule umeme unakatika, umeme ukikatika hakuna uwezo wa kutumia mtandao wa tarakilishi! Bogu ni nyenzo nzuri sana kwa mtu kama Mkina ambaye anafanya kwenye nyanja ya habari. Tunajua kuwa waandishi wengi wanaandika habari zao kisha zinapitiwa na watu wengine ambao katika kuhariri wanaweza kubadili habari nzima. Na wakati mwingine kuna habari ambazo hazichapwi kabisa hasa zikiwa zimechora makampuni yanayotoa matangazo kwenye gazeti lenyewe au kampuni ambazo wenye gazeti wana hisa au urafiki na wenye kampuni. Au wakati mwingine mhariri anaweza kuona habari ni moto akapata woga kuitoa. Nadhani kwa waliofanya kwenye vyombo vya habari wanaelewa tatizo la habari "kuhaririwa." Sasa kwa teknolojia rahisi na nyepesi ya blogu, watu wa kawaida, sio waandishi tu, tunaweza kuitumia kupashana habari, kuwasiliana, kuelimishana, kukosoa, kuhoji, kupinga, n.k. bila hofu ya kukosa fedha za wenye matangazo, kufukuzwa kazi na mwenye gazeti, kuhaririwa na mhariri mwoga au asiyekupenda, n.k. Blogu inafanya kila mtu kuwa mwanahabari! Unaona, kwa mfano, kwenye blogu hii naweza kusema kuwa VIONGOZI WOTE WA TANZANIA NI WEZI NA WALAGHAI! Wakiniletea za kuleta zaweza kuwaambia, "Ishilieni mbali! Kitoe!" Jambo ambalo siwezi kusema kwa urahisi gazetini! Je wanaweza kuifungia hii blogu????? Waambie wajaribu!

Kwa ujumla teknolojia hii ya mtandao wa tarakilishi inaleta mapinduzi makubwa. Tunakumbuka jinsi Mkapa alivyofungia kile kitabu cha Mwembechai Killings
(bonyeza hapa ukione) lakini muda sio mrefu kikazuka mtandaoni ambapo tunaweza kukisoma na serikali na maguvu yake yote ya dola haiwezi kufanya lolote. Tukio hili, kwa wale tuonaofuatilia mabadiliko makubwa ya kijamii, kisiasa, kitamaduni, na kifikra yanayoletwa na teknolojia hii, liliashiria jambo fulani kubwa sana mbele yetu. Kuna shairi maarufu sana hapa Marekani liitwalo: The Revolution Will Not Be Televised (Mapinduzi Hayataonyeshwa Kwenye Luninga.) Sasa watu wamebadili utabiri huu, wanasema: The Revolution Will be Digitized! Wanasema hivi wakiashiria mapinduzi makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Najaribu kutafsiri hii kwa Kiswahili. Anayeweza anisaidie! Digital kwa Kiswahili sijui ni nini. Nikikosa tafsiri yake nitaitunga. Ndio lugha inavyojengwa na kukua. Lugha haitoki mawinguni. Hatuhitaji kusubiri watu wajenge mnara wa Babeli ili lugha ikue au izaliwe. Lugha hujengwa na sisi wenyewe. Nisaidieni maana yake, kama hakuna tutaanzisha wenyewe.

Sikumbuki nilikuwa nataka kusema nini nilipoanza kuandika hiki kipande. Mkono ulikuwa unaniwasha. Ngoja nirudi kwenye shughuli nyingine niliyokuwa naifanya. Baadaye.


0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com