11/21/2004

FIDELIS TUNGARAZA AHOJI

Watanzania tutajiheshimu lini?
Ufuatao ni waraka wa Mtanzania anayeishi Helsink, Ufini, Fidelis Tungaraza, kufuatia habari za kuuawa kwa Mtanzania mwenzetu, dada yetu, mwanetu, jirani yetu, binadamu mwenzetu, mlalanjaa mwenzetu, shangazi yetu, binamu yetu....
Mtanzania huyu aliuawa kinyama na askari wawili wenye ngozi isiyo na kemikali muhimu sana ya Melanin. Nawaambia askari hawa, "Mbwa mwizi wa machinjioni!" Soma kwa makini utaelewa kwanini blogu hii nimeiita: Jikomboe. Safari yetu ya kujijua na kuthamini utu wetu ni ndefu ila najua kwa nia moja tutafika. Waraka wenyewe huu hapa chini:

Ndugu mhariri wa gazeti, ndugu viongozi wa serikali, na Watanzania wenzangu wengine, Ninatuma ujumbe huu kwa kustushwa, kusikitishwa, na kukasirishwa kutokana habari ya kuuawa kwa mwanamama wa Kitanzania na askari wahuni wa Kiingereza. Nimestushwa, kusikitishwa, na kukasirishwa kwa unyama na mauaji ya Mtanzania mwenzetu. Pia nimestushwa, kusikitishwa, na kukasirishwa na jinsi gazeti hili ambalo linasomwa na wasomaji wa Kiswahili ulimwenguni kote kupitia kwenye tovuti yao kwa jinsi lilivyoandika juu ya mauaji haya ya kinyama ya Mtanzania mwenzetu, hususani kichwa cha habari cha mauaji haya ya kinyama kama kilivyo hapo chini:

Askari Waingereza wadaiwa kuua changudoa D'Salaam


Ndugu Mhariri wa gazeti na viongozi wa serikali niawaombeni mlichukulie suala hili kwa uzito wa kina kwa upande wa kesi ya mauaji, na pia kwa jinsi gazeti hili lilivyochapisha habari hizi kwa kumuita 'changudoa' Mtanzania mwenzetu aliyetendewa ufuska na kuuawa kinyama. Kwa wale wote ambao wamewahi au bado wanaishi nchi za watu weupe tunajua jinsi suala kama hili ambavyo lingekuwa limewekwa katika vyombo vyao vya habari kama ingelikuwa wao ndiyo wametendewa kitendo kama hicho. Suala hili lingelitokea Ulaya, Amerika, Asia, au Uarabuni pengine lingeandikwa 'Askari wanaharamu, wahuni wa Kiingereza wasemekana kuua raia wetu mwanadada mwananchi maskini mnyonge mpole' Kuonyesha tu jinsi wanavyojithamini na kuthaminiana. Ndugu zangu wote tunaohusika na suala hili kwa njia moja au nyingine nawaombeni tulifuatilie suala hili.
Tanzania Nakupenda kwa Wote,
Fidelis Tungaraza, Helsinki, Finland.


Kisa chenyewe hiki hapa toka gazeti la Majira:

Askari Waingereza wadaiwakuua changudoa D'Salaam
*Walitoka Iraki vitani kuja kupumzika
*Yadaiwa walifanya mapenzi ufukweni
Na Kulwa Mzee

WANAJESHI wawili wa Uingereza wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya mauaji. Wanajeshi hao, Nigel David (23) na Brett Richard (20), walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Bi. Pellagia Khaday. Akisoma mashitaka hayo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Patrick Byatao, alidai kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 10 mwaka huu katika ufukwe wa hoteli ya Silver Sands. Inadaiwa Waingereza hao walimuua Bi. Conjesta Ulikaye. Hata hivyo hawakutakiwa kujibu mashitaka hayo kwa sababu Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya mauaji. Habari zilizopatikana mahakamani hapo zinadai kuwa wanajeshi hao walitoka vitani Iraki na walifika nchini kwa ajili ya mapumziko. Inadaiwa wakiwa kwenye ufukwe huo, mmoja wa washitakiwa alifanya mapenzi na changudoa huyo na kumlipa dola 70 (70,000/-) na kumshawishi ili afanye mapenzi pia na mwenzake kwa ahadi ya kumwongezea kitita. Alikubali, lakini haikufahamika walielewana kitu gani na baadaye walionekana washitakiwa wote wawili wanashirikiana kimapenzi na mwanamke huyo. Inadaiwa marehemu alifika katika eneo la tukio kwa ajili ya biashara ya kujiuza akiongozana na mwenzake ambaye alipata Mzungu mwingine. Washitakiwa walirudishwa rumande, upelelezi haujakamilika na kesi itatajwa Novemba 29 mwaka huu.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com