11/25/2004

LEO NI KULA BATA HADI WATUTAMBUE!

Leo Marekani nzima ni siku ya kula bata! Ni sikukuu ya thanksgiving hapa Marekani. Maduka kwa siku kadhaa zilizopita yalikuwa yakiuza bata kwa wingi kwa ajili ya siku ya leo. Sikukuu hii ya kula bata, mahindi, na keki ya maboga iitwayo thanksgiving ilianza kusherehekewa rasmi mwaka 1789. Lakini inaaminika kuwa thanksgiving ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1621. Sikukuu hii kama zilivyo sikukuu nyingine kama krisimasi na pasaka, imejengwa juu ya historia ya uongo. Inadaiwa kuwa siku hii ni siku ambayo wavamizi wa nchi hii ya Marekani (kumbuka hii nchi ni ya "Watu wa Kwanza" kama makabila ya wahindi wa asili wanavyopenda kujiita) walikaa kwa upendo na amani wakala chakula na watu wa asili wa nchi hii. Watu wengi wameanza kufundisha watoto wao ukweli wa sikukuu hii na ukweli wa historia ya mauaji ya halaiki, mikataba ya ulaghai, na wizi uliofanywa na wahamiaji waliokuja toka Uingereza. Rafiki yangu, Malaika, ambaye amenipigia simu dakika chache zilizopita kunikaribisha nikale bata anasema kuwa leo asubuhi alikuwa akimfundisha mwanaye juu ya ukweli wa sikukuu hii.

Kwahiyo kama kuna kiyama ya bata basi ni Novemba 25. Malaika anasema alianza kupika toka jana. Siku hii watu hula siku nzima huku wakitembeleana, kujumuika kifamilia, na wengine (hasa wanaume) kutazama mpira wa "miguu" wa Marekani. Huu mchezo wanauita mpira wa miguu (american football) wakati ambapo asilimia 99.99 ya mchezo huu wanatumia mikono! Nashindwa kuwaelewa. Basi Malaika anasema jikoni kwake kumeshehena chakula: bata, viazi vitamu, keki, mboga za majani, soseji, n.k. Anasema kuwa hofu yake ni kuwa mimi sili nyama na eti nisipokula bata leo sijasherehekea thanksgiving. Jamani, nile bata nisile?


Nimemtaja rafiki yangu Mailaika nikakumbuka makala niliyowahi kuandika juu yake iliyokuwa inauliza kama WamarekaniWeusi ni Waafrika. Nitaitafuta na kuipandisha ndani ya blogu. Haya ngoja nielelekee kwa Malaika ingawa sijaamua kama nitashiriki katika ulaji wa bata wa kitaifa au la.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com