MAPINDUZI YATAKUWA BLOGUNI
Yule mshairi mahiri wa hapa Marekani, Gil Scott-Heron, ana shairi liitwalo The Revolution Will Not Be Televised (kongoli hapa ulisome). Sasa sisi wanablogu tunakuja na yetu. Tunasema kuwa MAPINDUZI YATATOKEA BLOGUNI (The revolution Will be Blogged!). Tazama jamaa wa Kona Yangu anavyochanja mbuga na kutimulia vumbi wabunge, wana si-hasa, na wahariri wenye mikono inayotetemeka. Halafu kuna jirani yetu wa Mawazo na Mawaidha. Anakwenda mwendo wa Kimombasa, ambako meli hupita barabarani na nyumba zina gorofa ndani kwa ndani. Yeye tayari ameshamlima "Baba" Moi. Eti "Baba." Ilibaki kidogo tu wangemwita mungu! Unakumbuka kila taarifa ya habari Kenya ilikuwa lazima ianze na habari za "Baba." Mara kakohoa. Mara kalala mchana. Kila jumapili lazima tuambiwe eti kaenda kanisani. Hivi alikuwa anatumia mdomo huo huo kudanganya wananchi kwa kuombea mola au alikuwa ana mdomo mwingine?
Haya, kuna ndugu yetu Mponji wa Furahia Maisha. Anauliza, "Ulaya kunani?" Kaahidi mambo yako jikoni. Epua upesi!
Kuna yule dada yetu Ory Okolloh wa Kenyan Pundit. Anaambaa kwa blogu ya ung'eng'e toka Harvard. Katundika hadharani furaha yake kwa kuona wanablogu wa Kiswahili wanavamia uwanja. Ndio, tumeingia na baraka za mizimu ya mababu. Jamani, mnakumbuka wimbo wa marehemu Kalikawe wa Mizimu? Katika nyimbo alizoandika ule wimbo. Halafu kuna wanablogu Waafrika wengine kama akina Mshairi, Uaridi, Beginsathome, na kadhalika.
0 Maoni Yako:
Post a Comment
<< Home