MIZIMU ILIMPIGIA KURA JOJI KICHAKA?
Moja ya masuala ninayofanya siku hizi katika uwanja wa taaluma ni kusoma na kufuatilia kwa karibu mabadiliko makubwa ya kitamaduni, kiuchumi, kimahusiano, kisiasa, kisheria, na kisera yanayoletwa na mapinduzi ya tarakilishi na mtandao wa tarakilishi. Kwahiyo moja ya mambo ambayo nilikuwa nafuatilia kwenye uchaguzi uliomalizika hivi karibuni ilikuwa ni matumizi ya teknolojia hii mpya katika ujenzi wa demokrasia. Kwa mfano, nilikuwa ninatafiti jinsi ambavyo shirika la America Coming Together na The League of Pissed Off Voters wanavyotumia tarakilishi za mezani na mkononi, simu za mkono, na tovuti katika kampeni na harakati. Lakini jambo jingine nililokuwa nalitazama kwa makini lilikuwa ni upigaji wa kura-pepe (e-voting). Moja ya maswali ambayo watu wengi wamekuwa nayo ni hili: Unapobonyeza tarakilishi yako kumpigia mgombea wako kura, utajuaje kuwa tarakilishi hiyo imeorodhesha kura yako? Utajuaje kuwa kura yako imekwenda kwa uliyemtaka? Utajuaje kuwa waliotengeneza mashine hizo hawana chama wanachokipenda kwahiyo wameunda tarakilishi zao ili kura ziende kwa wanayempenda? Tuamini kwa kiasi gani upigaji kura kwa tarakilishi?
Katika kituo 1B eneo la Gahanna hapa Ohio, tarakilishi zilimpa Joji Kichaka kura 3,893 kabla hata wapiga kura hawajapiga kura hata moja. Mwishowe ikawa kuwa kura zilizopigwa kituoni hapo zilikuwa nyingi kuliko idadi halisi ya wapiga kura. Kulikuwa na wapiga kura 638, Joji Kichaka alipata kura kwa ujumla kura 4,258! Soma habari zaidi hapa. Kumbuka kuwa kamnpuni iliyotengeneza tarakilishi za kupigia kura hapa Ohio, Diebold, imekuwa ikichangia fedha chama cha Republican na wakuu wa kampuni hii wamekuwa wakiitwa kwenye tafrija za chama hiki na chai za ikulu!
0 Maoni Yako:
Post a Comment
<< Home