11/02/2004

UCHAGUZI MAREKANI: WANAKABANA KOO

Vyama viwili vikubwa vinavyoendeleza udikteta wa vyama viwili vimekabana koo katika uchaguzi uliofanyika leo hapa Marekani. Dakika chache zilizopita nimerudi toka kujitolea na shirika liitwalo America Coming Together ambapo tulikuwa tunakwenda nyumba hadi nyumba kuhimiza watu kwenda kupiga kura, kuuliza wale ambao wameshapiga kura kama wamekumbana na matatizo yoyote, kutoa usafiri kwa wale wasio na usafiri wa kwenda vituoni, na msaada wa kutunza watoto kwa wale wasio na fedha za kulipa mayaya. Miongoni mwa watu waliojitolea ni Wazanzibar wawili, Mussa na Omari, wanaoishi hapa Toledo.

Toka jua lilipochomoza mahakama zimekuwa zikipokea kesi toka kwa wagombea na vyama mbalimbali vya wananchi. Baadhi ya hukumu zilitolewa alfajiri hata kabla upigaji kura haujaanza. Na kesi nyingine ziko mbioni. Nimeambiwa kuwa kuna mtu kauawa huko Florida, baadhi ya watu wamepigiwa simu na kuambiwa kuwa vituo vya kura vimebadilishwa (walipokwenda kwenye "vituo vipya" walikuta kuwa habari hizo ni za uongo!), huko Michigan makaratasi yamesambazwa yakisema, "Ili uchaguzi uwe huru na haki, siku ya kupiga kura imesogezwa hadi tarehe tatu. Tarehe mbili ni kwa ajili ya wafuasi wa Republican na tarehe 3 ni kwa ajili ya Democrat." Habari hizi ni za uongo maana mwisho wa kupiga kura ilikuwa leo saa moja unusu usiku.

Kwa ufupi kuna kazi. Wafuasi wa John Kerry na wengine wasiompenda Joji Kichaka wanajiandaa kwa maandamano makubwa hapo kesho. Kuna vyama kama November 3, This Time We Are Watching, League of Pissed Off Voters, n.k. vimekuwa vikijiandaa kwa tarehe 3: maandamano, mapambano na polisi, mwamko wa umma, n.k.

Shirika la American Civil Liberties Union lina mradi ambao unatumia camera za mtandao usiwaya ili kurekodi vitisho kwa wapiga kura na unyama wowote wa polisi. Unaweza kubonyeza hapa kutazama video hizo moja kwa moja.. Ukitaka kufuatilia kesi mbalimbali za uchaguzi zilizofunguliwa na shirika hili kongoli hapa. Pia unaweza kubonyeza hapa ili kupata taarifa za moja kwa moja za matokeo kadri kura zinavyohesabiwa. Bonyeza hapa ili uone mlolongo wa matatizo yaliyojitokeza leo hii.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com