NASAHA FUPI ZA REHEMA REHEMA NCHIMBI: MIZIMU, MAJINI, VINYAMKERA NA UCHAGUZI WA MAREKANI
Mzalendo mwenzetu, mwanahistoria, mwalimu wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam, Rehema Nchimbi, anayesoma nchini Afrika Kusini kaniandikia kunijibu barua pepe yangu niliyomwandikia kumwambia kuwa Rais Joji Kichaka kapigiwa kura na mizimu ya watu wa kale. Kanijibu kwa mtiririko wa nasaha za kifasihi ambazo nimeona tuzisome wote. Naweka nasaha hizo hadharani. Hivi ndivyo alivyonijibu (nami nakubaliana naye):
Ndugu yangu, nashukuru sana kusikia kutoka kwako. Poleni sana na hiyo hali ya Joji kichaka. Ilikuwa ni lazima mizimu impigie kura kwani hata yeye ni mzimu wa hao mizimu yenye makampuni makubwa ambayo yanapora huko Iraq. Hakika muda haukuwa mwafaka kwa Kerry kwani azma yao ya kufilisi Iraq na kujineemesha kwa rasilmali za huko ulikuwa ndiyo kwanza mbichi kabisa. Wanahitaji uongozi wa kichaka ili wafanikishe mambo yao. Hapo hakukuwa na uchaguzi ila kiini macho, lakini kura tayari walikuwa wamezipanga, na ninahakika hata hazikuhesabiwa kwani hawakuwa na haja ya hizo hesabu zenu, wao tayari walikuwa na hesabu zao. Ndiyo hivyo tena, ulimwengu wa utawala wa mashetani, wapiga kura ni mizimu, na mitambo inatawaliwa na majini, na wapambe ni vinyamkela, nk. Binadamu kama nyinyi hamkuwa na nafasi yenu, subirini, safari nyingine kama hayo mashetani yatakuwa yametosheka na yatakuwa tayari kuachia ngazi. Msilalamike kwani hakuna anayewasikia, wote ni mashetani na mizimu yao.
Kila la heri, Mungu awe nawe. Ukombozi daima
rehema
0 Maoni Yako:
Post a Comment
<< Home