Nimefika hapa Helsinki kama masaa matatu yaliyopita. Nadhani kama nilikuwa ninaishi Bwagamoyo ingebidi niende kwa Mzee Shomari kutazama nyota yangu isije ikawa ni mkono wa mtu.
Kwanini nasema mkono wa mtu? Ilianza alhamisi jumatano iliyopita nilipotuma pasipoti yangu ubalozi wa Ufini kule New York. Jamaa wa Fedex akaniambia kuwa nitume kwa njia ya gharama kuliko zote ndio itafika haraka. Kwakuwa siku zilikuwa zimebaki mbili kabla wiki kuisha, na jumatatu yake ilikuwa ni sikukuu na ndio nilitakiwa kuondoka, nikafanya alivyoniambia. Basi kifurushi changu kikafika ubalozini asubuhi alhamisi saa moja na dakika ishirini. Ubalozi saa hiyo umefungwa! Kumbe ukituma kwa njia ile ya haraka kabisa kifurushi kinapelekwa asubuhi ya majogoo. Ningetuma kwa njia nyingine kingefika kati ya saa nne hadi saa sita ambapo ofisi ingekuwa wazi. Basi walipokipeleka kifurushi mara ya pili tayari wanaohusika na visa walishaondoka kazini. Hiyo ni alhamisi!
Kijasho kikaanza kutoka. Ijumaa baada ya kupiga simu mara tisa, kila mara nikiambiwa kuwa maofisa wa visa wana wageni, nilipata nafasi ya kuongea na anayehusika. Akasema amepokea maombi asubuhi hiyo ya ijumaa, ila tatizo ni kuwa kompyuta zina matatizo. Kama zikiwa zimeshatengenezwa kwenye saa sita atashughulikia, kama bado basi hatakuwa na la kufanya.
Kijasho kikazidi.
Saa nane nikapiga simu kuulizia. Nikaambiwa ameshatoa visa na kutuma kwa Fedex kwahiyo nitaipata jumamosi. Basi jumamosi nikasubiri weeeeeeeee.......wapi! Nikapiga simu kwa jamaa wa Fedex...yapata saa kumi jioni. Dada upande wa pili wa simu akatema maneno yaliyonimaliza nguvu kabisa. Akasema, "Desanjo Maka....." (Hivi ndivyo wengi wanatamka jina langu.) Kisha akasoma anuani na kuniuliza kama ni yangu. Nikajibu ndio. Akasema kuwa pasipoti yangu iko jimbo la Indiana na haitanifikia hadi jumanne wiki inayofuata (yaani jana) kwani jumatatu ilikuwa ni ni sikukuu!!
Mkono wa mtu!! Au ni kisirani tu ambacho naweza kukiondoa kwa kuoga kwa magadi???
Nifanyeje? Niende Indiana nikaichukue? Siwezi maana kisheria Fedex hawawezi kunipa hadi walete kwenye anuani inayotakiwa.
Haya. Ikabidi nibadili tiketi ili niondoke jummane kwani jamaa wa Fedex waliniambia kuwa nitapata kifurushi changu kabla ya saa nne na nusu asubuhi. Basi jummane asubuhi nimejiondokea zangu kwenda sehemu kwa dakika chache. Narudi nyumbani saa tatu nakuta karatasi inayosema kuwa jamaa wa Fedex ameniletea kifurushi ila kwakuwa hakunikuta ameondoka na ataleta tena kesho, yaani jumatano!
Kijasho tena...mkono wa mtu!
Nikapiga simu Fedex wakaniambia kuwa watamfuta derevea kwa njia ya simu ili wamwambie alete tena. Mpaka saa sita kasoro jamaa hajaja. Ndege inaondoka saa nane. Nikapiga simu tena Fedex. Wakaniambia kuwa bado wanajaribu kumtafuta dereva!
Kwanini nisiache kwenda? Nikaanza kujiuliza maana kukaa kiroho juu namna hii huwa sipendi. Lakini wakati huo huo nataka kunywa chai na kaka Ben na Jakaya. Saa sita inapofika jamaa wa Fedex huyo.
Nikapumua. Huyo mbio uwanja wa ndege. Kufika uwanja wa ndege nikakuta kumbe mambo bado. Jamaa wa Northwest Airline wanasema wanaona kuwa ninatakiwa kusafiri ila hawaoni tiketi...baada ya dakika kumi wananiambia kumbe natakiwa niende Continental Airline. Huko nako ilichukua dakika karibu 20 kabla hawajaweza kuona tiketi yangu. Lakini kabla hawajanipa lazima waende Northwest Airline...sikutaka wala kujua wanaenda kufanya nini. Nikabaki nawatazama wanaongea, wanaangalia kwenye kompyuta, mara wakapiga simu...zimebaki dakika 25 ndege kuondoka!
Haya, mwishoni nikapata tiketi. Sasa yule jamaa anayekagua mabegi akaanza kukagua begi langu kama vile ndege yangu inaondoka kesho...Naona itabidi nianze kuweka nyoka ndani ya begi. Jamaa kavuruga kila kitu nilivyopanga ndani ya begi. Viatu kule, nguo huku...ovyo.
Haya kuelekea ndani ya ndege. Kama kawaida (hii hunitokea mara zote ninazosafiri na kila mara nauliza wananiambia kuwa kinachochagua nani akaguliwe kwa kina ni kompyuta) nikaambiwa niende pembeni na kuanza kusachiwa kwa ustadi zaidi ya wengine na kuulizwa ninakokwenda, kuna nini, nani kanunua tiketi, ililipiwa kwa kadi au fedha taslimu na mambo kama hayo.
Basi nikapanda ndege hadi Newark, New Jersey. Pale nikapanda ndege nyingine ya kwenda hadi Amsterdam. Nikakuta kizaazaa kingine. Tiketi yangu ni 15E. Hapo kwenye kiti hicho kuna jamaa mwingine mwenye tiketi nambay 15E!! Suluhisho likapatikana. Nikakaa pengine.
Nafika Helsinki ndani ya basi nakutana na mhariri wa gazeti la mtandaoni la Malaysiakini, ndugu Vicknesan. Tunatazama ratiba tunakuta tumechelewa kongamano ambalo lilikuwa ni muhimu sana kwetu kuhusu vyombo vya habari. Tunakwenda hotelini na bila kubadili nguo (ndio, wala hatukuoga!) tunakwendá kwenye jumba la mkutano. Tunakuta wajumbe ndio wanatoka chumba cha mkutano.
Hivi sasa Maria Shaba wa Tanzania anaimba kufunga semina kuhusu wanawake na maendeleo duniani. Wimbo unakwenda:
I love my sisters
Deep down in my heart...