9/08/2005

MAMA SHABA ANAULIZA KAMA KWELI WAAFRIKA NI MASIKINI

Mama Maria Shaba, mwenyekiti wa Tanzania Association of Non-Governmental Organizations (TANGO), aliongea jana wakati wa mjadala kuhusu wanawake na maendeleo. Alisema kuwa kuna umuhimu wa kubadili tafsiri ya umasikin. Alionya kuwa Waafrika wanatakiwa kuwa makini sana kutokana na vyombo vya habari/uongo vya magharibi kusema kila mara kuwa sisi ni masikini. Unapoambiwa kuwa wewe ni masikini kila kukicha mwishowe unaamini kabisa kuwa wewe ni masikini hata kama ukweli ni kuwa wewe ni tajiri.
Akauliza kama sisi ni masikini kwanini mabepari wamekazana kuwekeza Afrika? Kwanini makampuni yao yanapeleka huduma na bidhaa zake kwa waafrika? Na kama ni kweli kuwa sisi ni masikini kiasi ambacho hata fedha wanazodai kutukopesha hatuwezi kulipa kwanini basi wanaendelea kutukopa kila siku??
Hivi sasa kuna kwaya moja inatumbuiza. Kumbe Wafini wanajua kuimba kama wagogo?

2 Maoni Yako:

At 9/08/2005 12:39:00 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Ndesanjo,ni kweli kabisa sisi sio masikini kama inavyodhaniwa na wenzetu wa magharibi,hususani kutokana na utajiri wa maliasili tulionao.Lakini umasikini wa fikra je?Huu ndio mbaya na ndio unaotuangamiza hivi sasa.Hatuthamini chetu,chetu chochote kile ni kibovu,kibaya,hakina thamani.Chochote tulichonacho hatukitaki,tunakwenda kwa nguvu ya umasikini wa fikra.Kwangu mimi huu ndio umasikini kuliko wowote ule.Tuanze kupambana na huo kwanza.

 
At 9/13/2005 01:10:00 PM, Blogger Indya Nkya said...

Kuna umasikini mwingine mbaya sana pia Jeff. Huu ni ule wa kukubaliana na hali yoyote ile. Watanzania hasa tunaongoza kwa hili. Chochote kinachojitokeza watanzania tunaridhika nacho. Umeshawahi kuona daladala ikipakia mpaka inatisha halafu ukilalamika abiria wenzako watakuambia kama unataka ustarabu chukua teksi? Au wakakushauri kwamba hii ndio nchi yetu bwana tufanyeje sasa. Tunaridhika kwa kila uchafu. Ukimkemea dereva anayeendesha gari vibaya, abiria wenzako watakuambia aha haomadereva ndio walivyo. Huu, ni umasikini mbaya sana ambao nadhani pia ni mwendelezo wa utapiamlo wa fikra.

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com