9/10/2005

Helsinki: Onyesho la kumaliza mkutano

Baada ya wajumbe wa mkutano wa Helsinki 2005 kukubaliana kuwa mwaka 2007, serikali ya Tanzania itaandaa mkutano mwingine kutazama utekelezaji wa maazimio ya mkutano huu....na kuwa kabla ya mwaka huo kamati ndogondogo zitakuwa zikikutana kuratibu juhudi za kufanikisha nia ya kujenga demokrasia na kuondoa umasikini, wajumbe waliagwa kwa tamasha kubwa. Kwanza nilitaka kuacha kwenda mkutanoni maana nilikuwa nimealikwa kwenye harusi moja iliyokuwa inavuma maana ilikuwa inasherehekewa kiafrika na pia nilikuwa nimekaribishwa klabu ya Chelsea kukaa na kujiburudisha na Watanzania wanaoishi hapa Helsinki. Lakini baadaye niliamua kuwa nitakwenda klabu ya Chelsea kisha baadaye niende kwenye tamasha. Na ninasema kuwa sijilaumu kwenda kwenye tamasha.

Kwenye klabu ya Chelsea nilishuhudia mjadala mzito sana sana katika ya wajumbe wa kikao kile, au tuiite kiti moto. Issa Michuzi alikuwa ndio mwenyekiti, akikazana kuzuia wajumbe kupunguza hamasa na kuacha kila mjumbe kumaliza anayotaka kusema. Fide alikaribia kupanda juu ya meza akielezea kuwa mifano tunayotoa ya kusema kuwa nchi kama Malaysia na Singapore zilitawaliwa kama Tanzania lakini zimepiga hatua. Mjadala ulikuwa mpana hasa ukigusia karibu kila jambo kuhusu Watanzania, viongozi wetu, na mfumo wetu wa maisha na utawala.

Kwanini Watanzania tuko nyuma hivi? Lilikuwa swali kuu.

Kulikuwa na mtazamo tofauti kidogo kati ya Watanzania wanaoishi nje na wale waliotokea nyumbani. Sikuongea sana, nilipenda kusikiliza. Baadaye usiku nilifikiri kwa undani yaliyozungumzwa nikagundua kuwa kila lililokuwa linasemwa na pande zote lilikuwa ni sahihi. Ingawa kulikuwa na kutokukubaliana kila mmoja akionyesha mapungufu ya uchambuzi yakinifu wa mwingine, ninaona kuwa wote walikuwa wanasema mambo ambayo yana ukweli ndani yake. Kubwa nadhani ni kutafuta eneo ambalo litaweza kuunganisha mitazamo hiyo ambayo kwa juujuu utaona kuwa inakizana.

Basi baadaye mimi na Michuzi na Vkii wa gazeti la mtandaoni la Malyasiakini la nchini Malaysia tukaenda kwenye tamasha ambapo tulikaa hadi leo asubuhi (Michuzi aliwahi kuondoka) na kuishia kuzunguka mji mzima tukitafuta chakula.

Sisiti kusema kuwa onyesho lile, hasa lile la mpiga kinanda cha mkono (accordian) Kimmo Pohjonen ni kati ya maonyesho ya hisia kali sana ambayo nimetazama karibuni. Mama Maria Shaba wa Tango alichoweza kusema ni kuwa, "Huyu bwana alikuwa anafanya tambiko la kujiponya kama tunavyofanya kule Bwagamoyo kwenye sherehe za kupandisha maruhani. Sisi kwetu tunadharau sanaa kama ile huyu unaona alivyoweza kuteka umati."

Kumtazama Kimmo ilikuwa ni kama vile kuwa katika ibada fulani hivi. Matumizi yake ya viungo, sauti, kelele, teknolojia, na taa vilinifanya kujisikia kama niko hekaluni.

Namtafuta Mama Shaba nimwambie kuwa aliitaja Bwagamoyo alipokuwa akimzunguzia Kimmo bila kujua. Kwani baada ya onyesho niliongea na Kimmo. Alinishangaza sana alipoanza kuongea nami Kiswahili. Kumbe amesoma muziki wa asili wa Kigogo kule Bwagamoyo na Dodoma. Na alisema kuwa itakuwa ni dhambi asiponiambia kuwa hakuna mtu hapa duniani anayemweshimu kama marehemu Hukwe Zawose. "Muziki wangu na kila kitu nilichokuwa nafanya naweza kusema ni hisia nilizopewa na Zawose.

1 Maoni Yako:

At 9/10/2005 12:09:00 PM, Anonymous Anonymous said...

Naam,
pande mbili za mazungumzo yale ni 1: Watanzania toka nyumbani na 2: Watanzania waishio nje ya nyumbani. Upande wa Watanzania waishio nyumbani wao wanatetea kwamba "dili" siyo makosa ila ni mfumo wa maisha yetu. Kwa hiyo wewe gawa na chukua kisicho chako, hujumu, dhulumu, onea, yote hayo safi tu. Sisi tulio nje tunatazama mambo ya nyumbani kwa kulinganisha na mifumo ya nchi tunazoishi kwa hiyo tunang'ang'ania kwamba serikali na watendaji wake wautumikie umma kwa ajili ya maendeleo ya jamii nzima siyo ya kwao binafsi.
Hapa Finland tuna mtindo wa kuwapokea na kuzungumza na Watanzania wanaokuja hapa kwa ziara za muda mfupi iwe kutokea nyumbani au nje ya nyumbani kama ulivyokuja wewe. Ndugu yangu, wale wanaotokea nyumbani mfano mmoja umeuona pale Sports Pub Chelsea! Basi ninakuhakikishia wa namna ile ni asilimia tisini na tisa (99%)! Utashangaa na kusikitishwa kuona mtumishi wa serikali jinsi anavyotetea "dili" na mambo ya kifuska wakati akiwa katika ziara ya kiserikali. Kama huna kaba ya roho unaweza kujikuta unamdharau, au unamtukana, au unatupiana makonde na Mtanzania mwenziyo huku ugenini.
Kwa sababu ya mambo yao yasiyoeleweka siku hizi Watanzania tuishio Finland katika mikutano na sherehe mbali mbali za Kitaifa hapa Finland hatuimbi wimbo wa "Mungu Ibariki Afrika, Wabariki Viongozi wake" kwa sababu tunajiona tunamchanganya Mungu kumuomba awabariki watu wa "dili". Badala yake tunaimba "Tanzania Nakupenda Kwa Moyo Wote"

Kimmo Pohjonen nilikuwa naye Chuo Cha Sanaa Bagamoyo tulikuwa tunasoma wote kwa Hayati Mwalimu Zawosse na kulala chumba kimoja. Kimmo ninaweza kusema kwamba ni mwanafunzi aliyelifuzu Rimba la Hayati Mwalimu Zawosse kwa kiwango cha hali ya juu sana.
Alipofariki Hayati Mwalimu Zawosse, Kimmo alitayarisha siku ya kumpa heshima na kumkumbuka Hayati Mwalimu Zawosse, miongoni mwa waalikwa katika siku hiyo tulikuwa wahitimu wa Chuo Cha Sanaa Bagamoyo tuishio Finland tukiongozwa na Mwalimu Arnold Chiwalala, Menard Mponda na Aliko Mwakanjuki. Kwa ufupi ilikuwa ni jioni ya huzuni kubwa.

Muda na shughuli zilitunyima muda wa kuweza kukutana na kujadili mambo mengi sana ambayo nilikuwa natarajia tungekaa, kuyatafakari, na kuyajadili. Hata hivyo ilikuwa vizuri sana kukutana nawe tena tangu tulipoachana miaka kumi iliyopita wakati dreadlocks zako zilikuwa kama miba ya mbigiri na sasa zimekuwa ndefu mpaka mabegani(Huyu ni Fidelis Tungaraza wa kawaida hana analolifanya bila kutumbukiza mzaha). Ngoja nifunge walaka wangu kwa mtindo wa wanasiasa wa Tanzania: "Kwa haya machache naomba niishie hapa na nikutakie kila heri katika shughuli zako za kila siku. Kidumu chama cha wanablog, kidumuuu! Zidumu fikra za wanablog, zidumuuu! Asante sana,
Fidelis Tungaraza, Helsinki, Finland.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com