Mwaka 1992. Shule ya sekondari ya Ilboru, Arusa. Nimejikalia zangu bweni la Mawenzi, mara naona miguu mirefu, miembamba ya mwalimu mkuu msaidizi inaingia bwenini na fimbo mkononi. Nikitoe au nibaki? Nilijiuliza. Kila upande nasikia kelele za miguu. Watoro wanakimbia na kuruka madirishani.
"Soo."
"Noma."
"Tuishie."
Watoro wanapeana taarifa za ujio wa Medukenya.
Nikajiuliza, "Kwanini nikimbie wakati sijafanya kosa?" Nikabaki. Akapita vyumba vvya chini kisha akaja juu. Akanikuta nimeketi kitandani. Sikumbuki nilikuwa nafanya nini. Akacharuka, "Wewe ndio unaongoza kundi la watoro sio?"
"Hapana." Nikamjibu.
"Hapana kivipi. Wenzako si hao wanakimbia huko nje?" Nikabaki kimya. Namtazama. Akanisogelea, akavuta sweta niliyokuwa nimevaa sehemu ya begani huku akiniamuru, "Twende ofisini ukanieleze vizuri."
Hao kiguu na njia hadi ofisini kwake.
"Jina lako nani tena?"
"Gregory"
"Una la kujitetea? Nikikuadhibu utasema nimekuonea?"
"Ndio utakuwa umenionea."
"Nimekuonea kivipi?"
"Sijafanya kosa lolote."
"Hebu acha masihara. Wewe umejificha kule Mawenzi wakati wenzako wako katika vipindivya dini kisha unasema kuwa huna kosa?" Alianza kupandisha mori. Mimi nimetulia tu.
"Sijajificha mwalimu."
"Wenzako wako wapi sasa hivi?" Aliniuliza huku akinionyesha ratiba inayoonyesha kuwa wakati huo ilikuwa ni vipindi vya dini.
"Mimi huwa siendi kwenye vipindi vya dini." Niliangusha bomu. Likatua kichwani kwake kwa kishindo kilichomyanyua toka kitini alikokaa na kuanza kunisogelea na fimbo yake tayari kunichapa.
"Naona tunataniana. Yaani unakiri kuwa mtoro sio leo tu bali siku zote!" Aliropoka.
"Mimi sio mtoro. Sihudhurii vipindi vya dini maana hakuna dini inayowakilisha mtazamo wangu wa kiimani." Bomu jingine. Hili lilimrudisha kwenye kiti.
"Gregory acha utundu wako. Kwani wewe sio mkristo?"
"Hapana mwalimu. Sina dini. "
Wakati huo nilikuwa mfuasi wa imani ya Kirasta ambayo niliichukulia kama mfumo wa maisha zaidi ya dini. Kwahiyo wakati wa vipindi vya dini nilikuwa najisomea Biblia mwenyewe. Nilikuwa bado niko katika safari ya utafiti na kujitafuta. Ila nilishaamua kuwa mimi sio mkristo. Kabla ya hapo nilikuwa Mluteri kutokana na sababu za kihistoria na kijiografia. Wamisionari toka Ujerumani walifika Old Moshi ambako wakazi wake wengi ni Waluteri. Ina maana ningezaliwa Rombo au Kibosho, uwezekano mkubwa ningekuwa Mkatoliki. Unaona jinsi dini zetu hizi tunazofikia hatua ya kutoana macho tumezipata kwasababu za kijiografia tu? Hatunazo kwakuwa tulitafiti na kuchambua na kusaka na kutafuta. Hapana, ni kutokana na tulipozaliwa. Ningezaliwa Zanzibar, uwezekano mkubwa ningekuwa Muislamu. Basi wakati huu nakutana na Medukenya nilikuwa kwenye safari hii muhimu sana ya kutafuta ukweli juu ya Mwafrika bila kupitia katika falsafa za walioleta utumwa na ukoloni (waarabu na wazungu).
"Huna dini kivipi? Kwani wazazi wako ni dini gani?" Aliniuliza.
"Wazazi ni Waluteri."
"Sasa inakuwaje unasema huna dini?"
Hapa alinipa nafasi ya "kumhubiria" na kuotesha mbegu ya ukombozi wa fikra.
"Imani na masuala ya kiroho sio mambo ya mkumbo. Haya ni mambo ya mtu binafsi. Wazazi wangu kuwa Waluteri haina maana kuwa lazima mimi nami niwe Mluteri."
"Dini ni ya wazazi wako." Aliniambia huku akionyesha kuwa na hamu ya kunisikiliza lakini wakati huo huo akitaka bado kuonyesha ubabe wa ki-ualimu.
"Nani kasema dini ni ya wazazi? Imeandikwa wapi?" Nilimuuliza kisha nikamwambia kuwa kama dini ni ya wazazi, basi wazazi wetu wameasi maana huko nyuma mababu zetu hawakuwa Wakristo au Waislamu. Kwahiyo kuna wakati ambapo wazazi wetu waliasi dini za wazazi wao na kufuata dini mpya zilizoletwa na wamisionari na mabwana wa biashara ya utumwa. Isitoshe, biblia ambayo yeye anaiamini inasema kuwa kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe.
Kijasho kilimtoka lakini hakutaka kuonyesha.
"Hizo fikra umepata huko mtaani zinakupotosha. Mtazamo huu unaweza hata kukuharibia maendeleo yao darasani." Aliniambia na kuniuliza dini yangu.
"Sina dini. Ila ninafuata mfumo wa maisha wa Kirasta ambao unajumuisha masuala ya imani juu ya mungu."
"Hebu shika chini. Urasta si uhuni tu wa huko mtaani? Hebu shika chini acha ukorofi wako. Uvivu umekujaa unatafuta njia za kuuhalalisha." Mara alinibadilikia. Kawa mbogo.
"Urasta sio uhuni mwalimu. Huu ni mfumo wa maisha unaomtazama Mwafrika, historia na utamaduni wake kama kielelezo kamili cha namna ya kuishi, kuabudu, kula, kutafakari, n.k."
"Nasema shika chini. Uhuni huo unauacha getini. Sio hapa."
"Hunichapi mwalimu. Urasta ni Uafrika. Sio uhuni. Kama ni uhuni mbona tunasoma biblia mnayosoma nyie?"
"Kama unasoma biblia si ungeenda kule chapel ukajiunga na wenzako?"
"Suala sio biblia. Suala ni tafsiri. Kama suala ni biblia si kusingekuwa na madhehebu mengi namna hii ya kikristo. Hawa waislamu wanasoma biblia."
"Gregory acha kupoteza muda. Shika chini."
"Huwezi kunichapa wakati sina kosa."
Mpaka wakati huu nilishajua kuwa nimeshinda. Alionekana kutaka kunichapa kama njia ya kutotaka kushindwa na mwanafunzi. Yeye ni mwalimu mkuu msaidizi, mtu mzima, na mrefu, atashindwaje na mwanafunzi? Kichwa kilikuwa kinanielemea kwa furaha. Sikujua nilipata wapi nguvu za kumjibu namna ile. Medukenya alikuwa akiongopeka. Sio kama Bino, mwalimu mkuu...ambaye naye tulikuja kushusha nguvu zake siku ile pale kwenye uwanja wa mpira wa shule ya msingi...kisa cha siku nyingine hiki (Hashimu, Isa, Mgeta, Mponezya, mnakumbuka?).
Mara akaweka fimbo chini na kuniambia niandike barua kwake kueleza msimamo wangu juu ya kuhudhuria vipindi vya dini. Barua hiyo hadi leo sijaiandika. Kilichofuata ni kuwa kila ijumaa wakati wa vipindi vya dini mimi nilikuwa naondoka zangu kupitia njia ya dukani kwa Kishuu (ingawa njia fupi ilikuwa ni ile ya kupitia Bino Road, ambayo wanafunzi hatukuipenda maana Bino alikuwa akiitumia) kwenda kwa Babu Fulani Mkushi Karudi, rasta aliyekuwa mhandisi wa ndege nchini Jamaika lakini akaamua kuondoka Babiloni kuja Sayuni kuwa mkulima na mtabibu wa kutumia vyakula. Babu alikuwa na misimamo mikali hasa. Alikuwa hagusi pesa, mara nyingi anakula chakula kibichi, nyumba yake haikuwa na mlango (mlango kazi yake nini?), nyumba yake ilikuwa imejengwa kwa nyasi....Fulani anahitaji kuandikiwa kitabu kabisa.
Toka siku ile Medukenya hakuwahi kuingia kwenye anga zangu tena.