8/31/2005

LEO NI SIKU YA BLOGU DUNIANI


Leo ndio ile Siku ya Blogu duniani. Wazo la kuwa na siku kama hii lilitoka kwa mwanablogu huyu hapa. Maelezo zaidi kuhusu siku hii yapo hapa kwa Kiswahili. Shukrani kwa Mawazo na Mawaidha aliyefanya tafsiri hiyo katika "wiki" maalum ya siku hiyo.

Siku hii wanablogu wanaopenda kushiriki wanachagua wanablogu watano ambao wanatoka katika tamaduni tofauti au wana mitazamo tofauti na yao.

Mimi nimechagua watu toka tamaduni tofauti. Sikupenda kutafuta watu kutokana na mitazamo yao. Wanablogu hao watano ndio hawa:

1. Mama wa Yousuf: Huyu ni mwandishi wa wa Kipalastina. Anaandika juu ya ulezi wa mwanaye na kazi ya uandishi katika nchi iliyokaliwa kwa nguvu na na Waisraeli. Kongoli hapa.

2. Jilltxt: Nimechagua blogu ya mwanataaluma, Jill, kutokana na blogu yake kuwa na viunganishi na habari nyingi kuhusu masuala ya uhusiano kati ya fasihi, taaluma, na blogu. Ninapenda watu wengi kufuatilia kwa undani juu ya mahusiano hayo. Ingawa toka apate kazi ya utawala, pamoja na kuendelea kufundisha, haandiki tena mara kwa mara, bado blogu yake ni benki ya taarifa nyingi na za kuelimisha. Kongoli hapa.

3. Blogu kuhusu uchaguzi wa wabunge Azerbaijan: blogu hii nimeichagua kutokana na ukweli kuwa wengi wa wasomaji wa blogu hii ni Watanzania na hivi sasa kampeni za uchaguzi zimepamba moto Tanzania. Nimetaka kuonyesha jinsi ambavyo teknolojia hii inarahisisha kazi ya upashaji habari za uchaguzi. Kita hapa.

4. Bwana Afigani: Hii ni blogu ya jamaa aliyeko Afghanistani. Nimemchagua huyu kutokana na shauku ya kutaka kujua wanablogu katika nchi kama Afghanistani wanafanya nini. Uzuri mwanablogu huyu anabandika picha hapa na pale, kwahiyo unaweza kuona hali ilivyo nchini humo. Kingita hapa.

5. Blogu ya kimbunga cha Katrina: Nimechagua blogu hii kwa nia ya kutaka kuonyesha jinsi ambavyo blogu zinaweza kutumika kutoa taarifa za haraka wakati wa maafa. Wakati wa maafa ya tsunami, blogu zilikuwa ndio chanzo kikuu cha habari na picha kwa haraka zaidi hata ya mashirika makubwa ya uongo (au habari kwa neno jingine) kama CNN. Nilikuwa natafiti wanablogu wanafanya nini kufuatia maafa yaliyoletwa na Katrina. Nenda hapa.

8/30/2005

Wanablogu wanaongoza sauti ya upinzani dhidi ya udhalimu Misri

Katika nchi ambayo vyombo vya habari vinamilikiwa na serikali na vile vya binafsi vina mahusiano ya karibu na wakuu wa nchi, wanablogu wanaongoza sauti ya upinzani dhidi ya dikteta Hosni Mubarak wa Misri. Kuna habari hiyo hapa. Na mmoja wa wanablogu hao ni mwanamama huyu.

8/28/2005

Habari kuhusu wanablogu wa Tanzania

Nimemaliza kuandika habari fupi kuhusu wanablogu wa Tanzania wanaoandika kwa kiingereza, kiingereza na kiswahili, na wanasiasa wanaoanza kublogu. Habari hii iko kwenye blogu ya mradi wa Sauti za Dunia. Kongoli hapa uisome.

8/26/2005

Blogu Nyingine za Watanzania Hizooooo...

Kwanza kabisa toka jumapili iliyopita nimekuwa nasikiliza wimbo wa Fela uitwao Trouble Sleep Yange Wake Am. Nimekuwa naupiga na kuurudia masaa yote. Ngoma za Tony Allen na mdomo wa bata wa Fela siwezi kuelezea. Katika wimbo huu kuna sehemu anasema:
Rafiki yangu katoka jela majuzi
Anatafuta kazi
Anazunguka huku na kule usiku na mchana
Polisi wamemsimamisha na kumwambia
Bwana nakukamata kwa kosa la kuzurura!
Hata sasa ninavyoandika ninasikiliza wimbo huu. Nimemtaja Fela kwa nia ya kuwaambia wasomaji walioniuliza maswali kadhaa juu ya Fela kuwa nitawajibu.
************************************************************************
Kuna wanablogu wapya ambao ukipata muda watembelee na kuwakaribisha. Kwanza kabisa yuko ndugu Swai. Swai anajitambulisha kwa namna ya pekee. Huu ndio utambulisho wake:

Nimetulia ni mtaalamu wa mambo flani ya uchawi wa kizungu si unaelewa iweje transistor itoe sauti au picha ya mtu...upo hapo babake...ndio mambo yangu hayo.

Ninaishi Mbezi beach ndani ya heka kumi nimejenga Jumba la kufa mtu naishi humo na mwanangu mmoja na Chui wangu pamoja na walinzi kumi na mbili ndani na nje. Nina gari ndogo za kutembelea kumi ambazo ni Range rover new model ya mwaka huu, Benzi S 500 jeusi lina seat za leather nyekundu,Jeep jeupe kali,Valnuet V2500 black,Ford Fury 3000, Free lander, Land crueser VX V12, BMW new model na nyingine nyingi sizikumbuki. Ninamiliki makampuni kibao hapa mjini yenye mitaji ya kuanzia billioni 100 na kuendeleaYaani kwa kifupi nina pesa ya hatari. Nina utaratibu wa kutoa misaada kwa waitaji jaribu kuniona nikusaidie lakini msaada usizidi bilioni 50.
Huyo ndio Swai.
Mwanablogu mwingine anayeandika kwa kiingereza ni ndugu Peter John. Mtembelee hapa.

Siku ya Blogu Duniani: Tarehe 30 Mwezi Huu

Mwanablogu toka Israeli, Nir Ofir, ndiye aliyetoa wazo la tarehe 31 mwezi wa nane kuwa ni siku ya blogu duniani. Wazo hili lilimjia pale alipotambua kuwa tarehe 31 Agosti ikiandikwa hivi "3108" inaweza kusomeka kama neno "blog." Halafu anasema kuwa amegundua kuwa ingawa mtandao wa kompyuta umeelezewa kuwa utasaidia kuifanya dunia kuwa kijiji, hali halisi inaonyesha kuwa (akitumia mfano wa wanablogu) kuwa wanablogu wanasoma wanablogu wale wenye mawazo kama yao au waliotoka katika nchi zao. Hata viunganishi tunavyoweka kwenye blogu ni vile vya wanablogu wenye mawazo au mitazamo kama yetu.

Basi akaona kuna haja ya kuwa na Siku ya Blogu Duniani. Na ndio hiyo tarehe 31 mwezi ujao. Katika siku hiyo unachotakiwa kufanya ni kuwatambulisha wanablogu watano ambao wametoka katika utamaduni tofauti na wako na pia wana mitazamo tofauti na yako.

Mradi wa Sauti ya Dunia unazungumzia pia siku hiyo.

Nawasihi wale wanaoweza washiriki.


8/25/2005

Masahibu ya wanaoblogu kwa lugha zaidi ya moja

Mwanablogu Ethan anajadili kwenye blogu yake masuala ya blogu na lugha. Anagusia blogu zisizo za kiingereza kama blogu za Kiswahili na changamoto waliyonayo wanablogu wanaotumia lugha zaidi ya moja kama Msangi. Ethan msome hapa. Mwanzoni mwa mjadala huu anaongelea mambo ambayo yanaweza yasikuvutie, endelea tu hadi katikati na kisha umalize.

8/24/2005

Unaifahamu Afrika Vizuri?

Kama unadhani unaifahamu Afrika vizuri, jaribu mchezo huu wa jamaa wa SchoolNet. Jaribu zoezi gumu kuliko yote.

8/23/2005

Lazima Nichague Shetani Bora?

Kwanini haiwezekani?
Wananiambia kuwa haiwezekani.
Kwanini?
Eti wananiambia kuwa haiwezekani ukawa hauko CCM na ukawa hauko upinzani.
Haiwezekani.
Lazima uwe na upande.
Lazima uwe kushoto au kulia.
Ukiikosoa CCM, wanakuja juu na kusema, "Wewe unashabikia upinzani."
Ukikosoa upinzani, wanakuja juu, "Umetumwa na CCM."
Ukikosoa upinzani na CCM kwa pamoja wanabaki na maswali.

Wananiambia, "Haiwezekani!"
Nawauliza, "Kwanini?"
Kwani lazima kuwa na upande?
Wananiambia lazima nichague shetani mwenye afadhali.
Lazima nitafute mwivi na muongo mwenye afadhali.
Lazima nichague shetani mmoja kati ya wawili.

Kwanini kuwe na ulazima huo?
Naendelea kuuliza.
Embe bovu pande zote. Lazima nilile?
Mimi sitaki shetani wa upande wa kuume,
Wala shetani wa kushoto.
Shetani mwenye afadhali au shetani asiyefaa kabisa
Bado ni shetani.

Inawezekana.

Mungu Bila Dini, Dini Bila Mungu...

Muda mrefu sijaongea kirefu kuhusu masuala mbalimbali ya kusafisha fikra zetu. Soma. Kama nimekugusa pabaya, hiyo sio nia yangu.
***************************************************************************
Haiwezekani!
Waakujia juu, "Haiwezekani!"
Haiwezekani. Kivipi.
Hawatakubali. Mishipa itawatoka.
Maswali watakurushia. Mate yatakurukia.
Utashangaa, iweje hawaelewi jambo rahisi namna hii?
"Haiwezekani mtu asiwe na dini!" Watakwambia huku wakijiweka tayari kwa ubishi.
Ubishi.
Wanabisha jambo linalohusu nafsi na imani yako.
Wewe unawaambia kuwa nafsini mwako huamini kitu kinachoitwa dini. Huna dini, sio muislamu wala mkristo (maana dini kwao ni hizi mbili tu).
Wanakataa. Haiwezekani. Kila binadamu ana dini.
"Hawezekani kivipi wakati mimi ni binadamu na sina dini?" Unawauliza.
Wanajibu, "Acha kutuhadaa, kila binadamu ana dini. Ina maana huamini kuwa kuna mungu?"
Wakiuliza swali hili lazima nicheke kwanza.
Swali hilo hufuatwa na maswali mengine mawili:
"Sasa ina maana ukifa utazikwaje?"
Swali la pili, "Sasa ukifa utakwenda wapi?"
Mahesabu ya imani za watu hawa yako hivi (Idya, kama nimekosea mahesabu nisahihishe):
binadamu + dini = imani juu ya mungu (yaani mungu yupo)
binadamu - dini = mungu hayupo

Hawajui kuna tofauti kubwa sana kati ya dini na kumwamini mungu. Wakati wengi wetu tunadhani kuwa dini kazi yake ni kutufanya tumjue mungu, kumwamini na kumtii, ukweli ni kuwa dini nyingi zinatuwekea ukuta wa chuma usionekana ambao unatuzuia tusimjue mungu. Ukiwa hutaki kumjua mungu au unataka kudhani kuwa unamjua, nitakushauri uwe na dini.
Najua sentenso hiyo ya mwisho inaweza kukufanya ujiulize kama "zimenitoka" au bado "zipo."

Dini inakufanya umjue mungu kupitia mawazo na mitazamo ya watu wengine (karibu wote ni wanaume) ambao wanavaa kanzu na majoho wakiongea kwa utaratibu ili uone kuwa wana tofauti sana na wewe na kuwa wana ukaribu na mungu. Wengine hudiriki kutuambia kuwa huongea na mungu. Ila ukiwaambia wakuite saa wanaongea naye ili usikilize au kushiriki, watakwambia kuwa kama huna roho safi huwezi kuongea naye. Lakini ninaposoma busara za Yeshua (Yesu/Isa) nakuta akisema kuwa mungu anatafuta wale waliopotea. Wale wasio na "roho safi." Na ndio maana Yeshua alikuwa akishinda vijiweni na wacheza kamari na wachakaramu wengine. Miyahudi ikamjia juu, "He, wewe mbona unajumika na wenye dhambi?"
Unajua aliwajibu nini? Kasome kitabu unachoamini kuwa ndio ramani na dira yako hapa dunini ingawa kinakusanya vumbi sebuleni kwako ulikokiweka kama mapambo. Kila siku unahangaika na magazeti ya ushambenga lakini kitabu unachodai kimeandikwa na mungu mwenyewe hukisomi...
Turudi kwenye hoja ya msingi.

Kwahiyo unachojua kuhusu dini ni mawazo ya viongozi wa dini yako. Mawazo ya binadamu wengine kama wewe. Mawazo yao hayo ndio yanakuwa dira yako wewe ambaye una akili na uwezo wa kujitafutia ukweli mwenyewe. Viongozi hawa, wakati mwingine, kama hawajui jambo wanapenda kukwambia kuwa jambo hilo ni "fumbo takatifu." Waulize kuhusu tungo ya utatu. Watakwambia hilo ni fumbo. Yaani mungu wako anakufumbia baadhi ya mambo. Hataki uyajue!
Dini inakufanya uwe mvivu. Hutasoma biblia au kurani kwasababu kuna viongozi wa dini yako ambao kazi yao ni kusoma vitabu hivyo na kukutafsiria mara moja kwa juma. Au wakati mwingine mara moja au mbili kwa mwaka iwapo wewe ni wale wanaoenda kanisani misa za usiku au siku ya krisimasi.

Dini inakufanya udhani kuwa kuna mashindano kati yako wewe mkristo wa kilutheri na mkristo wa kiangikana, au shahidi wa yehova dhidi ya mkatoliki, au mashindano kati ya muislamu wa sunni na yule wa shia, au mashindano kati ya muislamu na mkristo...mashindano ya kwenda mbinguni. Dini inakufanya uamini kuwa watu wote wasio na imani kama yako watakwenda unakoita motoni. Wewe na wenzako ndio mnajua hiyo njia nyembamba iliyozungukwa na malaika weupe (ndio malaika weupe, hakuna mweusi) wenye mavazi meupe ya kuelekea kwenye uzima wa milele. Pengine ndio maana tunajichubua ili tufanane na hao malaika.

Kuna watu ambao huniambia kuwa dini huleta amani. Hivi ina maana kule Rwanda kulipotokea mauaji ya halaiki Warwanda hawakuwa na dini? Au hakukuwa na dini nchini humo? Utashangaa kuwa kati ya watuhumiwa wa mauaji hayo wako viongozi wa dini. Je Sudan? Je Kashmir? Je Iraki? Hakuna dini huko? Serikali ya Marekani inayopenda vita kama sijui imechanjiwa au kulaaniwa inaongozwa na watu wasio na dini? Joji Kichaka anasema kila siku lazima asome biblia. Anadai kuwa amempokea bwana. Ameokoka kama vile mwinjilisti Kakobe.
Tuache nchi hizo, twende kule zilikozaliwa dini zinazoitwa "kuu" duniani: uislamu, ukristo, na uyahudi. Twende kule walikotokea manabii wa dini hizi. Kule walikotembea na kufundisha. Twende kule mnakotumia mamilioni ya fedha kwenda kuhiji. Twenda Mashariki ya Kati. Twende Palestina. Twende Yerusalemu. Huko karibu kila mtu ana dini. Kama sio mkristo, basi ni muislamu, kama sio muislamu basi ni myahudi.

Dini moja inafundisha amani na unyenyekevu (uislamu), nyingine upendo (ukristo) na nyingine kushika amri kumi. Twende huko tutazame jinsi ambavyo dini inaleta amani!

Nyooshea kidole nchi yenye amani kutokana na watu wake kuwa na dini. Tazama Indonesia, nchi inayoongoza kwa idadi kubwa ya waislamu, je inaoongoza pia kwa amani? Linganisha Uholanzi na Indonesia. Uholanzi ina watu wengi wasio na habari na masuala ya dini. Nchi hii ina sheria na sera za umma zinazopingana na imani na amri za "dini kuu." Katika nchi hiyo ukahaba ni halali, kutoa mimba, kuvuta lile jani ambalo wakristo na waislamu wanaovuta sigara inayoua mamilioni hudai kuwa linakaa kichwani miaka saba, wagonjwa wanaruhusiwa kumaliza maisha yao iwapo wako katika mateso na hawapona, n.k.
Hivi ikatokea wananchi wa Indonesia ambao ni "wacha mungu" wakaruhusiwa kuhamia Uholanzi ambako kumejaa "makafiri" na sheria za "kikafiri" (kwa mujibu waumini wa kiislamu) unadhani watakubali au watakataa? Je watasema, "Mimi nabaki Indonesia nchi yenye baraka za mungu siwezi kwenda kuishi nchi ya makafiri." Thubutu! Hakutakuwa na ndege za kutosha za kubeba Waindonesia wanaotaka kuhamia Uholanzi. Kwanini? Ningedhani kuwa nchi zenye wacha mungu (yaani waislamu, wakristo, na wayahudi wengi, ndio zingekuwa nchi zenye amani sana na ustawi. Ndio nchi ambazo watu wengi wangekuwa wanataka kwenda kuishi na pia kuiga mifano ya nchi hizo. Lakini wapi! Nchi ambazo watu wengi (ikiwa ni pamoja na wale wanaodai wana dini) wanataka kwenda kuishi na zenye amani ni zile ambazo hazina usongo na mambo ya dini hata kidogo.
Tazama Ufilipino, karibu kila mtu ni mkatoliki, waliobaki ni waislamu. Je wanaongoza kwa upendo aliohubiri Yesu na amani aliyohubiri Muhammad.?
Waislamu neno "amani" wamelifanya kabisa kuwa ni sehemu ya salamu. Asalaam Aleikum. Wayahudi nao neno amani wamefanya kuwa ni sehemu ya salamu. Wanasema: Shalom. Lakini tazama mahusiano ya makundi haya mawili na hizo salamu zao za "amani."
Hivi na kule Kongo hawana dini? Makanisa yanajaa kila jumapili. Ila nchi imejaa damu.

Kwahiyo watu wengi wanaamini kuwa kama binadamu wasingekuwa na dini, wangekuwa watu wabaya na waovu sana. Mimi hujiuliza, binadamu anaweza kuwa mwovu zaidi ya alivyo sasa? Kuna uovu gani uliobakia? Au mnadhani yanayotokea Palestina, Iraki, Sudani, Kongo, yaliyotokea Rwanda, Cambodia, Vietnam, Aghanistan, Ujerumani ya Hitler ni hadithi? Maovu makubwa kabisa kwenye historia tunayoijua yametokea katika kipindi ambacho wanadamu wana hiki kitu mnaiita dini.

Biashara ya utumwa ya Atlantiki miaka zaidi ya 400. Ile ya waarabu ilichukua miaka mingi zaidi maana ilianza kabla hii ya Atlantiki. Mauaji ya wayahudi na Hitler. Bomu la atomiki huko Japani. Ubaguzi wa rangi Marekani na Afrika Kusini. Vita vya Wazungu vya Kwanza na vya Pili (vilihusisha waasia pia kama Japani). Mauaji ya halaiki Rwanda. Ukoloni. Yote haya yamefanyika katika kipindi ambacho wanadamu wengi wanasema kuwa wana dini.

Hivi wezi wanaoiba sirikalini na wengine kuuza nchi hawana dini? Wananchi wenye hasira kali wanaoua binadamu wenzao bila huruma kwa kuwa wamedaiwa kuwa wezi, hawana dini? Wala rushwa na wana magendo, hawana dini?

Najua moja ya hoja inayotolewa ninaposema mambo haya ni hii, "Vita na maovu hayo hayajaletwa na dini." Nakubaliana kwa kiasi fulani. Nasema kwa kiasi fulani kwakuwa historia iko wazi juu ya maovu yaliyoletwa na dini. Ila hata kama maovu hayo hayakuletwa na dini, tunaweza kujiuliza: kama dini inaleta amani iweje mambo hayo yote yanayoharibu amani yatokee? Nikikwambia unipe mfano wa amani iliyoletwa na dini itakuwa kazi ngumu sana kuliko nikikutaka unipe mfano wa maafa yaliyoletwa na dini. Mifano ya dini kuharibu amani na hata tamaduni za jamii mbalimbali imejaa.

Tukichimba zaidi hoja hii tunaweza kwenda kwenye hoja nyingine ambayo sitaiingilia kwa undani. Hoja hiyo ni kuwa huenda watu "wenye dini" ukweli ni kuwa "hawana dini."

Kwa upande mwingine unapochunguza sana kitu tunachoita dini unagundua kuwa dini ni pazia.N Nikizungumzia Waafrika nitasema kuwa dini inakuzuia usimjue mungu wako wala manabii zako.
Hivi wewe na akili zako zote unadhani Afrika nzima haijawahi kuwa na manabii? Kweli jamaa wametupata. Unadhani kabisa manabii wote duniani hakuna aliyetoka miongoni mwa watu wako. Unadhani kabisa bara zima la Afrika halina sehemu takatifu za kuhiji hadi uende Roma au Yerusalemu. Au Makka kwenda kubusu jiwe na kumpiga shetani kwa mawe. Kijijini kwenu pale yako maeneo ya kuhiji lakini kwa jinsi walivyoteka fikra zako hutakaa ujue.

Halafu unajua mtu ukiwa Mwafrika huna haja ya dini hata kidogo. Dini utakuwa nayo pale atakapotokea mtu kuja kukwambia kuwa utamaduni wako haufai. Ukweli ni kuwa tamaduni zetu zinatupa mwongozo kwa kila jambo, yakiwemo masuala ya kiroho na kiimani. Wewe unaweza kuyaita dini. Kwahiyo uafrika una misingi na falsafa yake kuhusu mungu ambaye unaweza kumwamini bila kuwa na dini. Falsafa na miongozo kuhusu mungu iliyoko katika utamaduni wa Mwafrika, kwa mtazamo wangu, vinatosheleza. Hakuna kitu kipya ambacho uislamu, ukristo au uyahudi unaweza kunifundisha. Kwanza amri kumi ambazo ni msingi wa dini hizi zinazoonekana kuwa ni "bora" zaidi ya nyingine zilikuwa Afrika miaka mingi kabla Musa, aliyesema kuwa kapewa mlimani na yehova, hajazaliwa. Ngoja nirudie ili usidhani nimekosea: NINASEMA KUWA AMRI KUMI "ZA MUSA" ZILIKUWEPO AFRIKA KABLA MUSA HAJAZALIWA!
Soma historia.
Sio ile historia unayodanganywa shuleni na walimu waliodanganywa kama wewe mashuleni na vyuo vya ualimu. Tafuta historia yetu. Sijui wewe ulikwenda shule gani, ila shule nilizokwenda mimi asilimia zaidi ya 90 ya historia niliyofundishwa ilikuwa ni uongo mtupu.

Wakati dini yako inakupa amri isemayo, "Mpende jirani yako kama nafsi yako," utamaduni wa Afrika unakupa falsafa hii: Mtu sio mtu bila watu (Kwa Ki-Xhosa, "Umtu Ngumtu Ngabantu). Kwa maneno mengine tunaambiwa tupendane. Falasafa hiyo ndio inakupa itikadi ya ujamaa, falsafa ya harambee, n.k. Marasta wao wanakuja na dhana kama hiyo wanaposema, "I and I." (Bada ya kusema "mimi na wewe," marasta husema, "Mimi na mimi." Kwa kiingereza, "I and I.")
Unadhani kanuni ya mtu sio mtu bila watu imetoka kwa shetani?
Je nimekugusa pabaya?

8/22/2005

Tuzo kwa Waandishi walioko Afrika

Kuna tuzo kadhaa zinazohusu waandishi walioko barani Afrika. Tarehe ya mwisho kuingia katika kinyanganyiro cha tuzo hizi sio mbali. Kwahiyo, hima!
Kwanza kabisa Tume ya Uchumi ya Afrika inakaribisha waandishi kuingia katika mchuano wa Africa Information Society Initiative Media Awards. Kongoli hapa. Halafu jamaa wa GKP wakishirikiana na Panos-London wanatoa tuzo kwa mwandishi atakayetoa kazi nzuri inayoendana na mada hii: Where is the money for bridging the digital divide?"

Mbona Mimi Sikuletewa Shahada Nyumbani?

Labda ningekuwa mgombea urais wa maisha ningetumiwa shahada nyumbani. Mtafiti kanitumia habari hii. Isome mwenyewe.

8/21/2005

Unamfahamu mwanablogu wa Black Looks?

BBC wana habari kuhusu mwanablogu wa Nigeria, Ekine, anayeishi nchini Uhispania. Isome hapa.

Podikasiti ya Kishona

Kuna dada yetu wa Zimbabwe na mumewe muingereza wanafundisha Kishona na tamaduni za Zimbabwe kwa kutumia teknolojia ya podikasiti. Kongoli hapa.

Blogu na Podikasiti barani Afrika

Jamaa wa Balancing Act wana makala kuhusu ziara ya Andy Carvin, , mkurugenzi wa Digital Divide Network nchini Ghana na matumizi ya teknolojia za blogu na podikasiti barani Afrika. Isome hapa.

8/20/2005

Usije ukabaki kujua mambo ya Waarabu na Wayahudi tu!

Ndugu yangu, usije ukabaki kujua tu habari za Waarabu na Wayahudi. Nenda hapa ujifunze mawili, matatu.

Sijui Niende Mashindano ya Madevu...

Mashindano ya kimataifa ya madevu yanafanyika mwezi wa kumi mwaka huu. Kama Osama na Mullah Omari (yule kiongozi wa Talibani mwenye jicho moja) wanakwenda itabidi nisiende maana najua sitaweza kuwashinda. Nitamuuliza Maalim Seif wa CUF kama ana mpango wa kwenda. Nakumbuka wakati Salimin Amour (nimesahau kumwita, Dakta) akiwa rais wa Zanzibar walikuwa wakirushiana madongo na Maalim Seif. Basi Salmin akamwambia Seif akanyoe kwanza madevu kabla ya kuanza kuota kuwa rais wa Zanziba. Maalim Seif akajibu mapigo akasema, "Kwetu wasio na ndefu makazi yao ni jikoni sio ikulu kuongoza nchi!"

Watanzania na Blogu Zao

Nimemaliza kuongeza blogu mpya katika orodha ya blogu za Tanzania katika ukurasa wa Wiki wa mradi wa Sauti za Dunia (Global Voices). Tazama orodha hiyo hapa.

Kumbe hata lugha yao tunaiweza: Blogu mpya ya Kiingereza

Nadhani mwanablogu Idya wa Pambazuko alipokutana na Ethan kwenye mlo wa jioni na pia warsha ya masuala ya blogu wakati alipokuwa (Ethan) kwenye ziara Afrika Kusini ndipo alipoamua rasmi kuwa atablogu pia kwa kiingereza. Ameanza tayari. Mtembelee hapa. Na Ethan ametoa maoni yake hapa kuhusu Idya kublogu kwa kimombo.

8/19/2005

Helsinki Conference 2005: Utandawazi na Demokrasia

Mwaka 2002 serikali za Tanzania na Ufini zilianzisha majadiliano yenye nia ya kufanya wimbi wa utandawazi (yaani utandawizi) kuendana na misingi ya demokrasia (domoghasia au mkumbokrasia kama anayoita Idya). Majadiliano hayo yanaendelea mwezi ujao huko Ufini katika jiji la Helsinki ambapo Rais wa Tanzania wa sasa na ajaye watahudhuria. Nenda hapa.

Teknohama na mabadiliko ya jamii

Teknolojia ya habari na mawasiliano inabadili mambo kila kukicha. Kwa mfano, ile dhana mpya ya "uandishi wa umma" imepanuka. Dhana hii kwa kifupi ni kuwa kutokana na ugunduzi wa zana mpya za habari na mawasiliano, uandishi wa habari umekuwa sio tu kazi ya "waandishi wa habari" bali kila mwananchi mwenye jambo la kusema, kuhoji, kutaarifu, n.k. Sasa hata upigaji picha za kwenye magazeti sio kazi ya wapiga picha waliobobea. Mtu yeyote anaweza kuwa mwandishi wa picha na hata akatengeneza senti. Hata wewe ukitaka unaweza kutengeneza noti kama una jicho la picha. Kongoli hapa.
Mabadiliko mengine ni yale yanayotokea katika gazeti moja kule Seattle ambapo maoni ya mhariri hayaandikiwi tu na wahariri bali yanaandikwa kwa ushirikiano kati ya wahariri na wasomaji. Nenda hapa.

8/16/2005

Mwandishi wa Kenya akataliwa kibali Tanzania

Je uamuzi wa serikali unaweza kuchukuliwa vipi katika mazingira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki? Soma kisa chenyewe hapa.

8/15/2005

Padri Karugendo na makala ya Nyerere Hakuwa Malaika Lakini...

Msomaji Sakour alinitaarifu juu ya kosa katika anuani iliyoko katika makala ya Padri Karugendo. Nilitakiwa kuongeza herufi "c" mwisho wa anuani ya makala yake. Wasomaji wengine wamenitaarifu kuwa bado hawawezi kuisoma. Naiweka tena hapa. Nadhani wote mtaweza kuisoma. Tafadhali kongoli hapa utaisoma.

8/13/2005

Sauti za Dunia zimekuwa za 'kidunia"

Mradi wa Sauti za Dunia (Global Voices) umekuwa wa kidunia. Ethan anatuambia kuwa mradi huu ambao una nia ya kutoa uwanja kwa wanablogu kutoa maoni na kupashana habari bila kupitia ukiritimba na vizingiti vinavyowekwa na dola na tawala za kidhalimu umekua kwa kasi toka ulipoanza miezi saba iliyopita. Kwa kipindi hiki haya yametokea:
- blogu ya mradi huu imetembelewa na watu zaidi ya 7000 kwa siku
- mwezi wa saba pekee ulikuwa na watu robo milioni waliotembelea ukurasa wa Sauti za Dunia
- blogu ya Sauti za Dunia ni kati ya blogu 200 zinazotajwa sana duniani
- blogu hii ilikuwa ni kati ya blogu 100 zilizotajwa kwa wingi kwa mwezi uliopita
- kwa mwezi uliopita wanablogu katika nchi 36 wanaoandika kwa lugha 11 wameelekeza viunganishi kwenye blogu ya mradi huu
Ethan pia anatuambia juu ya chaguo la Yahoo la mradi huu.

Soma aliyoandika Ethan katika blogu yake na pia katika blogu ya Sauti za Dunia.

8/12/2005

Mwanablogu mwingine wa Kiswahili toka Kanada

Jeff Msangi ni Mtanzania anayesoma katika Chuo Kikuu cha York nchini Kanada. Pia ni mwanasafu wa gazeti la Tanzania Daima linalotolewa nchini Tanzania. "Ugonjwa" wa kublogu umemkumba. Kaanza kublogu hapa. Mtembelee na kumkaribisha.

8/09/2005

Uislamu na Ukristo Dini Ipi ya Kweli?

Sijaweka makala zangu muda mrefu. Leo naweka makala mbili mpya. Moja inakuuliza kama uliwahi kukaribishwa kwenye ndoa hizi. Nyingine inatokana na swali ambalo nimeulizwa mara nyingi sana na wasomaji: Je Uislamu na Ukristo Dini Ipi ya Kweli?

8/08/2005

Je Mwanamke ni haki kuendesha swala ya kiislamu?

Ametishiwa kuuawa. Wako watu wanataka kabisa kuondoa uhai wake kutokana na mawazo na fikra zake. Badala ya kupambana naye hoja bin hoja na fikra juu ya fikra baadhi wanaona kuwa dawa ni kumuua. Ulevi wa dini ni ulevi mbaya sana. Unaweza kuondoa kabisa uwezo wa kufikiri. Kama mtu una mawazo tofauti na yangu kwanini nikuue?
Sijui kama umewahi kumsikia Profesa Amina Wadud ambaye anatia hasira sana baadhi ya waislamu kutokana na mawazo yake kuhusu uislamu. Huyu ndiye mwanamama ambaye mwaka 1994 aliongoza swala msikitini nchini Afrika Kusini na mapema mwaka huu aliongoza sala ya kiislamu ndani ya kanisa la kikristo baada ya misikiti mitatu kumkatalia. BBC wana habari kuhusu tukio hilo. Profesa Wadud katika swala hiyo, kama ilivyo kawaida yake, alikuwa akimuita mungu wa kiislamu, Allah, kwa kutumia vijina vya kiume na kike toka lugha ya kiingereza, yaani "He" na "She" maana anaamini kuwa ni kosa kumpa mungu jinsia moja tu yaani ya kiume kama inavyofanywa kwenye uislamu (nami naongeza: hata kwenye kitu kiitwacho ukristo). Na hili ndio tangazo la swala ya kiislamu aliyoendesha kanisani.
Waislamu walimjia juu sana alipohutubia Canada mwanzoni mwa mwaka huu. Hapa anasahihisha baadhi ya yaliyoripotiwa katika habari kuhusu hutba yake hiyo ya Canada.
Profesa Wadud ambaye alizaliwa katika familia ya Kimethodisti na baadaye aliingia katika imani ya Kibudha kwa muda mfupi kabla ya kuingia dini ya waarabu ya kiislamu ni mwalimu wa masuala ya uislamu katika idara ya Falsafa na Dini katika chuo kikuu cha Virgnia Commonwealth. Mwaka 1992 aliandika kitabu hiki hapa. Profesa
Kuna mahojiano yake hapa ambapo kati ya mambo anayosema ni kuwa ni kosa kubwa ya "sharia" ambayo imetokana na mfumo dume kuongelea masuala ya wanawake wakati ambapo wanawake hawakuhusishwa katika kuunda vipengele hivyo vya sharia vinavyowahusu. Pia unaweza kusoma mawazo yake zaidi na kutazama na video yake hapa. Kuna hutba yake nyingine hapa kuhusu Maandiko, Jinsia, na Mageuzi katika Uislamu.
Soma zaidi juu ya tafsiri tofauti ndani ya uislamu juu ya wanawake kuongoza swala kama maimamu.

8/07/2005

Esther naye na blogu ya kiingereza

Esther anablogu kwa kimombo toka Dasalama. Mtembelee na kumpa maneno mawili matatu ya kumkaribisha.

Florence anablogu kwa Kiswahili na kiingereza

Kuna mwanablogu mpya (kaanza mwezi uliopita) toka Dasalama. Anablogu kwa Kiswahili na kiingereza. Mtembelee na kumkaribisha kwenye ulimwengu wa blogu.

8/06/2005

Mwanablogu Mpya toka Dodoma

Kivale ni mwanablogu mpya toka "mji mkuu" Dodoma ambaye anatuambia kuwa masikini hafilisiki, ila akipata...

Narekebisha viunganishi vya makala zangu na Freddy

Nafanya marekebisho ya viungo vya makala zangu na Freddy Macha kwani havifunguki. Samahanini.

Wananchi walipokagua silaha za maangamizi za Marekani

Wakati natembelea tovuti ya shirika la Grace nimekutana na habari hii kuhusu wananchi wa Marekani na Canada waliojiunga ili kufanya ukaguzi, kama ule uliokuwa ukifanywa na wakaguzi wa Umoja wa Mataifa na mashushushu wa Marekani kule Iraki, wa silaha za maangamizi.

Nyama, Nyama, Nyama...

Tazama sinema hii ya Meatrix juu ya nyama zinazouzwa kwenye migahawa ya vyakula vya papo na hapo na ile ya mlolongo. Jamaa waliotengeneza filamu hii kwa ajili ya shirika la GRACE pia wana sinema nyingine iitwayo Store Wars.

Padri Karugendo na Nyerere Hakuwa Malaika

Msomaji Sakour Soud kanitaarifu kuwa nilikosea anuani ya makala ya Padri Karugendo iitwayo Nyerere Hakuwa Malaika Lakini.... Nimerekebisha.

8/04/2005

Barua Toka Kwa Mchungaji

Nimeandikiwa barua hii toka kwa mchungaji (au ni mwinjilisti?). Anajijua. Niliandikiwa nilipokuwa nimetupa mkono blogu. Isome kisha cheka:

Barua toka kwa mchungaji
Rudi kundini angalau tujue u mzima au vipi. Tutakutenga sasa na hatutakulisha chakula cha bwana mpaka utakapoanza tena kutoa sadaka ya ahadi. Nakukumbusha pia kama hutoi ahadi mtoto wako hatabarikiwa wala hatutambatiza. nakukumbusha pia kwamba mwaka jana hukutimiza ahadi yako uliahidi 20,000 ukatoa 15 ujue kuna deni la sivyo hutapata huduma za kiroho. Mwaka huu hujajaza fomu ya ahadi pia ni lazima uahidi utatupa ngapi ili tuweke kwenye mahesabu yetu. Nakukumbusha pia tarehe 34/13/28910 kutakuwa na sadaka ya mavuno safari hii ujue ni kahawa kwani miezi iliyopita kulikuwa na sadaka ya mavuno ya mahindi. Usijali sana kama huna kahawa utaweza pia kutuletea chochote hasa mahindi kwa sababu ndizi hazina bei. Pia tunakumbusha umuhimu wa kutoa noti kanisani kama sadaka kwani hizi shilingi zinakuwa nzito sana halafu zinatoboa mifuko. Tatizo jingine ni kwamba shilingi zinapoteza muda wa wazee wa kanisa kuhesabu.
Mungu wa Yakobo Isaka na Ibrahim akubariki uingiapo na utokapo sasa na hata milele hasa utakapokuwa umetimiza sadaka yako ya ahadi na mavuno.
Wako Mchungaji wa Usharika

Ulijua Mwanablogu alitiwa ndani huko Iraki?

Sijui kama habari hii uliipata au ilikupita. Mwanablogu wa blogu wa Secrets in Baghdad alitiwa ndani na baadaye kuachiliwa huru.

Padri Karugendo anasema Nyerere hakuwa malaika lakini...

Naanza kupandisha makala za Padri Karugendo. Msome akisema Mwalimu Nyerere Hakuwa Malaika Lakini..., kisha anaandika Rais Huchaguliwa na Mungu Lakini..., halafu anaandika kuhusu kitabu kilichozua utata mkubwa The Da Vinci Code, anazungumzia uchaguzi mkuu (mimi nauita wizi mkuu) kwa kusema Tuseme Ukweli, pia anazungumzia uongozi wa Mkapa kwenye Kaini na Abeli na anamalizia leo kwa kuuliza Hivi Kazi za Mbunge ni Zipi? Haya faidi uhondo.

Nenda hapa kama utapenda kusoma zaidi juu ya kitabu anachozungumzia Padri Karugendo cha Da Vinci Code. Huyu ndiye mwandishi wa kitabu hicho.

Nilikuwa nasema nini tena?

Wiki hii ndio kumbukumbu ya unyama wa Marekani dhidi ya wakazi wa Hiroshima na Nagasaki. Hapo mwaka 1945 Marekani ilikuwa taifa la kwanza na pekee kutumia silaha za maangamizi dhidi ya raia wasio na hatia yoyote dhidi ya nchi hii. Mabomu ya atomiki yaliangushwa na kuua wengi na mionzi ya sumu kuathiri hata wale ambao walikuja kuzaliwa baadaye.

Nimesikia mahojiano, ingawa dakika za mwisho, katika redio ya
NPR, ya mmoja wa marubani waliorusha madege yaliyoangusha mabomu hayo. Bwana huyo anasema kuwa hajuti hata kidogo na wala hakosi usingizi. Anasema kuwa anaamini kabisa kuwa uamuzi wa kuangusha mabomu hayo ulikuwa ni sahihi kwani baada ya unyama huo vita wanavyoita vya dunia visingemalizika.

Historia hii ya matumizi ya silaha za maangamizi huko Japani ni muhimu sana katika kipindi hiki ambacho Marekani inaambia nchi kadhaa duniani kuwa hazina haki ya kuwa na silaha za nyuklia, sumu, na baiolojia. Wakati Marekani ndio nchi pekee ambayo imetumia silaha hizo dhidi ya nchi nyingine na ndio nchi yenye silaha nyingi na hatari kabisa kuliko nchi yoyote duniani, imesimama kidete kama vile haina mshipa wa aibu kutaka nchi kama Korea ya Kaskazini na Iran zisiwe na silaha hizo.

Unaona uchaguzi wa Irani hivi majuzi.
Rais mpya wa Irani amechaguliwa kwasababu ya Marekani. Marekani haimpendi lakini ajabu ni kuwa Marekani hiyo ndio ilimpa Urais. Wairani hawataki nchi nyingine eti ijipe haki ya kuiambia nchi yao ifanye nini na nini isifanye. Hivyo wako waliopiga kura kuchagua mtu ambaye ambaye siasa zake ni za kuiambia Marekani, “Nendeni kuzimu.”

Nani kaipa Marekani hiyo haki ya kuamua nchi zipi zina haki ya kuwa na silaha kali kama za nyuklia? Kwanini Marekani iwe na haki ya kuwa na silaha hizo lakini sio Irani au Korea ya Kaskazini? Ukimuuliza yule bwana wa Texas anayejifanya kuwa ni kma mtume Paulo, yaani katumwa na Yesu, Joji mwana wa Kichaka maswali haya atakwambia kuwa Marekani ina mfumo wa kidemokrasia kwahiyo ni sawa nchi hii ikiwa na silaha hizo ila nchi kama Korea ya Kaskazini na Irani zina madikteta vichaa ambao wanaweza kuanamiza dunia.

Mpige kofi na swali hili: Je sio Marekani hiyo unayodai kuwa ni nchi ya kidemokrasia ambayo ndio katika historia imetumia silaha mbaya kabisa dhidi ya raia ilipoangusha mabomu ya atomiki? Muulize hivi mfumo wa utawala wa Pakistani ni bora zaidi ya ule wa Irani? Maana unaona Pakistani ina silaha za nyuklia lakini Marekani imefunga domo. Ni kitu gani kinaipa Pakistani alama ya vema ya kuwa na silaha hizo ila sio Irani? Na kwanini zile nchi ambazo hazitaki kuwasikilizeni ndio ambazo hazina haki ya kuwa na silaha hizo ila nchi vibaraka wenu ndio zina haki hiyo?

Kwanza kwanini, bado umemkalisha Joji kiti moto, nchi yenu isiongoze vuguvugu la kidunia la kujenga dunia mpya isiyo na silaha za maagamizi hata kidogo? Na ukitaka kupata utamu wa majibu ya maswali haya usimruhusu Joji aulize wasaidizi wake majibu. Mwambie hakuna “kudesa.” Atoe majibu kichwani mwake mambo ya “kuangalizia” ni ya darasa la pili na la tatu!
Sijui ni lini Marekani itajifunza. Katika historia yake imetoa maamuzi mengi sana yenye madhara makubwa kwake na dunia nzima lakini haijifunzi. Walipokuwa wanakula sahani moja na akina Osama na jamaa wenye madevu wa Talibani walikuwa sijui wanafikiria nini. Ikaja Septemba 11, yaani 911 kama namba ya simu ya kuita manjagu hapa. Sasa tunaona yale madrasa yaliyojengwa na kuendeshwa na Matalibani yanamepeleka majonzi Uingereza. Kule Iraki ndio sijui wanafanya nini. Jana askari 14 wa Marekani wameuawa wakati Joji anadai kuwa nchi hiyo iko tayari kushughulikia suala la ulinzi na amani peke yake. Yaani wamekwenda kuibadili Iraki toka kuwa nchi hadi kuwa chuo cha mafunzo ya ugaidi. Nadhani Osama sasa anahamishahamisha vitu vyake kuelekea Iraki. Huko ndio hawa jamaa wanaona kuna utamu. Ndio jikoni.

Tuache hiyo, jinsi ambavyo siasa za Marekani zilitengeneza mazingira ya Talibani kutawala Afghanistani na kutumia sharia kali za kukata watu vichwa katika viwanja vya mpira...yaani kama watu wanavyokwenda uwanjani kumtazama Beckham akipiga krosi, kule Afghanistani watu walikuwa wanakwenda viwanjani kutazama watu wakikatwa vichwa. Sasa Iraki nako utawala kama wa Talibani umejitokeza kwenye miji kadhaa kama Basra. Na kwakuwa miji yenye utawala kama wa Talibani ina amani kiasi, Marekani imeamua kukaa kimya. Ifanyeje? Haijui cha kufanya.

Leo ni kati ya zile siku ambazo ninaanza kuandika jambo nikifika huku chini nakuwa nimesahau kuwa nilikuwa nataka hasa kusema nini. Na kwakuwa nina mambo kadhaa ya kufanya, sitaki kurudi kule juu kuanza kusoma upya. Nadhani mtanielewa ninasema nini.

Mkutano wa BlogHer

Mkutano ule wa Blogher ambao nilikuwa niende ila sikuweza ni hapa. Tazama mkono wa kushoto upate undani wa mkutano toka kwa waliohudhuria.

Ukipewa zawadi ya kanga lazima uivae?

Msomaji Oscar Munishi kanichekesha sana. Kaniachia ujumbe hapa bloguni kufuatia niliyoandika jana kuhusu Kikwete ambaye ni muislamu kupewa biblia ili aongoze Tanzania. Mifano ya Munishi imenipendeza na nimeamua niiweke hapa kwani unaweza ukawa hujasoma maoni yake. Siweki kila alilosema naweka mifano yake miwili. Ninadhani anamaanisha kuwa Kikwete kupewa biblia inaweza kuwa ni jambo la mfano tu, hiyo biblia huenda ikakusanya vumbi bila kutumiwa. Huyu ndio Oscar Munishi:
mr ndesanjo nikikupa zawadi ya kanga leo je wewe ni lazima uivae? nikikupa panga leo kwani nimekuambia utumie kuchinja nalo watu au ukatie kuni? au ni lazima ulitumie?

8/03/2005

Unaweza kutumia biblia kuongoza Tanzania?

Kuna ndoa ambayo ilifungwa muda mrefu kidogo. Hii ni kati ya matajiri wachache na wanasiasa nchini Tanzania. Huenda hukualikwa. Ukiacha ndoa hii, kuna nyingine ambayo inaanza kuiva. Hii ni ndoa kati ya viongozi wa dini wanaojiitwa au kuitwa na baadhi ya watu "watumishi wa mungu" na wanasiasa.
Kawaida, matajiri wakiunga mkono upinzani, basi ujue wako tayari kuingia matatani na sirikali na hatimaye kufilisika. Watachunguzwa kama wanalipa kodi. Leseni na biashara zao zitapigwa tochi na mambo kama hayo. Viongozi wa dini za kuazima wakiunga mkono viongozi wa upinzani, utasikia viongozi toka yule wa juu kabisa anayekula sahani moja na wakoloni kama Blair wakisema kuwa viongozi wa dini wasichanganye dini na siasa.
Lakini viongozi hawa wa dini na pia matajiri wakiwaunga wao mkono, mmh...kimya!
Sasa tumeona jinsi viongozi wa dini wanasimama mbele ya waumini wakidai kuwa Kikwete ameteuliwa na mungu. Sijui mungu wameongea naye lini. Kutokana na kuteuliwa huko na mungu wameamua kumpigia kampeni na wengine kumchangia fedha wakati yuko kwenye serikali na chama chenye mali. Kali ni kuwa wanampa biblia ili atumie kuongoza ingawa yeye ni muislamu. Biblia waliyompa inasema kuwa Yesu alisulubiwa wakati Kurani yake inamwambia kuwa hakusulubiwa.
Tuache hilo. Tujiulize: hivi anaweza kutumia biblia kuongoza Tanzania? Biblia inasema, "Mimi ni bwana mungu wako usiwe na miungu wengine ila mimi." Hakuna katikati. Ama umchague Yehova au uende motoni. Katiba ya Tanzania inasema kuwa kila mtu ana haki ya kuabudu chochote atakacho. Sasa sijui "watumishi" hawa wa mungu wanataka Kikwete aongoze vipi kwa kutumia vitabu hivi viwili ambavyo vinapingana kabisa.
Sio hilo tu. Ina maana kama atatumia biblia kuongoza, basi itabidi asukume bunge lipitishe sheria ya kufanya amri kumi kuwa ni sehemu ya sheria za nchi. Kwa maana hiyo kumtamani mke wa mwenzio, kuzini, kutoikumbuka siku ya sabato, kumshuhudia mwenzako uongo, kutomwamini mungu mmoja wa waisraeli (ingawa sisi ni Watanzania!), n.k. itakuwa ni kosa la jinai. Itabidi wanawake wasiwe wabunge au walimu maana biblia inakataza wanawake kusimama mbele ya wanaume, au wakiwa wabunge labda wawe na chumba chao wenyewe na wakiwa walimu labda wawe wanafundisha tu wanawake. Itabidi wanawake walazimishwe kufunika vichwa kama mtume Paulo alivyofundisha. Itabidi makasino yote yafungwe maana kamari ni kinyume na neno la bwana. Itabidi nguruwe ipigwe marufuku maana biblia inasema kuwa ni kinyume na mapenzi ya mungu kumla mnyama huyu...hapana, nadhani hili lina utata maana tunaambiwa kuwa katazo hilo liko kwenye agano wanaliita la kale!
Naandika makala kuhusu ndoa hii kwa ajili ya safu ya jumapili hii kule nyumbani. Ngoja niendelee.

Sikiliza Sauti ya Amerika Jumamosi hii

Leo asubuhi nimefanya mahojiano mafupi na Abdulshakur Aboud wa Sauti ya Amerika (Voice of America) kuhusu teknolojia ya blogu. Mahojiano hayo yatarushwa jumamosi katika kipindi cha maswali na majibu. Unaweza kusikiliza kupitia intanet.

Msomaji Anahoji Kifo cha Garang

Msomaji mmoja (nimemwandikia kumuuliza kama ni sawa nikimtaja jina, kwa sasa sitamtaja), kaniandikia akiuliza maswali kadhaa kufuatia kifo cha Yohana Garang. Ninaweka waraka wake bila kuhariri chochote:

Ndio brother ni siku nyingi hatujawasiliana, umri wangu siyo mkubwa sana ni wakati, na katika kipndi chote hicho nimesha shuhudia (kwa kusikia) vifo vya viongozi wengi na watu wengi maarufu, lakini hakuna kifo kilicho nisikitisha kama cha huyu Mzalendo. Na kwambia bro, huyu ndio Mzalendo wa mwisho katika Afrika aliye baki. Sitaki nizidi kuongea mengi juu yake ilakuna jambo moja nataka unisaidie kufafanua katika makala zako ili na wengine wapate faida,
Bro, nilipo sikia kifo chake, sikuweza kupata usingizi usiku nilikaa na kufikiri usiku kucha,
kwa nini vifo karibu vyote vya viongozi wazalendo wa kiafrika vinahusisha Ajali ya ndege hasa isiyo kuwa na sababu za msingi 'Freak Accident'? ukianzia Samora Michel, Habyarimana na mwenzake yule wa Burundi cypriane Ntayaramira? wakitokea Tanzania kwenye Mkutano,

Samora yeye alitoka kwenye mkutano pia Lusaka, Na huyu tunaambiwa naye alitoka kwenye mkuatano Uganda, Je, hapo kuna kosa mkono wa mtu kweli? Hizo ndege zinazotengenezwa ulaya wanazo tumia Viongozi wetu zina usalama kweli?, najaribu kuwaza kwamba Wazungu walivyo wajanja hawawezi kufunga kamtambo kwenye hiyo ndege wakawa na uwezo wakukikontroli kule kwao wakitaka ianguke wanabonyezatu, Au bro, hii nibiashara maana wazungu walimtumia na kumsaidia sana Savimbi kwa miaka mingi baadae naona walimchoka wakampiga risasi,charlse taylor, Kabila,Osama, Saddam, orodha ni ndefu, sasa wa me amua kumchoka GARANG, naona kunamaslahi fulani wanapata,wakisha mtumia hawataki kuendelea nae tena, walikuwa wanafanya nae siasa sasa wanataka mtu mwingine wa kufanya nae biashara. bro, sorry , kwa barua hii ndefu, naomba ukae ufikirie utanielimisha zaidi katika makala zako, UJUMBE ITABIDI TUBORESHA USAFIRI WETU WA UNGO!!

8/02/2005

Nguvu Mpya, Mtazamo Ule Ule

Haya nimerudi. Nguvu mpya, mtazamo ule ule. Katika kipindi hiki cha ukimya nimefanya mambo kadhaa. Kati ya niliyofanya nimesoma kitabu kitwacho You Are Being Lied To : The Disinformation Guide to Media Distortion, Historical Whitewashes, and Cultural Myths. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa makala za watu mbalimbali zilizohaririwa na Russ Kick wa kampuni ya Disinformation. Kuna makala moja iliyoandikwa na David Thomas, The Bible Code: Scientific, Statistical Proof of God? Or Just Another Lie? Makala hii inatokana na kitabu kilichopigiwa makofi sana na wakristo wenye msimamo mkali kiitwacho The Bible Code. Kitabu hiki kilichotolewa mwaka 1997 na mwandishi wa habari Michael Drosnin kinadai kuwa ndani ya Biblia kuna ujumbe wa siri. Unaweza kujua ujumbe huu kwa kuunganisha herufi na namba kadha wa kadha. Mwandishi David Thomas kwenye kitabu cha You are Being Lied To anasema kuwa kwa kutumia kanuni iliyotumiwa kudai kuwa Biblia ina ujumbe wa siri unaotabiri dunia ya kesho hatakuwa amekosea akisema kuwa hata vitabu kama War and Peace cha Tolstoy, Origin of Species, na Kurani vina ujumbe wa siri kwa wanadamu. Kwa kutumia kanuni za mahesabu alizotumia Drosnin kuandika kitabu chake cha The Bible Code utapata ujumbe kama alioupata kwenye biblia kwenye vitabu hivi. Sio vitabu hivyo tu vina “bible code” bali pia aliweza kupata ujumbe wa siri kwenye maoni ya mhariri ya gazeti la the Chicago Tribune na Unabomber Manifesto ya Ted Kaczynski. Soma hapa kwa habari zaidi kuhusu dhana ya "bible code."

Lakini sehemu niliyoisoma na kushukuru mababu kuwa mbavu zangu ziko salama ni mahojiano kati ya Russ Kick na “Baba Mtakatifu” wa watu wasioamini kuwa kuna mungu, Warren Allen Smith. Mahojiano haya yalihusu kitabu alichoandika Warren Smith kiitwacho Who is Who in Hell. Smith anaonyesha jinsi dunia yetu ilivyojaa vitu kama vitabu, majengo, teknolojia, picha, vituo vya luninga, muziki, n.k. vilivyotokana na kazi za watu wasiomwamini mungu. Anasema kuwa kama unaamini kuwa watu wasiomwamini mungu ni makafiri na mashetani basi usitumie Intaneti, Hotmail, Microsoft Word, Internet Explorer maana vyote hivi vimetokana na “makafiri” wasiomwamini mungu. Pia usitazame CNN au sinema kama The Godfather, Jurassic Park, Chinatown, usiingie katika majengo yaliyobuniwa na mbunifu maarufu wa majengo duniani Frank Wright, usitazame michoro ya Picasso, Frida Kahlo, usisikilize miziki ya R.E.M, Mozart, Beatles, Beethoven, Barry Manilow, n.k., usitumie “pasteurized milk” (maziwa ya mtindi ya kwenye makopo), usitumie huduma za shirika la Msalaba Mwekundu, usisome vitabu kama The Great Gatsby, Robinson Crusoe, Oliver Twist, A Tale of Two Cities, Moby Dick, The Three Musketeers, The Grapes of Wrath, The Color Purple…kazi/vitu vyote hivi vimetokana/milikiwa na watu wasio na dini au kuamini mungu.

Nimekuwa pia nikisikiliza CD ya Fight to Win ya Femi Kuti. Wimbo uitwao ’97 umenihuzunisha kiasi maana anaimba juu ya kifo cha baba yake, Fela, na dada yake ‘Sola. Anakumbuka jinsi maelfu ya watu walivyotembea kwa masaa saba (kutokana na kujaa watu) kwenda kupumzisha roho wa Fela katika nyumba ya Eledumare. Katika wimbo mwingine anasema kuwa watawala wa Afrika ambao wanaiharibu na kuua watu huku wakiwatumikia wazungu lazima tuwatambue kwa jina lao halisi: Wasaliti wa Afrika.

Na wasaliti wa Afrika ndio nitakuwa nawazungumzia sana. Hasa nitakapokuwa nikiandika kuhusu ule mchezo wa kuigiza niliohudhuria kule Uskoti na maendelezo ya mchezo huo. Pia tutakavyokuwa tukikaribia Wizi Mkuu Tanzania hapo Oktoba tutakapotakiwa kuchagua “mwizi huyu au yule.”

Na hivi jamani
John Garang, helikopta ile ilianguka kwa matatizo ya hali ya hewa au ilitunguliwa?
Haya. Nina barua pepe elfu kumi kidogo za kusoma na kujibu. Makala za kuandika na nyingine mpya za kupandisha. Pia makala mpya za padri Karugendo. Na mapitio ya blogu za Kiswahili kwa ajili ya Global Voices. Bila kusahau makala na vipande toka mchezo wa kuigiza wa wakuu wa makuhani wa ubepari, yaani G8, na uzoefu wa kublogu wa waandishi wengine toka Afrika kupitia Panos.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com