8/03/2005

Unaweza kutumia biblia kuongoza Tanzania?

Kuna ndoa ambayo ilifungwa muda mrefu kidogo. Hii ni kati ya matajiri wachache na wanasiasa nchini Tanzania. Huenda hukualikwa. Ukiacha ndoa hii, kuna nyingine ambayo inaanza kuiva. Hii ni ndoa kati ya viongozi wa dini wanaojiitwa au kuitwa na baadhi ya watu "watumishi wa mungu" na wanasiasa.
Kawaida, matajiri wakiunga mkono upinzani, basi ujue wako tayari kuingia matatani na sirikali na hatimaye kufilisika. Watachunguzwa kama wanalipa kodi. Leseni na biashara zao zitapigwa tochi na mambo kama hayo. Viongozi wa dini za kuazima wakiunga mkono viongozi wa upinzani, utasikia viongozi toka yule wa juu kabisa anayekula sahani moja na wakoloni kama Blair wakisema kuwa viongozi wa dini wasichanganye dini na siasa.
Lakini viongozi hawa wa dini na pia matajiri wakiwaunga wao mkono, mmh...kimya!
Sasa tumeona jinsi viongozi wa dini wanasimama mbele ya waumini wakidai kuwa Kikwete ameteuliwa na mungu. Sijui mungu wameongea naye lini. Kutokana na kuteuliwa huko na mungu wameamua kumpigia kampeni na wengine kumchangia fedha wakati yuko kwenye serikali na chama chenye mali. Kali ni kuwa wanampa biblia ili atumie kuongoza ingawa yeye ni muislamu. Biblia waliyompa inasema kuwa Yesu alisulubiwa wakati Kurani yake inamwambia kuwa hakusulubiwa.
Tuache hilo. Tujiulize: hivi anaweza kutumia biblia kuongoza Tanzania? Biblia inasema, "Mimi ni bwana mungu wako usiwe na miungu wengine ila mimi." Hakuna katikati. Ama umchague Yehova au uende motoni. Katiba ya Tanzania inasema kuwa kila mtu ana haki ya kuabudu chochote atakacho. Sasa sijui "watumishi" hawa wa mungu wanataka Kikwete aongoze vipi kwa kutumia vitabu hivi viwili ambavyo vinapingana kabisa.
Sio hilo tu. Ina maana kama atatumia biblia kuongoza, basi itabidi asukume bunge lipitishe sheria ya kufanya amri kumi kuwa ni sehemu ya sheria za nchi. Kwa maana hiyo kumtamani mke wa mwenzio, kuzini, kutoikumbuka siku ya sabato, kumshuhudia mwenzako uongo, kutomwamini mungu mmoja wa waisraeli (ingawa sisi ni Watanzania!), n.k. itakuwa ni kosa la jinai. Itabidi wanawake wasiwe wabunge au walimu maana biblia inakataza wanawake kusimama mbele ya wanaume, au wakiwa wabunge labda wawe na chumba chao wenyewe na wakiwa walimu labda wawe wanafundisha tu wanawake. Itabidi wanawake walazimishwe kufunika vichwa kama mtume Paulo alivyofundisha. Itabidi makasino yote yafungwe maana kamari ni kinyume na neno la bwana. Itabidi nguruwe ipigwe marufuku maana biblia inasema kuwa ni kinyume na mapenzi ya mungu kumla mnyama huyu...hapana, nadhani hili lina utata maana tunaambiwa kuwa katazo hilo liko kwenye agano wanaliita la kale!
Naandika makala kuhusu ndoa hii kwa ajili ya safu ya jumapili hii kule nyumbani. Ngoja niendelee.

1 Maoni Yako:

At 8/04/2005 12:20:00 AM, Anonymous oscar munishi said...

kaka kwanza hongera sana kwa upembuzi wako,sijui unayaandika haya ili kuwafanya watu wafikirie mambo hayo kwa undani au ni kuwachanganya walengwa.
mr ndesanjo nikikupa zawadi ya kanga leo je wewe ni lazima uivae?
nikikupa panga leo kwani nimekuambia utumie kuchinja nalo watu au ukatie kuni?au ni lazima ulitumie?
mr ndesanjo je nikisema nahakika wewe ni mjamaika kwa sababu ya rasta je ni lazima wewe uwe mjamaika? je unajua sababu nyingine ya kunifanya mimi nikuite mjamaika?
japokua viongozi hawa wanayasema haya hayamaanishi ni kweli! na inawezekana pia ni kweli! mimi na wewe hatujui ila msemaji ndio anajua.
tuna uhuru wa kusema kila tujisikialo ila tu tusiende kinyume na shera za nchi yetu, na Mtanzania ana haki ya kusikilizakila jambo na anatakiwa atafakari kila jambo na ndio maana aliyesema hayo hakuwalazimisha watu kuamini hayo.Na kuumpa Kikwete Biblia haimaanishi kuwa aisome na aitumie!
Hata chuoni tunapewa fedha za vitabu likini sio wanafunzi wote watumizo fedha hizo kununua vitabu.
hayo machache yanatokana na upeo wangu mdogo kaka natumai utajaribu kuchambua kwa kina zaidi na kujaribu kugusia hasara ya dini kuongelea siasa kwani siasa mbovu pia pia itakua na hasara moja kwa moja kwao,labda mi nawe tunatakiwa kujua didi si kisiwa kwamba siasa ipo mbali na dini ipo mbali.

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com