8/23/2005

Mungu Bila Dini, Dini Bila Mungu...

Muda mrefu sijaongea kirefu kuhusu masuala mbalimbali ya kusafisha fikra zetu. Soma. Kama nimekugusa pabaya, hiyo sio nia yangu.
***************************************************************************
Haiwezekani!
Waakujia juu, "Haiwezekani!"
Haiwezekani. Kivipi.
Hawatakubali. Mishipa itawatoka.
Maswali watakurushia. Mate yatakurukia.
Utashangaa, iweje hawaelewi jambo rahisi namna hii?
"Haiwezekani mtu asiwe na dini!" Watakwambia huku wakijiweka tayari kwa ubishi.
Ubishi.
Wanabisha jambo linalohusu nafsi na imani yako.
Wewe unawaambia kuwa nafsini mwako huamini kitu kinachoitwa dini. Huna dini, sio muislamu wala mkristo (maana dini kwao ni hizi mbili tu).
Wanakataa. Haiwezekani. Kila binadamu ana dini.
"Hawezekani kivipi wakati mimi ni binadamu na sina dini?" Unawauliza.
Wanajibu, "Acha kutuhadaa, kila binadamu ana dini. Ina maana huamini kuwa kuna mungu?"
Wakiuliza swali hili lazima nicheke kwanza.
Swali hilo hufuatwa na maswali mengine mawili:
"Sasa ina maana ukifa utazikwaje?"
Swali la pili, "Sasa ukifa utakwenda wapi?"
Mahesabu ya imani za watu hawa yako hivi (Idya, kama nimekosea mahesabu nisahihishe):
binadamu + dini = imani juu ya mungu (yaani mungu yupo)
binadamu - dini = mungu hayupo

Hawajui kuna tofauti kubwa sana kati ya dini na kumwamini mungu. Wakati wengi wetu tunadhani kuwa dini kazi yake ni kutufanya tumjue mungu, kumwamini na kumtii, ukweli ni kuwa dini nyingi zinatuwekea ukuta wa chuma usionekana ambao unatuzuia tusimjue mungu. Ukiwa hutaki kumjua mungu au unataka kudhani kuwa unamjua, nitakushauri uwe na dini.
Najua sentenso hiyo ya mwisho inaweza kukufanya ujiulize kama "zimenitoka" au bado "zipo."

Dini inakufanya umjue mungu kupitia mawazo na mitazamo ya watu wengine (karibu wote ni wanaume) ambao wanavaa kanzu na majoho wakiongea kwa utaratibu ili uone kuwa wana tofauti sana na wewe na kuwa wana ukaribu na mungu. Wengine hudiriki kutuambia kuwa huongea na mungu. Ila ukiwaambia wakuite saa wanaongea naye ili usikilize au kushiriki, watakwambia kuwa kama huna roho safi huwezi kuongea naye. Lakini ninaposoma busara za Yeshua (Yesu/Isa) nakuta akisema kuwa mungu anatafuta wale waliopotea. Wale wasio na "roho safi." Na ndio maana Yeshua alikuwa akishinda vijiweni na wacheza kamari na wachakaramu wengine. Miyahudi ikamjia juu, "He, wewe mbona unajumika na wenye dhambi?"
Unajua aliwajibu nini? Kasome kitabu unachoamini kuwa ndio ramani na dira yako hapa dunini ingawa kinakusanya vumbi sebuleni kwako ulikokiweka kama mapambo. Kila siku unahangaika na magazeti ya ushambenga lakini kitabu unachodai kimeandikwa na mungu mwenyewe hukisomi...
Turudi kwenye hoja ya msingi.

Kwahiyo unachojua kuhusu dini ni mawazo ya viongozi wa dini yako. Mawazo ya binadamu wengine kama wewe. Mawazo yao hayo ndio yanakuwa dira yako wewe ambaye una akili na uwezo wa kujitafutia ukweli mwenyewe. Viongozi hawa, wakati mwingine, kama hawajui jambo wanapenda kukwambia kuwa jambo hilo ni "fumbo takatifu." Waulize kuhusu tungo ya utatu. Watakwambia hilo ni fumbo. Yaani mungu wako anakufumbia baadhi ya mambo. Hataki uyajue!
Dini inakufanya uwe mvivu. Hutasoma biblia au kurani kwasababu kuna viongozi wa dini yako ambao kazi yao ni kusoma vitabu hivyo na kukutafsiria mara moja kwa juma. Au wakati mwingine mara moja au mbili kwa mwaka iwapo wewe ni wale wanaoenda kanisani misa za usiku au siku ya krisimasi.

Dini inakufanya udhani kuwa kuna mashindano kati yako wewe mkristo wa kilutheri na mkristo wa kiangikana, au shahidi wa yehova dhidi ya mkatoliki, au mashindano kati ya muislamu wa sunni na yule wa shia, au mashindano kati ya muislamu na mkristo...mashindano ya kwenda mbinguni. Dini inakufanya uamini kuwa watu wote wasio na imani kama yako watakwenda unakoita motoni. Wewe na wenzako ndio mnajua hiyo njia nyembamba iliyozungukwa na malaika weupe (ndio malaika weupe, hakuna mweusi) wenye mavazi meupe ya kuelekea kwenye uzima wa milele. Pengine ndio maana tunajichubua ili tufanane na hao malaika.

Kuna watu ambao huniambia kuwa dini huleta amani. Hivi ina maana kule Rwanda kulipotokea mauaji ya halaiki Warwanda hawakuwa na dini? Au hakukuwa na dini nchini humo? Utashangaa kuwa kati ya watuhumiwa wa mauaji hayo wako viongozi wa dini. Je Sudan? Je Kashmir? Je Iraki? Hakuna dini huko? Serikali ya Marekani inayopenda vita kama sijui imechanjiwa au kulaaniwa inaongozwa na watu wasio na dini? Joji Kichaka anasema kila siku lazima asome biblia. Anadai kuwa amempokea bwana. Ameokoka kama vile mwinjilisti Kakobe.
Tuache nchi hizo, twende kule zilikozaliwa dini zinazoitwa "kuu" duniani: uislamu, ukristo, na uyahudi. Twende kule walikotokea manabii wa dini hizi. Kule walikotembea na kufundisha. Twende kule mnakotumia mamilioni ya fedha kwenda kuhiji. Twenda Mashariki ya Kati. Twende Palestina. Twende Yerusalemu. Huko karibu kila mtu ana dini. Kama sio mkristo, basi ni muislamu, kama sio muislamu basi ni myahudi.

Dini moja inafundisha amani na unyenyekevu (uislamu), nyingine upendo (ukristo) na nyingine kushika amri kumi. Twende huko tutazame jinsi ambavyo dini inaleta amani!

Nyooshea kidole nchi yenye amani kutokana na watu wake kuwa na dini. Tazama Indonesia, nchi inayoongoza kwa idadi kubwa ya waislamu, je inaoongoza pia kwa amani? Linganisha Uholanzi na Indonesia. Uholanzi ina watu wengi wasio na habari na masuala ya dini. Nchi hii ina sheria na sera za umma zinazopingana na imani na amri za "dini kuu." Katika nchi hiyo ukahaba ni halali, kutoa mimba, kuvuta lile jani ambalo wakristo na waislamu wanaovuta sigara inayoua mamilioni hudai kuwa linakaa kichwani miaka saba, wagonjwa wanaruhusiwa kumaliza maisha yao iwapo wako katika mateso na hawapona, n.k.
Hivi ikatokea wananchi wa Indonesia ambao ni "wacha mungu" wakaruhusiwa kuhamia Uholanzi ambako kumejaa "makafiri" na sheria za "kikafiri" (kwa mujibu waumini wa kiislamu) unadhani watakubali au watakataa? Je watasema, "Mimi nabaki Indonesia nchi yenye baraka za mungu siwezi kwenda kuishi nchi ya makafiri." Thubutu! Hakutakuwa na ndege za kutosha za kubeba Waindonesia wanaotaka kuhamia Uholanzi. Kwanini? Ningedhani kuwa nchi zenye wacha mungu (yaani waislamu, wakristo, na wayahudi wengi, ndio zingekuwa nchi zenye amani sana na ustawi. Ndio nchi ambazo watu wengi wangekuwa wanataka kwenda kuishi na pia kuiga mifano ya nchi hizo. Lakini wapi! Nchi ambazo watu wengi (ikiwa ni pamoja na wale wanaodai wana dini) wanataka kwenda kuishi na zenye amani ni zile ambazo hazina usongo na mambo ya dini hata kidogo.
Tazama Ufilipino, karibu kila mtu ni mkatoliki, waliobaki ni waislamu. Je wanaongoza kwa upendo aliohubiri Yesu na amani aliyohubiri Muhammad.?
Waislamu neno "amani" wamelifanya kabisa kuwa ni sehemu ya salamu. Asalaam Aleikum. Wayahudi nao neno amani wamefanya kuwa ni sehemu ya salamu. Wanasema: Shalom. Lakini tazama mahusiano ya makundi haya mawili na hizo salamu zao za "amani."
Hivi na kule Kongo hawana dini? Makanisa yanajaa kila jumapili. Ila nchi imejaa damu.

Kwahiyo watu wengi wanaamini kuwa kama binadamu wasingekuwa na dini, wangekuwa watu wabaya na waovu sana. Mimi hujiuliza, binadamu anaweza kuwa mwovu zaidi ya alivyo sasa? Kuna uovu gani uliobakia? Au mnadhani yanayotokea Palestina, Iraki, Sudani, Kongo, yaliyotokea Rwanda, Cambodia, Vietnam, Aghanistan, Ujerumani ya Hitler ni hadithi? Maovu makubwa kabisa kwenye historia tunayoijua yametokea katika kipindi ambacho wanadamu wana hiki kitu mnaiita dini.

Biashara ya utumwa ya Atlantiki miaka zaidi ya 400. Ile ya waarabu ilichukua miaka mingi zaidi maana ilianza kabla hii ya Atlantiki. Mauaji ya wayahudi na Hitler. Bomu la atomiki huko Japani. Ubaguzi wa rangi Marekani na Afrika Kusini. Vita vya Wazungu vya Kwanza na vya Pili (vilihusisha waasia pia kama Japani). Mauaji ya halaiki Rwanda. Ukoloni. Yote haya yamefanyika katika kipindi ambacho wanadamu wengi wanasema kuwa wana dini.

Hivi wezi wanaoiba sirikalini na wengine kuuza nchi hawana dini? Wananchi wenye hasira kali wanaoua binadamu wenzao bila huruma kwa kuwa wamedaiwa kuwa wezi, hawana dini? Wala rushwa na wana magendo, hawana dini?

Najua moja ya hoja inayotolewa ninaposema mambo haya ni hii, "Vita na maovu hayo hayajaletwa na dini." Nakubaliana kwa kiasi fulani. Nasema kwa kiasi fulani kwakuwa historia iko wazi juu ya maovu yaliyoletwa na dini. Ila hata kama maovu hayo hayakuletwa na dini, tunaweza kujiuliza: kama dini inaleta amani iweje mambo hayo yote yanayoharibu amani yatokee? Nikikwambia unipe mfano wa amani iliyoletwa na dini itakuwa kazi ngumu sana kuliko nikikutaka unipe mfano wa maafa yaliyoletwa na dini. Mifano ya dini kuharibu amani na hata tamaduni za jamii mbalimbali imejaa.

Tukichimba zaidi hoja hii tunaweza kwenda kwenye hoja nyingine ambayo sitaiingilia kwa undani. Hoja hiyo ni kuwa huenda watu "wenye dini" ukweli ni kuwa "hawana dini."

Kwa upande mwingine unapochunguza sana kitu tunachoita dini unagundua kuwa dini ni pazia.N Nikizungumzia Waafrika nitasema kuwa dini inakuzuia usimjue mungu wako wala manabii zako.
Hivi wewe na akili zako zote unadhani Afrika nzima haijawahi kuwa na manabii? Kweli jamaa wametupata. Unadhani kabisa manabii wote duniani hakuna aliyetoka miongoni mwa watu wako. Unadhani kabisa bara zima la Afrika halina sehemu takatifu za kuhiji hadi uende Roma au Yerusalemu. Au Makka kwenda kubusu jiwe na kumpiga shetani kwa mawe. Kijijini kwenu pale yako maeneo ya kuhiji lakini kwa jinsi walivyoteka fikra zako hutakaa ujue.

Halafu unajua mtu ukiwa Mwafrika huna haja ya dini hata kidogo. Dini utakuwa nayo pale atakapotokea mtu kuja kukwambia kuwa utamaduni wako haufai. Ukweli ni kuwa tamaduni zetu zinatupa mwongozo kwa kila jambo, yakiwemo masuala ya kiroho na kiimani. Wewe unaweza kuyaita dini. Kwahiyo uafrika una misingi na falsafa yake kuhusu mungu ambaye unaweza kumwamini bila kuwa na dini. Falsafa na miongozo kuhusu mungu iliyoko katika utamaduni wa Mwafrika, kwa mtazamo wangu, vinatosheleza. Hakuna kitu kipya ambacho uislamu, ukristo au uyahudi unaweza kunifundisha. Kwanza amri kumi ambazo ni msingi wa dini hizi zinazoonekana kuwa ni "bora" zaidi ya nyingine zilikuwa Afrika miaka mingi kabla Musa, aliyesema kuwa kapewa mlimani na yehova, hajazaliwa. Ngoja nirudie ili usidhani nimekosea: NINASEMA KUWA AMRI KUMI "ZA MUSA" ZILIKUWEPO AFRIKA KABLA MUSA HAJAZALIWA!
Soma historia.
Sio ile historia unayodanganywa shuleni na walimu waliodanganywa kama wewe mashuleni na vyuo vya ualimu. Tafuta historia yetu. Sijui wewe ulikwenda shule gani, ila shule nilizokwenda mimi asilimia zaidi ya 90 ya historia niliyofundishwa ilikuwa ni uongo mtupu.

Wakati dini yako inakupa amri isemayo, "Mpende jirani yako kama nafsi yako," utamaduni wa Afrika unakupa falsafa hii: Mtu sio mtu bila watu (Kwa Ki-Xhosa, "Umtu Ngumtu Ngabantu). Kwa maneno mengine tunaambiwa tupendane. Falasafa hiyo ndio inakupa itikadi ya ujamaa, falsafa ya harambee, n.k. Marasta wao wanakuja na dhana kama hiyo wanaposema, "I and I." (Bada ya kusema "mimi na wewe," marasta husema, "Mimi na mimi." Kwa kiingereza, "I and I.")
Unadhani kanuni ya mtu sio mtu bila watu imetoka kwa shetani?
Je nimekugusa pabaya?

4 Maoni Yako:

At 8/23/2005 11:37:00 AM, Blogger Jeff Msangi said...

Ndesanjo,
Huu ni mkuki moyoni kwa walio wengi.Binafsi sijui ninasimama wapi katika yote haya.Ninachoweza kutamka bayana ni kwamba uliyoyasema hapa ni mazito na hayatakiwi kuwa maneno matupu kwako mwenyewe na kwetu sote.Ni muhimu sana kujiuliza kuhusu hizi dini tunazoziabudu na kuwatoa ngeu wengine wasioziabudu.Si ni kweli kwamba wengi kati yetu ni wakristo au waislamu kwa sababu tu tumekuta wazazi wetu tayari wanaabudu dini hizo? Wangapi wanabisha?Ndesanjo ametoa changamoto,sote tujiulize.Sidhani kama Ndesanjo anataka watu waasi dini zao(nirekebishe Ndesanjo kama nimekosea).Ila anatoa mwanya kwenye amani rasmi,isiyo ya kuulizana na kutengana kwa sababu za kidini.Tuamke!Kazi murua sana Ndesanjo.

 
At 8/23/2005 08:34:00 PM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Hujakosea Msangi uliposema sitaki watu waasi dini zao. Ila kama una dini ambayo manabii zake wote wametoka nyika ya mbali, watakatifu wake wametoka nchi na tamaduni za wengine, majina yanayotambulika na kukubalika kwenye dini hiyo yametoka tamaduni za wengine, maeneo matakatifu ya kuhiji yako kwenye ardhi ya wengine, sala katika dini hiyo inatolewa kwa lugha toka nyika za mbali, misahafu yake imeandikwa kwa lugha za wengine, wateule wa mungu katika dini hiyo ni watu wa mataifa ya mengine, malaika na mungu katika dini hiyo hawafanani nawe (ila shetani anafanana nawe), dini hiyo haijali wala kuheshimu hata kidogo mtazamo wa kiimani wa watu wako...sitasita kukwambia uachane kabisa na hiyo dini. Tena uharakishe maana anayekuteka kiroho ndio amekushamaliza kazi ya kukutawala kwa njia nyingine zilizobakia kama za kiuchumu, kielimu, kisiasa, n.k.

 
At 8/23/2005 08:37:00 PM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Ngoja nifafanue kidogo. Nimeseme "wateule katika dini hiyo wametoka mataifa mengine." Hapa nilikuwa namaanisha uteule kama ulioko kwenye biblia unaosema kuwa mungu amechagua waisraeli kuwa ni taifa lake teule. Iwapo watu wangu hatupo kwenye hayo makabila 12 yaliyoteuliwa na yenye viti "mbinguni" basi usinihesabu ndani ya imani hiyo.

 
At 8/24/2005 05:23:00 AM, Anonymous Anonymous said...

Kwanza hujakosea mahesabu kabisa. Mahesabu ni sahihi. Pili Hitler na Musolin walisaidiwa na kanisa kufanya maovu yao. Tatu amri kumi hazina uhungu-dini wowote. Ukitaka kujua hili nenda katika jamii ambayo haijuhi chochote kuhusu dini za kuja. Yote yanayosemwa kwenye amri kumi za mungu ni makosa kabisa kwa jamii hizo na hakuna aliyewasomea amri kumi za mungu. Hizi ni amri za asili. Binadamu anazaliwa akiwa na utashi wa kumtosha kwamba kuiba, kuzini nakadhalika ni uovu.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com