1/29/2006

Blogu Mpya, Nguvu za Teknolojia Mpya, na Kadhalika

Kasri la Mwanazuo katuletea mwanablogu mpya. Juhudi zake nazipongeza. Mwanablogu huyo ni Mustapha ambaye amekuja na Hotspot. Mkaribishe na uwe unamtembelea. Bonyeza hapa uende nyumbani kwake. Kuja kwa Mustapha kumetokea dakika chache kabla sijakaa chini kuandika kifupi juu ya masuala ya teknolojia na vyombo vya habari. Huwa sichoki "kuhubiri" juu ya masuala haya kwani mapinduzi ya teknolojia ya habari, mawasiliano, na maarifa yananikuna sana. Mapinduzi haya faida zake kwa nchi kama zetu unaweza usizione lakini ukiwa unatazama mbali na una uwezo wa kuona "picha kamili" utajua kuwa mapinduzi haya yatabadili mambo katika nchi zetu kwa kiasi kikubwa. Kama sio sasa, ni hapo baadaye kidogo.

Moja ya mambo ambayo yanabadilika kutokana na teknolojia mpya ni mahusiano kati ya magazeti na wasomaji. Mahusiano kati ya wahariri, waandishi, na wasomaji wao. Kwa miaka mingi magazeti yamekuwa ni chombo cha habari cha mstari mmoja ulioonyooka ambapo habari, maarifa, na elimu vinatoka katika vyombo hivyo na kwenda kwa wasomaji. Mahusiano kati ya magazeti na wasomaji ni mahusiano kati ya mtoaji na mpokeaji. Magazeti yanatoa habari na maarifa, sisi wasomaji tunapoke. Wasomaji ni walaji. Barua za wasomaji tunaweza kusema kuwa ndio njia kuu ya kufanya mahusiano kati ya magazeti na wasomaji kuwa ya nipe nikupe. Magazeti yanatuambia jambo nasi tunapata nafasi ya kujibu, kuhoji, kuuliza, kusahihisha, kupongeza, n.k kupitia barua za wasomaji. Pia tunaweza kuandika kukemea jambo au kumtaka kiongozi afanye au aache kufanya jambo fulani. Zaidi ya hapo wasomaji hatuna sauti. Sisi ni magolikipa.

Kama hujawahi kufanya kwenye magazeti hutajua kuwa ni barua chache sana ambazo wasomaji wanaandika zinapata nafasi ya kusomwa na wahariri na kuchapishwa gazetini. Nyingi huishia kapuni. Na wakati mwingine, "barua za wasomaji" huandikwa na waandishi wa habari wenyewe! Kuna mambo ya ajabu sana ndani ya vyombo vya habari (ndio maana wakati mwingine mimi huviita vyombo vya uongo). Unaweza kusoma habari isemayo, "wananchi wengi waliohojiwa na gazeti hili..." ukaamini kabisa kuwa wananchi wengi waliohojiwa kumbe "wananchi" hao wako kichwani mwa mwandishi. Hajaenda kokote, hajahoji mtu yeyote.

Tofauti na magazeti-jadi ambapo msomaji ni msomaji, mtandao wa tarakilishi (Intaneti) umeleta jambo jipya. Mtandao huu, baadhi ya watu wanauita: soma-andika. Mtandao wa tarakilishi umejengwa kwa namna ambayo inaruhusu mtu kusoma na pia kuandika. Kwa mfano, kama umesoma jambo hapa kwenye blogu ukawa hukubaliani nalo au hukuelewa unaweza kuandika kupinga au kutaka ufafanuzi. Walaji na wazalishaji wanakuwa kitu kimoja. Wasomaji wanakuwa waandishi, waandishi wanakuwa wasomaji (wanasoma yaliyoandikwa na wasomaji wao). Mahusiano ya vyombo vya habari mtandaoni na wasomaji yanabadilika na kuwa ya mistari miwili ya nipe nikupe.

Ngoja nikupe mfano mdogo wa jinsi teknolojia inabadili mambo. Nimekuwa nikiandika magazetini rasmi toka mwaka 1992/93. Toka wakati huo hadi majuzi nilikuwa siwezi kujua wasomaji wangu wanawaza nini, ukiachia mbali wale ambao nilikuwa nakutana nao ana kwa ana. Lakini nilipoanza kuweka anuani yangu kwenye makala zangu nikaanza kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na wasomaji wangu. Wasomaji wananiuliza maswali kutaka ufafanuzi, wananipa mapendekezo ya makala za kuandika, wananiunga mkono, wananishushua, wananiponda, wananikumbusha ahadi nilizoweka za kuandika kuhusu jambo fulani, n.k. Nimeandika makala nyingi kutokana na mapendekezo ya wasomaji. Hili ni badiliko kubwa sana.

Blogu zinatuwezesha kwa kiasi kikubwa kufanya mambo ambayo yamekuwa hayawezekani katika magazeti-jadi ya kuuzwa mtaani. Huku bloguni tunaandika. Wasomaji wetu nao wanaandika. Mara yanatokea majadiliano. Sio mtu mmoja tu anawaambia wengine ambao wanasoma bila kuwa na uwezo wa kujibu, kuunga mkono, au kuuliza maswali. Hapana. Blogu inawezesha nyanja ya habari kutoka kwenye zama za wasomaji kuwa kama watu wasio na mawazo, habari, au fikra. Watu wanaopaswa kusoma tu, kupokea bila kutoa. Tunatoka kwenye zama hizo na kuingia kwenye zama ambazo nyanja ya habari inakuwa ni aina fulani ya majadiliano. Mazungumzo. Nipe, nikupe. Mzalishaji ni mlaji na mlaji ni mzalishaji. Kila mtu anakuwa mwanahabari. Hili ndio linafanya blogu kupata umaarufu kwa haraka. Siku hizi zinatolewa hadi skolashipu kwa ajili ya kublogu. Sio mchezo. Bonyeza hapa uione (lazima uwe mwanafunzi wa chuo kilichopo Marekani).

Katika kujaribu kubadili mahusiano kati yake na wasomaji, kwa kutumia teknolojia mpya, magazeti kadhaa yanafanya majaribio ya aina mbalimbali. Kwa mfano, gazeti la Wisconsin State Journal linatumia wasomaji wake kuamua habari zipi ziwekwe ukurasa wa mbele. Wasomaji wanapiga kura. Bonyeza hapa usome kuhusu jaribio hili. Mwaka jana gazeti la Seattle Post-Intelligencer lilianzisha jaribio ambalo tahariri inaandikwa na wahariri wa gazeti hilo na wasomaji wake. Kongoli hapa na hapa kwa undani. Kuna gazeti kama News and Record ambalo limeanzisha ukurasa uitwao Town Square katika tovuti yake ambapo wasomaji wanapewa nafasi ya kuandika habari wenyewe. Bofya hapa uwatazame. Magazeti mengi yanachofanya hivi sasa ni kuwa na waandishi wao ambao wanakuwa na blogu. Blogu hizo zinakuwa ni uwanja wa majadiliano kati ya gazeti na wasomaji wake. Ukiachilia mbali maagazeti hayo, teknolojia mpya zimezalisha miradi mipya kabisa kwenye nyanja ya habari. Kwa mfano, kuna Wikinews, mradi ambao habari zinaandikwa na wasomaji. Zinaandikwa na mtu yeyote. Tazama hapa. Halafu kuna jamaa walioanzisha mradi kabambe wa uandishi wa umma huko Korea ya Kusini, Ohmynews. Ohmynews ina habari ambazo zinaandikwa na wananchi. Wasomaji wakisoma habari wakaipenda wanaweza kumlipa aliyeandika habari hiyo. Bonyeza hapa utazama toleo la kiingereza la Ohmynews.

Kwa ufupi, nilikuwa namkaribisha Mustapha , kumpongeza Kasri kwa kutuletea huyu ndugu, na kusema kuwa tunalofanya kupitia katika blogu zetu hizi ni sehemu ya mapinduzi ambayo yanabadili kabisa mahusiano kati ya watoa habari na wapokeaji.

1/28/2006

Zaidi juu ya Creative Commons: kitabu cha bure na zoezi la pekee la kuhariri

Huu ni mmoja wa mifano ya faida za Creative Commons. Majuzi kimetolewa kitabu cha kufundisha watu wa nchi zinazoitwa "zinazoendelea" juu ya ujenzi wa mtandao usiwaya (wireless network kwa kimombo). Kitabu hiki kimetolewa chini ya nembo ya Creative Commons. Kinapatikana bure. Na kuwakuwa kiko chini ya Creative Commons, mtu yeyote yule anaruhusiwa kukitoa kitabu hiki katika lugha yoyote ile (na hata kuongeza mambo ambayo anaona ni muhimu ila hayako katika kitabu mama). Yote hii unaruhusiwa kufanya bila kuomba ruhusa kwa mtu yeyote kwa masharti kuwa kitabu hicho usikitoe kwa minajili ya kibiashara na pia lazima toleo lako liwe chini ya Creative Commons. Kitabu chenyewe ukibonyeza hapa utakipata. Hapa kuna ukurasawa wa "wiki" wa kitabu hicho.

Kuna mfano mwingine wa mabadiliko makubwa yanayojitokeza kutokana na teknolojia mpya na vuguvugu kama la Creative Commons. Mwaka 1999, Larry Lessig, mwanzilishi wa vuguvugu hili, alitoa kitabu kizuri sana kiitwacho Code and Other Laws of Cyberspace. Hili lilikuwa ni toleo la kwanza. Toleo la pili, yaani Code v. 2, ni muendelezo na upanuaji wa hoja na uchambuzi ulioko katika toleo la kwanza. Kwa staili ya ki-Creative Commons, toleo hili la pili badala ya kuandikwa na Larry Lessig peke yake kama ilivyo kawaida katika nyanja ya vitabu, toleo hili linaandikwa/linahaririwa na watu mbalimbali. Ina maana kuwa hata wewe unaweza kushiriki katika kuandika toleo la pili la kitabu hiki. Bonyeza hapa uone zoezi hili la kipekee.

Mawaziri Kuapa kwa Biblia na Kurani: Imani tumezibebabeba tu?

Wiki iliyopita, kwa ajili ya ukurasa wangu katika gazeti la Mwananchi, niliandika makala kuhusu mawaziri wapya kuapa kwa kutumia kitabu "kitukufu" na "kitakatifu" baada ya kuteuliwa. Soma baadhi ya hoja nilizotoa dhidi ya tendo la kuapa:

Baada ya rais mpya kuteua baraza jipya la mawaziri, kilichofuata kilikuwa ni tendo la kula kiapo. Tukio hili limezungumzwa sana mtaani hasa kutokana na kitendo cha Kingunge Ngombale Mwiru (nitampa zawadi ya jina zuri) kuapa kwa kunyoosha mkono bila kushika kitabu "kitukufu" au "kitakatifu" (kurani au biblia) kama wengine walivyofanya.

Wakati ambapo kwa watu wengi kuapa bila kutumia kitabu cha dini ilikuwa ni habari kubwa, kwangu mimi kitendo cha wafuasi wa Isa/Yesu kuapa ndio ilikuwa habari kubwa kabisa. Ni habari ya binadamu kuwa na tabia ya kufanya mambo kutokana na mazoea bila kutafiti kwa kina juu ya usahihi wa jambo lenyewe. Ni tabia inayotokana na utamaduni wa kuiga mifumo ya sheria, utawala, na demokrasia ya nchi nyingine tukidharau uwezo wetu wa kuunda mfumo wetu wenyewe.

Tendo la mawaziri kuapa wakitumia kitabu kitakatifu au kitukufu hatujaanzisha sisi. Utamaduni wa mashahidi kuapa mahakamani kwa kutumia vitabu hivyo hatujauanzisha sisi. Tumeiga toka kwa wengine kama ambavyo tumeiga karibu kila kitu.

Kwanini habari kwangu sio Kingunge kuapa mikono mitupu bali Wakristo na Waislamu kuapa? Jibu la swali hili liko katika kitabu cha Matayo, mlango wa 5, aya ya 33 hadi 37. Katika aya ya 34 Yesu/Isa anakataza wafuasi wake (Waislamu na Wakristo ni wafuasi wake) kuwa wasiape kamwe.

Hivi ndivyo asemavyo toka aya ya 33 hadi ya 37: "Tena mmesikia kuwa watu wa kale waliambiwa: `Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana. Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Ukisema, `Ndiyo`, basi iwe `Ndiyo`; ukisema `Siyo`, basi iwe kweli `Siyo`. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu."

Anasema kuwa ingawa huko nyuma kuna manabii waliwaambia wanadamu kuwa wanaweza kuapa, yeye anabadili na kusema kuwa usiape kamwe. Hii haikuwa kwa mara ya kwanza kwa Yesu/Isa kutengua mafundisho ya zamani. Unakumbuka, ingawa iliandikwa “jino kwa jino, jicho kwa jicho,” yeye alikuja na kusema geuza shavu. Mchukie adui yako akabadili kwa kutuambia kuwa tuwapende na tena tuwaombee. Aligeuza sheria ya kupiga mawe hadi kuwaua wanaokamatwa katika uzinzi. Alibadili sheria kuhusu talaka. Alibadili maana ya kuzini kwa kusema kuwa hata ukitamani umeshazini.

Nimetoa mifano hii kukupa picha kidogo ya baadhi ya mambo aliyobadili likiwemo suala la kiapo. Anatuambia kuwa kipimo cha ukweli wa kauli yetu isiwe ni kiapo. Anasema ukisema “ndiyo” iwe “ndiyo” na ukisema “hapana” iwe “hapana.” Ukisema utatii katiba na kutumikia wananchi, basi tii katiba na kutumikia wananchi. Hakuna la kuongeza wala kupunguza. Sema ukweli na simama kwenye hiyo kweli, usianze kuingiza jina la Mungu ili kutufanya tuone kuwa unayosema ni kweli.

Nimekuwa najiuliza kwanini wafuasi wa Mwalimu huyu wamekuwa hawafuati mafundisho yake? Je inawezekana kuwa ufuasi wao ni wa jina tu na sio imani ya dhati na uelewa wa mafundisho yake? Amesema waziwazi usiape. Wewe unaapa, tena kwa kutumia kitabu chenye maneno yake yanayokukataza. Je hili ni tatizo la kufuata tamaduni za wengine bila kuhoji? Au ni tatizo la kuwa wafuasi wa Isa/Yesu bila kusoma mafundisho yake?

Lakini tukiacha hoja hii ya kuwa Isa/Yesu amekataza wafuasi wake kuapa, kuna hoja nyingine ambayo niliwahi kuitoa huko nyuma. Nitairudia kwa kifupi. Haiwezekani kutumia Kurani au Biblia kuapa kuwa utalinda katiba ya nchi ukitegemea kuwa Mungu atakubariki na kukusaidia ili utimize kiapo hicho. Kwa sentensi chache sana nitakueleza ni kwanini kisha nitakuacha ili iwe tafakari yako siku hii ya mungu jua (ndio maana ya jumapili).

Kurani na Biblia zinasema kuwa Mungu ametoa amri kumi. Amri ya kwanza inasema, “Mimi ni Bwana Mungu wako usiwe na miungu wengine ila mimi.” Hili sio ombi. Inaitwa amri. Anasema wazi kuwa anataka umwamini na kumwabudu yeye tu. Yeye Yehova/Allah. Tuje kwenye katiba yetu: katiba yetu inatoa uhuru wa kuabudu. Ina maana kuwa unaweza kuabudu Mungu mmoja au miungu 10, hutakuwa umevunja sheria ya nchi. Sio hivyo tu, unaweza pia kutokuwa na imani yoyote na usiwe umevunja sheria ya nchi.

Kwa maneno mengine, wakati Yehova/Allah anakwambia, “Niabudu mimi” katiba inasema “Abudu chochote kile.” Je Mungu aliyekupa AMRI ya kumwabudu yeye tu, anaweza kukubariki ili uendeleze katiba inayosema abudu chochote kile? Yaani Mungu atakuwa anakubariki ili uendeleze mwongozo ambao unawapa wanadamu ruhusa ya kuvunja amri yake ya kwanza. Tena amri hii sio ya kumi bali ni ya kwanza. Kama katiba ingesema mwamini mungu mmoja ambaye ni Yehova/Allah, basi nisingeshangaa iwapo waumini wa Kikristo na Kiislamu wangekuwa wanamuomba mungu awasaidie kuilinda hiyo katiba. Lakini katiba haisemi hivyo. Inapingana kabisa na mafundisho ya Allha na Yehova. "Usiwe na miungu mingine ila mimi" sio sawa na kusema kila mtu ana haki na uhuru wa kuamini atakacho.

Kwahiyo kitendo cha kutumia kitabu kinachokutaka uwe na Mungu mmoja kuapa kuwa utalinda katiba inayokuruhusu uwe na mungu yoyote, mmoja au miungu wengi, au hata usiwe na imani kabisa, n.k. kinaonyesha kuwa huenda imani zetu tumezibebabeba tu. Au tumebebeshwa.

1/27/2006

Juu ya Vuguvugu la Creative Commons

Majuzi niliandika kuhusu Tanzania kukubaliwa rasmi kuanzisha tawi la Creative Commons na kuwa Paul Kihwelo, mkuu wa kitivo cha sheria, Chuo Kikuu Huria, ndiye mwongoza mradi upande wa kisheria. Baadaye tunatakiwa kutafuta mwongoza mradi upande wa uhamasishaji. Kama hukusoma niliyoandika siku hiyo, bonyeza hapa. Ukisoma sehemu ya maoni utaona kuwa Mark Msaki ameongelea suala moja ambalo kwa muda mrefu limekuwa lilibishaniwa katika duru za wanazuoni wa masuala ya sheria, sayansi ya jamii, uchumi, na falsafa. Hoja yenyewe ni kuwa sheria ya hatimiliki inachochea ubunifu na ugunduzi. Na kuwa kama kama hakuna faida za kiuchumi/kifedha, watu hawatabuni au kujihusisha na kazi za ugunduzi. Kwahiyo vuguvugu kama la Creative Commons ambalo linachochea watu kuachilia huru kazi zao (iwe ni vitabu, muziki, sinema, n.k.) na kuondoa ukiritimba wa maarifa na elimu, linaweza (vuguvugu hilo) kuondoa msukumo wa kubuni, kutunga, kugundua, n.k.

Hoja hii ina mapengo mengi sana. Mfumo wa hatimiliki una kazi zake. Tunaounga mkono vuguvugu la Creative Commons hatusemi kuwa mfumo wa hatimiliki uondolewe kabisa. Tunasema kuwa mfumo huu unahitaji kufanyiwa mageuzi ili kuendana na upepo wa wakati, teknolojia zilizopo leo hii, na kukidhi matakwa ya umma. Tunachosema ni kuwa tunaweza kutumia itikadi ya ujamaa kwenye kazi ambazo zimekuwa zikifungwa pingu na sheria ya hatimiliki ambayo inakidhi mahitaji ya msukumo wa soko. Msukumo wa soko, kama apendavyo kusema Desmond Tutu, sio mungu. Sio mwanzo na mwisho wa kila kitu.

Zipo faida mbalimbali kwa umma iwapo mfumo wa hatimiliki uliopo (duniani kwa ujumla) utafanyiwa marekebisho. Kwa mfano, tazama suala la dawa za kuongeza maisha ya wenye Ukimwi. Dawa hizi zimegunduliwa (makampuni mengi ya madawa huiba elimu ya jadi ya dawa toka nchi za Kusini) na makampuni ya Magharibi. Dawa zao ni ghali sana kiasi ambacho watu wachache sana wenye ugonjwa huu katika nchi za Kusini wana uwezo wa kuzinunua. Makampuni ya Brazili, India na kwingineko yanatengeneza dawa-chapa kama hizo kwa bei nafuu zaidi. Kutokana na sheria ya hatimikili kitendo cha kampuni hizi kutengeneza dawa hizo bila ruhusa ya makampuni ya Magharibi yaliyozigundua ni kosa. Kitendo cha dawa-chapa hizi kuwa za bei ambayo masikini wengi wanaweza kuimudu kuliko ile ya makampuni ya Kimagharibi hakina nafasi kwenye mjadala. Suala kuu ni hatimiliki na haki ya makampuni haya kufaidi kwanza kwa maiaka kadhaa kabla makampuni mengine hayajaruhusiwa kuzitengeneza. Kwahiyo kumekuwa na kesi mbalimbali ingawa makampuni ya Magharibi yanarudi nyuma kwakuwa yameona kuwa dunia inayaona kama wanyama vile kwa kutaka kuzuia masikini wasio na kipato kupata dawa wanazoweza kununua.

Mfano mzuri wa umuhimu wa vuguvugu la Creative Commons ni huu: Shirika la Habari la BBC linaruhusu Muingereza yoyote kutumia bure chochote BBC walichohifadhi. Kama kuna Muingereza anatengeneza filamu, katika filamu hiyo akawa anahitahi sauti ya simba au tembo au akawa anahitaji video ya mbuga fulani ya wanyama, badala ya kufunga safari kutafuta wanyama hao anaweza kutumia video za BBC. Bure. Kila Muingereza hulipa kodi ya kuendesha BBC. Kwahiyo kila Muingereza ana haki ya kufaidika na kazi za BBC. BBC wakifuata mfumo wa hatimiliki uliopo itabidi wazuie Waingereza ambao ndio hasa wanaoipa uhai BBC kufaidi. Ni sawa na Tanzania. Redio Tanzania inaendeshwa kwa fedha zetu. Je hatimiliki ya kazi zake na rekodi zake zote ni za Watanzania wote? Vuguvugu la Creative Commons linasukuma Redio kama Redio Tanzania kupanua hatimiliki ya kazi zake kuwa ya Watanzania wote ambao kodi yao ndio uhai wa redio hiyo. Bonyeza hapa usome kuhusu BBC kuamua kuweka kazi zao zote chini ya Creative Commons. Unaambiwa kuwa ili umaliza kutazama video walizonazo, unapaswa kutazama video hizo kwa miala 68, usiku na mchana (masaa 24)!

Kuna mtazamo kuwa hatimiliki husaidia sana wagunduzi, watunzi, wanamuziki, n.k. Sio mara zote. Tazama kwenye muziki. Wanamuziki wengi wanapata hela zao sio kwenye kuuza CD bali kwenye maonyesho ya hadharani, matangazo, n.k. Wanaofaidi hasa kazi za wanamuziki ni makampuni ya kurekodi. Utashangaa kuwa makampuni haya ndio huwa yanamikili haki za nyimbo za wanamuziki. Na ndio huchukua sehemu kubwa ya pato linalotokana na kuuza CD. Sasa katika mwelekeo wa ki-Creative Commons, imekuja kampuni inaitwa Magnatune. Kampuni hii inauza CD. Asilimia 50 inakwenda kwa mwanamuziki (hakuna kampuni inayompa mwanamuziki asilimia 50. Hata wanamuziki unaowaona matajiri wanapunjwa wote). Zaidi ya mwanamuziki kupata asilimia 50, mwanamuziki huyo ndiye anayemiliki haki za muziki wake na sio kampuni hiyo. Bonyeza hapa uone kampuni hiyo.

Profesa Kembrew ni mtu wa utani sana. Yeye ni kati ya wanazuoni wanaoandika sana kuhusu mapungufu ya mfumo wa hatimiliki uliopo hivi sasa. Katika kuonyesha mapungufu yake, Profesa Kembrew aliamu kusajili msemo wa kiingereza,"Freedom of Expression." Baada ya kuusajili msemo huu amepewa haki ya kuweka nembo ya "haki zote zimehifadhiwa". Yaani hivi: Freedom of Expression©. Kwahiyo hivi sasa yeye ndiye anayemiliki msemo huo. Bonyeza hapa usome kihoja hicho kwa undani.

1/25/2006

Ujenzi wa Huduma cha Kublogu ya Kiswahili

Moja ya matatizo ya huduma za kublogu tunazotumia hivi sasa ni lugha. Huduma hizi zimetengenezwa kwa udhanifu kuwa watumiaji ni wazungumzaji wa Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kishirazi, n.k. Kiswahili hakipo. Tatizo jingine ambalo lipo katika huduma kama blogger.com (ambayo wengi tunatumia) ni kukosekana kwa muundo wa kupanga kazi tunazoandika katika makundi ya kimaudhui. Hili ni tatizo kubwa sana hasa kama mtu unapanga kublogu kwa muda mrefu.
Ina maana hapo baaadaye ukitaka kutafuta habari uliyoandika miaka mitatu iliyopita, itakupasa ukumbuke mwezi na tarehe ili uweze kuipata kwa urahisi. Kama hukumbuki uliandika mwezi gani itakubidi utumie muda mrefu kuisaka. Fikiria, je ikiwa imepita miaka saba? Lakini pia kuna suala la wasomaji kuja kwenye blogu yako na kutaka kusoma habari ulizoandika huko nyuma. Kama wanataka kusoma habari ulizoandika kuhusu utamaduni, watazipataje? Au hadithi. Au labda umekwenda kwenye blogu ya Michuzi baada ya miaka miwili, ukawa unatafuta picha ya jiji la Dasalama au ya Mwanza. Utaipataje hiyo picha? Namna rahisi ya kuipata picha hiyo ni kama amehifadhi picha zake kutokana na maudhui. Kwa mfano, maudhui yanaweza kuwa ni: utamaduni, siasa, michezo, uchaguzi, mikoani, Ughaibuni, Rais, Wabunge, Wanawake, Muziki, Historia, Hadithi, n.k.

Nikienda kwenye blogu ya Makene, nikataka kusoma mashairi yake. Bila kujua aliandika lini na mwezi gani itakuwa vigumu sana. Lakini akiwa na uwezo wa kupanga mambo kwenye blogu yake kutokana na maudhui, kila akiandika shairi analiweka kwenye maudhui ya kundi ya ushairi. Hivyo msomaji akienda hapo anabonyeza kwenye maudhui ya ushairi na kuweza kuona mashairi yake yote. Ukija kwangu ukataka kusoma mambo niliyoandika kuhusu utamaduni au kuhusu blogu, utapata tabu sana maana hakuna mpangilio wa kimaudhui. Kunapokuwa na makundi haya yaliyopangwa kimaudhui kunasaidia msomaji kuweza kupata habari ulizoandika huko nyuma kwa urahisi. Inakusaidia hata wewe mwenye blogu kujua mambo uliyoandika yako wapi. Tunapaswa kutatua tatizo hili. Tutalitatua.


Sasa rafiki yangu Chris wa NonProfit Design (bonyeza hapa uone blogu yake) na mimi tunalipatia tatizo la lugha kwenye huduma za kublogu dawa ya kudumu. Kwa kutumia huduma huria ya kublogu ya Wordpress, tunaunda toleo la Kiswahili. Wordpress tayari ina matoleo ya lugha kadhaa. Kiswahili kwa sasa hakimo. Uzuri wa Wordpress ni kuwa ni programu huria hivyo iko wazi kwa mtu yeyote kufanya chochote atakacho (iwapo una ujuzi sahihi).

Mwisho wa wiki Chris alinitembelea tukaa pamoja kwa siku mbili (alikuja na mbwa wake aitwaye IO). Tulitazama kwa undani jinsi ambavyo tunaweza kusaidia wanablogu wote wa Kiswahili kuhama toka walipo hivi sasa na kuweza kuwa na mpangilio wa mambo waliyoandika katika makundi ya kimaudhui na pia hatua za kufuata ili kujenga toleo la Kiswahili la Wordpress. Katikati ya kucheza na kodi za programu mbalimbali za tarakilishi, tulikuwa tukicheza mpira wa meza (ambapo nilimfunga mabao yasiyohesabika. Kama unabisha muulize! Richard Shilangale, unakumbuka kuwa wewe ndiye ulinifundisha kucheza mpira wa meza?). Pia tuliongelea masuala ya Creative Commons maana shirika lake ndilo linalojenga tovuti ya tawi la Creative Commons Tanzania na pia kuihifadhi tovuti hiyo. Bonyeza hapa usome aliyoandika mwenyewe kuhusu toleo la Kiswahili la Wordpress.

**Da Mija: wewe ndio umenikumbusha neno maudhui. Lilinitoka kabisa. Kila nikilitafuta neno linalonijia ni hadhira! hadhira na maudhui wapi na wapi?

Karibu Sana Pambazuka

Baada ya kimya cha muda mrefu ambacho kilinifanya nitake kuunda tume au kutumia makachero wa FBI kumtafuta, mwanablogu Nkya wa Pambazuka amerudi. Tena kwa kishindo na kasi mpya. Sijui hii kasi mpya kaambukizwa na Kikwete na wana mtandao? Ukienda katiba blogu yake utakuta ameandika juu ya madakitari ambao serikali iliwafukuza. Madakitari hawa walikuwa wakidai waongezewe mshahara na serikali ilikuwa ikisema, kama ilivyozoea, kuwa inashughulikia suala hilo. Sijui serikali yetu huwa inatumia miaka mingapi kushughulikia tatizo kama hilo. Toka tupate uhuru, kwa mfano, sirikali imekuwa ikishughulikia tatizo la mshahara usiotosheleza wa walimu. Hadi leo bado inashughulikia. Huenda ndio maana Sumaye alikuwa akituambia kila mara kuwa sirikali yetu hufanya kazi usiku na mchana. Sirikali mpya nayo sijui kama hufanya kazi usiku kucha. Nkya anasema kuwa kitendo cha kufukuza madakitari ni sawa na taifa kupoteza miaka 3,800 ya elimu. Kwa taifa kama Tanzania, kupoteza miaka yote hii sio jambo la mzaha. Bonyeza hapa uone alivyopata miaka hiyo. Nkya anatamani jambo moja: lini kipindupindu kitapiga hodi ikulu? Bonyeza hapa utajua kwanini. Nkya aliwahi kutoa msamiati mmoja. Aliita demokrasia "mkumbokrasia." Mfumo wa siasa na jamii ambapo wananchi wanashiriki kama washabiki. Sasa katika mambo mapya aliyoandika nimekuta ameviita vyama tuviitavyo vya upinzani, "vyama vya ushindani." Nadhani anamaanisha kuwa katika mfumo wa vyama vingi, kazi kubwa ya vyama ni kushindana (zaidi ya kupingana) kuweza kushawishi umma kuwa vina uwezo na mipango bora zaidi ya kuongoza nchi.

1/22/2006

Unamjua Spika Wa Wanablogu?

Nimeamka asubuhi hii na kwenda moja kwa moja kwenye ukumbi pepe wa mjadala kuhusu neno muafaka la Kiswahili la teknolojia hii ya blogu. Nikasoma mawazo mazuri sana ya wachangiaji, nami nikaweka neno langu. Napenda uende pale ili ujue mjadala umefikia wapi. Kuna masuala fulani ya kinadharia kuhusu lugha na kuhusu blogu ambayo yamejitokeza. Ila pia mjadala huu umetuletea Spika. Unajua Liberia wamepata rais mwanamke. Ujeremani wamepata Kansela mwanamke. Chile wamepata raisi mwanamke. Tanzania imepata waziri wa fedha mwanamke. Kuna jambo linatokea duniani hivi sasa. Nasi tumepata spika mwanamke. Ukitaka kumjua nenda kwenye ukumbi pepe wa majadiliano ya neno blogu. Spika huyu tumekuwa tukimwita Mheshimiwa ila napendekeza tumwite ndugu. Naona neno ndugu lina maana nzuri zaidi ya mheshimiwa. Watwawala wetu wanaitwa waheshimiwa...si ndio?
Haya, bonyeza hapa.

1/20/2006

Creative Commons Tanzania!

Furaha niliyonayo sijui nifanye nini. Au niseme nini.
Ngoja nianzie mwaka jana mwezi wa sita: mwezi wa sita mwaka jana nilikwenda jiji la Egoli/Jozi (au Johannersburg, kama hujui), Afrika Kusini, kwenye mkutano wa Commons-Sense kwenye chuo kikuu cha Wits. Mkutano huu ulikuwa ni wa ufunguzi wa tawi la shirika la Creative Commons nchini Afrika Kusini. Bonyeza hapa usome hisia nilizopata nilipotembelea hapo kwa Madiba.

Creative Commons in vuguvugu linaloendeleza mfumo wa hatimiliki mbadala (kwa kiingereza: "copyleft" badala ya "copyright"). Kwahiyo badala ya kazi zilizoko chini ya hatimiliki kusema "Haki Zote Zimehifadhiwa" kama ambavyo mfumo wa hatimiliki uliozoeleka ulivyo, Creative Commons inatoa nafasi kwa wamiliki wa kazi mbalimbali kuweza kusema, "Baadhi ya Haki Zimehifadhiwa," au "Hakuna Haki Zilizohifadhiwa." Kimsingi, mfumo huu, tofauti na mfumo wa hatimiliki uliozoeleka ambao una kila chembe za falsafa za kibepari, umejengwa juu ya falsafa kama vile Ujamaa au Ubuntu. Msingi wa Ubuntu ni huu: mtu sio mtu bila watu. (bonyeza hapa kusoma kwa kifupi kuhusu ubuntu). Kwahiyo sio vigumu sana kwa Waafrika kuelewa mantiki ya vuguvugu kama Creative Commons. Afrika Kusini ndio nchi ya kwanza Afrika kuwa na tawi.

Vuguvugu la Creative Commons nimekuwa nikilifuatilia kwa muda mrefu. Nilipokwenda mkutano wa Afrika Kusini na kukutana na wanaharakati wengine wa vuguvugu hili na pia "baba" wa Creative Commons, Larry Lessig (bofya hapa kuna blogu yake) mwili mzima ulinisisimka. Kabla ya hapo nilikuwa nimewagusia marafiki zangu kadhaa Tanzania juu ya vuguvugu hili ila hakuna aliyeonekana kujali. Walinisikiliza tu. Nikawaacha. Sasa mwezi Septemba nikiwa njiani kwenda Helsinki, Ufini (ambapo ndipo nilikutana na Michuzi na blogu yake kabambe ilipozaliwa...blogu yake ina uraia wa Ufini!), nikiwa uwanja wa ndege Uholanzi nikakutana na Paul Kihwelo, ambaye zaidi ya kuwa mshikaji wangu, ni mkuu wa kitivo cha sheria, Chuo Kikuu Huria Tanzania. Tukaongea kidogo nikamgusia kuhusu Creative Commons na umuhimu wa kujenga vuguvugu lake Tanzania. Hatukuwa na muda wa kutosha. Tukakubaliana kuandikiana. Basi kukutana kwetu pale uwanja wa ndege kumezaa matunda. Na ndio furaha yangu niliyonayo. Paul ni kati ya watu ambao akikwambia kuwa atafanya jambo, ujue kuwa atafanya.

Ombi letu kwa ofisi inayoshughulikia uanzishwaji wa matawi ya Creative Commons katika nchi mbalimbali kutaka kuanzisha Creative Commons Tanzania limekubaliwa. Kwahiyo shughuli rasmi ya kujenga tawi la Creative Commons na kuwezesha wasanii, watunzi, shule, vyuo, wanasayansi, n.k. kutoa kazi zao kupitia Creative Commons imeanza. Paul Kihwelo ndio mwanasheria muongozaji wa zoezi zima la kuanzisha tawi lake nchini Tanzania. Zoezi hili litakuwa chini ya kitivo cha sheria, chuo kikuu huria (moja ya masharti ya kuanzisha tawi ni kuwa lazima kuwe na taasisi ambayo ndio itasimamia). Jumapili tutawasiliana na Paul kuhusu ujenzi wa tovuti maana katika masharti ya mradi huu ni kwamba lazima kuwepo na tovuti. Tayari kuna mashirika mawili ambayo yako tayari kutoa nafasi ya bure ya kuhifadhi tovuti yetu. Kesho ninakutana na Chris Blow wa shirika la NonProfit Design, ambaye yuko tayari sio tu kuhifadhi tovuti hiyo bali pia kuiunda.

Ukibonyeza hapa utaona jina la Tanzania tayari limeingizwa katika nchi ambazo ziko mbioni kuunda Creative Commons (Tazama upande wa chini sehemu isemayo: Upcoming Project Jurisdictions).

Watu wengi ukiongea nao kuhusu masuala ya faida ya kuwa na hatimiliki ya "baadhi ya haki zimehifadhiwa" au "hakuna haki zilizohifadhiwa" badala ya mfumo wa "hazi ZOTE zimehifadhiwa," mawazo yao yanakuwa yanakwenda tu kwenye masuala kama ya muziki. Vuguvugu kama la Creative Commons linagusa maeneo mengi sana kwenye jamii. Hasa maeneo yanayohusu maarifa na elimu. Mfumo wa hatimiliki uliopo hivi sasa unapendelea watu wahodhi maarifa na elimu wakati ambapo Creative Commons inataka kuachilia huru maarifa na elimu. Kutokana na Creative Commons, kuna vitabu ambavyo unaweza kuvipata bure. Bila hata sumni. Kwa mfano, bonyeza hapa upate kitabu kimojawapo.

Lakini pia Creative Commons inaachilia huru maarifa ya vyuo vikuu kwa ajili ya faida ya watu wote hata kama sio wanafunzi waliolipa ada wa chuo chenyewe. Kwa mfano, chuo cha MIT kimeweka masomo yake wazi mtandaoni kwa watu wote wanaotaka kufaidi bure. Bonyeza hapa.
Hata chuo kikuu cha Rice nacho kinaunga mkono vuguvugu hili. Bonyeza hapa. Blogu yangu iko chini ya Creative Commons. Huenda umewahi kuona nembo ya Creative Commons ukashindwa kujua inafanya nini hapa. Ni kwamba kazi zilizoko hapa haziko chini ya mfumo wa "haki zote zimehifadhiwa." Ina maana kuwa kama unataka kuzitumia (iwe ni picha, makala, kisa, shairi, n.k.) sio lazima uiombe ruhusu au unilipe.

Bonyeza hapa ukitaka kusoma zaidi juu ya Creative Commons (kwa kiinglishi).

1/18/2006

Mwanablogu Kimazichana....bado namchekicheki

Mwanablogu mpya, Kimanzichana, bado nimnacheki kinamna. Sijui wewe. Mtembelee kwa kubofya hapa. Je ni mtu wa kejeli, dhihaka, sanifu, ucheshi, n.k.?

Karibu Ibrahim Bwire na Blogu Yako

Ni kweli kuwa bado blogu za Kiswahili ni chache ukilinganisha, kwa mfano, na blogu za Kiingereza za Wakenya. Ni kweli kuwa ni Watanzania wachache hivi sasa wenye uwezo, nafasi, na ujuzi wa kutumia tarakilishi na mtandao wa tarakilishi. Ninafurahi kuwa ukweli huu hauzuii wenye nia ya kublogu kufanya hivyo. Ukitazama historia ya magazeti, kwa mfano, nchini Tanzania utakuta kuwa kuna wakati kulikuwa na gazeti moja. Kuna wakati magazeti yalikuwa machache mno na tena hayakuwa yakisambazwa nchi nzima. Na tena yalikuwa yakisomwa na watu wachache sana. Na tena kulikuwa na watu wengi wasiojua kusoma. Lakini mambo yamekwenda hadi tumefika wakati ambapo huwezi kusoma magazeti yote yanayotolewa kwa siku. Na magazeti hayo yanafikia watu wengi zaidi. Blogu nazo kuna siku tutakaa na kusema, "unakumbuka enzi zile watu walikuwa hawajui blogu ni nini?" Utafika wakati huo. Jitihada zinafanyika. Kwa mfano, blogu zetu siku si nyingi zitaanza kusomwa asubuhi redioni na kwenye luninga kwenye vipindi vile wanavyosoma magazeti ya siku. Yaani kama wanavyosoma magazeti ya siku ndivyo watakuwa wanasoma blogu zetu, jambo ambalo litasaidia tunayoandika kufikia watu wengi zaidi. Tunajua kuwa redio ndio chombo cha habari kinachofikia watu wengi zaidi duniani hivi sasa. Tutaingia kwenye chombo hicho. Kwahiyo upo uwezekano wa kutumia vyombo vya habari vinavyofikia watu wengi kusambaza cheche tunazotoa kwenye blogu zetu.
Tararira yote hiyo nilitaka kumkaribisha mwanablogu mpya, ndugu Bwire (asante sana Kasri la Mwanazuo kwa kutuletea). Bwire anasema kuwa weka kila kitu kando, fikra ndio mambo yote. Bonyeza hapa umtembelee.

1/16/2006

Blogu ya mwongozo wa jinsi ya kublogu

Kutokana na maswali ninayopata toka kwa watu wenye nia ya kublogu na hamasa kubwa waliyonayo watu wengi wenye kutaka kutumia teknolojia hii kutoa mawazo yao, kujieleza, na kuelimishana na wengine, nimeamua kujenga blogu maalum ya mwongozo kwa wanaotaka kublogu na pia wale ambao tayari wanablogu. Blogu hii itasaidia watu wa kawaida wanaotaka kublogu, itakuwa na eneo la waandishi wa habari wanaotaka kublogu, kutakuwa na ukurasa kwa ajili ya wanaharakati au wenye mashirika yasiyo ya kiserikali wanaotaka kublogu, ukurasa wa kusaidia wanasiasa wanaotaka kublogu, ukurasa wa kusaidia wanaoblogu jinsi ya kutangaza blogu zao, ukurasa wa maelezo kwa wale wanaotaka kublogu bila kujulikana kuwa wao ni akina nani (kwa mfano, kama unafanya ofisi ya rais na unaona mambo ambayo unadhani ni muhimu umma ukajua lakini hutaki rais ajue kuwa wewe ndiye unayetoboa siri!), n.k. Iwapo kuna suala ambalo ungependa liwe na ukurasa wake, usisite kuniambia. Majina ya kurasa zenyewe yako upande wa kuume wa blogu hiyo, chini ya orodha ya miezi. Blogu hiyo utaiona kwa kubonyeza hapa.

TUMKUMBUKE MARTIN LUTHER KING

Leo ni siku ya kitaifa nchini Marekani ya kumkumbuka mpigania haki za watu weusi na binadamu wote, Dakta Martin Luther King. Ninakupa viungo kadhaa vya hotuba zake ambazo zilikuwa zinasisimua mno kutokana na ufundi wake wa kuhubiri. Bonyeza hapa uone video za hotuba zake. Hapa kuna video ya mahojiano. Bofya hapa kwa mkusanyiko wa video mbalimbali.
Kuna hotuba zake mbili muhimu sana kusikiliza: ya kwanza ni ile ya "Nina Ndoto." Bonyeza hapa usikilize. Hotuba ya pili ni ile ya "Nimefika Kileleni Mlimani" ambayo utaipata ukibonyeza hapa.

1/15/2006

Mtanzania Aanzisha Huduma ya Kublogu Tanzania

Mike Mushi, ambaye ndiye aliyeunda tovuti za Uchaguzi Tanzania na KikweteShein, ameunda tovuti inayotoa huduma kwa wanaotaka kuanzisha blogu zao bure. Bado ninaipitiapitia tovuti hii kuitazama inavyofanya kazi ili niweze kuifanyia marejeo. Bonyeza hapa uitembelee.

Vita ya Msituni Inahamia Kwenye Mtandao Pepe

Jamaa wa gazeti la Washington Post wana habari moja nimeisoma dakika hii kuhusu wapiganaji wa msituni Afrika wanavyotumia zana mpya za mawasiliano (blogu zikiwemo) na pia jinsi ambavyo mtandao wa tarakilishi unavyoweza kusaidia wapinzani wa serikali zenye tabia ya kufungia magazeti na redio. Binafsi nadhani habari hii ni nzuri ila mwandishi hakuifanyia utafiti wa kutosha. Bonyeza hapa uisome.

1/14/2006

Edison Hataki Kupitwa na Blogu

Blogu zitatapakaa nchi nzima. Ingawa itachukua muda, hii isituzuie tusianzishe safari hiyo sasa ya wananchi kuwa waandishi. Edison hataki kupitwa na mapinduzi haya ya zana za kupashana habari. Kwa kutumia blogu yake mpya anasema kuwa "saa ya ukombozi ni sasa, tusingoje kesho." Isije ikawa huyu ni Mtikila amejipa jina jipya!
Edison karibu. Bonyeza hapa uende uwanjani kwake.

1/09/2006

Jarida Pepe la MBONGO

Unakaribishwa kwa mikono miwili na bilauri ya maji na ndugu yetu Semkae Kilonzo. Anakukaribisha kwenye tovuti ya habari iitwayo Mbongo (ambapo utakutana na kona ya Michuzi). Kilonzo kaniambia jambo moja la msingi sana. Anasema kuwa ni jambo la busara iwapo tutaunganisha nguvu za blogu na tovuti katika kujenga jamii mpya. Nadhani swali moja ambalo ndugu yetu hawaweza kuliepuka toka kwetu ni lugha inayotumika kwenye tovuti ya Mbongo. Kilonzo, mbona?
Bonyeza hapa utembelee tovuti hiyo.

Nikisomwa na Mwalimu Mmoja Kama Bwaya Inatosha

Bwaya kaniuliza swali swali zuri sana. Anataka kujua kama makala zangu (ambazo baadhi ziko ndani ya blogu hii, upande wa kuume chini ya picha yangu) na za wengine zinasomwa na Watanzania? Bonyeza hapa usome aliyoandika. Bofya hapa usome swali lake jingine kuhusu makala zangu.
Sijui nijibu swali lake la makala zinasomwa au la kwa upande gani. Ngoja niseme hivi: historia ya mabadiliko ya jamii duniani inaonyesha kuwa kundi dogo sana huwa ndio linaongoza mabadiliko hayo. Kwahiyo unapotaka kuleta mabadiliko unaweza kuwa umegusa watu wachache sana. Muhimu ni aina ya watu uliowafikia. Kwa mfano, walimu kama wewe. Kitendo cha kuwa wewe utakuja kuwa na kazi ya kutengeneza fikra na akili za vizazi vijavyo kimenifanya nifurahi sana kujua kuwa unasoma makala zangu. Hata kama nchi nzima ni wewe peke yake unazisoma, nitaridhika kabisa maana najua kuwa idadi ya watakaosoma makala zangu kupitia wewe (yaani kutokana na mafunzo na maarifa utakayowapa uliyoyapata kwenye makala zangu) ni wengi. Ninatazama jambo hili kwa misingi hiyo.

Lakini pia makala inaweza kusomwa na watu watatu, ila kwakuwa tunaishi kwenye jamii ambayo bado ina utamaduni wa gumzo mtaani, kwenye mabasi, majumbani,n.k., wako wengi ambao hawajaisoma hiyo makala lakini watapata yaliyoko kwenye makala hiyo kupitia wale watatu waliosoma.

Nakubaliana na Bwaya kuwa watu wetu hawapendi sana kusoma masuala nyeti. Wanataka habari nyepesi nyepesi. Lakini napenda tuwatambue wale wachache wenye moyo wa dhati wa kujisomea masuala mazito. Wapo na wanaongezeka. Wapo na wanawavuta wengine. Wapo na kila siku nasoma barua zao pepe wanazoniandikia wakishukuru, wakitaka ufafanuzi zaidi, wakitoa mapendekezo ya mada wanazotaka niandike, wakinikumbusha mada nilizowahi kusema kuwa nitaziandikia na kadhalika.

Kuna wanafunzi ambao wanasoma makala zangu na kujadili katika vilabu walivyoanzisha viitwavyo Jikomboe. Kuna walimu wanaotumia makala hizo kufundishia. Kuna wazazi wananiambia kuwa wanazijadili na familia zao. Wako vijana wameanzisha vikundi mtaani vya kusoma makala zangu kwa pamoja na kuzichanachana (kuzichambua). Wako ambao pia wameitikia wito ambao nimekuwa nautoa mara kwa mara kwa vijana kuunda makundi ya kujadili masuala nyeti ya katiba, utamaduni, historia, n.k. Kundi moja la vijana hawa limeniandikia hivi karibuni kunikumbusha jambo nililozungumzia katika makala moja niliyoandika miaka mitatu iliyopita!

Kwahiyo makala zangu (na zile za akina Boniphace na Jeff) wanaweza wasisome Watanzania wote, ila kumbuka kuwa wale wanaosoma wanaishi miongoni mwa Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine wanakuwa kama wamezisoma kupitia mijadala, mabishano, gumzo, n.k., na wale waliozisoma.

Lakini narudia kusema kuwa watu wachache ndio huleta mabadiliko. Au niseme, watu wachache huongoza mabadiliko. Halafu niseme kuwa kama ninasomwa na mwalimu mtarajiwa Bwalya...ninajisikia kuwa kazi yangu sio bure. Hata wasiponisoma Watanzania wote. Mwalimu mtarajiwa mmoja anatosha kabisa.

Kuhusu utamaduni wa kujisomea, kweli hili ni tatizo kubwa nchini kwetu. Utatuzi wake unahitaji juhudi zetu binafsi kwenye familia, juhudi za watunga sera, taasisi, na serikali. Ukitaka kujenga utamaduni wa kujisomea wa nchi nzima utakata tamaa. Usianze na nchi. Anza na waliokuzunguka. Kama hujaweza kujenga utamaduni wa kujisomea wa watoto jirani zako au ndugu zako, huwezi kuanza kufikiria nchi. Utamaduni wa kujisomea wa nchi unaanza kujengwa majumbani, mitaani, nyumba kumikumi, n.k., kasha unakuja kuwa utamaduni wa taifa. Nakumbuka mimi kaka yangu alinisaidia sana kuwa na ari ya kujisomea. Nikiwa darasa la pili alinipeleka maktaba ya mkoa mjini Moshi akaniandikisha nikawa mwanachama. Toka wakati huo hadi leo nimekuwa “mgonjwa” wa kujisomea. Siku hizi nasoma kitabu zaidi ya kimoja kwa wakati mmoja (sina maana dakika hiyo hiyo).

Basi kitendo cha kaka yangu kunifanya nitambue utamu ulioko ndani ya kurasa za vitabu. Nikatumbukia kwenye kujisomea vitabu hadi ikafika wakati nikawa najifanya kuwa naenda shule kumbe nakwenda maktaba, shule siendi. Maktaba nilikuta vitabu ambavyo vilinigusa sana tofauti na vitabu vya shuleni. Masomo shuleni na vitabu tulivyokuwa tukitumia vilikuwa kama pombe ya mbege iliyotiwa maji. Masomo shuleni yalikuwa hayanipi changamoto. Sisemi kuwa huu ni mfano wa kuigwa ila nataka kuonyesha tu jinsi ambavyo nilijawa na hamasa ya kujisomea baada ya kaka yangu kunifungua macho. Toka wakati huo, ukitaka kunipata nenda maktaba au maduka ya vitabu. Utanikuta kwenye kona nimejikalia sakafuni ninachimba. Mji wowote ninaokwenda. Nchi yoyote ninayokwenda.

Kwahiyo tuna wajibu wa kuanza kubadili wale watu waliotuzunguka. Watoto wa jirani yako, watoto wa kaka yako, ndugu wa kuzaliwa tumbo moja, washikaji zako mtaani, n.k. Nikifanya hivyo, na yule akafanya hivyo, na wale nao, ndivyo tunabadili nchi.

Lakini pia tusidharau kabisa nguvu ya vyombo vya uongo (habari). Kuna nguvu nne duniani ambazo ndizo zinatufanya tuwe kama tulivyo. Nguvu hizi ndio zinatujengea mtazamo tulio nao kuhusu maisha: vyombo vya uongo/habari, dini, utamaduni-maarufu, na mfumo wa elimu.

Nje ya hapo hakuna kitu. Sasa tunaweza pia kutumia nguvu hizo hizo kupindua hali ilivyo na kujenga jamii mpya. Tunaweza kujenga hiyo jamii mpya hata tukifikia asilimia 0.5 ya Watanzania wote. Hasa walimu kama Bwalya. Fikiria mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi wangapi katika uhai wake. Sasa ukifikia mwalimu mmoja ni sawa na kufikia idadi ya wanafunzi atakaowafundisha. Na hao wanafunzi atakaowafundisha kuna ambao watakuwa walimu. Nao watafundisha wanafunzi wangapi? Na kuendelea.

1/08/2006

Uzuri wa Ugonjwa Huu ni Kuwa Una Dawa. Tutautibu!

Nimesoma aliyoandika Chemi akitushauri kupenda urembo wa asili. Amezungumzia pia yale mashindano ya "miss world." Sijui nitasema nini katika waraka huu ila najisikia kuandika kidogo kuhusu hili suala na mengine yanayohusiana nalo. Bonyeza hapa usome Chemi aliyoandika Chemi. Chemi amehoji vigezo vinavyotumika kuchagua mwanamke mmoja kuwa ni mrembo kuliko wote duniani.

Kitendo tu cha dunia yetu ya leo kutumia muda na fedha ili watu washindane kuwa nani mzuri zaidi kinahitaji kuchambuliwa kwa kina zaidi. Ukiingia ndani sana katika uchambuzi wa suala hili utakuta masuala ya mwili wa mwanamke kufanywa kama chombo cha biashara, burudani (kwa macho na tamaa za mwili za wanamume), na mwili huo kuwa ni matangazo ya biashara. Kuna itikadi inayofanya yote hayo. Katika itikadi hii mwanamke anakuwa ni chombo kinachojumuisha tu mwili (matiti, miguu, macho, nywele, rangi ya ngozi, kucha, tabasamu, mwendo, n.k.). Akili na nafsi havina nafasi. Mfumo wa ubepari ulivyo na uchu wa kufanya kila kitu kuwa bidhaa umehamisha ukandamizaji wa wanawake kwa kuupa sura ya kibiashara ambayo inaficha makucha ya ukandamizaji au kuyapa sura mpya inayofanana na ukombozi. Utaona kuwa mwanamke wa nchi za magharibi anadhani kuwa haki zake keshazipata na kuwa mwanamke anayekandamizwa ni yule aliyeko nchi za Kiislamu au Afrika wakati ambapo mwili wake (mwanamke huyo wa magharibi au yule wa Afrika anayetaka kujifanyakama huyo wa magharibi) umekuwa ni malighafi ya mfumo wa kibepari ambao bado unaongozwa na itikadi ya mfumo dume. Kama jinsi ambavyo mashirika ya umma yanavyobinafsishwa ndivyo mwili wa mwanamke unabinafishwa katika mfumo wa soko. Kinachobakia ni kuwa mwanamke anaonekana katika jamii kutokana na mwili wake na mwanaume anaonekana kutokana na anayofanya na fikra zake. Mtazamo huu unaotokana na kasumba ya mfumo dume ndio unafanya magazeti mengi kutoa safu maalum kwa waandishi au wanasafu wanaume. Na wanawake wachache wanaopewa safu wanatakiwa kuandika tu masuala ya haki za wanawake (ambapo kwa upande mmoja sio jambo baya lakini kunakuwa na mtazamo kuwa wanawake hawawezi kuongelea masuala mengine mazito kwenye jamii zaidi ya haki za wanawake).

Sasa turudi kwenye dhana kuwa dunia inaweza kumpata mwanamke mrembo duniani. Swali linakuja: mwanamke huyo atapatikanaje wakati ambapo vigezo vya urembo vinatofautiana katika mataifa na tamaduni mbalimbali? Wakati unawaza kuhusu swali hilo utajikuta ukisema kuwa tatizo sio tu vile vigezo vya kimagharibi vinavyochukuliwa kama ndio vigezo vya "dunia." Utaanza kuhoji pia mantiki ya mwanamke kupita mbele ya wanaume na wanawake na nguo ya kuogelea (tena wakati akiwa haendi kuogelea!). Au kama nilivyosema hapo awali, mantiki nzima ya kushindana eti nani mzuri zaidi duniani. Tunarudi kwenye hoja ya mwanamke kuwa ni chombo. Kuwa bidhaa kama vile mche wa sabuni au gari. Chini ya msukumo wa soko na mfumo wa utamaduni-beberu unaoendesha mashindano kama "miss world" falsafa ya mtazamo kuwa mwanamke ni chombo cha burudani kwa mwanaume na pia ni kama bidhaa sokoni imejificha chini utamaduni-maarufu unaotufanya tuone kuwa mashindano hayo ni sehemu tu ya burudani inayofurahisha na kutufanya tufurahie maisha. Na wakati mwingine anayeshinda au kukaribia kushinda akiwa ni mtu wa kwetu, tunajenga imani nzito kabisa kuwa mashindano hayo ni tukio muhimu sana duniani. Utamaduni huu unafanya sehemu kubwa ya maisha kuwa ni kama vile tamthilia ndani ya luninga, maisha ni aina ya kujirusha katika bahari ya umagharibi. Utamaduni huu unafanya itikadi ya soko na utamaduni-beberu vinakuwa sio rahisi kuonekana.
Katika dunia hii ambayo maisha yanakuwa sawa na tamthilia ya kwenye luninga au kituko fulani, masuala ya maarifa, heshima ya utamaduni mseto, mijadala ya masuala ya msingi kwa wanadamu na jamii endelevu havina nafasi yoyote. Ndio maana inakuwa rahisi kwetu kufuatilia mashindano ya "miss" world kwa karibu zaidi kuliko Mkutano wa Jamii-Habari uliofanyika Tunisia mwaka jana. Ndio maana ni rahisi kwetu kufuatilia kwa furaha na hamasa iliyokaribia kuwa uendawazimu vituko vya kwenye luninga kama Big Brother au habari za udaku magazetini. Ndio maana ni rahisi zaidi kujua nani kashinda mashindano ya “miss” Tanzania zaidi ya jina la mwanafunzi aliyepata maksi za juu kabisa kwenye mtihani wa kidato cha nne. Ndio maana ni rahisi kufuatilia kwa shauku nani atashinda “miss” world kuliko nani atapata tuzo ya Nobeli ya Amani.

Kuna itikadi ndani ya haya yote. Itikadi hii ndio iliyofanya kifo cha Diana (aliyewahi kuwa mke wa mwana wa mfalme wa Uingereza, Charles) kuwa ni tukio kubwa kabisa kwa zaidi ya wiki moja huku kifo cha Mama Tereza (aliyefariki kipindi hicho hicho) kuwa ni habari za ukurasa wa ndani kwenye magazeti na habari za sekunde au dakika kadhaa kwenye luninga zilizokuwa zikirusha matangazo ya Diana asubuhi, mchana, jioni. Ni falsafa hii, tunaporudi kwenye suala la mwanamke, inafanya matangazo mengi ya biashara kuwa yana picha za wanawake maana miili yao ni kama kitega uchumi kwenye mfumo wa soko. Miili yao inaweza kuongeza idadi ya wateja wako, kama wanavyoamini watengeneza matangazo.

Turudi kwenye suala la Chemi la vigezo. Nani kasema kuwa dunia inaweza kufikia makubaliano juu ya uzuri wa mwanamke na hata wa mwanaume? Tafsiri na vigezo vya uzuri vinatokana na utamaduni, mazingira, na wakati. Tamaduni tofauti zina vigezo tofauti. Katika vigezo hivi hakuna kigezo bora zaidi ya kingine. Kwahiyo vigezo vya ulimbwende ni tofauti kati ya jamii na jamii ila sio kuwa kuna bora zaidi ya kingine maana kila kigezo kinakidhi mahitaji ya jamii yake. Vigezo vya jamii moja vinaweza visiwe na maana yoyote ukivihamisha kwenye jamii nyingine. Ila kigezo ni bora kwa yule aliyeko kwenye utamaduni uloizalisha kigezo kinachotumika. Inaweza ikatokea kutokana na sababu za utumwa kitamaduni na kifikra, jamii moja ikadhani kuwa vigezo vyake ni vya ovyo na kutaka kuiga vigezo vya wengine kama tunavyofanya sisi. Huu ni ugonjwa, tena mbaya sana lakini uzuri wake ni kuwa una dawa.

Kama mnavyojua, wazungu na waarabu kwenye jamii za mwambao wamekuwa wakitupeleka puta miaka na miaka. Puta hii wamemkuwa wakitumia mbinu na mifumo mbalimbali. Karibu ukitazama kila upande utaona putaputa hii ya wazungu na waarabu. Putaputa ya kutufanya tujisahau, tujione kuwa sisi si kitu, sisi ni washenzi, na wao ni bora na mfano wa kuigwa. Kwahiyo mila na desturi zao zinafaa kuigwa zote bila kujali kama zina faida au la. Dini zao ni za kweli na zetu ni za uongo. Manabii wao ni wa kweli na wa kwetu ni wa uongo.
Juzi nimeweka maoni kwenye picha ya baraza la mawaziri iliyoko kwenye blogu nzuri ya picha ya Michuzi. Katika picha hiyo mawaziri wetu walivyovaa ukikata vichwa vyao ukaulizwa useme mawaziri hao ni wa serikali ya nchi gani huwezi kujua. Hawaonyeshi kabisa kuguswa na hisia za utaifa na azma ya kutangaza na kuheshimu utamaduni wetu kupitia mavazi. Gadaffi, ambaye ni mwarabu, siku hizi anatangaza mavazi yetu zaidi ya sisi wenyewe. Maoni niliyotoa hapo ni haya:
Mavazi ya mawaziri wetu yanasema mengi kuhusu fikra zao, athari za elimu (maana sio unaona kuna madokta na maprofesa?), athari za msukumo wa utamaduni-maarufu wa magharibi na mustakabali wa utamaduni utaifa wetu. Hata waziri wa utamaduni naye pia?? Lakini sijui nashangaa nini wakati jina lake (Seif Khatib) linaonyesha amevaa begani mwake utamaduni wa akina nani
.
Utaona kuwa nilikuwa nashangaa kuwa hata waziri wa kulinda na kuendeleza utamaduni wetu hakuvaa vazi la utamaduni anaotakiwa kuulinda na kuuendeleza. Lakini katika kushangaa huko nikakuta najishangaa mwenyewe kwa kumshangaa waziri huyo kwani hata jina lake mwenyewe halijatoka katika utamaduni anaotakiwa kuulida na kuuendeleza. Kama jina lake tu ni la kuazima kwanini nitegemee avae mavazi ya kutukuza utamaduni usio na jina linalomfaa? Anaitwa Seif Khatib. Yaani waziri wetu wa utamaduni amebeba jina la kiarabu huku akiwa “anaendeleza na kulinda” utamaduni wetu. Ugonjwa huu, uzuri mmoja, unatibika. Tutautibu kwa njia yoyote ile. Bonyeza hapa uone picha hiyo kwa Michuzi.

Tutazame mifano zaidi ya gonjwa hili baya lenye dawa. Mifano: unaweza kwenda Rombo ndani ndani kabisa, ukakuta duka limepewa jina la kiingereza wakati ambapo mwenye duka na wateja wake hawafahamu kiingereza sawasawa. Tazama vikundi vya sanaa za maonyesho. Wakati vikundi hivi kazi yake, kama katiba zao zinavyosema, ni kuendeleza utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika, majina yao ni ya kiingereza. Unakutana na Tanzania One Theatre, Muungano Cultural Troupe, OYA Theatre Group, Chemchem Art Group, Albino Revolution Cultural Troupe, Chang'ombe Youth Center, Nyunyusa Dancing Troupe, Roots and Kulture, n.k.

Kitendo cha kudai kuendeleza utamaduni wa Mtanzania au Mwafrika na kushindwa kabisa kupata jina la kundi toka katika utamaduni unaouendeleza ni kielelezo cha jinsi gani ugonjwa unaotokana na ukoloni mamboleo, ukoloni uchwara, na ubeberu wa kitamaduni ulivyotuathiri. Kwahiyo usishangae unapoona eti "miss" Afrika akiwa ni yule mrembo aliyechaguliwa na wazungu na kwa kutumia vigezo toka katika tamaduni zao na msukumo wa soko na itikadi za kibepari. Msukumo huu wa soko unatoka pande nyingi ikiwemo pamoja na makampuni ya nguo, vipodozi, kampuni za madawa, mahospitali (yanayofanya upasuaji wa kupunguza watu unene), makampuni ya matangazo, vyombo vya uongo (habari), n.k. Makampuni yote haya yanafaidika kwa namna moja au nyingine dunia inapokuza vizazi vyake kwa ndoto kuwa mwanamke mwembamba ndiye kilele cha uzuri. Kwa maneno mengine, mfumo wa kibeberu unafaidika sana na ugonjwa tulionao Waafrika. Na kama mnavyojua mfumo huu umekuwa ukitutumia na kutumia rasilimali zetu miaka na miaka huku ukijibadili kutokana na upepo wa wakati. Kulikuwa na wakati wa ukabaila, ubepari, na ubeberu. Mifumo hii ndio ilizalisha utumwa, ukoloni, ukoloni mamboeo, utandawizi (kuna tofauti kati ya utandawazi ambao ni mpana zaidi na utandawizi ambao ni mfumo unaoendeshwa na itikadi inayotaka dunia nzima kutawaliwa na kundi dogo la wanaume wa kizungu wanaoishi Ulaya na Marekani).

Niishie hapa. Siku kama leo ni zile siku ninapoandika bila kujua hasa ninaelekea wapi na nitaishia wapi. Kama nimezurura huku na kule bila kuishika mada sawasawa nisamehe. Huu ulikuwa ni mtiririko wa hisia na fikra. Kumbuka hii ni jumapili jioni na ninamsikiliza Bob Marley kwa sauti ya juu! Uhuru!

1/07/2006

Somo, Ngoma, na Tambiko la Kwanzaa





















Nikifundisha watoto (unajua tena samaki mkunje angali mbichi) maana ya Kwanzaa na umuhimu wake kwa watu wenye asili ya Afrika. Katika picha nyingine hiyo: huyo ni Barry akifungua somo la Kwanzaa kwa ngoma baada ya kutoa tambiko. Barry ni Mmarekani Mweusi ambaye amejifunza kupiga ngoma aina ya Djembe katika nchi ya Guinea, Afrika Magharibi. Mikono yake migumu kama tairi la nyuma la trekta aina ya Kubota (hivi Makubota yaliishiaga wapi?). Juu ya Kwanzaa soma niliyoandika hapo chini na pia bonyeza hapa.
Bonyeza juu ya picha zenyewe uzione kwa karibu zaidi.

Kwanzaa: Meza ya Umoja (na kanga za Mnazi Mmoja!)
















Nadhani baadhi mnafahamu kuwa mimi husherehekea sikukuu ya Kwanzaa. Moja ya mambo yanayofanywa wakati wa kusherehekea sikukuu hii inayoenzi maadili ya Kiafrika ni kuandaa meza ya Kwanzaa inayojumuisha vyakula, mishumaa, kikombe cha umoja, n.k. Unaona mwenye kwenye picha hii. Unaweza kuwa uliwahi kuona kanga hizi zikiuzwa pale Mnazi Mmoja. Meza hii niliandaa kwenye mhadhara ambao nilifundisha watoto weusi juu ya sikukuu hii na umuhimu wake kwao kama watu wenye asili ya Afrika. Baada ya tambiko, mafundisho, na ngoma, tulijumuika katika karamu. Neno karamu (ambalo liko katika wimbo wa Lionel Richie wa All Night Long) ndio hutumika wakati wa sikukuu ya Kwanzaa. Pia wakati wa sikukuu hii wamarekani weusi wanaojali Uafrika wao husalimiana "habari gani." Kutegemea na maadili ya siku hiyo (yako saba) mtu atajibu. Kama ni siku ya ujima, ukimsalimu atajibu, "Ujima."
Bonyeza hapa usome zaidi kuhusu Kwanzaa.
Bonyeza juu ya picha ili uzione vizuri zaidi.

Mkutano wa Podikasiti: podikasiti darasani

Mkutano ndio unafikia mwisho. Umebaki muda wa mvinyo, kujuana zaidi na kubadilisha kadi. Mada tuliyokuwa tukiijadili awali ya matumizi ya podikasiti kufundishia unaweza kuiona kwa kubonyeza hapa. Kiungo nilichotoa hapo chini kinaweza kukupa shida kuipata. Hiki cha sasa kinakupeleka moja kwa moja. Unaweza kuona mfano wa kazi ya watoto wa shule waliyofanya kwa kutumia teknolojia ya podikasiti. Bonyeza hapa.

Kinachofuata sasa ni Jikomboe kupanuka. Kwa sasa Jikomboe, yaani blogu hii, ni kama gazeti pepe langu. Sasa itapanuka kuwa sio gazeti pepe tu bali redio pepe na luninga pepe (podikasiti ya video). Mwambieni Mengi akae chonjo, wanablogu tunaingilia nyanja ya habari kwa ari mpya na nguvu mpya (nakopa maneno yaliyotumika kutufanya tuamini kuwa tunajenga nchi mpya kwa sura zile zile au sura mpya zenye mtazamo kama zile sura za zamani).

Kama tusemavyo kule Moshi ninawaambia, "Watashaa." Kama hujui maana yake muulize Mtafiti.

Matumizi ya Podikasiti Kufundishia

Hivi sasa tunajadili matumizi ya teknolojia ya podikasiti kufundishia wanafunzi. Unaweza kusoma yote tunayojadili katika ukurasa huria wa "wiki" kwa kubonyeza hapa.
Kuna wahudhuriaji zaidi ya mia moja katika mkutano huu kuhusu podikasiti. Unadhani watu weusi tuko wangapi? Huwezi kuamini...Kama zama za mapinduzi ya viwanda zilitupita, tusikubali zama za maarifa na habari zitupite. Haiwezekani.

Umemuona mwanablogu huyu?

Niko ndani ya ukumbi panaponyikia mkutano huu niliouzungumzia jana. Mara naona waraka pepe toka kwa Silvery Duttu akiniambia kuwa blogu yake iko tayari kutangazwa. Usisumbuke na kiingereza alichokiweka hapo, hii itakuwa blogu ya Kiswahili ili kuenzi lugha anayoitumia asubuhi, mchana, jioni. Bonyeza hapa umtembelee kumkaribisha.

1/06/2006

Mtandao wa Tarakilishi na Ustawi wa Lugha

Moja ya sababu kubwa zilizonifanya nianze kublogu kwa Kiswahili ni imani kuwa ili dunia ya leo na kesho (ambayo ni ya zama za habari na maarifa) iwe yetu sote, tunapaswa kutumia teknolojia mpya za habari na mawasiliano kukuza, kuhifadhi, na kuendeleza lugha mbalimbali za wana dunia. Dunia yetu ina lugha kama 6000 hivi lakini ni lugha 12 tu ambazo zinatawala katika mtandao wa tarakilishi. Na katika hizo 12 ni lugha mbili au tatu ambazo hasa ndio zinatumika kueneza habari na maarifa. Wakati huo huo wataalamu wa lugha wanatangaza kila mwaka idadi ya lugha zinazokufa. Lugha inapokufa ni sawa na kuungua kwa moto kwa maktaba kubwa kuliko zote duniani. Unajua lugha, zaidi ya kuwa ni chombo cha mawasiliano, ni hazina au benki ya maarifa, mila, na utamaduni. Maarifa ya jamii huhifadhiwa kwenye lugha. Ili ujue dawa za mitishamba zinazotumiwa na Wa-Kahe, kwa mfano, unapaswa kujua Kikahe. Kikahe kikifa basi na elimu hiyo ya dawa inakufa (nimetumia mfano huu maana ni watu wachache wanajua kuwa Kikahe ni lugha na pia kwakuwa hii ni kati ya lugha ambazo zinapotea). Njia mojawapo ya kuhifadhi lugha ni kuitumia. Lakini ninalopenda kusisitiza hapa ni kuwa unapoitumia lugha au kitu chochote katika teknolojia pepe au elektroniki unakuwa umehifadhi milele na milele. Kublogu ni tofauti na kuchapisha kitabu ambapo kinaweza kuungua, kupotea, kuliwa na mchwa au panya, kuibiwa, n.k. Unapohifadhi mambo kwa njia za elektroniki au pepe unakuwa umehifadhi daima.
Kwahiyo visa tunavyoandika, mashairi, habari, maoni, n.k. vinachangia kuiweka lugha yetu katika mtandao pepe. Zaidi ya kuwa tunahifadhi tunayoandika na pia kuwezesha wengine kuyasoma wakati wowote, popote pale, tunaongeza idadi za lugha mtandaoni na hivyo kufanya mtandao usiwe tu ni mahali pa wale wenye kuzungumza Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kijapani, Kijerumani, n.k. Jitihada zetu ni moja ya jitihada za kufanya mtandao pepe kuwa wa kidemokrasia na unaojumuisha sauti za tamaduni na lugha mbalimbali. Kama mtandao pepe ni kijiji cha dunia, basi hicho kijiji kisiwe na lugha moja tu bali lugha mbalimbali za wanadunia.
Basi nilipoanza kublogu kwa Kiswahili nilikuwa nikisema jambo moja kwenye kila mahojiano niliyokuwa nikifanya. Wakati ule ilikuwa ni habari nzito. Eti, "kuna jamaa anablogu kwa lugha ya Kiafrika." Walikuwa wakiniuliza kwanini ninablogu kwa Kiswahili ninawambia kuwa ninaendeleza kazi waliyokuwa wakiifanya akina Ngugi na Chinweizu. Ngugi, kama unakumbuka, aliandika kitabu chake kiitwacho "Decolonising the African Mind." na Chinweizu (Mloyi unakumbuka maandiko yake ya Negro negropobia?) aliandika Decolonising African Literature. Katika vitabu hivi walikuwa wakitutaka tuondoe ukoloni mamboleo na ukoloni uchwara katika akili zetu. Walikuwa wakizungumzia hasa fasihi andishi. Wakati ule mapinduzi ya teknolojia za mawasiliano yalikuwa hayajafika katika hatua tuliyoko hivi sasa. Kwahiyo wakati ule ukiongelea fasihi andishi unazungumzia vitabu. Hivi sasa tuna ulimwengu mpya ambao umetuletea maandishi pepe, fasihi pepe, riwaya pepe, n.k. Tuna mtandao pepe. Kinachofanyika hivi sasa ni muendelezo wa kazi za akina Ngugi na Chinweizu. Muendelezo huu, katika mahojiano, nilikuwa nikisema, "I am simply decolonising the Internet."
Na hiyo ilikuwa ni moja ya sababu zilizonifanya nianza kunyonya titi la mama hata kama la mbwa kwa kutumia teknolojia ya blogu. Sasa sio mimi peke yangu au sisi wenyewe tunaoona umuhimu wa kuwa na lugha mbalimbali katika mtandao pepe. Shirika la Sayansi, Elimu, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetoa ripoti kuhusu matumizi ya lugha mbalimbali katika mtandao wa tarakilishi. Shirika hili linaamini kuwa dunia itakuwa bora zaidi pale ambapo lugha nyingi zaidi zitaanza kutumika katika mtandao wa tarakilishi. Katika ripoti yake limesema:
UNESCO has been emphasizing the concept of “knowledge societies”, which stresses plurality and diversity instead of a global uniformity in order to bridge the digital divide and to form an inclusive information society. An important theme of this concept is that of multilingualism for cultural diversity and participation for all the languages in cyberspace.

Kusoma ripoti nzima (katika pdf) bonyeza hapa.

Naanza Mwaka wa Kirumi kwa Mkutano

Kesho naenda mkutanoni katika chuo kikuu hiki hapa. Mikutano haitakaa iishe dunia hii. Unadhani? Naanza mwaka wa Kirumi kwa mikutano. Mkutano huu ni tofauti kidogo na mikutano mingi tuliyoizoea. Kuna aina ya mikutano ambayo siku hizi inayoitwa "mikutano huria" au wakati mwingine wanatumia neno ambalo nimelishindwa kulitafsiri: unconference. Ni kama kusema vile "mkutano usio mkutano"! Mkutano huria ni mkutano ambao hauna watoa mada na wapokea mada. Wahudhuriaji wote ni watoa mada. Kila mmoja ni mshiriki. Kila mmoja anachukuliwa kuwa ni mtalaamu na ana jambo la kusema au kuchangia. Hii ni tofautina mikutano ambayo kunakuwa na wasikilizaji wanaoketi kimya huku "mtaalamu" au "msomi" "akiwaelimisha" juu ya jambo fulani.
Katika mkutano huria, wanaohudhuria ndio wanaoamua nini kijadiliwe au mada zipi ndio muhimu. Na ndivyo mkutano ninaohudhuria kesho ulivyoandaliwa. Bonyeza hapa usoma kuhusu mikutano huria. Mkutano huria ninaodhudhuria kesho unahusu masuala ya podikasiti. Soma kwa kifupi kuhusu podikasiti hapa. Mkutano unaitwa Podcastercon 2006. Bonyeza hapa usome tovuti kuhusu mkutano huo na hapa usome blogu ya mkutano huo.
Nitaandika zaidi juu ya mkutano huo nikiwa mkutanoni hapo.


Unajua Jinsi Ya Kuandika Kuhusu Afrika?

Binyavanga Wainaina ameandika makala moja nzuri sana ambayo inatumia kejeli kutazama jinsi ambavyo watu weupe wanavyolitazama bara la Afrika. Katika makala hii anatoa ushauri wa jinsi ya kuandika habari za Afrika. Lakini, kama nilivyosema hapo awali, ushauri wenyewe ni kejeli fulani hivi. Bonyeza hapa usome makala yenyewe.
Binyavanga ni mwanzilishi wa jarida la fasihi nchini Kenya liitwalo Kwani?, ambalo unaweza kulisoma kwa kubofya hapa. Pia unaweza kusoma zaidi juu yake kwa kubonyeza hapa.
Asante Kenyan Pundit kwa makala hii.






1/05/2006

Ethan Zuckerman Kafurahia Blogu ya Mwandani

Mwandani kaandika kisa kimoja kikali sana. Nilipokuwa namsoma nilikuwa najisemea, "Hivi bila blogu habari kama hii Tunga angeitoa wapi?" Ingebidi labda atafute gazeti au labda atume barua pepe kwa marafiki zake. Kisa murua sana maana kinaonyesha masahibu ya kuishi Ughaibuni na pia madhara ya vyombo vya habari vya magharibi ambavyo habari za Afrika kwao ni zile zinazohusu maafa au ufedhuli wa watwawala. Pia kisa hiki kinaonyesha jinsi ambavyo wananchi wengi wa magharibi wana ufahamu mdogo sana wa dunia iliyowazunguka.
Furaha yangu imekuwa kubwa zaidi nilipogundua kuwa sisi wazungumzaji tu wa Kiswahili waliofurahia aliyoandika Mwandani bali pia wazungumzaji wa Kiingereza. Rafiki yangu na mmoja wa waanzilishi wa mradi wa Sauti za Dunia, Ethan Zuckerman, amependa sana aliyoandika Mwandani. Amemzungumzia Mwandani kwenye blogu yake (na niliposoma pale kuna msomaji mwingine alishatoa maoni na kusema amependa sana). Bonyeza hapa usome aliyoandika Ethan kuhusu Mwandani. Bonyeza hapa usome alichoandika Mwandani.



1/02/2006

Mjadala wa Neno Muafaka la Teknolojia ya Blogu Unaendelea

Ule mjadala wetu kuhusu neno muafaka la teknolojia hii ya blogu bado unaendelea. Maneno ambayo yamependekezwa hadi hivi sasa ni haya:
Duru, Kasiri, Lipuli,Vuga, Dondoo, Lipuli, Vuga, Uwanja wa Fikra Komavu, Gazeti Tando, Ngwanga, Bawazi, Dimba, Pukutu, Dafinapepe, na Ungo.
Bonyeza hapa ili usome sababu za kupendekezwa kwa maneno haya. Mtu yeyote anaweza kushiriki kwenye mjadala huu hata kama sio mwanablogu.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com