1/06/2006

Mtandao wa Tarakilishi na Ustawi wa Lugha

Moja ya sababu kubwa zilizonifanya nianze kublogu kwa Kiswahili ni imani kuwa ili dunia ya leo na kesho (ambayo ni ya zama za habari na maarifa) iwe yetu sote, tunapaswa kutumia teknolojia mpya za habari na mawasiliano kukuza, kuhifadhi, na kuendeleza lugha mbalimbali za wana dunia. Dunia yetu ina lugha kama 6000 hivi lakini ni lugha 12 tu ambazo zinatawala katika mtandao wa tarakilishi. Na katika hizo 12 ni lugha mbili au tatu ambazo hasa ndio zinatumika kueneza habari na maarifa. Wakati huo huo wataalamu wa lugha wanatangaza kila mwaka idadi ya lugha zinazokufa. Lugha inapokufa ni sawa na kuungua kwa moto kwa maktaba kubwa kuliko zote duniani. Unajua lugha, zaidi ya kuwa ni chombo cha mawasiliano, ni hazina au benki ya maarifa, mila, na utamaduni. Maarifa ya jamii huhifadhiwa kwenye lugha. Ili ujue dawa za mitishamba zinazotumiwa na Wa-Kahe, kwa mfano, unapaswa kujua Kikahe. Kikahe kikifa basi na elimu hiyo ya dawa inakufa (nimetumia mfano huu maana ni watu wachache wanajua kuwa Kikahe ni lugha na pia kwakuwa hii ni kati ya lugha ambazo zinapotea). Njia mojawapo ya kuhifadhi lugha ni kuitumia. Lakini ninalopenda kusisitiza hapa ni kuwa unapoitumia lugha au kitu chochote katika teknolojia pepe au elektroniki unakuwa umehifadhi milele na milele. Kublogu ni tofauti na kuchapisha kitabu ambapo kinaweza kuungua, kupotea, kuliwa na mchwa au panya, kuibiwa, n.k. Unapohifadhi mambo kwa njia za elektroniki au pepe unakuwa umehifadhi daima.
Kwahiyo visa tunavyoandika, mashairi, habari, maoni, n.k. vinachangia kuiweka lugha yetu katika mtandao pepe. Zaidi ya kuwa tunahifadhi tunayoandika na pia kuwezesha wengine kuyasoma wakati wowote, popote pale, tunaongeza idadi za lugha mtandaoni na hivyo kufanya mtandao usiwe tu ni mahali pa wale wenye kuzungumza Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kijapani, Kijerumani, n.k. Jitihada zetu ni moja ya jitihada za kufanya mtandao pepe kuwa wa kidemokrasia na unaojumuisha sauti za tamaduni na lugha mbalimbali. Kama mtandao pepe ni kijiji cha dunia, basi hicho kijiji kisiwe na lugha moja tu bali lugha mbalimbali za wanadunia.
Basi nilipoanza kublogu kwa Kiswahili nilikuwa nikisema jambo moja kwenye kila mahojiano niliyokuwa nikifanya. Wakati ule ilikuwa ni habari nzito. Eti, "kuna jamaa anablogu kwa lugha ya Kiafrika." Walikuwa wakiniuliza kwanini ninablogu kwa Kiswahili ninawambia kuwa ninaendeleza kazi waliyokuwa wakiifanya akina Ngugi na Chinweizu. Ngugi, kama unakumbuka, aliandika kitabu chake kiitwacho "Decolonising the African Mind." na Chinweizu (Mloyi unakumbuka maandiko yake ya Negro negropobia?) aliandika Decolonising African Literature. Katika vitabu hivi walikuwa wakitutaka tuondoe ukoloni mamboleo na ukoloni uchwara katika akili zetu. Walikuwa wakizungumzia hasa fasihi andishi. Wakati ule mapinduzi ya teknolojia za mawasiliano yalikuwa hayajafika katika hatua tuliyoko hivi sasa. Kwahiyo wakati ule ukiongelea fasihi andishi unazungumzia vitabu. Hivi sasa tuna ulimwengu mpya ambao umetuletea maandishi pepe, fasihi pepe, riwaya pepe, n.k. Tuna mtandao pepe. Kinachofanyika hivi sasa ni muendelezo wa kazi za akina Ngugi na Chinweizu. Muendelezo huu, katika mahojiano, nilikuwa nikisema, "I am simply decolonising the Internet."
Na hiyo ilikuwa ni moja ya sababu zilizonifanya nianza kunyonya titi la mama hata kama la mbwa kwa kutumia teknolojia ya blogu. Sasa sio mimi peke yangu au sisi wenyewe tunaoona umuhimu wa kuwa na lugha mbalimbali katika mtandao pepe. Shirika la Sayansi, Elimu, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetoa ripoti kuhusu matumizi ya lugha mbalimbali katika mtandao wa tarakilishi. Shirika hili linaamini kuwa dunia itakuwa bora zaidi pale ambapo lugha nyingi zaidi zitaanza kutumika katika mtandao wa tarakilishi. Katika ripoti yake limesema:
UNESCO has been emphasizing the concept of “knowledge societies”, which stresses plurality and diversity instead of a global uniformity in order to bridge the digital divide and to form an inclusive information society. An important theme of this concept is that of multilingualism for cultural diversity and participation for all the languages in cyberspace.

Kusoma ripoti nzima (katika pdf) bonyeza hapa.

3 Maoni Yako:

At 1/07/2006 01:21:00 AM, Blogger Mija Shija Sayi said...

"Maarifa ya jamii huifadhiwa katika lugha."..Ndesanjo umeniongezea elimu yangu juu ya matumizi lugha. Hili sikuwahi kulifikiria kiundani hivyo kwamba tunapoteza hadi madawa yetu ya asili kwa kuisaliti lugha. Nitawafundisha na wengine, hasa hiki kizazi kipya.

 
At 1/07/2006 01:53:00 AM, Blogger mark msaki said...

mwendo mzuri tunakwenda. cha msingi ni watu kama mimi kuhakiki mabesela yangu mara ninapoandika makala au maoni.

ndesanjo, nakutakia krismasi njema! nadhani wewe haufuati kalenda ya gregory

 
At 1/07/2006 02:18:00 AM, Anonymous Joji said...

Shukrani kwa maoni yako pia kazi yako nzuri!

QUOTE
ili dunia ya leo na kesho (ambayo ni ya zama za habari na maarifa) iwe yetu sote, tunapaswa kutumia teknolojia mpya za habari na mawasiliano kukuza, kuhifadhi, na kuendeleza lugha mbalimbali za wana dunia.
UNQUOTE
Nakuunga mkono kabisa.

Lakini kwa sasa shida Afrika ya Mashariki na ya Kati ni ukosefu wa miundo mbinu ili watu wote wafaidike.

Salamu.

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com