1/30/2005

JIFUNZE KISWAHILI

JIBINI = CHEESE

TOFAUTI YA "VEGETARIAN," "VEGAN," NA "RAW FOODIST" NA WENGINE

Binadamu tuna tabia za aina mbalimbali kuhusiana na vyakula. Kuna watu wasiokula nyama kutokana na sababu mbalimbali kama za dini au afya. Hawali chochote kinachotembea ardhini, ruka juu ya nchi, kuogelea baharini (samaki). Hawa wanaitwa ni wala majani, mbegu, na matunda, kwa kiingereza "vegetarians." Kuna wengine wasiokula sio tu nyama bali chochote kile kinachotokana na wanyama. Hawa kwa kiingereza (bado natafuta jina la kiswahili) wanaitwa vegans. Tofauti ya "vegetarians" na "vegans" ni kuwa "vegetarians" huwa wanakula mayai, jibini, kunywa maziwa, n.k. Wakati "vegans" hawagusi hivyo vitu na wengine wala hawavai nguo, mikanda, viatu, au kubeba mikoba iliyotengenezwa kutokana na ngozi za wanyama. Nenda hapa na hapa kupata undani wa "veganism."

Halafu kuna wengine ambao ndio funga kazi. Hawa ni wala vyakula vibichi. Kwa kimombo wanaitwa "raw foodist." Hawa hawapiki chakula hata siku moja. Kwa maana hiyo hawahitaji kuwa na jiko majumbani mwao! Inaaminika kuwa hakuna njia inayoharibu virutubisho vilivyomo ndani ya chakula kama kupika. Watu wengi hawafahamu kuwa binadamu walitembea juu ya dunia hii kwa miaka mingi sana kabla moto haujagunduliwa. Kwahiyo wanachofanya ma-raw foodist sio jambo geni. Wanadamu walikuwa wakila vyakula vibichi kwa miaka mingi sana. Na wako wanaoendelea hadi leo. Wasome hapa.

Kuna kundi pia la wanaoishi kwa kula matunda tu. Wala matunda wanaitwa "fructarians." Wasome hapa.

Kuna watu wengine wanaitwa "freegans" ambao wao chakula wanachokula ni kile ambacho kimeachwa, kusazwa, au kutupwa na watu wengine. Wasome hapa.

Kuna watu wengine ambao wanachukulia vegans na makundi mengine kuwa kama makundi madogo ndani ya mfumo mzima wa vegetarianism (ulaji wa mboga, mbegu, na matunda). Uchambuzi wangu wa makundi haya naweza kusema kuwa ni wa rahisi na juujuu kuliko ilivyo hasa. Tembelea hapa usome zaidi juu ya "vegetarianism" na mahusiano ya mfumo huu wa maisha na dini mbalimbali.


BLOGU YA SAUTI

Kuanzia sasa nitakuwa ninatumia teknolojia ya blogu ya sauti (audioblog) pamoja na hii ya maandishi. Kwahiyo hata nikiwa safarini, porini, milimani, vijijini, chooni, n.k. naweza kutumia simu ya mkono kuwasiliana nanyi ndugu zangu.

this is an audio post - click to play

TOVUTI BADO ZANITIA KICHEFUCHEFU

Tafadhali kama kuna mtu mwenye limao au ndimu anipatie ili niwe nakula kabla sijatembelea tovuti ya bunge la Tanzania na ile ya ikulu. Kila ninapotembelea tovuti hizi mbili za nchi inayojulikana kwa lugha ya Kiswahili, lugha ambayo ndio inajulikana na kutumiwa na wakesha hoi masaa 24, ninakaribia kutapika kama mtu aliyemeza konokono kwa bahati mbaya. Sijui kama ni mimi peke yangu ninayehoji sababu ya tovuti hizi kuwa katika lugha ya akina Tony Blair na Malkia Lizabeti na sio lugha inayotumiwa na akina Rafaeli (ndio, yule Rafaeli wa kwenye wimbo wa Saganda!), Kalubandike, Mama Giresi, Masanja, Zabuloni, n.k.
Ukitembelea tovuti ya ile ikulu iliyojengewa kuta kama ule wimbo wa Paul Ndunguru usemavyo, "Wanajenga kuta kuzuia wezi wenzao...," unakuta kuna salamu za mwaka mpya wa kirumi wa 2005 ambazo zimetolewa na Rais wa Tanzania kwa wananchi wa Uingereza!
"Inakuwaje rais wa Tanzania atoe salamu kwa wapiga kura wa nchi nyingine na sio wananchi wake?"
Usiniulize. Sina jibu.
Na kama huniamini nenda hapa ujionee mwenyewe. Ukiwa umefumbua macho utaelewa kwanini nimesema kuwa salamu ya Rais ni kwa ajili ya wananchi wa Uingereza.
Leo sio mara yangu ya kwanza kulalamika juu ya hili. Na sio ya mwisho. Lazima tukomeshe huu mchezo unaochezwa na waliozama katika bahari ya utumwa wa fikra.
Rafiki yangu mmoja anayesoma Afrika Kusini kaniambia kuwa tovuti hizi zimegharamiwa na shirika la maendeleo la "umoja" wa mataifa (UNDP). Kuna uwezekano kuwa tovuti hizi zinatumia lugha yao kwakuwa "msaada" umetoka kwao. Hili neno "msaada" karibu nitalifuta kabisa kwenye misamiati yangu. Naona limepoteza maana yake siku nyingi.

1/29/2005

NUKTA YA MWISHO

Hatimaye yule mwandishi wa BBC, Ivan Noble, ameweka nukta ya mwisho katika kitabu chake cha kumbukumbu kilichokuwa mtandaoni kikionyesha maisha yake baada ya kupatikana na kansa ya ubongo. Ameweka nukta ya mwisho baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya. Msome.
Kitabu chake cha kumbukumbu kilikuwa kikisomwa na watu 100,000 kwa siku.

MAKALA TATU MPYA

Jana nilipandisha makala moja mpya: Elimu ni Utumwa? Leo nimeweka nyingine tatu ambazo niliziandika nyuma kidogo. Zote hizi tatu zilitoka kwenye safu yangu ya Gumzo la Wiki. Makala ya wiki hii nitaiweka baada ya kutolewa gazetini. Makala za leo ni: 1. WEWE MWENYE RASTA NJOO! 2. NANI ATAWAKAMATA POLISI? 3. YESU/ISA NA WATANZANIA

KWA AJILI YA SANKOFA: U-DJ NA UTENGENEZA SINEMA

Sankofa, habari za masiku? Nitajibu waraka wako ambao umeniandikia muda kidogo. Nimesoma habari ya DJ Spooky nikakukumbuka. DJ Spooky (Paul Miller): anafanya jambo ambalo limenipendeza sana. Ameuganisha u-DJ na utengeneza filamu. Kama jinsi ma-DJ wanavyochanganya muziki (nyimbo, vyombo, vibwagizo, n.k.) ndivyo DJ Spooky anafanya. Ameitengeneza upya ile sinema ya Birth of a Nation, matokeo yake imepatikana filamu ya Rebirth of a Nation.
Pia utaona kazi kwenye tovuti yake mradi wa A Different Utopia ambao ni mchanganyiko wa muziki, insha, teknolojia ya flash katika kuelezea falsafa ya Fela Kuti kupitia makazi yake ambayo aliyaita Jamhuri ya Kalakuta.

NINATAMANI SANA SANA...

Ninatamani mambo mengi. Mojawapo ni hili: Ninatamani sana siku moja nikutane ana kwa ana na wananchi wanaoitwa, "wananchi wenye hasira kali." Hawa ni wale ambao wakisikia, "mwizi!" damu inawachemka, wanatafuta mawe, mitaimbo, nyundo, matairi, bisibisi, patasi, petroli, na viberiti ili wamuue mtu ANAYEDAIWA kuwa mwizi.

Ukikuta hawa wananchi wenye hasira kali wanaua binadamu mwenzao, mtafute aliyewasha kiberiti, kisha muulize, "Hivi jamaa kaiba nini?" au, "Kamwibia nani?" Utasikia majibu ya ajabu kweli.
"Ah, jamaa wanasema kaiba mtaa wa pili." Atakujibu. Anayekujibu hivyo ndiye aliyewasha moto uliomteketeza marehemu. Ukimuuliza akutajie majina ya hao " jamaa wanaosema" kuwa kaiba mtaa wa pili, atakachoweza ni kuwataja kwa jina la "jamaa." Atasema, "Jamaa waliomkamata ndio walimuona."
Jamaa ndio akina nani hao?
Hajui.

Msimamishe yule aliyemwangushia tofali kichwani lililomfanya marehemu atoe damu puani na machoni. Muulize swali, "Kafanya nini marehemu?"
Atakujibu, "Wamezidi hawa!"

Nimesema kuwa ninatamani sana kukutana na "wananchi wenye hasira kali." Nataka kuwauliza swali hili: Wezi wa kuku mnawapeleka jela. Wezi wa shilingi 1,000 mnawapiga mawe na kuwachoma moto hadi kufa, JE WEZI WA MAMILIONI YA UMMA MNAWAFANYA NINI?
Hizo "hasira kali" zinakuwa wapi wakati nchi ikipigwa mnada??

Natamani sana sana kukutana nao. Ukikutana nao naomba nisaidie kuwauliza swali hilo kisha nitumie majibu.
***********************************************************************************
Yesu akauambia umati, "Asiye na dhambi awe wa kwanza kurusha jiwe." Mara wakaondoka mmoja mmoja na kumwacha na yule mwanamke aliyeshatakiwa kwa uzinzi.

1/28/2005

MAKALA MPYA

Nimeweka makala mpya toka kwenye safu yangu ya Gumzo la Wiki katika gazeti la Mwananchi. Makala inaitwa Elimu ni Utumwa? Kama kawaida iko kwenye kona ya makala zangu, upande wa kuume, chini ya picha yangu. Kichwa cha makala hii kilikuwa ni hiki: Elimu ni Ufunguo wa Utegemezi. Nimekibadili kuwa swali: Elimu ni Utumwa? Makala hii ilipaswa kusomwa kama sehemu ya pili ya makala nyingine kuhusu usomi na wasomi. Nimeamua kupeleka mambo kinyume. Nimeanza kukupeni sehemu ya pili kisha niwapeni sehemu ya kwanza!

MAFUNZO KWA VIDEO KWA WAPENDA TEKNOLOJIA

Kuna mafunzo ya aina mbalimbali kwa njia ya video kwa wale wanaopenda masuala ya teknolojia. Kongoli hapa.

KISWAHILI LUGHA YETU

Terms of reference = Hadidu za rejea
Vinegar = Siki
Furniture = Samani

Kumbuka kuwa Ice ni barafu na snow ni theluji.

KWENDA KIGOMA NA KURUDI MAREKANI SIKU HIYO HIYO

Kumbe hivi karibuni Watanzania tulioko ughaibuni tutaweza kwenda Kigoma na kurudi ughaibuni siku hiyo hiyo. Itakuwa hivyo kama yaliyosemwa kwenye habari hii sio si-hasa bali ukweli.

KUTA ZIKIANGUKA LAZIMA TUSHANGILIE

Kuta zile zinazojengwa na wa-twawala (yaani watawala au "viongozi") kuzuia uhuru wa fikra na maoni zinapoanguka lazima tushangilie. Kama ilivyotokea hapa.

1/27/2005

BLOGU MPYA YA MTANZANIA ALIYEKO UGANDA

Ndio kunakucha katika ulimwengu wa blogu za Kiswahili. Kuna mwanablogu mpya wa Kiswahili. Huyu ni Innocent Kessy, Mtanzania aliyeko masomoni nchini Uganda. Mtembelee katika blogu yake ya Dira Yangu hapa.

1/26/2005

NOTEBOOK: AFRIKA

Kuna mwandishi mmoja wa gazeti la The Christian Science Monitor ambaye ana bloguluninga. Yuko Afrika. Sijaitazama vizuri. Itembelee. Bloguluninga inakuja juu sana hivi sasa. Nimepata habazi zake toka kwa Ethan.

PADRI KARUGENDO NA MAKALA ZAKE

Kutokana na maombi ya wengi kuhusu makala za uchambuzi na falsafa za Padri Karugendo, ambazo hutoka kila alhamisi katika gazeti la RAI (nguvu ya hoja) nchini Tanzania, ninaweka kona maalum kwa ajili ya makala zake. Hivyo mtaanza kumsoma hivi karibuni.

Ninapenda kutangaza kuwa mwezi ujao, ambao ni mwezi wa historia ya watu weusi hapa Marekani, kutakuwa na mfululizo wa mambo mbalimbali ya kukomboa fikra zetu katika kuenzi historia yetu. Afadhali ukose kuja hapa mwaka mzima ila sio mwezi wa pili!


1/25/2005

UNAMFAHAMU MSHAIRI HUYU?

Kuna mshairi mwingine ambaye staili yake ninaipenda sana. Napenda wasiomfahamu, wamfahamu. Huyu ni Saul Williams. Ukifika kwenye tovuti yake unaweza kusikiliza baadhi ya mashairi yake. Unaweza pia kusikiliza na hata kuchota CD yake ya hivi karibuni. Pia unaweza kutazama baadhi ya video zake. Nenda hadi mwisho wa ukurasa wa kwanza na ubonyeze panaposema: The Work. Unaweza ukawa umetazama filamu ya Slam ambayo aliicheza.

SUMAYE ANASHANGAA MIJINAUME...

Nenda kwenye blogu ya Furahia Maisha Yako. Kuna habari ya Sumaye kushangaa mijinaume inayopenda ngono kiasi ambacho inatoa machozi kabisa, na hata kutumia maelfu kwa ajili ya vitanda katika hoteli za kifahari lakini shilingi 100 ya kondomu hawatoi!
Ukifika hapo usiache kusoma sheria za kuvaa suti. Nimecheka kwa sauti, nadhani majirani wamepata mshtuko. Mwanablogu huyu alinichekesha wakati ule alipoandika sifa za uswahili.


BLOGU TOKA JUU YA KILIMANJARO

Sikuwa najua kuwa kuna watu wamekuwa wanablogu safari yao ya kupanda mlima ambao hauko mbali na nilipozaliwa. Blogu ya hao mabwana ni hii na habari yenyewe nimeikuta sebuleni kwa Mawazo na Mawaidha.

KICHWA NI UWANJA WA MATANGAZO

Ubunifu unalipa. Huyu bwana kaenda kwenye mnada wa eBay. Katangaza kuwa ananadi paji la uso wake kuwa ni ubao wa matangazo. Kajipatia dola za Kimarekani 37,375! Soma habari yake hapa. Na mnada wake huu hapa. Au nenda kabisa kwenye tovuti yake hii.


1/24/2005

JUMBA LA RAIS WA BABILONI MKUU

Huwa najiuliza: ni lini jumba hili litakaliwa na mwanamke? Au mtu mweusi...nadhani kwa mtu mweusi itakuwa vigumu maana jina la jumba lenyewe ni "white house." Jaza mwenyewe.
Litazame jumba lenyewe. Kongoli
hapa.



ZILE KUTA ZITAANGUSHWA LINI?

Uhuru wa kutoa mawazo, kufikiri, na kujieleza ni muhimu mno kwa mwanadamu. Hatuwezi kukubali uhuru huu kuchezewa ili kutimiza matakwa ya "watwawala" wachache. Ni kutokana na sababu hii ndio nimeweka kitabu kilichopigwa marufuku na sirikali Tanzania kinachohusu mauaji ya Mwembechai. Kitabu hiki kiko katika kona ya tovuti mchanganyiko, upande wa kuume wa blogu hii. Ingawa sikubaliani na mengi yaliyomo ndani ya kitabu hiki, huyu bwana ana haki ya kujieleza. Kama tutaruhusu tu wale wanaoandika mambo ya kusifia na kufurahisha wakubwa, maana halisi ya uhuru wa habari itakuwa imepondwapondwa.

Sasa kule Kenya ambako tulizoewa kusikia vyombo vya habari vikiimba habari za Moi (mara kenda kanisani, mara kakohoa, mara kanywa maji kijijini kwake...) zile kuta ambazo Ndimara Tegambwage na Horace Kolimba waliwahi kuzizungumzia (kuta zinazozuia maendeleo ya fikra) zinaongezeka urefu. Nimepata habari hii hapa ya mwandishi wa Kenya toka kwa mwanablogu huyu.


SUMAYE NA ULAJI

Mimi nadhani kuwa watu wanatania tu. Kwani Sumaye mwenyewe amewahi kusema kuwa anataka ulaji namba moja? (ulaji namba moja ni urais.) Nimekuwa nikisikia akitajwa kila mara kuwa ni kati ya watu watakaogombea nafasi ya kuwa mgombea urais, yaani ulaji, katika chama twawala. Mimi nabisha kabisa. Najua Sumaye ana busara kiasi fulani. Yaani mnataka kuniambia kuwa Sumaye hafahamu kuwa urais wa nchi yenye mzigo wa matatizo, shida, na tabu kama Tanzania hatauweza? Hebu acheni hiyo.
Kwani Sumaye katika uwaziri mkuu wake amefanya mambo yapi hasa ambayo yamegusa nyoyo za Watanzania kiasi ambacho waamke asubuhi na mapema kwenda kumpigia "kula"? Najua kuna mambo mawili makubwa ameyafanya katika kipindi chake cha uongozi:
1. Ameweza kuitetea sirikali bungeni dhidi ya wale wote wanaoipinga na kuisakama.
2. Amekuwa kila mara katika hotuba zake akitukumbusha kuwa, "Sirikali yenu inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mnakuwa na maisha bora" huku taa za ofisini kwao na majumbani zikiwa zimezimwa usiku. Hizo kazi wanazofanya usiku wanazifanyaje gizani?Au labda wanafanya kwa uweza wa kimiujiza. Au kuna kazi "fulani" wanazofanya "kwa ajili yetu" ambazo huwa hazihitaji taa!
Sumaye, hiyo sirikali "isiyolala" ni ya Tanzania ninayoijua mimi (iliyopakana na Kenya na Uganda) au ni nyingine?
Hii habari hapa ndio imenifanya kuandika haya yote.

FASIHI SIMULIZI NA WANDENGEREKO WA ASIA

Joe Tunga (mwenye kile kipindi cha uchambuzi na midundo ya Kiafrika, AFROWORLD, kila juamosi katika redio hii) kanitumia habari hii ya ndugu zetu wanaofanana na Wandengereko kabisa walivyookolewa na fasihi simulizi. Habari hii hapa.

1/23/2005

AMANI TANZANIA NI KIVULI

Mmoja wa wasomaji wangu, Bwana Komba, kaandika maneno mazito sana. Komba simfahamu zaidi ya kupitia mtandaoni. Lakini anayosema yanawakilisha hisia za Watanzania wengi. Nimehariri kidogo sana (sio maudhui bali herufi, vituo, n.k.) waraka wake. Nimeamua kuuweka hapa (bila idhini yake!) kwa watu wote wasome. Nimependa sana pale anapozungumzia kuwa amani Tanzania ni kivuli na kuwa jua likizama...
Huyu hapa Komba:
Nchi za kiafrika bado zinakumbatia watawala hadi sasa, hasa hata nchi yetu Tanzania. Watu wa mbali wanaona kama ni nchi ya Amani kumbe ni nchi ya kibepari inayo wanyanyasa wananchi wake kwani pengo la maskini na tajiri ni kubwa sana. Rushwa ndio mshahara wa viongozi wetu,hakuna kiongozi mwenye huruma na nchi yake,sasa mwisho utafika nasi wanyonge tutachoka na kulala ktk njia kuu ziendazo kwa wakubwa ili haki itendeke kwa wote.

Viongozi wetu ni wafisadi sana na ni waongo sana wakiwa kwenye majukwaa ya siasa utajua ni watu muhimu kumbe wanajifagilia tu ili wale vizuri. Jamani wananchi tuamke na twende kupigania haki zetu hawa waliopo ni makupe tu angalia jinsi wanavyoishi kama wako paradiso,wanajiona wao ndio miungu mtu. Tanzania amani imeisha kimebaki kivuli nacho jua likichwa kitaondoka sijui tutakimbilia wapi? Congo,au Burundi

RUMI na BENJAMIN

Nilimtaja Rumi kuwa ni kati ya washairi niwapendao mno. Nataka nikupe kipengele toka kwenye mashairi yake (tafsiri ni yangu):
Cheza kama hakuna anayekuona
Penda kama hujawahi kuumizwa roho,
Imba kama vile hakuna atakayekusikia
Fanya kazi kama huna haja na malipo
Ishi kama vile mbinguni ni hapa duniani.

Mshairi mwingine anayeniingia sana nafsini ni Benjamin Zephaniah. Ingia katika tovuti yake.

RASTAFARI: SEHEMU YA MWISHO

Ninamalizia viporo. Nimeweka sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala juu ya Urasta. Kama hujasoma mbili za mwanzo, zisome kwanza ndipo uisome hii ya mwisho. Nimeiweka katika kona ya makala zangu, mkono wa kuume, chini ya picha yangu. Inaitwa: Mungu wa Marasta anaitwa JAH.

Ninapenda kuwakumbusha wale wote walioko Tanzania ambao wamekuwa wakiniulizia juu ya vitabu vya Urasta kuwa kile kitabu kilichoandikwa na Horace Campbell kiitwacho Rasta and Resistance: From Marcus Garvey to Walter Rodney bado kinapatikana kwenye duka la TPH mtaa wa Samora, jijini DSM.
Pia kwa watakaoweza kukipata, kitabu cha Dr. Dennis Forsythe kiitwacho Rastafari: For the Healing of the Nation ni kizuri mno. Kama unataka kuzama kwa undani kabisa kwenye falsafa na theolojia ya Urasta na elimu-siri ya kiroho ya Waafrika, kitabu hiki kitakufaa.

SHAIRI: HISTORIA YA KIGANJA CHAKO

Tafadhali,
Leo
Kabla hatujashikana mkono
Kusalimiana,
Mambo, vipi,
Habari, nzuri,
Shikamoo, marahaba
Salaam aleikum…
Nipe historia fupi
Ya kiganja chako
Kwa siku nzima,
Kimekwenda wapi?
Kimeshika nini?
Kimegusa nini?
Kimekuna wapi?
Kimefuta nini?
Kimekamata nini?
Kimepapasa wapi?

Tafadhali sana
Nipe kwanza hiyo historia
Ndipo niamue

Kukupa mkono
Au la!

1/21/2005

RUMI JUU YA MAANA YA MAISHA NA KIFO

Watu wengi wanahofu kifo sana. Ingawa lazima kila mmoja wetu atafariki. Moja ya sababu kubwa ya kuhofia kifo tunaambiwa na wanasaikolojia ni kuwa hatujui tuendako. Tuna hofu ya tusikokujua. Tukifa tunakwenda wapi? Mbinguni, jehanamu, kuzimu, kusikojulikana, sayari ya mbali, mbingu ya saba, hatuendi kokote...
Imani nyingi duniani zimekuwa na mtazamo kuwa ukifa unazaliwa tena. Hii inaitwa Reincarnation. Maisha ni mzunguko kama wa jua. Kukicha jua linafufuka. Kukichwa jua linazama. Linafariki. Mzunguko wa maisha (kufa na kurudi).
Kuna wengine kama wafuasi wa Gautama Buddha (waumini wa Kibudha) wana imani kama hii lakini kuna tofauti fulani. Badala ya Reincarnation wanapendelea Rebirth.
Dr. Remmy Ongala kaimba sana juu ya kifo. Katika wimbo mmoja anauliza, "Kwanini nife?" Hili ni swali moja kati ya maswali makubwa mawili yanayomsumbua mwanadamu juu ya kifo. Jingine ni siku ya kufa. Hakuna ajuaye. Kuna wanaodai kuwa kila mmoja wetu kapangiwa siku yake ya kufa na Mungu. Wenye hoja hii inakuwa kama vile wanasema kuwa Mungu ndiye anatuua. Je mtu akifariki kwa kugongwa na mlevi ni Mungu kapanga? Mlevi kasaidia mpango wa Mungu? Au labda Mungu anapanga siku ila hapangi kifo kitakukuta vipi.

Dr. Ongala katika wimbo mwingine anasema siku ya kufa ni siku ya udongo. Lakini kuna wengine hawaendi udongoni. Wanachomwa moto. Hii inaitwa cremation. Wanahistoria wanatuambia kuwa hapo zamani kabla jamii nyingi hazijawa na makazi ya kudumu na wakati huo wakiona kuwa moto una nguvu fulani za kiroho, uchomaji wa marehemu ulikuwa ulifanyika. Kitendo cha mwili kuchomwa moto kilionekana kama ni mwili kuliwa na roho kuu ya moto. Tendo hili liliaminiwa kuwa lilimsaidia marehemu.


Ninachotaka hasa kukwambia ni hiki: Ukiamka asubuhi unatakiwa kukumbuka jambo moja. Kumbuka kuwa umepunguza siku moja katika maisha yako. Yaani umekaribia ile siku unayoiogopa kwa siku moja! Inatisha, eeh?

Mmoja wa washairi niwapendao mno, Jelaluddin Rumi, alipokuwa akifikiria suala hili la kifo na hasa lile swali la siku ya kufa na akifa atakwenda wapi aliandika maneno haya:

Siku nzima ninaliwaza,
kisha usiku ninalisema.
Ninatoka wapi ?
Ninapaswa kufanya nini hapa duniani ?
Sijui.

Nafsi yangu imetoka mbali na hapa,
hilo nina uhakika nalo...
Sikuja hapa kwa amri yangu.
Na siwezi kuondoka kwa amri yangu.
Yeyote aliyenileta hapa anapaswa kunichukua nyumbani...

1/20/2005

UZAWA, UZAWA, UZAWA...

Tatizo langu ni hili: haya mahubiri ya uzawa ni namna ya kupata "kula" (wengine mnaita kura) au ni imani ya dhati ya kuinua kiwango cha maisha cha wakesha hoi? Namzungumzia Iddi Simba. Msome.

BLOGU TOKA JUU YA MLIMA KILIMANJARO

Sikujua kuwa kuna watu walikuwa wanablogu safari yao ya kupanda mlima Kilimanjaro. Nimeipata toka kwa Mawaidha. Kongoli hapa upate blogu hiyo toka kilele cha Afrika.

JIB JAB WAMEKUJA NA NYINGINE

Wale jamaa wa Jib Jab ambao wanatengeneza katuni za kukejeli walioko madarakani wamekuja na katuni nyingine. Unaweza kuitazama na nyingine za nyuma hapa. Wameitoa hii mpya kuendana na kuapishwa kwa Joji Kichaka mvamizi wa nchi za watu na mnyonya mafuta.

1/17/2005

UNATAKA KUJIFANYA KUWA WEWE SIO WEWE?

Mambo ya mtandao achana nayo. Kuna mwalimu mmoja kule Norway, Jill Walker, anatumia tovuti hii kufundishia. Kama unataka kuwa David, basi unaweza kuwa David kwa kwenda hapa.

NINASOMA NINI?

Hivi sasa ninasoma jarida la Socialism and Democracy la Julai-Desemba 2004. Mada iliyopo ni: HIP HOP, RACE, AND CULTURAL POLITICS. Kati ya watu walioandika makala za aina mbalimbali kuhusu utamaduni wa hip hop, muziki wa rap, na masuala ya utamaduni na siasa ni Bakari Kitwana, Mumia Abu Jamal, Lawrence James, mkurugenzi wa vuguvugu la wasanii la G.A.M.E, na wengineo.

JIFUNZE KISWAHILI

Ni siku nyingi toka niweke mambo ya kutuelimisha juu ya kiswahili.
Majina ya Sayari:
Zohari: Saturn
Mshtarii/ Sumbula: Jupiter

Zuhura: Venus

MKE WA MARTIN LUTHER KING, JR

Mjane wa Dr. Marin Luther King, Jr, Coretta Scott King amesema kuwa ujumbe wa King bado unahitajika dunia ya leo. Habari zaidi za Dr. King nenda hapa.

NAWAL EL SAADAWI: KUTA HIZI ZITAVUNJIKA LINI?

Kuta zinazojengwa na "watwawala" kwenye nchi mbalimbali duniani kuzuia uhuru wa mawazo, fikra, na habari zitaanguka lini? Tazama yanayompata mwanamama Nawal El Saadawi wa Misri. Bofya hapa.

NINA NDOTO: UNAWEZA KUAMUA

Jumamosi iliyopita ilikuwa ni siku ya kuzaliwa kwa Dr. Martin Luther King, Jr. Leo jumatatu ni siku ya kitaifa ya Dr. King. Dr. King anakumbukwa kwa ile hotuba yake ya Nina Ndoto (isikilize). Rafiki yangu mmoja wakati tukijadili hotuba hii amenipa msemo mmoja ambao nimeamua nisiutafsiri:
You are not too old to dream. Kwahiyo nawe unaweza kuwa Martin Luther King wakati wowote ule. Unachotakiwa ni kuamua.


USISAHAU HILI DARASA

Niliwahi kukueleza juu ya darasa hili katika chuo kikuu cha Stanford ambalo mtu yeyote yule anaweza kuhudhuria bila kujali uko wapi. Darasa lenyewe limeshaanza. Unaweza kutazama video za vipindi vilivyopita. Kongoli hapa na hapa.

NINI KIPIMO CHA MAENDELEO?

Furaha na raha ni vitu tofauti. Unaweza kuwa na raha ila usiwe na furaha. Mfalme wa Bhutan anaona kuwa furaha lazima iwe ni moja ya vipengele vya kutazama maendeleo ya nchi.

1/16/2005

IBA KITABU HIKI!

Kuna watu ambao kabla hujafariki inabidi uwafahamu. Mmoja wa watu hao ni Abbie Hoffman. Ningependa ukipitie, au ukisome, moja ya vitabu alivyoandika. Kitabu hicho kinaitwa IBA KITABU HIKI (Steal This Book). Ndio, ikiwezekana usikinunue. Kiibe!
Kitabu hiki kiliandikwa mwaka 1972. Katika kitabu hiki Abbie anafundisha jinsi ya kupata kila kitu hapa duniani kama nguo, chakula, samani (furniture), usafiri, n.k. bure. Bure. Bila kutoa hata senti tano (jamani mnakumbuka Tanzania kuna enzi tulikuwa tunatumia senti tano? Nilikuwa nanunua lawalawa golololi). Anafundisha wanamapinduzi jinsi ya kuiba kwenye maduka makubwa ya kipebari. Unaweza kusoma kitabu chake bure au kiibe kabisa ukitaka kwa kwenda hapa. Nakala hii utakayoisoma imetolewa na jamaa waliokiiba toka katika maktaba ya bunge la Marekani.
Mwaka 2000 kulitolewa sinema juu ya maisha, harakati, na falsafa zake na mapambano dhidi ya utawala ya enzi zake. Sinema hii inaitwa IBA SINEMA HII (Steal This Movie).
Moja ya mambo ambayo aliwahi kufanya ni kufanya operesheni ya kujibadili sura na kujificha asikamatwe kwa miaka sita na majasusi wa FBI. Alibadili hata jina na kujiita BArry Freed.
Abbie ni kati ya watu ambao harakati kwao ni maisha. Kama hakuna harakati hakuna maisha. Historia yake inaonyesha kuwa alianza kupambana dhidi ya ukandamizaji toka akiwa na miaka minne. Wakati huu alikuwa akipambana na wanafunzi waliokuwa wakipenda kuonea wenzao. Angekuwa shule niliyosoma mimi angenisaidia wakati Gerisoni aliponikaribisha darasa la kwanza kwa mabuti!
Abbie alikuwa ni mmoja wa watuhumiwa wa moja ya kesi kubwa katika historia ya Marekani. Hii ni ile kesi ya Watu Saba wa Chicago (The Chicago Seven).

Abbie ameshafariki. Alijiua. Kabla ya kujiua alisema maneno haya akiwazungumzia watawala na mabepari: "It's too late. We can't win, they've gotten too powerful."
Abbie ameacha wafuasi wengi. Kwa mfano, kuna kundi unaweza kulitazama linaitwa Kikosi cha Abbie Hoffman. . Kikosi hiki hakina kiongozi wala wafuasi.

NAWAKUMBUSHENI TU

Nawakumbusheni. Hata mimi huwa nasahau kila mara: Mji mkuu wa Tanzania ni Dodoma.

TANZANIA: UTANI, UTANI...

Usiku.Watu wananoa mapanga.
Usiku. Nyumba zinawekewa alama nyekundu ya X.

Mchana wanarushiana maneno. Kichwa kwa kichwa. Ulimi kwa ulimi.
Mchana. Walinda amani wanaiharibu kwa kuua.
Kuua raia.
Piga. Fyatua. Ua. Fanya Fujo Uone

Utani, utani...mara imekuwa kweli.
Umesikia hii?

TUKAE KIMYA?

Ukifungua mdomo.Yakatoka maneno dhidi ya chama twawala, utaitwa mpinzani. Utaonekana unashabikia vyama vya upinzani. Ukiwa na domo kubwa watatafuta namna ya kukuonyesha "dawa yako." Utaona cha mtema kuni. Niliwahi kuuliza, "Hivi mtema kuni aliona nini?

Ukifungua mdomo. Yakatoka maneno dhidi ya vyama vya upinzani. Utaonekana msaliti.
"Kanunuliwa siku hizi." Wataanza kunong'onezana. Baadaye sauti itakuwa kubwa. Itakubidi uzibe masikio.
Umenunuliwa. Umesaliti.

Hivi haiwezekani mtu kuwa Mtanzania na kutoa mawazo na maoni yako kama mtu huru bila kuwa mfuasi wa chama "twawala" wala wa upinzani?

Kwanini nisiseme
Huku nina mdomo?
Nisifikiri
Huku nina fikra?
Nisitende
Huku nina haki?
Usinilaumu
Kwa dhuluma
Iliyoivaa nchi
kama kanzu,
Sikuwachagua.

Sijawahi kupiga kura
Toka nizaliwe
Wala sijilaumu.

1/15/2005

MIUNGU YA DUNIANI

Makampuni makubwa ya kibepari yamekuwa ndio miungu midogo ya duniani. Tunaishi kwenye dunia ambayo makampuni binafsi yamekuwa na nguvu na utajiri kuliko hata sirikali. Sirikali nyingi duniani hivi sasa zinafuata matakwa ya makampuni haya badala ya sauti ya umma. Tunaona jinsi yanavyonununua nchi kama mtu unavyonunua shamba. Tanzania nayo mnada wake unaelekea ukingoni sasa kama mnada wa nchi nyingine za Afrika. Kali zaidi ni hii ya makampuni haya kufikia hatua ya kumiliki hata mbegu! Kongoli hapa ujionee mwenyewe. Ewe mkulima, kaa chonjo!

SANAA-HARAKATI

Kuna aina ya sanaa-harakati ambayo nimekuwa nikiifuatilia kwa muda. Sanaa-harakati hii imejengwa juu ya falsafa ambayo bado ninatafuta tafsiri yake kwa Kiswahili (nisipoipata tafsiri yake nitatunga mwenywe. Si unafahamu lugha haiji kimiujiza? Wala hatuhitaji kusubiri mnara wa Babeli ujengwe. Lugha hutungwa na watu na watu ni sisi.) Kwa "kiinglishi" falsafa hii inaitwa Culture Jamming.
Moja ya makundi yanayojihusisha na sanaa-harakati ni kundi la 0100101110101101. Tazama hapa moja ya kazi zao katika mtindo huu wa sanaa-harakati. Kazi zao nyingine hizi hapa.
Hawa jamaa wananikumbusha wale jamaa wengine wa Yes Men.

SHAKESPEARE ALIKUWA NA NANI HII??

Haya madai kuhusu mwandishi maarufu wa Uingereza, Shakespeare, ni ya kweli? Eti alikuwa na….?!...soma mwenyewe hapa.

MGEUZIE JOJI KICHAKA MGONGO

Januari 20 Joji Dabliyuu Kichaka ataapa kuwa kiongozi wa sirikali iliyoivamia Iraki kwa sababu za uongo. Walituma matineja na mitutu huku wao wakinyemelea nyuma yao na mirija ya kunyonya "kiwese." Kuapishwa kwa Joji Kichaka kutaambatana na maandamano makubwa sehemu mbalimbali hapa Marikani na dunia nzima.
Siku hiyo Joji Kichaka ataapa kuwa Rais wa nchi hii kinyumea na maandiko ya kitabu anachodai anakisoma kila siku kiitwacho Biblia. Inawezekana hajasoma Matayo 5:33-37 maana angekuwa amesoma hapo sijui kama asingeapa kamwe kama mwokozi wake alivyofundisha. Si unajua kuwa Kichaka ameokoka? Eti ni mlokole. Akitembelea Tanzania labda ataenda kwa Kakobe.
Kati ya mbinu zitakazotumika siku hiyo ya tarehe 20 Januari ni kumgeuzia Joji Kichaka mgongo. Mbinu hii itawaruhusu wapinzani wa Kichaka kuweza kupita vizingiti vya polisi kama watu wa kawaida tu kisha baadaye wanafanya vitu vyao. Tembelea hapa. Wanaharakati wengine wamedai kuwa "Kichaka haendi kokote nasi hatuendi kokote." Wako na Joji sambamba. Wanakula naye bakuli moja. Tembelea hapa.

TAZAMA ONYESHOI HILI LEO HII

Kuna onyesho la muziki kwa ajili ya maafa yaliyoletwa na tetemeko la chini ya bahari huko Asia. Hapa nilipo onyesho ni saa mbili usiku leo hii. Huko uliko wewe sijui itakuwa ni saa ngapi. Nenda hapa.

CHUO KIKUU CHA BURE

Chuo kikuu hiki hakina karo, wala kufeli au kufaulu!

MARTIN LUTHER KING, JR

Dr. King aliwahi kusema, "Mwanzo wa mwisho wa maisha yetu ni pale tunapokaa kimya juu ya mambo ya msingi yanayotuhusu/ mustakabali wetu." Tazama hapa.

Hivi Dr. King angekuwepo leo hii angefanya au kusema nini? Kongoli hapa.
Halafu mtazame na kumsikiliza hapa.

Je mbinu, falsafa na mikakati yake inaweza kutumiwa leo? Hapa.





MWALALA?

Utawala bora liende
Wawala
Nanyi mwalala,
Ndotoni mkiimba
Amani na utulivu.
- toka shairi langu la UTAWALA BORA LIENDE.

KUAPISHWA KWA RAIS SIO IBADA

Yule bwana asiyemwanini mungu (kama hawa hapa), Michael Newdow, anadai kuwa tendo la kuapishwa kwa Rais wa Marikani sio ibada ya kikristo. Kaenda mahakamani: hapa. Aliwahi kwenda mahakamani kwa kesi hii.

1/14/2005

BIASHARA YA SILAHA

Vita kila mahala. Vita mashariki, vita magharibi...Vita kule, vita huku. Vita na uvumi wa vita. Vita. Vita. Vita. Taifa laondoka kupigana na taifa jingine. Watu wanyanyuka kuuana wenyewe kwa wenyewe.

Hivi silaha hutoka wapi? Hivi mabwana wa vita wanapata wapi silaha? Jielimishe kwa kwenda hapa.

HAKI ZA BINADAMU

Unafuatilia masuala ya haki za binadamu? Nenda hapa. Pia unajua juu ya unyama usio na mfano unaofanywa na sirikali ya Marikani inayotaka kuwa kinara wa demokrasia duniani? Kongoli hapa.

Je Tanzania ina askari watoto? Nenda hapa usome ripoti mbalimbali kuhusu haki za binadamu Tanzania.


MARTIN LUTHER KING, JR

Naamini unakumbuka jumatatu ijayo ndio sikukuu ya kumkumbuka Martin Luther King, Jr. Lakini wiki yote hii na ijayo ni wiki za kujikumbusha juu ya harakati na falsafa zake. Msome hapa. Pia walioko katika nchi hizi wanaweza kufuatilia sherehe za kumbukumbu yake.





1/12/2005

SILAHA ZA MAANGAMIZI

Hatimaye sirikali ya Joji Dabliyuu imenyanyua mikono. Ninazungumzia ule uchunguzi wa rundo la silaha za maangamizi (ambazo Marikani imezijaza hapa nchini na inataka kuhamishia nyingine kwenye sayari za mbali!) nchini Iraki. Unajua kimeishia wapi? Tazama hapa.

1/11/2005

LIBERIA

Liberia ilipata uhuru Julai 27, mwaka 1847. Ndio sijakosea, sio 1947 bali 1847. Lakini...
Tazama picha hizi.

MARTIN LUTHER KING, JR

Tunamkumbuka mhubiri, mtetezi wa haki, na mwanaharakati Dr. Martin Luther King, Jr. Kuna mengi sana ya kujifunza toka kwake. Hasa kwa vijana ambao wanajaribu kuleta mabadiliko nchini Tanzania, Kenya na kwingineko. Kwa kipindi hiki ambacho mahubiri ya jino kwa jino, ngangari na ngunguri yamechukua sura mpya katika siasa nchini Tanzania...kwani sasa kuna kitu kinaitwa "mapanga sha sha sha..."...harakati za watu ambao waliamini kuwa binadamu ana uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli kwa njia za amani zina mengi ya kutufunza. Watu kama Dr. King waliamini kuwa hata kama siri-kali mnayotaka kuibadili ina maguvu ya dola na inatumia maguvu hayo kunyamazisha raia na hata kuua, ziko njia za amani zinazoweza kushinda. Alisema kuwa hapendi dhana ya jicho kwa jicho maana haki inapokuja kupatikana kunakuwa hakuna mwenye macho! Haya, nenda hapa.

1/10/2005

UNAPENDA SANA VYAKULA VYA PAPO KWA HAPO VYA MAKIDONADI?

Unapenda vyakula vya papo kwa hapo au vyakula vya kuchukua vya Maki Donadi? Jaribu kutembeza macho hapa na hapa. Ukiweza (hasa walioko Ughaibuni) itazame sinema hii. Utaipenda. Nakuhakikishia. Kama unabisha, basi tupinge!

UTAKUWEPO MWAKA 2012?

Nini kitatokea ifikapo Desemba 21, 2012? Kwa mujibu wa kalenda ya Wamaya (watu wa asili wa Guatemala) siku hiyo kuna jambo litalalotokea. Wanahistoria, wanasayansi, wachunguzi wa mambo ya kale, wanahisabati, waandishi, n.k. wamekuwa wakitazama kwa undani mfumo wa maisha wa watu hawa ambao elimu na maarifa yao vimefanya baadhi ya watu kudai kuwa walitoka sayari ya mbali.
Je ni kitu gani kitatokea siku hiyo? Kutakuwa na mwamko mpya wa binadamu kujielewa na kurudi katika zama za upendo, jumuiya, na amani? Au bomu la nyuklia litalipuliwa? Au kutakuwa na maafa yanayotokana na nguvu za asili kama vile matetemeko, volkano, mafuriko, n.k.? Wamaya wana kalenda zaidi ya moja. Wanazo 17. Lakini kalenda ambayo inafanyiwa utafiti na wanazuoni wengi toka mwaka 1987 ni ile iitwayo Tzolk'in. Kuna makala nzuri hapa juu ya Wamaya na huo mwaka 2012.

MAKALA MPYA YA GUMZO LA WIKI

Nimeweka makala mpya ambayo imetoka katika gumzo la kila wiki katika gazeti la Mwananchi. Kama kawaida makala hiyo iko kwenye kona ya makala zangu, upande wa kuume, chini ya picha yangu, ndani ya blogu hii. Makala yenyewe inaitwa: TAFADHALI NISAIDIE...

WAANDISHI WANA YA KUJIFUNZA TOKA KWA WANABLOGU

Kumbe waandishi wa habari wana mambo mengi ya kujifunza toka kwa wanablogu? Mambo hayo kwa ufupi haya hapa. Tim Porter wa blogu ya First Draft ana orodha ya mambo 10. Kuna makala ndefu ya Steve Outing wa Taasisi ya Poynter. Kongoli hapa uisome.

USIMSAHAU MARTIN LUTHER KING, JR

Mwaka 1988, Rais Reagan (Reagan?!!, unaweza usiamini) alipitisha sheria ya kufanya kila jumatatu ya tatu ya mwezi Januari kuwa ni siku ya kukumbuka maisha, harakati, na falsafa za Dr. Martin Luther King, JR. Hii ndio sikukuu pekee inayoazimishwa kwa ajili ya mtu mweusi hapa ndani ya tumbo la Jitu (Nadhani unafahamu kwanini Malcolm X hana sikukuu ya kitaifa.)
Kwahiyo jumatatu ijayo ni sikukuu ya Dr. King. Ingawa sikukuu hii ya Dr. King ni ya kitaifa kuna majimbo ambayo hayaisherehekei. Kuna watu wengi ambao wanapinga kuwepo kwa sikukuu hii. Pia kuna waliotaka sikukuu iwe siku aliyozaliwa. Wengine wakataka siku aliyouawa. Hata kupitishwa kwake na bunge kulikuwa kwa kushikana mashati. Siku nne baada ya kuuawa kwa Dr. King mwaka 1968, mbunge wa chama cha Democratic wa Michigan, John Conyers, alipeleka muswada bungeni wa kutaka kuwe na sikukuu ya Dr. King. Ilichukua miaka 20 kwa sheria ya kuwa na sikukuu hii kupitishwa!
Kauli mbiu ya sikukuu hii kila mwaka ni hii: "Remember! Celebrate! Act! Day On, Not A Day Off!!"
Historia ya Dr. King ni ndefu. Moja ya mambo aliyofanya King ni kuongoza moja ya mgomo uliochukua muda mrefu katika historia ya migomo Marikani na duniani. Aliongoza mgomo wa mabasi kupinga sheria ya kubagua abiria kutokana na rangi zao. Mgomo huu ulidumu kwa siku 382 hadi pale Mahakama Kuu ya Alabama ilitamka kuwa sheria hiyo ilikuwa inakiuka katiba ya nchi.
Mwaka 1963 aliongoza moja ya moja ya maandamano makubwa katika historia ya Marekani yaliyoitwa "March on Washington." Ni katika maandamano haya ndipo alipotoa hotuba yake maarufu ya "Nina Ndoto" (I have a Dream).
Mwaka 1964 Dr. King alitunukiwa nishani ya amani ya Nobeli. Wakati wa kupokea tuzo hiyo alisema haya. Hotuba yake ya Nobeli nayo ina ujumbe mzito kuhusu mwanadamu na masahibu yake.
Dola 54,000 za Kimarekani alizopata kutokana na tuzo hii alizitumia kununulia vihamba (mashamba), magari ya kutanulia na kusafishia jina, na kujenga majumba ya kifahari ufukweni mwa bahari,!...We! Nakutania. Aligawanya fedha hizo kwa vyama vilivyokuwa vikipigania haki na usawa. Unadhani Dr. King alikuwa kama viongozi wetu fulani na fulani ambao majina yao unayajua?
Mwaka 1968 Dr. King aliuawa kwa risasi kama ilivyotokea kwa Malcolm X mwaka 1965. Au Mahatma Gandhi kule India. Au Lumumba. Au Che Guevara.
Sasa katika kumkumbuka Dr. King nakuomba usome aliyoandika (hasa katikati na mwishoni) kwenye Barua Toka Gereza la Birmingham. Pia ukienda hapa utaona aliyosema kuhusu vita na amani na pia hotuba zake zinazopendwa na wengi.
Muhimu zaidi msikilize kwa sauti yake mwenyewe akitoa hotuba yake ya "Nina Ndoto." Kongoli hapa.

BLOGU MPYA YA MTANZANIA

Kuna mtanzania mwingine mwenye blogu ya Kiswahili. Huyu ni mwandishi Reginald Simon. Mtembelee hapa. Idadi ya blogu za Kiswahili inaongezeka kwa mwendo wa kobe. Mambo mazuri hayahitaji haraka. Au?

BLOGU IMEOTESHA KIBARUA MAJANI

Kuna kazi. Tazama mwandishi huyu blogu yake imeotesha kibarua chake majani. Hapa.

UNAFUATILIA MAMBO YA PALESTINA?

Kama unapenda kufuatilia siasa na harakati za Wapalestina kutwaa ardhi yao iliyochukuliwa kwa nguvu na jamaa wanaojifanya kuwa wanamwabudu Yehova na kufuata mafundisho ya Musa nenda hapa.

UNATAKA KUCHOROPOKEA MARIKANI KUPITIA MEXICO?

Kama unataka kufanya hivyo, serikali ya Mexico inataka ujue haya ili uweze kufanikiwa kuingia ndani ya tumbo la Jitu (Marikani). Usishangae inakuwaje serikali moja inashauri wananchi wake jinsi ya kuingia kwa mafanikio bila visa katika nchi nyingine. Au labda serikali hii inajali uhai na usalama wa wananchi wake. Soma hapa.

TSUNAMI NA SIASA ZA "MISAADA"

Misaada inayomiminika kwa waliokumbwa na janga la tetemeko la chini ya bahari imeleta sura mpya katika siasa za misaada na pia kuzua mijadala. Kwa mfano, kuna mjadala uliozuka ukidai kuwa nchi za magharibi hazikuonyesha kujali wakati Iran ilipopata janga la tetemeko la ardhi lililoharibu kabisa mji wa kihistoria wa Bam Desemba, 2003. Lakini jambo ambalo mimi binafsi nimekuwa nikilifuatilia kwa karibu ni kitendo cha India kukataa misaada toka nchi yeyote ile. India imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na tetemeko hili ambapo zaidi ya wananchi wake 10,000 wamepoteza maisha (nadhani huu msemo,"wamepoteza maisha" sio mzuri sana...tuseme wamehamia kwingine!) Pamoja na India kukataa misaada, nchi hiyo imetoa misaada ya fedha, ndege, helikopta, n.k. kwa nchi nyingine kama Indonesia, Malyasia, n.k. Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Manmohan Singh alimwambia Joji Dabliyuu Kichaka kuwa nchi hiyo haina haja ya misaada na "tukiona tunahitaji misaada tutawaambia." Inaelezwa kuwa ingawa India ni nchi masikini unapotazama kipato cha kila raia, serikali ya nchi hiyo ni tajiri kiasi ambacho hivi karibuni imeshindwa kujua ifanye nini na fedha zake!
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanadai kuwa India imekataa misaada kwasababu za kisiasa. Inataka kuonyesha ulimwengu (nina maana nchi za magharibi) kuwa yenyewe nayo ni nchi yenye uwezo kiuchumi (na kijeshi pia, si unajua kuwa wana nyuklia tayari tayari kurushiana na Pakistani kama ikibidi?!). Mbinu hii ya kuonyesha uwezo wake itawasaidia katika kampeni za kuingia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kwanini nisikupe habari hii usome mwenyewe?

NINAKUMBUKA...

Ninakumbuka. Na sitakaa nisahau. Hata siku moja. Ni mwaka 2002, pale kwenye jumba la utamaduni la Urusi. Jumamosi jioni. Harusi ya Mrisho mwana wa Mpoto. Ni Mrisho yule wa Parapanda Theatre Lab. Wale wasanii wa "Tangulia Mwalimu," ambao vitu vyao unaweza kuvisoma hapa na hapa. Katika harusi hii ambayo haijapata mwenziye, usanii, na uafrika/utanzania vilipew kipaumbele. Kwa mfano, shampeni ilikuwa ni madafu! Na tafadhali usidhani hii ni porojo. Badala ya kufungua shampeni kama inavyofanywa kwenye harusi za wengi ambapo kizibo cha shampeni huruka hewani na shampeni yenyewe kumwagiwa kiasi huku watu wakishangilia (sijui huwa wanashangilia kitu gani...kizibo kuruka hewani? Ndio nini sasa!), kwenye harusi ya Mrisho dafu lilikatwa na maharusi kunyweshana!
Nitakupasha zaidi mengine yaliyojiri katika harusi hii ya kisanii na kitamaduni.
Hakika, sitakaa nisahau.

1/08/2005

IRAKI, IRAKI, IRAKI

Iraki itaumiza vichwa vya mabeberu kwa miaka mingi sana. Wanadhani ukiwa na maguvu ya kijeshi unaweza kuvamia nchi yoyote na kuwaamuru wawatii. Wawasikilize.
Msome mwandishi huyu.

UKIMWI JAMANI!

Ukimwi haumwonei huruma hata Madiba! Hapa.

1/06/2005

MFUMUKO WA USOMAJI BLOGU MAREKANI

Idadi ya wasomaji blogu iliongezeka kwa kasi mwaka jana katika nchi hii inayoongozwa na rais ambaye mpaka leo sijui alichaguliwa vipi, Joji Dabliyuu. Kongoli hapa.

JISOMEE HAYA KWA MUDA WAKO

Mwezi Oktoba mwaka jana kulifanyika mkutana wa wanazuoni wa Afrika na Ughaibuni katika jiji la Dakar, Senegal. Mada zilizojadiliwa hizi hapa.

UTUMWA MARIKANI UMEKWISHA...

Utumwa Marikani hivi sasa ni historia...hivi ndivyo mwalimu wako alivyokudanganya? Unafahamu H-2 Worker? Tazama hapa. Nimekumbuka kuwa yule mshairi mtembea pekupeku (havai viatu hata siku moja!) Mutabaruka, ana shairi juuya H-2 Worker. Kama huelewi kiingereza cha Kijamaika, Patois (inatamkwa "patwa"), unaweza ukaachwa nje kidogo. Shairi lenyewe hili hapa.

ZIGGY MARLEY NA KIRUNDI

Bob Marley, ametengeneza tangazo kwa ajili ya Redio Ijambo ya Burundi. Matangazo hayo ambayo ni kwa ajili ya kipindi cha shirila la Search for Common Ground, yako kwa lugha ya kiingereza na Kirundi. Sikiliza Kirundi cha Mjamaika kilivyo: Hapa, Hapa na hapa. Kongoli hapa, hapa, hapa, hapa, na hapa usikie baadhi ya matangazo yake kwa kiingereza akihimiza Warundi waishi kwa amani (ingawa wengi wao wanafahamu kifaransa zaidi ya kiingereza katika hizi lugha za wakoloni!)

MLANGO WA SITA WA UFAHAMU AU MACHALE!

Hivi majuzi nilikupa taarifa juu ya machale yalivyowacheza wanyama huko Asia kufuatia tetemeko la chini ya ardhi. Wanyama wana uwezo wa juu sana wa kutumia mlango wa sita wa ufahamu. Kama ulipitiwa na habari hizi zisome hapa na hapa. Binadamu nasi tuna uwezo kama huo ila kutokana na maisha ya kileo na "maendeleo" yake tumesahau kabisa jinsi ya kutumia uwezo huo. Tumesahau pia jinsi ya kutazama mwenendo wa wanyama, upepo, tabia za wadudu, n.k. kuweza kutabiri mambo kama mafuriko, tetemeko, ukame, n.k. Lakini kuna makabila ambayo bado hayajachafuliwa na hiki kitu tunachoita "maendeleo." Makabila haya hayajaathirika na utamaduni wa Kimagharibi. Wao bado wako kwenye "maendejana." Kuna makabila kama haya huko Asia ambayo watu wake, pamoja na kuwa wavuvi na kuishi karibu na bahari, hawakuathirika na janga hili maana machale yaliwacheza! Makabila haya yalihamia huko toka Afrika. Jisomee mwenyewe hapa usije ukasema hii ni hadithi.

1/05/2005

UNAIJUA "HUMAN CLOCK"?

Mambo ya intaneti hayo. Tazama hapa kisha linganisha na saa yako ya ukutani, mkononi, kwenye tarakilishi, nenda nje katazame jua liliko. Kuna watakaosema ni ubunifu, na wengine watadai huku ni kukosa kazi!

1/04/2005

SHAIRI: VIJANA, WAZEE, WAKULIMA, NA WASOMI

Vijana, Wazee, Wakulima, na Wasomi

Wazee wanawaasa vijana
wasichague kazi,
Vijana nao wanawashangaa
Hao wazee:
Mbona wao kazi wanachagua?

Wasomi wanawashauri wakulima
Wasikimbilie mijini,
Wakulima nao wanajiuliza:
Wasomi huko mijini
wao wanafanya nini?

WIMBO WA KWAYA DISKO

Kwanza kabisa kuna wanablogu wawili toka Kenya wanaoishi Ughaibuni ambao wametembelea nyumbani na wanablogu toka huko. Namzungumzia Mental Acrobatics na Kenyan Pundit. Kenyan Pundits kaandika jambo ambalo nimeona niwamegee wasomaji wangu. Anasema kuwa kuna wimbo wa injili/kwaya nchini Kenya ambao umekua maarufu kiasi kwamba unapigwa disko! Wimbo umezungumziwa katika habari hii hapa.

SHAIRI: KIVULI

KIVULI

Kivuli hukuandama
Hata kama hutaki.

Kivuli.

Ukiweza kukikamata
Tafadhali fanya hima
Kishike kwa mikono miwili
Kama mpiga makasia
Kisha niletee
Nikipake rangi
Ili wote tukione.

Kivuli.

Ukweli kama kivuli
Hukuandama
Hata kama hutaki

SHAIRI: WANATUKOJOLEA

WANATUKOJOLEA!
Walio juu
wanatukojolea
Walalanjaa,
tukijigusa,
Tukihoji,
wanatuambia,
Mvua imetunyeshea!

MAKALA MPYA YA URASTA

Hatimaye nimezipata zile makala za Urasta (namba mbili na tatu). Nimeweka sehemu ya pili. Nenda kwenye kona ya makala zangu uisome. Inaitwa Hivi Marasta Hawafi? Kama hujasoma sehemu ya kwanza, tafadhali isome kwanza kabla ya kusoma ya pili. Ya kwanza inaitwa Rastafari: Jiwe Walilolikataa Waashi...
Jana niliweka makala nyingine mpya niliyoandika siku za nyuma katika safu yangu ya Gumzo la Wiki katika gazeti la Mwananchi nchini Tanzania. Makala hiyo inaitwa Wamarekani Weusi ni Waafrika? Nayo iko hapo kwenye kona ya makala zangu (mkono wa kuume chini ya picha yangu). Kabla wiki haijaisha nitaweka sehemu ya mwisho ya makala ya Urasta.

1/03/2005

MAKALA MPYA

Kuna makala mpya niliyoahidi kuiweka muda mrefu uliopita. Nenda kwenye kona ya makala zangu (hapa bloguni) uisome. Makalza zangu ziko mkono wa kuume chini ya picha yangu. Makala yenyewe inaitwa: Wamarekani Weusi ni Waafrika?

KUNA JINA JINGINE MUAFAKA?

Kuna jina jingine muafaka la mtoto aliyezaliwa katika mazingira kama haya? Hapa.

CHAGUA: UTAMWOKOA MTOTO YUPI?

Sijui kama mnafuatili visa vya waliokoka janga la tetemeko hili la chini ya ardhi. Mama huyu alikuwa njia panda. Alikuwa na uwezo wa kuokoa mtoto mmoja. Naye alikuwa na watoto wawili. Amwokoe yupi na yupi amwache achukuliwe na maji? Kisa kizima hiki.

WANYAMA NA TSUNAMI

Bado naendelea kufuatilia habari za ndugu zetu (wanyama) na janga la tetemeko la chini ya bahari (tsunami). Soma kisa hiki. Huwezi amini!

1/02/2005

WANYAMA NA MLANGO WA SITA WA UFAHAMU

Watu zaidi ya laki moja wamefariki kutokana na tetemeko la chini ya bahari (tsunami). Imekuwaje binadamu wengi namna hiyo wamepoteza uhai lakini wanyama wakaokoka? Tunaambiwa kuwa wanyama wengi machale (mlango wa sita wa ufahamu) yaliwacheza. Walijua! Soma hapa na hapa.

1/01/2005

BLOGU ZA WANAZUONI/VYUONI

Wanazuoni hawako nyuma katika masuala ya blogu. Kwanza baadhi yao wanatumia blogu katika kufundishia. Hapa kuna orodha ya blogu za wanazuoni mbalimbali.
Pia kuna vyuo ambavyo vinawapa wanafunzi, walimu, na wafanyakazi wake blogu zao binafsi kama chuo hiki hapa.

NDOTO ZA NYUMBANI

Ziggy Marley ana wimbo unaitwa Dreams of Home toka albamu yake ya Conscious Party. Wimbo huu ukiusikiliza ukiwa ughaibuni unajisikia kutafuta ndege umyonyoe mabawa yake, uyavae, kisha uruke kwenda kwa Mama Afrika!

Wakati wa pilikapilika za sikukuu wanayoiita krisimasi, kuna rafiki yangu aliyeko Ughaibuni alikumbuka nyumbani hadi akajisikia kuwa mgonjwa. Hii ni sehemu ya ni maneno yake:

Lakini nenda Mashariki,magharibi nyumbani ni nyumbani.
Kule Rombo kumechangamka watu wa mijini wanamiminika kila dakika. Wakitoke sehemu mbalimbali. Zile mengele* zimefagiliwa, nyumba zimefunguliwa maana sikukuu imefika watoto, wajukuu, wamefika nyumbani. Ni sherehe, ni vyakukaanga tu, hakuna kuchemsha, ni mchele unaliwa, chapati na mburu*. Huku mbege ikiwa pembeni, redio one,KBC, na nyimbo za sikuku ya noeli zikirindima.Ni nani asiyeyajua haya? Tulie tulioko ughaibuni! Ama hakika nyumbani ni nyumbani.

**NB: mburu ni mbuzi kwa kichagga
- mengele ni sehemu ya mbele ya nyumba ambayo kawaida kule uchaggani inapambwa kwa maua.

USISAHAU KUMSIKILIZA NAMBIZA JOE TUNGARAZA

Usisahau kuwa kipindi cha redio cha Afroworld kinachoendeshwa na Mtanzania, Nambiza (au Dj Joe) ni jumamosi. Sikiliza kwa kwenda tovuti ya Radio Adelaide: www.radio.adelaide.edu.au , ukishafika hapo kongoli palipoandikwa "Listen Online."
Masaa ndio haya:
Walioko Marikani:
Midwest/East Coast: Saa 1 asubuhi.
West Coast: Saa 10 alfajiri.
Johannesburg: Saa 8 mchana.
DarEsSalaam: Saa 9 Alasiri.London: Saa 6 mchana.
Amsterdam: Saa 7 mchana.
Oslo, Stokholm, Copenhagen : Saa 7 mchana.
Helsinki: Saa 8 mchana.

DUNIA YA VICHAA

DUNIA YA VICHAA!

Ana akili timamu
Au hana?
Nilijiuliza.

Nywele ni msokoto,
Ni rasta au mlala barabarani?
Sikuwa na jibu.

Mara akanisogelea,
Akaniuliza jambo,
Sikumsikia vyema,
Nikamtaka arudie,
Hakurudia,
Akasema:
Kumbe unajua watu wote vichaa.

Vichaa?
Nikamuuliza nikishangaa,
Ndio, dunia nzima imejaa vichaa,
Akajibu akinikazia macho, na kuendelea:
Tazama yanayotokea duniani,
Ndio sababu nimeamua kutumia lile jani,
Bila hivyo nami nitachanganyikiwa.

Niseme nini?

Akaniambia hana makazi,
Kisha akaondoka.

Sijamuona tena hadi leo hii.
- Desemba 31, Marekani


FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com