1/30/2005

TOVUTI BADO ZANITIA KICHEFUCHEFU

Tafadhali kama kuna mtu mwenye limao au ndimu anipatie ili niwe nakula kabla sijatembelea tovuti ya bunge la Tanzania na ile ya ikulu. Kila ninapotembelea tovuti hizi mbili za nchi inayojulikana kwa lugha ya Kiswahili, lugha ambayo ndio inajulikana na kutumiwa na wakesha hoi masaa 24, ninakaribia kutapika kama mtu aliyemeza konokono kwa bahati mbaya. Sijui kama ni mimi peke yangu ninayehoji sababu ya tovuti hizi kuwa katika lugha ya akina Tony Blair na Malkia Lizabeti na sio lugha inayotumiwa na akina Rafaeli (ndio, yule Rafaeli wa kwenye wimbo wa Saganda!), Kalubandike, Mama Giresi, Masanja, Zabuloni, n.k.
Ukitembelea tovuti ya ile ikulu iliyojengewa kuta kama ule wimbo wa Paul Ndunguru usemavyo, "Wanajenga kuta kuzuia wezi wenzao...," unakuta kuna salamu za mwaka mpya wa kirumi wa 2005 ambazo zimetolewa na Rais wa Tanzania kwa wananchi wa Uingereza!
"Inakuwaje rais wa Tanzania atoe salamu kwa wapiga kura wa nchi nyingine na sio wananchi wake?"
Usiniulize. Sina jibu.
Na kama huniamini nenda hapa ujionee mwenyewe. Ukiwa umefumbua macho utaelewa kwanini nimesema kuwa salamu ya Rais ni kwa ajili ya wananchi wa Uingereza.
Leo sio mara yangu ya kwanza kulalamika juu ya hili. Na sio ya mwisho. Lazima tukomeshe huu mchezo unaochezwa na waliozama katika bahari ya utumwa wa fikra.
Rafiki yangu mmoja anayesoma Afrika Kusini kaniambia kuwa tovuti hizi zimegharamiwa na shirika la maendeleo la "umoja" wa mataifa (UNDP). Kuna uwezekano kuwa tovuti hizi zinatumia lugha yao kwakuwa "msaada" umetoka kwao. Hili neno "msaada" karibu nitalifuta kabisa kwenye misamiati yangu. Naona limepoteza maana yake siku nyingi.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com