Mwendo wa kama dakika tano kwa miguu toka nilipohamia hivi karibuni, Old West End, kuna kituo cha sanaa, Collingwood Art Center. Kundi la ngoma za Kiafrika na Karibiani la
Alma Dance Experience limetoa ukumbi wake wa mazoezi kwa ajili ya watu wanaopenda kupiga ngoma. Kwahiyo kila jumapili kuanzia saa saba na nusu watu wanajimwaga hapo na ngoma zao.
Kinachofanyika hapo kiingereza kinaitwa Drum Circle. Watu hutengeneza mduara kisha wanaanza kupiga ngoma. Hakuna anayeongoza. Hakuna kuongozwa. Upigaji unatokana na hisia ya mtu. Kila mtu anapiga ngoma, awe anajua au hajui. Ngoma zinapigwa wee hadi watu wanasuuzika roho zao.
Nilikwenda kwenye mduara wa ngoma kwenye kituo hiki kwa mara ya kwanza. Kulikuwa na watoto, familia, vijana, watu wa makamo, n.k. Watu wengi wanaohudhuria mduara wa ngoma huamini kuwa ngoma/muziki ni aina ya dawa. Ni dawa nzuri sana hasa kwa watu wanaoishi kwenye mfumo wa maisha ambao watu wanafanyishwa kazi kama punda ili kujenga ubepari. Bwana mmoja, kwa mfano, amesafiri umbali saa moja ili kuja kupiga ngoma.
Niliulizwa kama Afrika kila mtu anajua kupiga ngoma au kama Tanzania watu wanapenda kukaa pamoja na kupiga ngoma. Jibu nililowapa liliwashangaza sana. Ngoma tulizokuwa tukitumia zimetoka Afrika. Ngoma yangu kwa mfano imetoka Senegal. Wengi walikuwa na ngoma iitwayo Djembe ambayo ni maarufu sana. Ngoma aina ya Djembe haihitaji kuchomwa moto kama ngoma nyingine ili itoe mlio mzuri. Ngoma hii ina kamba ambazo unazikaza kwahiyo hakuna haja ya kutafuta kuni na kiberiti kila mnapotaka kupata magoma kitakita.
Ni kitu gani kinafanya wenzetu kupenda sana utamaduni wetu wa asili wakati sisi tunauponda? Kundi la Alma Dance Experience kwa mfano linajulikana hapa Toledo kwa ngoma za asili toka Afrika. Kundi hili limeundwa na watu weupe.
Nakumbuka nilipokuwa jimbo la Washington nilikwenda kanisa la Universal Church kwenye sherehe moja. Utashangaa kuwa makanisa ambayo waumini wake wengi ni weupe kama hili la Universal Church upigaji wa ngoma za asili za Kiafrika ni sehemu ya ibada. Ukienda makanisa ya watu weusi wa hapa Marekani au hata yale ya weusi waliohamia toka Afrika huwezi kukuta hata siku moja wakipiga ngoma.
Ukienda kwenye "mduara wa ngoma" popote pale utakutana na watu weupe na weusi wachache sana. Waotunza na kutukuza utamaduni wetu ni kizazi cha wale waliochangia katika kuuharibu. Lakini sisi kwanini hatuoni uzuri wa tulichonacho?
Ninasikia njaa. Ngoja nikatie ndani. Jana jamani nilishiba kama sijui nini. Nilikwenda kwa rafiki yangu toka Sierra Leone, Amira Alghali, ambaye alikuwa amepika ubwabwa wa kisamvu cha mawese. We! Nashangaa sikujing'ata ulimi. Haya ngoja nikale.
Kabla sijasahau. Yule jirani yangu anayefuatilia vifo na majeruhi huko Iraki anaendelea na kazi yake. Namba zilizoko kwenye mabango matatu mbele ya nyumba yake zimebadilika. Leo yapata mwendo wa saa kumi takwimu zilikuwa hivi:
WAIRAKI WALIOKUFA = 12,778
WAMAREKANI WALIOJERUHIWA = 7,230
WAMAREKANI WALIOKUFA = 1,032
Hiyo demokrasia ambayo rais mwizi wa kura Joji Kichaka (george bush) anadai kuwa inajengwa nchini Iraki iko wapi? Si tuliambiwa kuwa Wairaki wanamchukia sana Saddam kiasi ambacho askari wa Marekani watapokelewa kwa shangwe, vifijo, nderemo, na maua? Maua na nderemo vinaweza kusababisha vifo vya askari 1,032 na kujeruhi 7,230? Ngoja nikale.