IKO SIKU NITARUDI...
Kuna hii blogu inaitwa Aturi. Nimeitembelea muda mfupi uliopita. Jamaa mmoja kasema jambo ambalo limeniacha hoi. Kuna kitu kinaitwa The Myth of Return yaani kila mgeni aliyeko hapa ughaibuni huwa ana ndoto za kurudi makwao siku moja ila hakuna anayerudi! Hii imenikumbusha maneno ya Peter Tosh katika wimbo wake wa Equal Rights anaposema, "Kila mtu anatakwa kwenda mbinguni ila hakuna anayetaka kufa." Onaeli Mandambi (bado una kipindi cha Rege Radio One?). Kwa kumbukumbu ya "experience" za Moshi pale kwa Jere usiku tukimsikiliza Tosh akililia haki na Gregory Isaacs akilalama kwa tungo za mapenzi kama Night Nurse huku mchicha wa ugali ukichambuliwa. Kuna raha wakati mwingine kuogelea katika kumbukumbu za miaka ya nyuma.
Kuna bwana mmoja pale Moshi, sijui yuko wapi siku hizi, alikuwa akinikumbusha sana Peter Tosh. Nilikuwa nakutana naye kila jioni pale YMCA. Mrefu, mwembamba, mweusi, na ana sura ya ukaidi kama alivyokuwa Daktari Mitishamba (Bush Doctor) mzee wa "Ihalalishe" (Legalize It) Peter Tosh. Huyu bwana, jina nimemsahau, siku moja tumekaa pembeni ya bwawa la kuogelea la YMCA (Davis Mosha unakumbuka enzi zako na Nick Malisa pale bwawani? Mmoja wenu karibu azame. Hivi alikuwa ni nani vile??) basi huyu jamaa, ambaye ni rasta, alikuwa anasikiliza mhubiri aliyekuwa akiendesha ibada ukumbini. Rasta akamsikiliza wee....kisha akanitazama na kusema kwa kiingereza, "Church is big business." Akanyanyuka na kuondoka. Nilikuwa bwana mdogo wakati huo. "Kanisa ni dili?" Maneno haya niliyafikiria kwa miaka mingi iliyofuata kabla ya kuelewa kwa undani alichokuwa akisema.
Hivi nilikuwa nasema nini tena? Naona nimerukia mambo kibao hadi nimesahau nilichokuwa hasa nataka kusema. Hakuna ubaya. Haya, salimia nyumbani.
0 Maoni Yako:
Post a Comment
<< Home