9/12/2004

Pilikapilika

Niko katika pilikapilika za kuhama. Ninahama toka mtaa wa Leitchworth kuelekea mtaa wa Old West End hapa hapa Toledo, Ohio. Old West End ni mtaa wenye nyumba za kizamani zilizojengwa kwa mtindo uitwao Victorian. Majirani naona wameanza kunitazama kiajabuajabu. Mimi mweusi na mtaa umejaa ngozi nyeupe. Wengine wameanza kuniuliza, "Unafanya kazi gani?" Wanataka kujua kama wamepata jirani asiye na mbele wala nyuma atakayehatarisha usalama wao. Huu ni mtaa wa watu wanaokaa barazani jioni wakinywa mvinyo na kusoma magazeti kama Mother Jones, The Nation, na Village Voice . Wengi wameweka "sticker" za kumponda Bush kwenye magari yao au nje ya nyumba zao wameweka mabango yanayosema, "Rudisha majeshi nyumbani" wakionyesha kutokuunga mkono uvamizi wa kigaidi na kidhalimu uliofanywa na Rais Joji Kichaka dhidhi ya Iraki.


"Jina lako gumu kweli kutamka. Itanichukua muda. Umesema unafanya kazi gani?"
"Nafundisha." Nawajibu.
"Umetoka wapi?" Wananiuliza kutokana na lafudhi yangu.

Asubuhi, mchana, jioni: Jina lako gumu kutamka. Unafanya kazi gani? Umetoka wapi?

Kuna kitu kinaitwa white flight: watu weupe wana tabia ya kuhama mtaa kama ukianza kujazana watu weusi. Najua hii haitatokea maana nikishawaambia ninapofundisha na kuwa nimetoka Tanzania najua hujisemea moyoni, "Huyu ni tofauti." Hii tabia ya kusema kuwa watu weusi tuliotoka nje ya Marekani ni "tofauti" wakimaanisha kuwa sisi ni bora zaidi ya weusi waliozaliwa hapa inaniudhi kishenzi.

Ukitaka kuona baadhi ya nyumba za Old West End kongoli hapa.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com