8/29/2004

MAKALA MPYA

Nenda sehemu yenye makala zangu (pembeni mkono wa kuume) kisha ukongoli kwenye makala mpya niliyoiweka leo. Hii makala niliandika siku za nyuma. Inaitwa UMEDANGANYWA.

HOJI, USIOGOPE

Barua za watu wanaowasiliana nami zinaonyesha kuwa watu wengi bado wanatawaliwa na hofu ambayo imekuwa ikitumiwa na wanasiasa na dini kutupumbaza na kutufanya watumwa. Usiogope kuhoji lolote lile. Wewe kama biandamu una haki ambayo haitoki kwa mtu yeyote (awe rais, hakimu, polisi, kasisi au shehe) ya kuhoji kila kitu. Hoji. Pinga. Iwe ni serikali. Iwe ni dini. Uwe ni mfumo wa elimu. Iwe ni sheria. Iwe ni desturi. Una haki hiyo na hakuna kiumbe ambaye ataweza kukuzuia ukikataa kuwa kondoo.

Watatokea watu watakwambia kuwa ukihoji serikali utafungwa. Anayekwambia hivyo ndiye anapaswa kufungwa. Hoji serikali. Kama serikali uliyoichagua au iliyochaguliwa na wengi (kwa mujibu wa tume yao ya uchaguzi) haiwakilishi matakwa yako, kuna jambo moja la kufanya. IONDOE MADARAKANI. Iangushe. Ipindue. Chukua madaraka. Jiongozeni wenyewe!

Wengine watakwambia kuwa ukihoji mambo ya dini au Mungu utakuwa kichaa. Au utakwenda motoni. Wanaokwambia hivi tayari wanaungua. Muhoji hata Mungu. Anapenda sana kuhojiwa. Utawasikia wakisema, "Tafuteni nanyi mtaona," "Watu wangu wataangamia kwa kukosa maarifa." Laiti wangejua maana ya maneno haya.

Ndugu yangu, hoji usiogope. Kuhoji ni mwanzo wa uhuru.

TUNAKOKWENDA

Madaktari huko Ujerumani wameweza "kuotesha" taya mgongoni mwa Mjerumani mmoja aliyekuwa amepoteza taya lake kutokana na ugonjwa wa kansa. Mgonjwa huyo ameweza kula chakula kwa mara ya kwanza baada ya miaka 9. Soma undani wa habari hiyo kwa kubonyeza hapa.

Ujumbe wa leo

Ujumbe wa leo ni kipande kifupi toka kwenye shairi langu liitwalo TAFAKARI:

Mahakimu wanahukumu
Wala rushwa,
Lakini nao rushwa wanashiriki,
Wao nani atawahukumu?
Nani!

TUKIFUNGUA MDOMO

Tukifungua mdomo kusema
Wako watakaochukia
Na kununa,
Kutukamata
Kutufunga
Kutunyang'anya uraia,
Lakini usishangae,
Hawa ndio waliomsulubu masihi
Huku wanadai kumwamini.
- ndesanjo©
DSM, 2002.

8/27/2004

VITABU VYA URASTA

Kufuatia mfululizo wa makala nilizotoa katika gazeti la Mwananchi juu ya imani na falsafa ya Urasta, watu wengi wameniuliza wanapoweza kupata vitabu juu ya Urasta. Ukiwa Tanzania, kitabu ambacho kinaweza kupatikana kwa urahisi ni RASTA AND RESISTANCE: From Marcus Garvey To Walter Rodney. Kitabu hiki kiliandikwa na Profesa Horace Campbell wakati akiishi na kufundisha nchini Tanzania na kuchapwa na Tanzania Publishinga House. Nadhani unaweza kukipata katika duka la TPH lililoko mtaa wa Samora, jijini Dar Es Salaam. Kwa walioko ughaibuni, tafuteni kitabu kiitwacho RASTAFARI: Healing of the Nations. Hiki nadhani ni kiboko katika vitabu vyote nilivyosoma juu ya Urasta. Kimeandikwa na Rasta mwanasosholojia, Dennis Forsythe.

Baadhi ya Marasta hawapendi kitabu cha Horace Campbell kutokana na madai kuwa Profesa Campbell ni mfuasi wa itikadi ya Ki-Marx. Marx aliandika kuwa dini ni aina ya ulevi wa kupumbaza masikini ili waweze kutawaliwa. Marx hakuwa akiamini uwepo wa Mungu. Kwahiyo Rasta hao wanaona kuwa mtu kama huyo hawezi kuandika kwa usahihi juu ya imani ya Kirasta.

Campbell mara ya mwisho nilimwona Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Nadhani ilikuwa ni mwaka 2002 au mwishoni mwa 2001. Yeye kawaida katika mazungumzo yake huwa anatoa heshima kwa Jah Rastafari. Kwa mfano katika hotuba yake pale Mlimani, alimaliza hotuba yake kwa kusema, "Jah!" na waliokuwa wanajua jinsi ya kujibu wakajibu, "Rastafari." Amekuwa kwa miaka mingi akiandika na kutetea imani ya Kirasta katika duru za kitaaluma. Juu ya imani yake sifahamu. Ila nitafanya mawasiliano naye ili kuweka wazi. Kitabu chake nimekisoma na ninaona ni kitabu ambacho kina uchambuzi wa kina na historia ambayo kila Mwafrika anapaswa kuijua. Kuna mambo ambayo sikubaliani naye, ila kwa ujumla naona kitabu hiki kinafaa kusomwa. Hasa zaidi, watu wanaotafuta ukweli juu ya Rasta kwasababu za kitaaluma na utafiti. Kwa masuala ya kiroho, kitabu cha kusoma ni Rastafari: Healing of the Nations.
Jah! Rastafari!

8/26/2004

Mshahara wa "ukombozi" wa Iraki

Vita ya "ukombozi" wa Iraki ina mshahara wake. Kwa akina Joji Kichaka na wenzake, makampuni yao na yale ambayo wana hisa zake, yanapata tenda na faida za mamilioni ya dola. Ila kwa wazazi ambao wanao, wengine wenye umri wa miaka 18!, wanapigana huko Iraki mshahara wake ni msiba. Watoto wa akina Joji Kichaka na genge lake la watu wanaotaka kuunda "dunia mpya" ambayo itatawaliwa na kundi la watu wachache, watoto wao wako vyuo vikuu wakichukua shahada ili waje kuwa watawala kama wazazi wao. Jana jumatano, mzazi mmoja mlalahoi baada ya kuambiwa kuwa mwanaye kafariki huko Najaf, aliingia ndani ya gereji kuchukua kiberiti na petroli kisha akaingia ndani ya gari la wanajeshi waliomtembelea kumpa taarifa za msiba na kutia gari moto akiwemo ndani. Soma habari yake hapa.

MAMBO YA NYAKATI

Mazungumzo hapo chini yalikuwa yanafanywa na jamaa wawili katika bustani iliyoko nyuma ya kanisa la Kilutheri la mzunguko la Magomeni, jijini Dar Es Salaam, 2001. Nimetoa kwenye mkusanyiko wa mazungumzo, visa, na kejeli za mtaani "Mambo Ya Nyakati." Mkusanyiko huu nimekuwa nikiufanya muda mrefu kwa kalamu na rekoda.
*************************************************************************************


“Usimwone hivi jamaa yule.”
“Kwani vipi? Si chizi yule?”
“Kafika chuo kikuu.”
“Chuo kikuu kaenda lini kila siku yuko mtaani?”
“Hawa ndio wale waliofukuzwa na Mwinyi.”
“Mwinyi aliwaonyesha dawa yao. Ile mijinafunzi ya jabu sana. Walitaka serikali iwape hela hadi za sigara!”
“Sasa walipofukuzwa waliambiwa waandike barua za kuomba msamaha. Jamaa unayemwita chizi akakataa.”
“Mbishi huyo. Nenda kacheze naye drafti pale dukani kwa Mangi…hakubali kushindwa. Kila jioni hakosi taarifa za BBC. Akitoka hapo ni kubishana mambo ya siasa mtaa mzima.”
“Sio siasa tu. Usimuone vile, Kurani imefika na Kiingereza ndio usiseme. Anashusha aya kwa Kiarabu kama vile kaandika Kurani yeye.”
“Kujua Kiarabu na Kiingereza au kukariri Kurani huku huna kitu mfukoni ndio nini sasa? Anaishi kwa nyanya yake hadi leo. Unavyomuona pale kazi hana.”
“Tatizo lake watu wanadai ni laana. Eti kaachiwa radhi na wazazi.”


Shairi: UTAWALA BORA LIENDE©

Swali:
Utawala bora liende
Wawala
Nanyi mwalala?

Kura twapiga, sadaka twatoa
Kodi twalipa, swala twasali
Walalanjaa
Cha moto bado twakiona,
Kwanini?

Demokrasia ghasia, mafukara twauziwa
Jehanamu ya moto, masikini twatishiwa
Wa kusema wamesema
Wa kusikia ni viziwi,
Chukua Chako Mapema
Ni azimio la wapi?

Wale wa dini, siasa, enjioo*
Matumbo yamewajaa kwa hadaa
Hawakosi madaha, mzaha
Karaha, zinaa
Unashangaa
Awe yule wa msalaba
Au mwezi na nyota,
Wa bendera ya kijani
Nyeupe au Nyekundu,
Wa ofisi mfukoni
Kutumbulia ufukweni
Dola za wafadhili,
Hao lao moja.

Unafiki wauafiki
Viambaza vya utawala,
Enjioo mtaji poa
Wasomi changamkieni,
Myooshapo kidole kimoja
Vitatu vyawahukumu.

Kanisani, msikitini
Uhaini dhidi ya imani
Isaka, Ismaeli
Mababu wa akina nani?

Nukuu za maandiko
Anguko la kizazi
Dalili zi wazi,
Waza na kuwazua
Kwani kumepambazuka,
Wameasi desturi
Mistari ya manabii,
Kunga za mababu na mabibi
Kwenu tamthiliya ya punguani.

Utamaduni msalabani,
Siasa Babeli Mkuu,
Ijumaa, jumamosi, jumapili
Kwa kanzu na misahafu
Wawarubuni,
Leo katika Bunge
Mchezo wa kuigiza,
Viongozi kuwa "watawala twawala"
Ni aya ipi ya katiba?

Utawala bora liende wawala
Nanyi mwalala,
Ndotoni mkiimba
Amani na utulivu.

Amani na utulivu
Watawala ikulu wadai
Huku wakinywa divai,
Mavazi tai shingoni
Sisi viraka nguoni,
Jasho, kilio, machozi.

Amani, utulivu
Sitaki,
Sihitaji!

- Ndesanjo©, Tanzania/USA (2003)
*enjioo = NGOs (Non-Governmental Organisations)



"Vidonge" Vya Bob Marley Kwa Kiswahili

Watazame...
Hatia imewaganda
Ndani ya dhamira zao
Watafanya kila wawezalo
Kutimiza madhambi yao
Hawa ndio samaki wakubwa
Walao samaki wadogo.

Kama wewe ni mti mkubwa
Basi sisi ni shoka dogo
Lenye makali na tayari
Kukukatilia mbali
Kwa! Kwa! Kwa!

UZENI! UZENI! UZENI! ©

Uzeni,
Kila kitu uzeni.

Nasema uzeni,
wala bei msitutajie
Mikataba msituonyeshe
Uzeni,
Hata nafsi zetu wauzieni.

Zama za soko huria
Na utandawazi,
Rais atamka
Hotuba redioni.

Utandawizi
Soko holela
Karl Peters wa leo,
Wamasai kuchunga binadamu
Badala ya ng'ombe,
Bajeti kupelekwa Washington
Kabla ya Dodoma.

Dunia ya leo
Ukoloni mamboleo
Wajishinikiza.

Uzeni,
Nasema
Kila kitu uzeni!
- Ndesanjo Macha©, Mbezi, Dar Es Salaam, Tanzania, 2003.

8/25/2004

FREDDY MACHA: HADITHI NA MAKALA ZAKE

Niko mbioni kuweka makala na hadithi za mwandishi, mwanamuziki, na mshairi Freddy Macha. Makala hizi zinatokana na maisha yake Kanada, Uingereza, Brazili, Ujeremani, n.k. Hadithi nitakazoweka ndani ya blogu ni baadhi ya mkusanyiko wa hadithi zake utakaochapwa katika kitabu kitakachoitwa Mpe Maneno Yake.

8/24/2004

AMIRA ALGHALI

Karibu ndani ya blogu yangu! I know you don't speak Swahili, but since you were recently in Tanzania (although you dont remember the name of the places you visited!!!!), I assume you might recognize a few words!

8/22/2004

NIMERUDI

Ndio ndugu zanguni,
Nimerudi usiku wa leo. Nina rundo la barua pepe toka kwenu ambazo zitaweza kuzipitia na kujibu. Ninahitaji kupumzika. Ninashukuru walioniandikia. Walioniuliza maswali nitawajibu.

Ndugu Maka Patrick Mwasomola ninashukuru kwa kunikumbusha juu ya Siti Binti Saad (1880-1950). Nitaandika kidogo juu ya mwanamama huyu ambaye watu wanataka kumsahau ila historia inakataa.

Mwasomola katuma ubeti toka Diwani ya Shaban Robert, Siti Binti Saad, Kitabu cha Tatu:
Siti Binti Saad,ulikuwa mtu lini?
Ulitoka shamba,
na kaniki mbili chini
Kama si sauti ungekula nini?

Ninapumzika kisha nitarudi. Safari imenichosha. Nina mambo kadhaa mapya. Kaa chonjo!

8/18/2004

NINASAFIRI

Ninasafiri leo alfajiri au kesho usiku kuelekea jimbo la Vermont. Nitarudi jumapili. Sina uhakika kama nitakuwa hewani. Ninajaribu kutengeneza blogu hii ili niweze kutuma taarifa kwa simu nawe uweze kunisikiliza kama una spika kwenye tarakilishi (computer) yako. Nimejaribu kwa lisaa limoja sasa lakini bado sijafanikiwa. Ila ninakuachia zawadi ya makala tatu mpya. Ni mpya katika blogu ila ziliandikwa muda kidogo kwa ajili ya safu yangu ya kila jumapili katika gazeti la Mwananchi. Kwa mfano, makala ya Krisimasi bila Yesu niliandika Krisimasi ya mwaka jana. Makala hizo ziko chini ya picha yangu mkono wa kuume. Nenda soma, furahia. Hadithi ya mtoto wa kichagaa na mtoto wa kizungu itaendelea.

Pia niko mbioni kuweka kamera tovuti (webcam) ili ukija kwenye blogu yangu kama niko mtandaoni utaweza kuniona. Au sio? Kwaheri. Uhuru!

Hadithi: Mtoto wa Kizungu na mtoto wa Kichagga!

"Mbona huwa unanikodolea macho sana?" Nimeamua kuvulia maji nguo. Kila siku ninasema nitamuuliza. Leo nimeamua.
"Nakukodolea macho?" Ananiuliza huku akipitisha mkono kichwani kurudisha nywele zake ndefu nyuma.
"Ndio. Hakuna ubaya. Ninapenda kujua kwanini."

Ananitazama. Anatabasamu. Ananitazama tena. Kama ilivyo mazoea yake, anapitisha kichwani vidole vyake vyembamba vyenye kucha zenye matunzo kurudisha nywele nyuma. Yaelekea anapenda nywele zake sana. Jina lake ni Lisa. Mama ni mtaliano. Baba Mmarekani.

"Unataka nikwambie kwanini nakutazama?" Ananiuliza.
"Nataka uniambie ndio maana nimekuuliza."
"Napenda nywele zako." Anasema huku anatoa tabasamu la aibu. Kisha anarudisha nywele nyuma. Safari hii hatumii vidole. Anatikisa kichwa kidogo upande mmoja. Nywele zinatii amri.
" Naomba kushika nywele zako"

ITAENDELEA...
*******************************************************************************
Ndugu yangu kisa hiki kitaendelea. Rudi tena hapa ili usipitwe.

Ngugi Akaribishwa Nai-robbery!

Baada ya kuishi ukimbizini kwa miaka 22, mwandishi na mwanaharakati wa lugha za kiafrika, Ngugi wa Thiong'o amerudi nyumbani Kenya na kukaribishwa na ukweli wa hali halisi ya maisha ya jijini Nairobi, ambayo wengine wanaita Nairobbery. Soma habari za "ukaribisho" huo kwa kubonyeza hapa.

8/17/2004

Mradi wa Maneno ya Kiswahili

Kuna mradi wa kuingiza kiswahili katika teknolojia ya tarakilishi unaoendesha na kampuni ya Microsoft na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Mtu yeyote anaweza kushiriki katika mradi huu kwa kubonyeza hapa.
Najua kwa watu wasiounga mkono kampuni za kibeberu kama Microsoft mradi huu hautawafaa. Kuna watu, kama mimi, ambao tunaegemea zaidi katika programu za tarakilishi zilizo chini ya dhana ya "open source" ambapo programu hizi (tofauti na programu za Microsoft ambazo kanuni [code] zake ni siri na zinamilikiwa na kampuni hii) zinamilikiwa na mtu yeyote. Programu za tarakilishi za "open source" hazilindwi na sheria ya hatimiliki ambayo nia yake ni kutengeneza faida kwa wachache. Dhana ya "open source" au "free source" inabadili kabisa hakimiliki toka kuitwa "copyright" na kuitwa "copyleft." Watu wengine wanasema kuwa ujamaa wa kweli duniani hivi sasa unaonekana katika vuguvugu la "open/free source" (Open/Free Source Movement) ambalo linaichukua dunia kwa kishindo na kutishia Microsoft. Nchi kama Brazil, China, Vietman, n.k. ziko mbioni kuondoa kabisa matumizi ya Microsoft, hasa serikalini, na kuchukua programu za tarakilishi (software) zinazotokana na "open source" (hasa LINUX/GNU).

Kwa taarifa zaidi jinsi ambavyo "open source" inavyosaidia nchi za ulimwengu wa tatu kuondokana na ubeberu mpya kupitia kanuni za programu za tarakilikishi (software codes) bonyeza hapa.

Ukipenda kujua faida za "open source" kwa Afrika (na madhara ya Microsoft) bonyeza hapa.
Ili kujua kwa undani dhana ya "open source" bonyeza hapa.

KUMBE MKAPA UKO HIVI?

Huwa inatokea. Imetokea leo asubuhi, ingawa ni mara chache sana. Rais Mkapa wa Tanzania katoa hotuba ambayo imechemsha damu yangu kabisa. Ni mara chache sana huwa ninakubaliana na wanasiasa (wana si-hasa), au ninahamasika kwa kuwasikiliza au kusoma hotuba zao. Lakini asubuhi ya leo nimesoma hii hotuba ya Mkapa. Na kuisoma na kuisoma tena. Na tena. Na tena. Pamoja na kuwa Mkapa ni kati ya marais wa hotuba (yaani ambao kazi zao zinaonekana kwenye hotuba zaidi ya vitendo) nadhani ni haki kumvulia kofia kutokana na hotuba yake hii. Bonyeza hapa ili uisome.

8/16/2004

Mariamu Dukani Kwa Massawe

MARIAMU DUKANI KWA MASSAWE
Kama kawaida yake Mariamu anaomba soda ya bure.
“Soda za bure zimeisha.” Massawe anamjibu huku akijisogeza karibu na dirisha alikojiegemeza. Anaendelea kuomba huku akilegeza macho.
“Soda za bure zimekwisha. Hunisikii?”
“Hizo kwenye friji sio soda? Angekuwa nanihii ungesharuka kumpa duka zima.”

Ni saa mbili mbili asubuhi. Mariamu amejinasua kama kawaida yake. Massawe tamaa kwa Mariamu zimempalia. Lakini leo hataki kutoa soda bure kama afanyavyo kila Mariamu anapokwenda dukani kwake. Amechoka kuwa bwege. Ameanza kuwa “mjanja wa mjini.” Ni miezi sita imepita toka mtoto wa mjomba wake alivyomtoa MOshi na kumleta jijini aje kuuza duka la rejareja lililoko Mbagala Kizuiani.
“Yaani soda nitoe mimi, kufaidi wafaidi wengine.” Anajisemea.

Halafu, “Wewe jana umejifanya kupita kule sio?” Kulikuwa na ahadi ya kukutana jana jioni dukani kwa Massawe kisha waende Mpakani Guest House. Ni mara ya saba hii Mariamu anaacha kutimiza ahadi.
Mariamu anakataa, “Kupita kule wapi?”
“Usijifanye umesahau. Unadhani sikukuona? Ndio bwanako yule?”
“Bwanangu nani?”
“Yule mwendesha mikokoteni hajakupa hela ya kununua soda?”
“Mimi unaona ni mtu wa kununuliwa soda na msukuma mkokoteni?

Massawe anamsogelea Mariamu kama vile anataka kumnusa. Kisha, “Hivi umeoga wewe?”
Leo ni siku ya kumtolea Mariamu uvivu.
“Kwanini nisioge? Labda wewe hapo ndio huogi. Wachagga nyie mnavyopenda hela mnaweza hata mkasahau kuoga.”
“Mbona nasikia harufu ya janaba?”
“Jamani msikieni huyu. Labda wewe ndio unanuka janaba.”
Massawe anaendelea, “Wewe kule ulikolala umeoga?”
“Hebu mwoneni huyu. Kwanini nisioge?”
Massawe anacheka kwa kejeli na hasira iliyojificha, “Yule naye ana bafu? Maji kapata wapi? Bomba lao limekatwa.”
“Wewe ukilala na mwanamke humpi maji?”
“Kama ameyaleta yeye ataoga.”
“He, yaani umchafue tu?!”
“Nani kamchafua nani?”
“Wewe si ndio umemwagia?” Mariamu anasema huku akiondoka. Ameudhika.
“Uchoyo utakuua. Soda moja ya bure ndio imezua yote haya?”
“We unapenda vya bure tu sio?”

Mariamu hajibu. Anaondoka kwa mwendo wa maringo. Massawe anamtazama. Anazidi kumtamani. Donge la hasira na kukata tamaa linamkaba kooni. Kwa miezi miwili amekuwa akitoa soda za bure ila hajafanikiwa. Anashanga: kwanini waendesha mikokoteni, wapiga debe, madereva, makondakta “wanafaidi” ?

Kosa langu nini? Hana jibu. Anaapa kuwa soda za bure hazitoki tena. Kajifunza. Mjini shule, mjini chuo kikuu!

- Mbagala, Dar Es Salaam, Tanzania, 2001

8/14/2004

Rais wa Tanzania lazima...

Nitaanzisha kampeni ya kuweka kipengele kwenye katiba kinachosema kuwa Rais wa Tanzania lazima awe anafanya mazoezi ya mwili, si chini ya mara tatu kwa wiki. Pia lazima awe anakula chakula bora ambacho ni mboga kwa wingi, maji si chini ya bilauri nane kwa siku, na matunda. Vyakula hivi lazima viwe havina homoni au kemikali, na visitokane na mbegu za kijenetiki. Chakula cha Rais lazima kiwe kimetokana na jasho la wakulima wa Tanzania (yaani hakuna kula chakula toka nje ya nchi). Kwanini Rais wa nchi ambayo inadai kuwa kilimo ni uti wa mgongo ale matunda, maji ya mtunda, mboga, n.k. toka nje ya nchi?

Kutakuwa na kipengele pia kisemacho kuwa Rais akiwa na kitambi (yaani tumbo lililojaa mafuta yasiyotumika na wala kuhitajika mwilini) itabidi ajiuzulu! Naona itabidi pia kuwe na kipengele ambacho kinamzuia Rais kwenda kutibiwa nje ya nchi. Hii itamfanya ahakikishe kuwa nchi ina madaktari na vifaa vya matibabu vya kisasa kwa ajili yake na wananchi wake.

Kwanini tuwe na Rais ambaye hatunzi afya yake? Akishindwa kutunza mwili wake binafsi atawezaje kutunza nchi nzima????

Lakini msije mkasema kuwa haya ni madongo namtupia Rais Mkapa. Haya ni yenu mnayazua! Mimi humo simo.

Makala Mpya

Nimeweka makala mpya. Tazama mkono wa kuume, peleka kiteuzi, kongoli, kisha isome. Ni makala mpya hapa kwenye blogu yangu ila ilitolewa kwenye gazeti la Mwananchi zamani kidogo. Jumapili hii katika ukurasa wangu gazeti la Mwananchi ninaongelea masuala ya utamaduni, lugha za asili, na Ngugi wa Thiong'o. Makala inaitwa: Je mnamtabua Shetani Msalabani? Kicha hiki kinatokana na jina la kitabu cha Ngugi alichoandika kwenye karatasi za chooni akiwa jela kwa lugha ya Gikuyu kiitwacho Caitaani Mutharabaini (Shetani Msalabani). Nitaiweka makala hiyo hapa ndani jumapili jioni au jumatatu.

Kucheka ni Afya

Hivi unakumbuka enzi za "matani" shuleni? Kuna jamaa walikuwa nadhani hawalali, wanakesha wakitunga matani maana wakija shule kila asubuhi wana matani mapya makali makali. Walikuwa wakiogopeka. Nakumbuka kuna jamaa alikuwa akiitwa Prospa. Huyu hakuna mtu alikuwa anawezana naye.

Kuna mtu alinitumia haya matani ya Kikenya miezi kadhaa iliyopita. Yatazame. Unaruhusiwa kucheka. Kucheka ni bure. Na ni afya. Haya soma:

1.Wewe ni m-short mpaka ukikalia kwa pavement miguu ina hang kwa hewa.
2. TV yenu ni ndogo lazima ufunge jicho moja ndio uone picha.
3. We m-black mpaka una-sweat soot.
4. Manzii wako nim-ugly mpaka alikataliwa ku-act horror movie.
5. Nyumba yenu ni ndogo mpaka lazima utoke nje ku-change mind.
6. Kwenu nyinyi ni wengi mpaka kwa haos (house) kuna round-about.
7. Nyanya'ko mjinga mpaka ali-fail blood test.
8. Kwenu nyinyi ni mbumbumbu mpaka kupata driving licence ilibidi mpelekwe boarding school.
9. Wewe ni m-black mpaka mosquito ikitaka kukuuma lazima itumie tochi.
10. Nywele za watoto wenu ni ngumu mpaka mnazitumianga kama steel wool.
11. Ati siku moja ulitembea kiatu ikaisha, ukaendelea kutembea mpaka miguu ikaisha hadi kwa magoti.
12. Mko wengi kwa haos (house) mpaka kuna rush hours na kukinyesha kunakuwa na traffic jam.
13. Wewe ni m-short unatokanga kwa bed na parachute.
14. Wewe ni mrefu mpaka ni wewe huongezea jua makaa.
15. Chali yako ni mkonda alibloiwa na wind mpaka S.Africa na hana passport.
16.Shingo yako ni refu mpaka ukikunywa maziwa inafika kwa tumbo ikiwa mtindi.
17. Wewe ni mweusi ukikanyanga makaa unawacha footprint za black kwa makaa.

Patrick Balisidya

Ni huzuni iliyoje mwanamuziki Patrick Balisidya ametutoka. Tukumbuke kuwa Hukwe Zawose naye aliaga dunia mwaka huu. Wanamuziki hawa wawili walikuwa na kipaji cha ajabu. Ila ni Watanzania wachache ambao ukienda majumbani kwao utakuta wakiwa na miziki ya watu hawa. Inasikitisha kuwa Balisidya amefariki akiwa analalamika bila kusikilizwa na mtu yeyote juu ya kudhulumiwa vyombo vya muziki na serikali ya Tanzania. Historia ya dhuluma hii ni ndefu. Nitaigusia katika makala ninayoandika juu yake na wanamuziki wengine walioaga dunia wakiwa na majonzi ya kutupwa na jamii. Pitia tovuti hii ya BBC upate habari za maziko yake na pia uone mawazo ya baadhi ya watu kama akina Balozi Dola ambao walikuwa wakimfahamu kwa karibu.

8/10/2004

Dar Es Salaam, Julai 2003:

Nimeingia kwenye ofisi ya serikali. Binti anayepokea wageni ameketi anaongea na mtu kwenye simu yake ya mkono. Inaelekea wanaongea mambo yanayohusu harusi. Mambo ninayoyasikia ni kama,
“Ehe, hizo kadi ndio zinatolewa lini?”
“Na kikao kinafanyika lini na lini?
“Sare tunashona nini?”
"Lakini ndugu yako yule naye, yaani pale ndio amefika? Yaani mabinti wote wazuri pale ofisini kwake ameshindwa kupata wa kuoa?"

Nimesimama namtazama. Nimekuja ofisi hii ya serikali ninahitaji huduma. Hii ni ofisi ya serikali yangu. Ananyanyua macho na kunielekeza kwa kichwa niketi kwenye viti vikuukuu vilivyopo pembeni. Ninaketi. Kiti kinatoa mlio kama vile kinataka kuvunjika. Ninashtuka. "Kaa tu usiogope." Ananiniambia na kuendelea na gumzo. Mara anatokea binti mwingine akiwa na rundo la magazeti ya udaku. Anayaweka mezani, "Ukimaliza kusoma mpatie Halima. Bosi wake kaenda Bagamoyo kwenye semina. Kaboreka kweli. Hana kazi." Ananitazama kisha anamuuliza mwenziye, “Umemhudumia huyu kaka?”
“Bado,” anamjibu.
“Maliza basi simu hiyo umhudumie, mimi hadithi yangu ile ya wiki iliyopita nataka kuimalizia kabla Shomari hajaja. Nimemuomba anipeleke Kariakoo mara moja.”

Shomari ni dereva wa moja ya magari ya ofisi hii ya umma. Magari haya wanayatumia kama yao binafsi!

“Kaka samahani, hivi hizo ni nywele zako?," anayetaka kumalizia hadithi ya gazetini ananiuliza huku akitafuta ukurasa wenye hadithi yenyewe. Maneno yanashindwa kunitoka kwa kutokuamini ninachoshuhudia mbele ya macho yangu.

Ofisi ya umma imefanywa kama sebuleni kwa mtu! Sijaulizwa kilichonileta hapa. Sijahudumiwa. Naulizwa juu ua nywele zangu!

Naitazama ofisi hii. Nawatazama mabinti hawa wawili waliojichubua. Ninatikisa kichwa. Watanzania tunaamka asubuhi na mapema, sio kujenga nchi bali kuibomoa!

Hii Ni Dar Es Salaam

Kawaida mimi hutembea na kitabu cha kumbukumbu. Naandika matukio, mazungumzo, visa, mikasa, na masuala yote ninayoona yanafaa kurekodiwa na mwandishi mpita njia. Hii ni sehemu ya mambo niliyoandika nilipokuwa Dar mwaka jana. Soma:

DAR ES SALAAM, 2003
Zimepita siku kadhaa toka niwasili ndani ya Bongo. Niko ndani ya basi katika kituo cha mabasi Mwenge. Naelekea Mbezi Beach.
Mpiga debe anadai shilingi 100. Kondakta anagoma kutoa. Mpiga debe anakuja juu. Kondakta anakuwa mbogo. Mpiga debe naye anakuwa simba mla watu. Hasira zinawapanda kwa kasi ya mwanga. Mishipa inawatoka. Damu inachemka. Mpiga debe anatoa vitisho. Kondakta anatoa matusi. Vitisho. Matusi. Mate yanaturukia abiria. Matusi yanatuparamia. “Twende mnasubiri nini?”, abiria wanakuja juu. Mpiga debe anatafuta jiwe. Kondakta anachomoa chupa toka chini ya kiti. Wanatishiana. Abiria mmoja anayenuka pombe ananyanyuka na kumaka, “Yuko wapi? Aje huku tumwonyeshe kilichomyoa kanga manyoya.” Hivi ni nani alinyoa kanga manyoya?

Basi linaondoka kituoni kwa kasi. Tunabaki na mlevi ndani ya basi. Ataongea njia nzima. Jambo moja ambalo haachi kusema kila baada ya dakika mbili ni, “Mimi sijalewa hata kidogo. Mtu asije akafikiri kuwa nimelewa.” Hivi kwanini walevi hupenda kusema hawajalewa hata wakati ambapo hakuna aliyesema kuwa wamelewa? Huenda mlevi huyu akifika nyumbani ataamsha wanawe bila sababu. Huenda mke wake akapata kipigo bila kosa lolote. Njia nzima anashusha lawama nyingi tu kwa Mkuu wa Mkoa, Makamba. Makamba ameamuru baa zifungwe mapema. “Yaani anataka tukanywe bia nyumbani? Hana akili kabisa. Nani kamwambia bia ya nyumbani ina ladha? Nyumbani watu tunakunywa chai na maji. Bia ni baa sio nyumbani!” Anaongea kwa sauti ya juu.

Harufu ya pombe iliyochanganyika na mdomo unaonuka vinachafua zaidi hewa nzito na jasho ndani ya basi. Tumejazana. Joto ni kali. Hewa ni nzito. Mlevi anaendelea, “Hivi nyie makonda na wapiga debe wenu, nani aliwaambia kuwa abiria hatujui mabasi ya kupanda mpaka mtuelekeze?”

Hadi hivi sasa mimi bado najiuliza hili swali. Na jingine: nani alimyoa kanga manyoya? Mpiga debe yule naye bado hajui nini kilimyoa kanga manyoya. Walalanjaa wa nchi hii nadhani hivi sasa wanajua kilichomsibu kanga. Maisha yao ya kila siku ni sawa na mtu anayeonyeshwa cha “mtema kuni”.

Hivi mtema kuni alifanya nini? *****************************XXX******************************

MAKALA ZINASOMEKA SASA

Ndugu zanguni, sasa makala zinasomeka. Peleka kiteuzi (mouse) na kongoli kisha usome. Nyingine zinakuja. Asanteni.

8/09/2004

Umeshacheka leo hii?

Nimetoka hospitali kuwekewa "vibanzi" (hili neno, vibanzi, sina uhakika kama ni la kiswahili au kichagga!) kwenye sehemu ambazo mbavu zilivunjika na kukunjika kwa kucheka baada ya kutembelea tovuti ya Bill Powers (http://powers-mbongo.freeservers.com/) na kukuta vipande hivyo hapo chini. Kwakuwa kucheka ni afya nimeamua nikugawie na wewe kichekp. Ila hakikisha unatunza mbavu zako. Haya soma hapo chini:


1. Ukipiga yowe bila kusimama kwa miaka 8, miezi 7 na siku 6, utazalisha nishati tosha kupika kikombe kimoja cha chai. (sioni sababu ya kujisumbua kufanya> hivyo. Bora kutumia jiko la mchina) .
2. Ukitoa mashuzi bila kusimama kwa muda wa miaka 6 na miezi 9, utazalisha gesi ambayo itatosha kutungeneza nishati kwa ajili ya bomu la atomiki (hapo sibishi! Watanzania tuongeze mazao ya kunde na maharage na tutapewa kura ya veto Umoja wa Mataifa).

3. Inamchukua nguruwe dakika 30 kukamilisha "orgasm" au bao kwa lugha ya kimtaani. (Kuna mtu anataka kuwa> nguruwe?).

4. Binadamu na papa ndiyo wanyama pekee wanaofanya tendo la ngono kwa starehe (kwa nini nguruwe hakuwekwa kwenye hii list?)

5. Mende huweza kuishi siku 9 bila kichwa chake.

6. Simba huweza tendo la ngono zaidi ya mara hamsini (50) kwa siku. (Bado nguruwe nafaidi zaidi!).

7. Tembo ni mnyama pekee asiyeweza kuruka.

8. Jicho la bundi ni kubwa kuliko akili yake.(nimeshakutana na watu ambao wako namna hii)!

9. Mtu akikuudhi, inakuchukua misuli 42 ya uso wako kununa. Inakuchukua misuli minne (4) kumchapa kibao! (uamuzi ni wako).

Mapinduzi ya Zana Mpya za Habari na Mawasiliano

Kwa wale wanaofuatilia kwa karibu maendeleo ya zana mpya za habari na mawasiliano katika bara la Afrika, unaweza kuwa ukitembelea blogu yangu nyingine: http://digitalafrica.blogspot.com

MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Habari ya huyu bwana anayedai kuwa mapinduzi ya Zanzibar eti ni uhaini na kuwa ubaguzi wa rangi ulianza baada ya mwaka 1964, watu weusi walipotwaa madaraka, kuna watu waliikosa nilipoiweka siku za nyuma. Nenda kwenye hii tovuti usome anachosema huyu bwana aliyeko Uarabuni. Peleka kiteuzi chako hapa kisha kongoli usome changamoto hii.

8/07/2004

Abdulrahaman Babu

Miaka minane iliyopita mwezi kama huu, Mohammed Abdulrahaman Babu alitutoka. Tumkumbuke kwa kusoma historia yake fupi kwa kubonyeza HAPA. Na pia kwa wale wenye uwezo wa kukipata kitabu chake, African Socialism or Socialist Africa, tafadhali kipitieni. Kimeandikwa miaka mingi lakini ujumbe wake bado unatufaa hadi leo. Sina uhakika kama kinapatikana katika duka la TPH pale Samora, jijini Dar. Mlioko Dar mnaweza kujaribu.

NGUGI WA THIONG'O

Ngugi wa Thiong'o, yule mwandishi mahiri, mtetezi, na mtunzaji wa utamaduni wa Mwafrika toka nchini Kenya, amerudi nchini kwake baada ya kuishi uhamishoni kwa miaka 22 na kupokelewa kama shujaa. Bonyeza hapa usome habari hizo. Pia unaweza kwenda HAPA.

Ngugi, ambaye zamani alikuwa akiitwa James Ngugi, aliondoka Kenya mwaka 1982. Wakati huo alikuwa ameshatumikia kifungo kutokana na mchezo wake uitwao Ngaaika Ndeenda ambao serikali ya Kenya ilidai kuwa ulikuwa na ujumbe wa kihaini. Akiwa kifungoni aliandika vitabu viwili: Caitaani Mutharabaini (Shetani Msalabani) na Detained: A Writer's Prison Diary. Toka mwaka 1986, baada ya kuandika kitabu kiitwacho Decolonising the Mind, Ngugi aliamua kuwa hataandika tena vitabu vyake kwa kiingereza bali Kiswahili na Kikuyu. Wanaoweza kutafsiri, watafsiri kama ifanywavyo kwa waandishi wa kifaransa, kihindi, kiarabu, n.k. Kitabu chake kipya, Murogi wa Kagogo, kilichoandikwa kwa miaka 7 kwa lugha ya Kikuyu kinatolewa nchini Kenya mwezi huu. Tafsiri yake ya kiingereza iko mbioni kutolewa.

Sijui kama mlioko Dar Es Salaam mliweza kwenda kumsikiliza hivi majuzi alipoongea na umma pale Mlimani. Ambao hawakuwepo wanaweza kupata habari kwa kubonyeza hapa. Changamoto aliyoitoa natamani watu wasingeichukulia kwa mzaha. Ukoloni umetenganisha kichwa na kiwiliwili. Soma habari aliyoyasema pale Mlimani utanielewa. Kisha jiulize ni lini tutaviunganisha?

Nilipotea kidogo

Toka jumatano sijaonekana. Lakini tuko pamoja. Nilikuwa nimebanwa katika hizi mbio za paka na panya za ughaibuni. Unajua kuwa maisha hapa tunasema polepole sio mwendo, harakaharaka ina baraka. Baraka tele. Nilikuwa mbio, mbio. Ulimi nje. Nahema juujuu. Unajua ikifika mwisho wa mwezi wenye kodi na bili zao wananyoosha mkono. Unapewa dola kwa mkono huu, jamaa wengine wanakuja kuzichukua kwa mkono mwingine: kodi ya nyumba, bili za simu, umeme, mtandao wa kompyuta, bima, takataka, shule ya mtoto, malipo ya yaya, bili ya vituo vya luninga vya kulipia, malipo ya kila mwezi ya vitu vilivyonunuliwa kwa mkopo; fedha za petroli, chakula, mavazi, muziki, vitabu, video; fedha za kwenda filamu...orodha inanitia hasira. Tuishie hapo. Uzuri mmoja hakuna michango ya harusi, ubatizo, ubarikio, vikao vya harusi, n.k.

Ningekuwa pale Tabata au Mbagala si ninakwenda kwa mwenye nyumba na kumwambia, "Mwezi huu mambo hayajanikalia sawasawa." Ukiongea na mwenye nyumba vizuri kinaweza kueleweka. Hapa ukichelewesha kodi siku moja unaanza kutozwa faini! Kama ni pale Msasani Mikoroshini unaweza kwenda kwenye duka la Mangi au banda la Mzee Hemedi kuchukua nazi, sukari, chumvi, mafuta, mchele, unga kwa mkopo.

Sasa hapa nimezungukwa na masupamaketi makubwa makubwa, ukiwaambia wakukopeshe wanaweza waite gari la wagonjwa lije likuchukue. Lazima utakuwa huna akili timamu.

Kwa ufupi nimerudi ndani ya nyumba toka kwenye pilikapilika katika "nji" hii ya Rais Kichaka ambaye huenda akawa ndiye Rais mbumbumbu katika Marais wote waliowahi kutawala Marekani. Na sio ajabu akawa ndio rais mbumbumbu namba moja duniani hivi sasa. Hadi alipochaguliwa kuwa Rais, Bwana Kichaka alikuwa hajawahi kusafiri nje ya Marekani. Hadi anakuwa Rais alikuwa hajui kuwa Brazili kuna watu weusi. Brazili ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya watu weusi duniani baada ya Nigeria. Mpaka hivi majuzi alikuwa akiitaja Afrika anasema, "Nchi ya Afrika," wakati Afrika ni bara! Amekiri mwenyewe kuwa hana tabia ya kujisomea vitabu. Sijui kama alishawahi kukaa chini na kusoma kitabu akakimaliza. Nadhani huwa anajisomea Biblia mara kwa mara maana eti anadai kuwa ameokoka. Jamani!

8/04/2004

Chooni Nairobi!

*Tunaendelea na kitabu changu cha kumbukumbu:

NAIROBI, July, 2003
Tumefika Afrika. Bara langu nilipendalo ambalo huniangusha kila wakati. Kila upande nikilitazama naona maafa. Kama sio vita basi ni ukimwi. Kama sio wizi wa maliasili unaofanywa na kundi la watu waitwao “viongozi” basi ni rushwa, uzembe na uvivu. Kama sio vita vya kugombea dhahabu na almasi basi ni vita vya kikabila. Kama sio wizi wa kura basi ni wizi wa matumaini ya wananchi wa unaofanywa chini ya mwavuli wa ubinafsishaji, soko holela, na utandawizi.

Wakati nasubiri ndege kuelekea Dar Es Salaam toka Nairobi, naelekea chooni. Hapa ndipo ninajua kabisa kuwa nimerudi nyumbani. Baada ya kufungua mlango ambao ulikuwa hauna kitasa na rangi yake imebabuka, nilipigwa kofi kali la harufu nzito iliyokomaa ya mkojo na kinyesi.

Sehemu ya kukojolea, vibao vyake vya marumaru vimebadilika rangi toka rangi nyeupe na kuwa njanonjano hivi. Ndani ya chumba cha kwanza cha haja kubwa kuna mtu amejisaidia bila kusafisha. Pananuka, balaa!

Sehemu ya kusafishia mikono maji yanatiririka. Bomba hazifungi sawasawa. Inaelekea hakuna mtu anayejali kutunza maji. Juu ya sehemu hii ya kusafishia mikono, upande wa kulia, kuna tambara chafu na kuukuu. Sijui nani kaliweka hapa. Labda linatumiwa na wale wanaofanya “usafi” hapa. Sijui ni usafi gani huwa wanafanya. Mahali hapa ni pachafu kupindukia.

Tunapoelekea ndani ya ndege kuelekea Dar Es Salaam, afisa mmoja usalama ananiambia nitoe kofia niliyoivaa. Namuuliza, “Kwanini?” Anasema kuwa hiyo ni kawaida. Abiria lazima watoe kofia ili wasije wakawa wameficha silaha au chochote. Namwambia, “Sidhani kama hii ni kawaida yenu.”

Mwenzake anakuja na kuniambia kuwa kila mtu lazima avue kofia. Namuuliza, “Hata wazungu?” Anajibu, ‘Ndio. Kila mutu” Namwambia kuwa anasema uongo. Mzungu aliyekuwa mbele yangu amevaa kofia ila hakuambiwa aivue!

Nawaambia kuwa nitavua kofia iwapo mzungu aliyepita kabla yangu atarudishwa ili naye avuliwe kofia. “Au wanaobeba silaha na madawa ya kulevya ni ndugu zenu tu?” Nawauliza nikimaanisha Waaafrika. Nagoma kabisa kuvua kofia. Mmoja wa maafisa hawa anamwendea mzungu waliyemwachia apite bila kuvua kofia na kumrudisha ili akaguliwe tena. Nami navua kofia yangu.

Nimetoka ughaibuni ambako watu wenye rangi yetu wanabaguliwa kila kona. Ingawa ubaguzi wenyewe sio wa wazi. Narudi nyumbani nakuta ndugu zangu ndio wanaonibagua! Huzuni inanikaba koo. Afrika yangu itaamka lini?

Wakati uliotabiriwa na manabii?

*Naendelea kuwafungulia kitabu cha kumbukumbu. Baadhi ya yaliyomo katika kitabu hiki yametoka kwenye makala yangu ya kila jumapili, Gumzo la Wiki, katika gazeti la Mwananchi. Mengine yatatoka katika kitabu siku za usoni. Haya endelea:
***********************************************************************************

Amsterdam, July 2003:

Aliye mbele yangu ana pasi nyeusi ya Kimarekani. Ni kijana aliyejaza kidogo. Mwamerika Mweusi. Afisa Uhamiaji anaitazama pasi yake kisha anamrudishia. Ni kitendo cha sekunde chache. Pasi yangu ni ya kijani. Anaitazama. Ukurasa wa kwanza, wa pili, tatu, nne… hadi wa mwisho. Anarudi ukurasa wa kwanza. Anaifungua katikati anatazama. Anafungua ukurasa wenye picha yangu, anaitazama, kisha ananitazama kwa muda. Anaitazama tena.

Namkodolea macho. Nataka kumsemesha. Ninaacha. Nina uchovu wa safari. Watu kama hawa ninagombana nao kila siku huku ughaibuni. Nataka kumuuliza kama tatizo ni rangi yangu. Au ni ndevu zangu (ingawa zangu sio ndefu kama za yule bwana anayeishi mapangoni huko Afghanistani!) Au ni nchi niliyotokea?

Tanzania najua ni nchi ya amani na utulivu katika lindi la dhiki, rushwa, unyama wa polisi, na uongo wa kisiasa. Ni nchi ya “uwazi na ukweli.” Au huenda ni kweli vijana wanavyopenda kusema, “Ganda la kijani ni nuksi tupu,” wakimaanisha kuwa pasi ya Kitanzania haina baraka.

Afisa uhamiaji ananiuliza kama nina kadi ya kijani (green card). Nasema ndiyo. Namwonyesha. Anaitazama, anataka kunirudishia, anaitazama tena, kisha ananipa. Niko Amsterdam njiani kuelekea Tanzania. Hali ya dunia imebadilika. Vita. Hofu. Ugaidi. Uvumi wa vita. Mabomu ya kujitoa mhanga. Na bila kusahau silaha za maangamizi!

Nakumbuka wimbo wa Bob Marley wa Real Situation. Anasema:

Check out the real situation Nation war against nation.Where did it all begin?When will it end?Well, it seems like: total destruction the only solution,And there ain't no use: no one can stop them now.Ain't no use: nobody can stop them now

Maneno haya yanaelezea wakati tunaoishi leo hii. Labda huu ndio ule wakati ulionenwa na “manabii wa kuja.”

8/03/2004

MAJINA YA KISWAHILI

Nimekuwa nikifuatilia Wamarekani weusi wanaojipa au kuwapa watoto wao majina ya Kiswahili katika jitihada za kutukuza Uafrika. Unajua kuwa Wachina wanatumia majina ya Kichina, Wajapani ya Kijapani, Waarabu ya Kiarabu, Wahindi ya Kihindi, Waingereza ya Kiingereza, Waskotishi ya Kiskotishi, Wayahudi ya Kiyahudi, Warusi ya Kirusi. Sisi Waafrika ndio ambao tuna tabia mbaya sana ya kukimbilia Uarabuni au Ulaya kuazima majina ya kuwapa wanetu.

Huwa tunadhani kuwa majina ya Kiarabu kama Abdallah, Mohammed, Abdul, n.k. ni majina ya Kiislamu. Haya ni majina ya Kiarabu. Uislamu maana yake ni unyenyekevu na kujitoa kwa Mungu. Hauna uhusiano wowote na Uarabu. Unaweza kuwa Muislamu safi na ukaitwa Magesa, Mbonenga, Eliaichi, au Masanja. Tufahamu kuwa majina ya Kiarabu yalikuwepo miaka mingi kabla dini ya Uislamu haijaanza. Waarabu wametufanya tukadhani kuwa Uarabu ndio Uislamu. Ndio unaona watu wanavaa kamaWaarabu, wanatumia lugha yao, wanachukua majina yao, na hata wanataka kuongea kama wao wakidhani kuwa huo ndio Uislamu.

Wakristo nao wanadhani kuwa majina kama George, Charles, Grace, n.k. ni majina ya Kikristo. Tunajua kuwa hata ni majina toka Ulaya na Yesu ambaye ndiye wanamfuata hakutoka Ulaya. Hakuwahi kufika Uingereza, kwa mfano, na wala hakuongea Kiingereza. Hakufika Ufaransa wala Italia. Alikuwa myahudi. Alizungumza lugha ya Aramaic. Majina tunayoyaita ya Kikristo ni majina ya tamaduni zilizoleta "Ukristo wa Ulaya" Afrika (nasema Ukristo wa Ulaya maana Ukristo ulikuwepo Afrika kabla ya kuja kwa Wamisionari). Kwahiyo walipokuja wakadanganya wazee wetu kuwa majina kama Matengo, Nyundo, Ossu, n.k. hayakubaliwi machoni pa Bwana! Kuna maeneo ambayo hadi leo hii kanisa katoliki linakataza watu kutumia majina ya asili. Waumini wanaambiwa, "Hayo ni majina ya kinyumbani!" Hivyo wanashauriwa kuchukua majina ya "watakatifu," ambao kawaida huwa ni wazungu!

Waafrika tunaweza kuwa masikini kiuchumi na tukawa nyuma kwa teknolojia ya kisasa lakini hatuwezi kuwa masikini wa fikra kiasi cha kushindwa kuwa na majina yanayotambulisha na kuenze tamaduni zetu.

Kwa ufupi, hakuna kitu kama "majina ya kidini" huku duniani. Majina ni ya kitamaduni. Ndio maana unaona kuwa Waarabu wakristo wana majina ya Kiarabu ingawa sio waislamu. Sababu ni kuwa wanachukua majina ya utamaduni wao bila kujali kuwa wao ni wakristo au waislamu.

Wamarekani weusi wanapenda sana majina ya Kiswahili. Wanashangaa kuona watu tumetoka Afrika tukiwa na majina ya kikoloni hadi leo, na tukipata watoto tunaendelea kuwapa majina hayo hayo.

Yapo baadhi ya majina ambayo yananifurahisha sana kwakuwa yametungwa kwa ubinifu mkubwa. Moja ya majina yanayonimaliza ni Kalamu Ya Salamu.
Majina mengine ambayo nimekumbana nayo ni kama Talib Kweli (mwanamuziki wa Rap), Amiri Baraka (mwandishi, mwanaharakati, na mshairi), Haki Madhubuti (mshairi), Maulana Karenga (mwanzilishi wa sikukuu ya Wamarekani Weusi yenye jina la Kiswahili, Kwanzaa na Mkurugenzi wa Idara ya Masomo ya Waafrika katika Chuo Kikuu cha California, Berkley) na mke wake Tiamoyo Karenga, Maisha Ongoza, Mapinduzi Leo, Rafiki Mtumishi, Malaika Jabali (mcheza sinema), Fani Adili, Harambee Afrika, Ujamaa Muhammad, Akili Mali, Sheria Haki, Mtoto Wa Afrika, n.k.

Sikukuu ya Kwanzaa ambayo husherehekewa mwezi wa kumi na mbili kwa siku saba inatumia maneno mengi ya Kiswahili. Kila siku, kwa mfano, kwa siku saba wanajamii na wanafamilia hukumbuka na kuenzi nguzo moja. Kwahiyo kuna “seven principles” ambazo wanaziita kwa Kiswahili nguzo saba. Nguzo zote saba ni za Kiswahili: ujamaa, ujima, kujichagulia, kuumba,nia, umoja, na imani.

Wakati wa kusheherekea Kwanzaa, watu husalimiana kwa Kiswahili, “Habari Gani?” Na kama siku hiyo watu wanaenzi nguzo ya ujamaa, basi mtu atajibu, “Nzuri, ujamaa.” Kama ni siku ya nia, watasema, "Nzuri, nia."

Alama zinazotumika katika sherehe hii nazo zimepewa majina ya Kiswahili: mazao, mkeka, kinara, mishumaa saba, mhindi, kikombe cha umoja, zawadi, na bendera. Kama unataka kujua zaidi juu ya Kwanzaa nenda hapa: http://www.officialkwanzaawebsite.org/

Maulana Karenga ni mwanzilishi pia wa falsafa ya Kiafrika yenye jina la Kiswahili: Kawaida.

Nilikuwa nazungumzia juu ya majina ya Kiswahili kumbe nimesharukia kwenye Kwanzaa. Lakini yote ni katika kusema kuwa Kiswahili sio lugha ya kudharau na kuchezea. Tuikuze na kuiheshimu. Tukiipoteza lugha hii tutapoteza na nafsi zetu. Kumbuka maneno ya Shaban Robert, “Titi la mama litamu ingawa la mbwa.

****Ukipeleka kiteuzi (mouse) juu ya sehemu zenye rangi ya njano hapo juu na kubonyeza utapata habari zaidi****

Hivi...

Hivi wanasiasa wasipotudanganya kura tutawapa?
Inaelekea tunapenda sana kuambiwa kuwa tutajengewa barabara, hospitali, shule, n.k. Hata tunapojua kuwa tunadanganywa, bado tunafurahia. Hivi kinachomfanya Mtanzania afurahie kwa kupiga makofi, kuimba mapambio, na kupiga vigelegele anaposhangilia kudanganywa ni kitu gani?

Akija mgombea akasema, "Mkinichagua sitawajengea barabara wala shule wala hospitali. Mara baada ya uchaguzi hamtaniona hata siku moja. Sina fedha za kuzunguka jimbo langu la uchaguzi. Sitaki kuwadanganya. Nitakachofanya ni kuwa mwakilishi wenu bungeni. Basi." Atachaguliwa?

Hivi kura zisingekuwa kula, wagombea wangegombea?

TEMBELEA TOVUTI YA WATANZANIA

Kuna tovuti nzuri sana ya Watanzania. Unakaribishwa kuingia jamvini kujadili masuala. Kongoli hapa uione. Inaitwa kumekucha.com.

8/01/2004

Itazame sinema ya Bongoland

Sinema iliyotengenezwa na Mtanzania, Josiah Kibira, iitwayo Bongoland inaelekea kufurahiwa na kila waliotazama. Unaweza kuona kipande kidogo cha sinema hii inayoonyesha masahibu yanayokumba vijana wa Kitanzania wanaokuja kutafuta maisha hapa Marekani. Kongoli hapa uitazame.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com