8/03/2004

MAJINA YA KISWAHILI

Nimekuwa nikifuatilia Wamarekani weusi wanaojipa au kuwapa watoto wao majina ya Kiswahili katika jitihada za kutukuza Uafrika. Unajua kuwa Wachina wanatumia majina ya Kichina, Wajapani ya Kijapani, Waarabu ya Kiarabu, Wahindi ya Kihindi, Waingereza ya Kiingereza, Waskotishi ya Kiskotishi, Wayahudi ya Kiyahudi, Warusi ya Kirusi. Sisi Waafrika ndio ambao tuna tabia mbaya sana ya kukimbilia Uarabuni au Ulaya kuazima majina ya kuwapa wanetu.

Huwa tunadhani kuwa majina ya Kiarabu kama Abdallah, Mohammed, Abdul, n.k. ni majina ya Kiislamu. Haya ni majina ya Kiarabu. Uislamu maana yake ni unyenyekevu na kujitoa kwa Mungu. Hauna uhusiano wowote na Uarabu. Unaweza kuwa Muislamu safi na ukaitwa Magesa, Mbonenga, Eliaichi, au Masanja. Tufahamu kuwa majina ya Kiarabu yalikuwepo miaka mingi kabla dini ya Uislamu haijaanza. Waarabu wametufanya tukadhani kuwa Uarabu ndio Uislamu. Ndio unaona watu wanavaa kamaWaarabu, wanatumia lugha yao, wanachukua majina yao, na hata wanataka kuongea kama wao wakidhani kuwa huo ndio Uislamu.

Wakristo nao wanadhani kuwa majina kama George, Charles, Grace, n.k. ni majina ya Kikristo. Tunajua kuwa hata ni majina toka Ulaya na Yesu ambaye ndiye wanamfuata hakutoka Ulaya. Hakuwahi kufika Uingereza, kwa mfano, na wala hakuongea Kiingereza. Hakufika Ufaransa wala Italia. Alikuwa myahudi. Alizungumza lugha ya Aramaic. Majina tunayoyaita ya Kikristo ni majina ya tamaduni zilizoleta "Ukristo wa Ulaya" Afrika (nasema Ukristo wa Ulaya maana Ukristo ulikuwepo Afrika kabla ya kuja kwa Wamisionari). Kwahiyo walipokuja wakadanganya wazee wetu kuwa majina kama Matengo, Nyundo, Ossu, n.k. hayakubaliwi machoni pa Bwana! Kuna maeneo ambayo hadi leo hii kanisa katoliki linakataza watu kutumia majina ya asili. Waumini wanaambiwa, "Hayo ni majina ya kinyumbani!" Hivyo wanashauriwa kuchukua majina ya "watakatifu," ambao kawaida huwa ni wazungu!

Waafrika tunaweza kuwa masikini kiuchumi na tukawa nyuma kwa teknolojia ya kisasa lakini hatuwezi kuwa masikini wa fikra kiasi cha kushindwa kuwa na majina yanayotambulisha na kuenze tamaduni zetu.

Kwa ufupi, hakuna kitu kama "majina ya kidini" huku duniani. Majina ni ya kitamaduni. Ndio maana unaona kuwa Waarabu wakristo wana majina ya Kiarabu ingawa sio waislamu. Sababu ni kuwa wanachukua majina ya utamaduni wao bila kujali kuwa wao ni wakristo au waislamu.

Wamarekani weusi wanapenda sana majina ya Kiswahili. Wanashangaa kuona watu tumetoka Afrika tukiwa na majina ya kikoloni hadi leo, na tukipata watoto tunaendelea kuwapa majina hayo hayo.

Yapo baadhi ya majina ambayo yananifurahisha sana kwakuwa yametungwa kwa ubinifu mkubwa. Moja ya majina yanayonimaliza ni Kalamu Ya Salamu.
Majina mengine ambayo nimekumbana nayo ni kama Talib Kweli (mwanamuziki wa Rap), Amiri Baraka (mwandishi, mwanaharakati, na mshairi), Haki Madhubuti (mshairi), Maulana Karenga (mwanzilishi wa sikukuu ya Wamarekani Weusi yenye jina la Kiswahili, Kwanzaa na Mkurugenzi wa Idara ya Masomo ya Waafrika katika Chuo Kikuu cha California, Berkley) na mke wake Tiamoyo Karenga, Maisha Ongoza, Mapinduzi Leo, Rafiki Mtumishi, Malaika Jabali (mcheza sinema), Fani Adili, Harambee Afrika, Ujamaa Muhammad, Akili Mali, Sheria Haki, Mtoto Wa Afrika, n.k.

Sikukuu ya Kwanzaa ambayo husherehekewa mwezi wa kumi na mbili kwa siku saba inatumia maneno mengi ya Kiswahili. Kila siku, kwa mfano, kwa siku saba wanajamii na wanafamilia hukumbuka na kuenzi nguzo moja. Kwahiyo kuna “seven principles” ambazo wanaziita kwa Kiswahili nguzo saba. Nguzo zote saba ni za Kiswahili: ujamaa, ujima, kujichagulia, kuumba,nia, umoja, na imani.

Wakati wa kusheherekea Kwanzaa, watu husalimiana kwa Kiswahili, “Habari Gani?” Na kama siku hiyo watu wanaenzi nguzo ya ujamaa, basi mtu atajibu, “Nzuri, ujamaa.” Kama ni siku ya nia, watasema, "Nzuri, nia."

Alama zinazotumika katika sherehe hii nazo zimepewa majina ya Kiswahili: mazao, mkeka, kinara, mishumaa saba, mhindi, kikombe cha umoja, zawadi, na bendera. Kama unataka kujua zaidi juu ya Kwanzaa nenda hapa: http://www.officialkwanzaawebsite.org/

Maulana Karenga ni mwanzilishi pia wa falsafa ya Kiafrika yenye jina la Kiswahili: Kawaida.

Nilikuwa nazungumzia juu ya majina ya Kiswahili kumbe nimesharukia kwenye Kwanzaa. Lakini yote ni katika kusema kuwa Kiswahili sio lugha ya kudharau na kuchezea. Tuikuze na kuiheshimu. Tukiipoteza lugha hii tutapoteza na nafsi zetu. Kumbuka maneno ya Shaban Robert, “Titi la mama litamu ingawa la mbwa.

****Ukipeleka kiteuzi (mouse) juu ya sehemu zenye rangi ya njano hapo juu na kubonyeza utapata habari zaidi****

1 Maoni Yako:

At 8/06/2004 01:21:00 PM, Blogger Maka Patrick Mwasomola said...

Ni kweli baadhi yetu sisi waafrika tunapenda sana kutukuza majina ya kigeni kuliko ya kwetu.
Kwa mfano mimi nilikataliwa kubatizwa kule Turiani Morogoro mwaka fulani na padri wRoman Cathoric kwa kuwa eti jina langu ni Maka.Yeye alifikiri kuwa ni jina la Kiislamu kumbe ni jina la kilugha yaani Gwamaka na kifupi chake watu wananiita Maka.Kwa hiyo yule padri alikataa mimi nisibatizwe katika dhehebu la Roma akifiri kuwa jina langu ni la kiislamu.Hicho kitu kiliniumiza sana ijapokuwa nilikuwa kijana mdogo.Lakini baadaye nilikuja kungundua kuwa siyo kosa lake ni kuwa tu hakuelewa maana ninafikiri alifundishwa kuelewa hivyo.
Kutoka mwaka 1980 ninafikiri nikaja kubatizwa Moravian mwaka 1992.Simlaumu sana lakini sasa inatubidi tuelewed hivi vitu.Asante.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com