8/07/2004

Nilipotea kidogo

Toka jumatano sijaonekana. Lakini tuko pamoja. Nilikuwa nimebanwa katika hizi mbio za paka na panya za ughaibuni. Unajua kuwa maisha hapa tunasema polepole sio mwendo, harakaharaka ina baraka. Baraka tele. Nilikuwa mbio, mbio. Ulimi nje. Nahema juujuu. Unajua ikifika mwisho wa mwezi wenye kodi na bili zao wananyoosha mkono. Unapewa dola kwa mkono huu, jamaa wengine wanakuja kuzichukua kwa mkono mwingine: kodi ya nyumba, bili za simu, umeme, mtandao wa kompyuta, bima, takataka, shule ya mtoto, malipo ya yaya, bili ya vituo vya luninga vya kulipia, malipo ya kila mwezi ya vitu vilivyonunuliwa kwa mkopo; fedha za petroli, chakula, mavazi, muziki, vitabu, video; fedha za kwenda filamu...orodha inanitia hasira. Tuishie hapo. Uzuri mmoja hakuna michango ya harusi, ubatizo, ubarikio, vikao vya harusi, n.k.

Ningekuwa pale Tabata au Mbagala si ninakwenda kwa mwenye nyumba na kumwambia, "Mwezi huu mambo hayajanikalia sawasawa." Ukiongea na mwenye nyumba vizuri kinaweza kueleweka. Hapa ukichelewesha kodi siku moja unaanza kutozwa faini! Kama ni pale Msasani Mikoroshini unaweza kwenda kwenye duka la Mangi au banda la Mzee Hemedi kuchukua nazi, sukari, chumvi, mafuta, mchele, unga kwa mkopo.

Sasa hapa nimezungukwa na masupamaketi makubwa makubwa, ukiwaambia wakukopeshe wanaweza waite gari la wagonjwa lije likuchukue. Lazima utakuwa huna akili timamu.

Kwa ufupi nimerudi ndani ya nyumba toka kwenye pilikapilika katika "nji" hii ya Rais Kichaka ambaye huenda akawa ndiye Rais mbumbumbu katika Marais wote waliowahi kutawala Marekani. Na sio ajabu akawa ndio rais mbumbumbu namba moja duniani hivi sasa. Hadi alipochaguliwa kuwa Rais, Bwana Kichaka alikuwa hajawahi kusafiri nje ya Marekani. Hadi anakuwa Rais alikuwa hajui kuwa Brazili kuna watu weusi. Brazili ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya watu weusi duniani baada ya Nigeria. Mpaka hivi majuzi alikuwa akiitaja Afrika anasema, "Nchi ya Afrika," wakati Afrika ni bara! Amekiri mwenyewe kuwa hana tabia ya kujisomea vitabu. Sijui kama alishawahi kukaa chini na kusoma kitabu akakimaliza. Nadhani huwa anajisomea Biblia mara kwa mara maana eti anadai kuwa ameokoka. Jamani!

1 Maoni Yako:

At 8/08/2004 11:41:00 AM, Blogger Maka Patrick Mwasomola said...

Inashangaza,Mzee Bush ameokoka?Ameokoka katika misingi ipi?Kama kuna uokovu wa aina tofauti,tofauti.Basi kwa mantiki hiyo hata Bin Laden naye kwa misiongi ya imani yake yu ameokoka,pia ninafikiri hata Saddamu naye.Tofauti pengine ni misingi ya imani zao tu kwamba kila mtu anaona imani yake ndiyo bora au ya kweli kuliko ya mwingine.!

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com