7/16/2005

Nimekuwa najipumzisha...

Napumzika. Mwili na akili huwa vinahitaji kupumzika. Toka nirudi toka kwenye ule "mchezo wa kuigiza" wa wakuu wa makuhani wa ubepari (mkutano wa genge la wanaume nane, G8) sijaandika chochote hapa. Nimekuwa navuta pumzi, natafakuri, nanyoosha viungo, na kutembea milimani. Nadhani nitarudi rasmi kwenye blogu leo usiku au kesho. Au kesho kutwa. Nausikiliza mwili. Ukisema neno, miye natii. Nawe usiwe unasahau kupumzisha mwili na akili.

7/11/2005

Mahojiano BBC Kiswahili na BBC Network Africa

Ndio tumerudi mtaa wa Simba Mweupe, zilipo ofisi za Panos. Tayari tumemaliza mahojiano na kipindi cha BBC cha Go Digital. Nilikuwa na John Kamau. Pia tumefanya mahojiano mafupi kuhusu masuala ya Afrika na mkutano wa wakuu wa makuhani wa ubepari, yaani G8, na Mariam Omar wa idhaa ya Kiswahili ya BBC. Na kesho alfajiri saa kumi na moja na nusu (au ni kumi na moja kamili?...nitahakikisha) nitazungumzia masuala ya uandishi, blogu, na G8 katika kipindi cha BBC Network Africa. Kisha baada ya hapo nitaelekea uwanja wa ndege...chai sijui nitakunywa wapi. Mimi bila chai akili itaacha kufanya kazi! Kamau yeye ataongea na BBC Focus on Africa saa mbili asubuhi.

Hii ni London, jumatatu asubuhi

Baadhi yetu wanaondoka leo. Wengine, nikiwemo mimi, tunaondoka kesho. Nadhani niko tayari kuondoka. Bado jiji lina huzuni huzuni hivi. Siwezi kuficha kuwa asubuhi tulipopanda basi kuja hapa nilikuwa na hofui kidogo.

Dakika 20 zijazo mimi na John tutaondoka kwenda Bush House kwa ajili ya mahojiano ya kipindi cha BBC kiitwacho Go Digital. Ninapitia msururu wa barua pepe zilizojaa kashani.

7/09/2005

London

Tumewasili London. Kumekaa kihuzuni huzuni hivi. Ugaidi ni kitu kingine kabisa. Tumechoka, tumekwisha kabisa. Akili hata kufikiria ni vigumu. Kuna waliouliza makala za Padri Karugendo. Hizo mpaka nirudi kwa Joji.
Uhuru!

7/08/2005

Mchezo umekwishi kule Gleneagles

Ni saa tisa usiku. Nilikaa Gleneagles hadi saa sita usiku. Nilikuwa kati ya watu wa mwisho kuondoka maana nilijua nikija nyumbani nikiona kitanda nitalala, kama ambavyo nitafanya nikishamaliza kuandika hapa. Wakati naondoka kuelekea kwenye basi nilitazama kila upande bila kuamini kuwa sehemu iliyokuwa imejaa askari na watu wenye kamera, beji zinazoning'inia shingoni (kila mtu ilikuwa lazima awe na beji), makaratasi, kalamu, kompyuta za mapajani, wahudumu, n.k. ghafla imekuwa mahame. Askari walikuwa wameyeyuka. Wanaharakati wametoweka. Waandishi wamebaki wachache, nao ndio wanaondoka. Helikopta hazipo tena angani.
Natembea polepole na begi langu nikijiuliza, "hivi nilikuja kufanya nini hapa?"
Nilijiona kama mtu anayetoka ndani ya chumba cha maigizo akirudi kwenye dunia halisi. Kuna mwanafalsafa mmoja, sikumbuki ni nani, alisema kuwa dunia hivi sasa imekuwa kitu alichokiita, "media spectacle." Yaani maisha ni kama vile kioja kwa ajili ya vyombo vya uongo (vyombo vya habari). Na hivyo ndivyo ilivyokuwa pale Gleneagles. Mchezo wa kuigiza unaofanyika kila mwaka kwa jina la G8 Summit. Mchezo huu utaendelea mwaka ujao kule Urusi.
Nimepitia vyombo kadhaa vya habari kuona maoni ya watu juu ya tamko la makuhani wakuu wa ubepari la kuongeza "msaada" kwa nchi za Afrika. Wako wanaounga mkono na wanaopinga. Watu kama akina Bono na Geldof wakiunga mkono nitawaelewa maana wanataka kutudanganya kuwa kampeni zao kama Live 8 ndio zimefanya wezi hawa wa maliasili za Afrika (wakishirikiana na Waafrika) wakaamua "kuisaidia" Afrika. Akina Bono wanataka kutuambia kuwa akina Kichaka wameguswa na kauli ya walimwengu! Hivi unadhani watu bilioni mbili wakisema jambo, na mabosi watatu wa kampuni la kipebari kama Halliburton wakisema jambo, Joji Kichaka atasikiliza kina nani? Watu bilioni mbili? Thubutu!
Nikiwa ndani ya basi kabla ya kusinzia nilijichekea mwenyewe: baada ya tamko la "kuisaidia" Afrika kwa dola bilioni 50 (sijui nyumba ngapi zitajengwa ufukweni mwa bahari, na akaunti ngapi zitafunguliwa ughaibuni, na suti ngapi na vito vya thamani vitanunuliwa na watawala wa Afrika kwa hela hii) kila mwandishi wa kizungu alikuwa akiona mtu mweusi anataka kumhoji. Nilitamani ningevaa bango kusema, "Sitaki kuhojiwa!" Niliona kuwa hata wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari ya Blair, waandishi weusi walipewa nafasi ya juu kidogo tofauti na ilivyo kawaida katika mikutano mikubwa kama hii. Ghfala ngozi nyeusi ilionekana kama vile sijui ni kitu gani. Nyani wamejua kuvaa nguo?
Nililala sehemu kubwa ya safari ya dakika tisini toka Gleneagles hadi Edinburgh. Kisha teksi hadi Royal Circus namba moja. Ndipo nipo sasa na ninakaribia kwenda kulala.
Kesho asubuhi tunarudi London, jiji nilichukialo kwa mbio zake za kuwahi basi, treni, msongomano wa watu, na habari hizi za ugaidi zimenifanya nisiwe na raha ya kurudi pale.

Pazia limefungwa. Mchezo umeisha. Washeni taa. Twendeni nyumbani.

wakulima wa ulaya na ruzuku...

Wanaharakati wamekuwa wakitaka nchi za Ulaya na Marekani ziache kutoa ruzuku kwa wakulima wake. Je wakulima wenyewe wanasemaje? Niliongea na viongozi wa chama cha wakulima wa Uskoti.

Maamuzi ya mwisho makuhani wa ubepari...

Wale wakuu wa makuhani wa nchi zinazoongoza kwa ukandamizaji wametoa tamko. Wako jamaa ambao wameipinga vikali. Wasome hapa, hapa, na hapa.

Yaliyomkumba rais huyu alipotaka kuja Gleneagles

Sijui nicheke au nisikitike. Safari ndefu toka Afrika hadi London, njiani kuelekea Gleneagles, lakini...

Ungekutana na wakuu wa makuhani wa nchi nane kwa kahawa...

Ungewaambia nini? Kusema kweli sijui ningewaambia kitu gani. Ila Waafrika hawa niliohojiana nao wanafahama watakachowaambia. Nadhani mimi ningeweka vidonge kwenye chai ili walale kisha niwatie pingu!

Bono muda mfupi...

Sauti kupitia spika katika hema hili la waandishi wa habari inasema kuwa Bono na Geldoff watakuwa na mkutano na waandishi wa habari muda mfupi toka sasa. Sijui niende? Blair kamaliza mkutano wake. Sikwenda. Nilienda kula kisha nikaja kumalizia habari ninazoandika. Naona kama vile ni usumbufu kutembea hadi kwenye mahema ya mikutano ya waandishi wa habari kusikiliza wapiga hadithi wakati kuna luninga kila kona.

NANI ATAIELEZA AFRIKA?

Makala yangu kwenye gazeti la Metro la Uingereza inaelezea siku ya kwanza nilipotua mguu Gleneagles wanapokutana makuhani wakuu wa ubepari. Isome hapa.

Nina masikitiko makubwa maana kuna uwezekano kuwa marais wa Afrika hawataongea na waandishi wa habari. Wamekuja, wamekunywa mvinyo na makuhani wa ubepari na kupiga picha za pamoja, kisha kudanganyana kidogo halafu wanarudi Afrika. Nadhani watapitia kwanza kwenye mabenki kutazama akaunti zao, watacheki afya, "shopping" kidogo kisha warudi Afrika.

Wanablogu wa Kiislamu na mabomu London

Kwenye blogu ya Global Voices kuna taarifa kuhusu wanablogu wa kiislamu wakizungumzia mabomu London.
Leo ndio siku ya mwisho ya mkutano wa makuhani wakuu wa ubepari. Ukitazama maandalizi, muda, na fedha zilizotumika kwenye mkutano huu huwezi kuamini kwanini wanakutana kwa siku chache hivyo. Muda si mrefu tutaondoka. Wote hapa tuna hamu ya kukutana na marais toka Afrika walioalikwa kwenye makombo. Meza kuu ina wanaume nane. Jana wala makombo walikuwa ni viongozi wa nchi za Brazili, India, n.k.

7/07/2005

Kumbe mtuhumiwa alikuwa na blogu

Jamaa anayetuhumiwa kuteka watoto wawili alikuwa ana blogu. Blogu yake aliita "msumari wa tano" kutokana na hadithi kuwa msumari wa tano ulikuwa ndio umalize maisha ya Yesu, ila ulifichwa askari wa Kirumi wasiuone. Hii ndio blogu yake.

LEO GLENEAGLES

Leo nimekuwa hapa Gleneagles toka asubuhi, usisahau kuwa chakula ni cha bure!! Nimekuwa nikizunguka huku na kule kutafuta Waafrika toka vyama visivyo vya kiserikali na pia waandishi wa habari toka Afrika. Nimemuona mwandishi mmoja toka Tanzania, Ayoub Mzee, ambaye anafanya kazi Sky Channel hapa Uingereza.

Kuna wanaharakati wachache sana toka vyama visivyo vya kiserikali hapa Gleneagles. Jamaa fulani kaniambia kuwa wengi wako Edinburgh, hawakutaka kuja hapa. Eti wanafurahia maisha ya Uskoto. Hapa nimeona wanaharakati wanne tu. Nimewahoji tayari. Habari hiyo nitaiwekea kiungo hapa ikishatoka. Pia nimehoji baadhi ya waandishi wa habari wa Afrika. Nitamaliza kesho. Kati ya maswali ambayo nimekuwa nikiwauliza wanaharakati ni hili: ukipata nafasi ya kunywa kahawa na akina Joji Kichaka utawaambia nini?

Usiniulize mimi swali hili maana sitakubali kutumia muda wangu kunywa chai na Joji. Chai haitashuka.

Kesho ndio ilikuwa tuondoke kurudi London ambako kama mnavyojua kumetoka janga kubwa. Ila kwasababu viongozi wa Afrika watafaongea na waandishi jioni, imebidi tukae hapa hadi jumamosi. Je nikikapa nafasi ya kumuuliza Mkapa swali nimuulize nini?

SHAMBULIO LA BOMU. AFRIKA, NA G8

Wakati tukijiandaa kuja hapa Gleneagles wanapokutana wakuu wa makuhani wa ubepari, tulipata taarifa za shambulio la kigaidi huko London. Muda mfupi uliopita waziri mkuu wa Uingereza, Tony Balir, ameondoka ghalfa toka kwenye mkutano unaoendelea kwenda London. Tunaambiwa kuwa atarudi.

Swali ambalo limekuwa likiulizwa na wengi baada ya shambulio hili ni jinsi ambavyo mkutano huu una hatari ya kupeleka macho kwenye suala la ugaidi zaidi ya suala la Afrika. Mwandishi mmoja kaniambia kuwa viongozi wengi wanapoongea na vyombo vya habari hawazungumzii, kwa mfano, suala la mazingira ambalo liko mezani bali ugaidi. Kwa watu wengi kuna masikitiko kuwa Afrika itawekwa kando na ugaidi kuchukua mstari wa mbele. Mimi binafsi sioni kwanini watu wanasikitika. Nadhani kuna watu wanachukulia kuwa makuhani hawa ni wakombozi wa Afrika wakati ambapo wanachofanya ni kunadi bara letu kwa makampuni yanayomilikiwa na marafiki na jamaa zao. Na makampuni mengi wanamiliki wao wenyewe kwa kupitia hisa.

Kuna utani fulani unaendelea hapa. Waandishi wakitaka kwenda kula au bar ambako kila kitu ni bure wanasema, "Ngoja nikafanye umasikini kuwa historia." Wanasema hivi kukejeli kampeni iliyokuwa ikiungwa mkono na serikali ya hapa iitwayo MAKE POVERTY HISTORY.


7/06/2005

Nimetia mguu Gleneagles waliko makuhani wa ubepari

Tumerudi nyumbani toka Gleneagles, mwendo wa kama saa moja na nusu. Mpango uliopo hapa ni kuwa basi linaondoka toka hoteli ya Hilton? Sheraton? (sikumbuki...zote zinafanana) kupeleka waandishi wa habari. Basi tumefika pale tukashuka kwenye gari kisha tukapita sehemu ya kusachiwa, "Weka begi hapa, toa vitu mfukoni, njoo hapa, nyanyua mikono juu, onyesha soli ya viatu vyako..." Hizi ndio amri unazokutana nazo. Lakini kwa ujumla askari ambao nimekutana nao hapa toka nije ni wastaarabu sana. Baada ya kusachiwa tuliingia kwenye basi jingine dogo ambalo lilitupeleka kwenye kituo cha waandishi wa habari. Pale tukakabidhiwa begi. Kila mwandishi anapewa begi hili ambalo ndani yake lina biskuti, chokoleti, magazeti, na wiski aina ya Black Label ambayo imevundikwa kwa miaka 12. Wakati wanatupa nilitaniwa wenzangu, "Wanatuhonga nini?"
Ukiona kiasi cha fedha zilizotumika kwa mkutano huu ambao makuhani wakuu wa ubepari wanakutana kwa masaa sijui mawili kwa siku huwezi kuamini. Kwanza nilipokuwa ndani ya basi baada ya kulala, kuamka, kulala, na kuamka tena, nilijiuliza: Kwanini viongozi waliochaguliwa na watu waje kujificha mbali hivi? Eneo lote limezungushwa waya, juu kuna helikopta zinazunguka, chini askari wamejaa kila upande...kweli hawa ndio makuhani wakuu.
Basi tukaenda kwenye tafrija ya waandishi wa habari ambapo kulikuwa na maakuli ya nguvu ya Kiskoti, mvinyo, wiski, na vitu vingine ambavyo majina yake sijui na sikuthubutu kuuliza nisionekane kuwa nimeshuka mjini leo! Hivi majuzi Rais wa Ufaransa, Chirac, alidai kuwa mapishi ya Uskoti ndio mabaya zaidi Ulaya baada ya mapishi ya Ufini. Waingereza wamechukia na kudai kuwa, "afadhali yetu sisi hatuli konokono na miguu ya chura." Jamaa ambaye anatuandalia chai asubuhi ni Mfaransa, leo nilimuuliza kama amewahi kula miguu ya chura akacheka karibu akaukie.
Wakati tunajichana tuliambiwa mambo kadhaa kuhusu nchi ya Uskoto: simu, luninga, dawa ya penisilini, vyote viligunduliwa hapa. Mfumo wa kileo wa vyuo vikuu na vitivo ulianzia hapa. Uskoti inaongoza kwa utoaji wa machapisho ya kitaaluma duniani (ukilinganisha machapisho na idadi ya wananchi wake).
Wakati tunajichana tulipitiwa na mkutano wa waandishi wa habari na Bono na kampuni yake. Maura, mwandishi tuliye naye hapa toka Msumbiji, amesikitika sana kutomuona Bono. Anapenda sana miziki ya kundi la Bono la U2. Msome Maura akizungumzia muziki wa rapu kule Msumbiji.
Mapema leo kulikuwa na mapambano kati ya polisi na waandamanaji. Kulikuwa pia na maandamano yaliyopewa kibali yaliyoongozwa na akina Bono na Geldof. Imeshangaza wengi kuona kuwa serikali ya Uingereza inavyounga mkono akina Bono na pia waandaaji wa Make Poverty History. Unaweza kuamini kuwa waziri wa mambo ya misaada ya kimataifa wa Uingereza, Hilary Ben, alikuwa kwenye maandamano ambayo wengi waliamini kuwa yalikuwa yakipinga ubepari. Maandamano ya kuipinga serikali yanahudhuriwa na mtumishi wa hiyo serikali. Watu sasa wameanza kusema kuwa hawa wakuu wa makuhani wametuzidi kete maana hata maandamano wanaandaa wao kwa kutumia watu wengine.
Jioni saa kumi nilikuwa kwenye mjadala unaohusu uwezo wa maandamano kubadili jamii kwenye kipindi cha Simon Mayo Radio Five Live. Muda sio mrefu uliopita, Joel, ambaye amewasili leo toka Uganda alifanya mahojiano na radio open source. Mahojiano hayo hayakumalizika maana mawasiliano yalikatika.

Sasa nitaandika kifupi juu ya siku ya kwanza kufika pale Gleaneagles kwa ajili ya blogu ya Panos, kisha nikalale maana kesho asubuhi na mapema tunakwenda kule waliko wezi wakuu wahedi! Ratiba inaonyesha kuwa msafara wa rais wa Tanzania utawasili kesho. Nimepewa namba ya kupiga ili kujua kama Mkapa atapatikana kwa ajili ya mahojiano.

Nimewasili Gleneagles

Baada ya mwendo kama wa saa moja na nusu, nimewasili Gleneagles. Hivi sasa tunakunywa mvinyo na kula vyakula vya Kiskoti. ">

Sikiliza Mahojiano BBC saa tisa hadi kumi saa za Uingerzeza

Ninaondoka kwenda kwenye mjadala kwenye kipindi cha redio cha BBC kiitwacho Simon Mayo Show. Mjadala unahusu suala la maandamano na kama huwa yanaleta mabadiliko yoyote. Unaweza kusikiliza kwenye redio au mtandaoni.

7/05/2005

Kuondoa umasikini ni kuondoa ubepari

Kuna harakati za wabunge hawa toka nchi mbalimbali duniani za kutaka Benki ya Wezi (benki ya dunia) na shirika ambalo bango moja kwenye maandamano ya jumamosi lilisema kuwa kirefu chake ni International Mother F**** (IMF) yaendeshwe kidemokrasia. Hivi sasa kura za wanachama wa vyombo hivi vya kibaguzi zinategemea uwezo wa kiuchumi wa nchi. Kwahiyo utaoana kuwa Marekani ikitaka kupitisha au kupinga jambo lolote kwenye vyombo hivi watafanikiwa bila kipingamizi chochote. Na jamaa hawa ndio wanasema kuwa wanataka kuifundisha dunia demokrasia.
George Monbiot alisema jambo moja zuri sana jana. Alisema kuwa akina Bono na Geldoff wanashindwa kujua jambo moja muhimu sana: hakuna uwezekano wa kubadili vyombo hivi vya njururu. Vyombo hivi vimeundwa ili kuendeleza matakwa ya nchi tajiri ambazo zinategemea sana umasikini wa nchi za Kusini. Umasikini wa nchi zetu ndio njia pekee ya kuwafanya wao kuwa matajiri. Usitegemee, kwa mfano, Waswisi wataipa Ghana msaada wa kujenga viwanda vya kutengeneza chocolate. Waswisi wanataka kununua cocoa toka Ghana kwa ajili ya viwanda vyao, Ghana ikiwa na uwezo wa kutengeneza chocholate wenye viwanda Uswisi unataka wale polisi?
Monbiot anasema kuwa hakuna njia yoyote ya kuondoa umasikini duniani bila kuhoji, kukabiliana, na kuuondoa mfumo wa ubepari unaowapa viongozi wachache na makampuni ya maswahiba wao au makampuni yenye hisa zao uwezo wa kuamua jambo lolote kwa niaba ya dunia nzima.
Tazama sura halisi ya mfumo huu wa ubepari: makampuni ya Makidonadi na Walt Disney yanatumia fedha za matangazo kwa mwaka mzima ambazo ni zaidi ya bajeti ya elimu na afya ya nchi 18 duniani.

WANABLOGU WAPYA WA KISWAHILI

Pamoja na kazi niliyonayo ya kuandika habari hii ya City Water kwa ajili ya tovuti ya Panos, siwezi kuacha kuwatangaza wanablogu hawa wapya wa Kiswahili. Yuko huyu mwandishi wa habari, ndugu Ngurumo, na bwana Sagati, ambaye sifahamu anafanya nini.

Wakulima wa Uskoti, eco-village, n.k.

Leo waandishi wote toka Afrika na wafanyakazi wa Panos London tuna furaha maana tumepata vitambulisho vya kutuwezesha kuingia unakofanyika mkutano wa wezi wakuu duniani. Kwa maana hiyo huenda nikagongana na Joji Kichaka akiwa ametoka chooni. Sijui nitamwambia nini. Nadhani nitabadili njia. Kipenzi chao mkuu, rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa (au Makapa kama jinsi wazungu wanavyotamka) naye atakuwepo. Naye nikukutana naye sijui nimwambie nini. Najua cha kumwambia. Nitamkaripia (ndio, rais ni mtumishi wetu) kisha nitamwamuru arudi Tanzania haraka sana aachane na hawa wezi watamlostisha!
Asubuhi leo tumekutana na viongozi wa chama cha wakulima wa Uskoti, NFU-Scotland. Mazungumzo yetu nao yalihusu ruzuku kwa wakulima wa Ulaya na Marekani na masahibu ya wakulima wa Afrika. Hawa jamaa wanasema kuwa ni kosa kubwa sana kwa wanaharakati kudai kuwa nchi za Ulaya ziache kutoa ruzuku kwa wakulima wake. Wanasema kuwa watu wengi hudhani kuwa wakulima wote Ulaya ni matajiri wakati ambapo wanachama wao wengi wana mashamba ya kawaida tu tofauti na wakulima kama wa Marekani. Wakatuambia kuwa kuna hatari ya kuwafanya wakulima duniani waanze kugombana wao kwa wao wakati ambao wana maslahi yanayofanana.
"Sisi hatuna sababu ya kugombana na wakulima wa Afrika. Ila vyombo vya habari vikiandika kuhusu wakulima vinatoa picha ambayo inaweza kuleta hali ya kuchukiana. Sisi sote ni wakulima." Mkurugenzi wa chama hicho, Andy Robertson alituambia.
Kwa maana hiyo, wakati baadhi ya wanaharakati wanadai kuwa nchi za Ulaya zisitoe ruzuku, wakulima hapa Uskoti wanasema kuwa ruzuku itolewa kwa wakulima dunia nzima. Ila wanataka ruzuku inayotolewa isiwe ni ile inayoharibu bei za bidhaa za mashambani kwenye soko la dunia.
Tulipowauliza kuwa hawaoni kuwa kitendo cha serikali yao kuwapa ruzuku kinawapa uwezo zaidi wa kushindana na wakulima wa Afrika ambao wana uwezo kidogo, walidai kuwa kwa kiasi kikubwa washindani wao sio wakulima wa Afrika. Sababu ni kuwa wao hawalimi pamba, kahawa, chai, tumbaku, n.k. Wanasema mazao wanayolima sio mazao ya wakulima wa Afrika. Kwa ufupi, wakulima wa Uskoti wanachukia sana wanaposikia wanaharakati wakitaka serikali ya nchi hii kuacha kutoa ruzuku.
Mchana wa leo tulikwenda kwenye kijiji kiitwacho Eco-Village. Ni umbali kama wa saa moja hivi toka hapa. Kijiji hicho ambacho ni cha muda kiko chini ya watu wanaotaka kujenga jamii zenye kujali mazingira na demokrasia ya moja kwa moja. Tulipofika hapo tulikutana na mtangazaji wa BBC ambaye pia ni mwanablogu, Paul Mason, akatuambia kuwa waandishi hawaruhusiwi kuingia ndani ya kambi. Tunachoweza kufanya, alituambia, ni kuongea na wahusika nje ya kambi hiyo. Basi tukaamua kuuza maneno. Nilikuwa mimi, Machrine toka Uganda na Dr. Banda wa Panos Kusini mwa Afrika. Tukasema tumetoka Afrika, sisi sio sawa na waandishi wa magazeti makubwa hapa Uingereza. Nikaingiza hii: nimetoka Tanzania ambapo tulikuwa tuna siasa ya ujamaa inayofanana na itikadi ya kijiji chao.
Wakadai wamekubaliana kuwa hakuna waandishi maana waaandishi huwa wanawaandika vibaya. Basi mmoja wetu akauliza, "Unaweza kutuitia kiongozi tuongee naye? Nani mwenye kauli ya mwisho?" Swali hili tuliuliza maana hatukuwa tukijua kwa undani itikadi yao. Basi dada aliyekuwa akiongea nasi akashtuka na kusema, "Hapa hatuna mtu anayeitwa kiongozi, hatuna madaraja au matabaka. Hatuna mtu mmoja anayeamua kwa ajili ya wengine. Ndio maana tunapinga mfumo wa demokrasia ya uwakilishi. Maamuzi yetu tunafanya kwa makubaliano."
Baada ya "kuwalilia" sana waliamua kujadiliana na baada ya muda wakatuambia tumeruhusiwa kuinga kijijini ila lazima tuache rekoda, kamera, kalamu, kila kitu nje ya kijiji. Basi hapo tukaingia ndani. Ndani kuna nini? Rudi tena nitaendelea kwani nina kazi ya kumaliza kabla ya kulala na kesho asubuhi kwenye Gleaneagles kunakifanyika mkutano wa "kuigawa" Afrika kama alivyofanya Bismarck. Kazi ninayofanya ni kuandika habari kuhusu kampuni ya City Water iliyokuwa imepewa jukumu la kubinafisha maji jijini Dasalama. Toka tufike hapa nimekuwa nikifuatilia suala hili ikiwa ni pamoja na kuonga na Cliff Stone, mmoja wa wakurugenzio waliofukuzwa nchini.
Tafadhali tazama wanablogu wa Afrika wanasema nini juu ya tamasha la muziki la wazungu la "kutetea" Afrika la Live 8. Msome John Kamau akiblogu kwenye BBC Online. Nisome kwenye gazeti la Metro la hapa kwa Blair. Kisha fuatilia mjadala huu hapo kesho.

7/04/2005

Blogu mbalimbali za G8

Unaweza pia kufuatilia yanayotokea hapa kupigia blogu hizi maalum kwa ajili ya wezi nane, G8:
Gazeti la the Guardian, blogu ya Paul Mason wa BBC Newsni8t, blogu ya Open Democracy , blogu ya gazeti la Red Pepper , IndyMedia nchini Uskoti na Technorati.
Nasikia kuwa katika viongozi waliokaribishwa kuwa watazamaji kwenye mkutano wa viongozi waliojichagua wenyewe kuwa ndio wapitisha sera kuu za uchumi wa dunia hii ni rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa. Nitamtafuta nipige naye picha niweke ukutani ili nije kuwaonyesha vitukuu wangu wakati nikiwapa historia ya jinsi bara letu lilivyochukuliwa na makampuni toka nje.
Wakati wa maandamano makubwa ya Make Poverty History nilifanya nilihojiana na Waafrika waliotoka Afrika kuja Uskoti kuandamana. Kuna makala niliyoandika ikiuliza kijiji alichozaliwa Tony Blair huko Afrika.

BLOGU MPYA YA MWANDISHI WA HABARI WA KENYA

Mwandishi wa habari wa Sunday Standard la Kenya, John Kamau, ameingia rasmi kwenye ulimwengu wa blogu. Ni furaha ilioje kuona mwandishi wa habari wa Kenya anafungua njia kwa waandishi wengine nchini humo. Mtembelee Kamau hapa. Kamau hivi sasa yuko hapa Edinburgh.

Monbiot: Bara Zima La Afrika Litakuwa Mali ya Makampuni

Leo mji ulisimama. Maanakisti walikuwa wakifanya vitu vyao. Toka asubuhi hadi usiku saa mbili barabara kuu hapa Edinburgh, Princes, ilikuwa imefungwa. Askari wa kuzuia fujo walikuwa wametanda kila mahali, helikopta zikizunguka angani. Waandamanaji wenye msimamo mkali na itikadi inayopinga aina yoyote ya utawala walikuwa wakipimana na polisi. Polisi na waandamanaji hawa walitazamana siku nzima. Polisi wakiwa wamebeba ngao na vikopo vya gesi walizuia njia, maanakisti wakasimama barabarani hapo wakipiga ngoma, filimbi, wakiimba, na kucheza. Nilipopita mitaa hiyo kwenye saa kumi na moja jioni na mwandiki toka Kenya, John Kamau, tulijiuliza kama maandamano hayo yalikuwa yakifanyika Kenya au Tanzania ni kitu gani kingetokea? Tulisema, kwa utani, kuwa Waingereza wangetuma ndege ikachukue Askari wa Kuleta Fujo (wao hujiita askari wa kuzuia fujo) toka Kenya na Tanzania ili wawaonyeshe jinsi ya kuwashughulikia waandamanaji.
"Hivi unadhani askari wa Bongo au Kenya wangeweza kusimama wakitazamana na waandamanaji siku nzima?," nilimuuliza Kamau.
"We, askari kule nyumbani wana muda wa kupoteza? Saa hizi watu wangekuwa wanapelekea ndugu zao chakula cha jioni hospitali na wengine wakitafauta namna ya kuwatoa ndugu zao vituo vya polisi." Alinijibu. Mwandishi toka Sierra Leone Salamatu Turay amechukua picha hizi toka kwenye maandamano hayo. Mwandishi wa BBC Paul Mason naye ana picha toka katika maandamano hayo.
Maandamano haya yalikuwa yameandaliwa na jamaa ambao wamekuja hapa Uskoti kuwazuia wezi nane wanaotaka kukutana kuzungumzia jinsi ya kuifanya dunia kuwa shamba la mtu binafasi.

Leo tumekutana na kufanya mahojiano na mwanasafu wa gazeti la the Guardian George Monbiot. Monbiot amewahi kufanya kazi nchini Tanzania na Kenya. Moja ya mambo aliyokuwa anazungumzia leo ni suala la mbinu za viongozi wa nchi nane kutaka kubinafsisha bara zima la Afrika. Anasema kuwa tatizo moja la kampeni kama Make Poverty History na Live 8 ni kuwa kampeni hizi hazitishii madaraka na maslahi ya mfumo wa ubepari. "Watu wanadhani kuwa unaweza kuondona umasikini bila kuondoa mfumo wa soko huria." Monbiot anaamini kuwa mfumo wa soko huria ni moja ya vyanzo vya umasikini duniani. Anasema kuwa lazima tuanze kuelewa ubaya wa mfumo huu kwa kutazama jinsi ambavyo viongozi wa nchi nane tu duniani wana uwezo wa kutoa maamuzi juu ya wananchi wote duniani. Nchi hizi nane ndio pia zenye nguvu za kupitisha maamuzi yao kwenye vyombo kama Benki ya Mabepari (benki ya dunia), Shirika la Fedha Duniani, Umoja wa Mataifa, n.k.

Monbiot anasema kuwa wanachofanya viongozi wa nchi nane zinazoongoza kwa wizi duniani ni kutoa maamuzi yanayoonekana kama vile nia yake ni kusaidia watu masikini, vyombo vya habari vinaingia kwenye mtego, na watu kama Bob Geldoff na Bono wanashangilia kwa kunywa mvinyo na viongozi hao. Viongozi wa Afrika, alituambia, wanachofanya hivi sasa ni kukubali lolote lile ambao wanaambiwa na viongozi wa nchi za Magharibi. "Wanampenda sana rais wako Benjamin Mkapa." Aliniambia huku akicheka. Nilimwambia kuwa nikiona kiongozi anapendwa na kukumbatiwa na mtu kama Kichaka au Blair, ninakuwa na mashaka sana na kiongozi huyo. Kiongozi wanayempenda ni yule ambaye anawasaidia katika jitihada zao za kuliweka bara la Afrika katika mikono ya makampuni ya marafiki zao.

****************************************************************************

Mwandishi toka Sierra Leone, Salamatu Turay, ambaye tuko naye hapa Edinburgh ameandika makala kwenye gazeti la hapa Uingereza juu ya maandamano ya kwanza ya amani aliyohudhuria maishani mwake. Gazeti hili kila siku litakuwa habari tutakazokuwa tukiandika kwa mtazamo wa Afrika.

John Kamau toka Kenya
ameandika makala nzuri sana kwenye gazeti la The Guardian.

7/03/2005

Mahojiano na Waafrika walioandamana Edinburgh

Katika maandamano yaliyofanyika jana kwa jina la Make Poverty History, kazi kubwa niliyofanya ilikuwa ni kuzunguka huko na huko, kusukumana na kusukumwa, nikitafuta waliko waandamanaji toka Afrika. Kuna jambo ambalo siwezi kuelezea vizuri, nikiona mtu mweusi ambaye katokea Afrika lazima nitamtambua. Hata kama ameishi Ughaibuni kwa miaka nenda rudi, nitajua tu huyu ni Mmatumbi au Mmanyema!
Mahojiano hayo nimeandika kwa ajili ya tovuti maalum ya masuala ya G8 ya Taasisi ya Panos. Kwanza kuna mahojiano na wale waliosafiri toka barani Afrika kwa ajili ya kuandamana, kisha kuna wale ambao wameloea huku Ughaibuni.

Nimetoka kuwasikiliza jamaa wa Yes Men

Toka asubuhi tulikuwa kwenye mkutano mbadala wa G8. Tumewasikiliza jamaa wengi kama Samir Amin, Walden Bello, Trevor Ngwane (toka Afrika Kusini). Toka asubuhi ilikuwa ni kusikiliza, kuandika, kupiga makofi, na mbinja. Pia tumeweza kuhojiana na mama mmoja toka World Development Movement juu ya sakata la ubinafsishaji maji katika jiji la Dar Es Salaam. Mama huyu amekuwa akilifuatilia suala hilo kwa muda.

Lakini yote nadhani tukio kuu kwangu leo ni kukutana na kuwasikiliza jamaa wa Yes men. Jamaa hawa ambao hujifanya kuwa ni wawakilishi wa mashirika makubwa kama WTO, Benki ya Dunia, n.k. hualikwa kwenye mikutano na watu wanaoamini uongo wao ambao kwao ni aina ya harakati. Walituonyesha filamu mbalimbali za matukio ambayo wameshiriki bila kujulikana kuwa wao ni jamaa tu wasio na uhusiano wa mashirika wanayowakilisha. Wamewahi kuhojiwa na BBC, CNBC (ya Marekani) bila vituo hivi vya luninga kujua kuwa walikuwa wanahoji watu ambao sio. Watembelee hapa nyumbani kwao.

Blogu na siasa Tanzania

Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimeanzisha blogu kwa ajili ya viongozi wake wa kitaifa, nadhani na baadaye itakuwa kwa wanachama wake. Nitakuwa nafuatilia kwa karibu matumizi ya blogu katika siasa hasa kipindi cha uchaguzi.

Hapa Edinburgh ndio tumeamka na tunakaribia kunywa chaia, mpishi ananiambia kuwa chai ya leo inaitwa "full Scottish breakfast." Baada ya hapo tutaingia mitaani. Tafadhali usisahau kutembelea blogu mpya ya Panos ambayo inaendeshwa na waandishi toka Afrika.

7/02/2005

Polisi Edinburgh

Pamoja na ukweli kuwa polisi walikuwa wamejaa kila kona wakati wa maandamano, polisi hawa hawakuwa kama askari wa Tanzania ambao wana kazi kubwa mbili: kunyanyasa wananchi au kula rushwa. Niliwaendea polisi mara tatu kutaka msaada: kuuliza njia, kutafuta choo, na mgahawa. Askari waliongea nami kwa upole kama vile mimi ni ndugu yao. Amani iliyotawala maandamano hayo ilitokana na sababu nyingi, mojawapo ni kitendo cha polisi kuwa walinzi kuhakikisha watu wanaandamana vyema. Nchi nyingi Afrika (hata nchi za Magharibi) ukiwa uaandamana, ukiona polisi unajua kuwa utaona cha mtema kuni siku hiyo.

Katika mambo yaliyoniingia sana wakati wa maandamano ni vikundi vya ngoma. Sikuona kundi hata moja linalopiga ngoma kama wanajifunza. Makundi yote yalikuwa kama vile yako mashindanoni. Acha tu, hadi hivi sasa nasikia milio ya ngoma kichwani. Ngoma zilikung'utwa sio mchezo. Kingine kilichoambatana na ngoma ni filimbi.

Hivi sasa Stevie Wonder yuko jukwaani katika tamasha la Live 8.

Baada ya kutumia muda mwingi kuhojiana na waafrika waliokuwa wakiandamana, nilikwenda kwenye mgahawa mmoja kujipatia kitu cha kuingiza mdomoni maana nilikuwa karibu nianguke kwa njaa. Utamu wa kuwa katikati ya ngoma, nyimbo, dansi, filimbi, mabango, kelele, n.k. ulinifanya sikujua kuwa karibu "nife" njaa. Wakati natoka kwenye mgahawa nilishtuka kuona watu wote wanaoandamana wamesimama na kukaa kimya. dakika chache zilizopita mtaa mzima ulikuwa umejaa kelele, lakini sasa ghafla kimya. Kulikoni? Mara wakati najiuliza watu wote wakapiga mayowe, makofi, na mbinja kwa ghafla. Baadaye nakuja kujua kuwa ilipofika saa tisa kamili kila mtu alitakiwa kukaa kimya kwa dakika moja.
Nilikutana na jamaa wa kundi la Revolution, ambalo ni tawi la vijana la chama cha Socialist Workers Party. Wakati maandamano yalikuwa na ujumbe kuwa Make Poverty History (Fanya Umasikini Uwe Historia), wao walikuwa wakisema: Make Capitalism History. Niliongea nao kwa muda. Waliniambia kuwa mpango mzima wa Make Poverty History haufai maana nia yake ni kushawishi viongozi wa nchi za kibepari walete mabadiliko wakati ambapo dawa ya umasikini kuuondoa kabisa mfumo wa kibepari. Wanasema kuwa ubepari unahitaji umasikini kwahiyo huwezi kutumia mfumo wa ubepari kuondoa umasikini wakati ambao msingi wa mfumo huo ni kuwepo kwa tabaka la wanaonyonya na wanaonyonywa.

Kwahiyo suluhisho ni nini? Niliwauliza. Jibu lao ni kuwa serikali za kibepari zinapaswa kupinduliwa na mfumo mzima wa uchumu kujengwa upya. Hakuna kupoteza muda kujadiliana na manepari, waondoe madarakani kwa njia yoyote ile.

Kwa taarifa yako: gharama ya ulinzi wa washiriki wa mkutano wa G8 na eneo lenyewe ni kubwa zaidi ya pato la mwaka la nchi kama Malawi!

Tazama picha hapa za maandamano.

Mtanzania aliyekuja Edinburgh

Asubuhi leo niliondoka na waandishi Machrine na Maura kwenda katika kanisa la Uskochi pembeni na jumbe la makumbusho hapa Edinburgh. Kulikuwa na mkutano kuhusu wakulima na mabadiliko ya hali ya hewa. Katika mkutano huo Davinder Sharma wa Forum for Biotechnology and Food Security (India) alisema kuwa wakati watu zaidi ya 20,000 wanakufa kwa njaa nchini India, nchi hiyo inazalisha kwa mwaka chakula cha akiba ambacho ukikiweka kwenya magunia ya kuyapanga moja juu ya jingine, kutakuwa na uwezekano wa magunia hayo kufika kwenye nyota. Mkulima toka Burkina Faso alitumkubusha kuwa maana ya neno Burki Na Faso: "Nchi ya watu waaminifu." Lakini furaha ya kuhudhuria mkutano huu niliipata pale jamaa mmoja aliponiuliza, "Wewe si Ndesanjo?" Huyu alikuwa ni Joseph Mzinga, Mtanzania anayefanya kazi nchini Zambia. Mzinga yuko hapa Edinburgh akiwakilisha sauti ya wakulima wa Afrika katika harakati za kupinga tamaa ya kundi la nchi nane.

Kuna tatizo limetoa nashindwa kupata kidude cha rangi na wakati mwingine kidude cha kuweka viungo. Najaribu kutafuta chanzo.

Picha za Maandamano ya Edinburgh

Kuna picha hapa za maandamano ya leo jijini Edinburgh.

maandamano na tamasha la Live 8

Leo watu, nadhani ni zaidi ya laki mbili, wameandamana katika jiji la Edinburgh. Nilikuwa katikati ya msongamano wa watu waliokuwa wamebeba mabango, wakipiga ngoma, filimbi, wakicheza, wakisambaza vipeperushi, n.k. Waandishi wote tulikwenda kwa pamoja lakini muda sio mrefu tulishapoteana. Kazi kubwa niliyokuwa nikifanya ilikuwa ni kuongea na waandamanaji toka Afrika. Nimekutana na Waafrika toka Tanzania, Uganda, Nigeria, Ghana, Msumbiji, n.k. Mimi nilirudi yapata saa tisa nikiwa nimechoka kabisa. Kwakuwa ninafanya kazi kwenye blogu mpya ya Panos na pia tovuti yao, nitakuwa naandika kifupi hadi nikipata muda wa kutosha. Hivi sasa tamasha la Live 8 linaendelea. Tunatazama kwenye luninga. Muda mfupi uliopita alikuwa akiimba Mariah Carey. Jukwaani alipanda na kwaya ya watoto wa Afrika Kusini, ambao ni yatima kutokana na wazazi wao kufariki kwa Ukimwi. Kama saa moja lililopita, ilionyeshwa filamu ya wimbo aliyotumia Bob Geldof kuchangisha fedha kwa ajili ya baa la njaa Ethiopia. Mara akashangaza watu pale alipoonyesha picha ya mmoja wa watoto walionekana kukaribia kufa kwa njaa na kusema kuwa mtoto huyo alinusurika na kuwa yuko Hyde Park, London. Mara binti mmoja mzuri mno akajitokeza na kusalimu kwa lugha ya Amharic. Baada ya hapo Madonna alipanda jukwaani na kumkumbatia binti huyu na kumbusu kwenye pambaja za mdomo. Mmoja wa wahariri tulio nao hapa akashtuka, "Ah, anambusu Madonna!"

Hivi sasa kuna jamaa anaimba ambaye simfahamu na sidhani kama nina nia ya kumfahamu!

Toka tuanze kutazama nimemuona Kanda Bongo Man na Youssou Ndour wakitumbuiza kule katika ukumbi walikopelekwa wanamuziki toka Afrika. Kamera zikielekezwa huko tunaonyesha dakika mbili kisha tunarudishwa kwa wanamuziki weupe. Dunia hii ya ajabu sana, Hata wale wanaodai wanatetea masikini na Waafrika wanatakiwa kusaidiwa sana kuondokana na kitu wazungu wanaita White Supremacy, dhana kuwa weupe ni bora kuliko watu wengine duniani.

Tazama blogu ya Panos hapa.

7/01/2005

Maandamano makubwa kesho...mji umejaa askari

Tumewasili salama hapa Edinburgh. Usiku wa leo nilikwenda kutembea katikati ya jiji. Katika pitapita zangu nimekutana na Watanzania watatu. Mmoja anatoka kule kijijini kwetu! Dunia ina mambo.

Mji mzima umejaa polisi na walevi. Kila mtu anaelekea kuyumba kwa kulewa. Wako wanaopigana mabusu, kukumbatiana, kugombana, n.k. Polisi wamejazana kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya maandamano makali kuanzia kesho kupinga sera za wezi wakuu duniani. Maduka mtaa ya Princess yamewekewa mbao ili kuzuia mawe toka kwa waandamanaji. Tunaambiwa kuwa hapa usckochi kutakuwa na wanaume wazungu 8 (viongozi wa G8), wapinga mifumo yote ya utawala (anarchists??) 10,000, na wanaharakati 100,000. Kuna kazi. Mabango kila mahali.

Vyombo vya habari hapa Uingereza vina picha kubwa ya "watakatifu" wawili, Tony Blair na Bob Geldof. Geldof anaamini kuwa juhudi za wapinga mfumo wa kibepari zimefanikiwa kwani mabepari hao wanapokutana wiki ijayo watakubali kusaidia masikini. Geldof sijui anatumia kitu gani kufikiria. Hivi unawezaje kukaa kikao na shetani kupanga jinsi ya kumpindua huyo shetani? Ndio anavyotaka Bob Geldof. Kaandaa tamasha la muziki la LIVE 8 maeneo mbalimbali duniani. Tamasha linahusu Afrika ila wanamuzki wa afrika hawapo. Wanamuziki wa Afrika wamepewa ukumbi maalum kwa ajili yao peke yao. Tena baada ya kutokea malalamiko. Mwanzoni waafrika hawakuwa kwenye ratiba yake, hata mji wa Johannersburg ambao ndio mji pekee wa Afrika utakaokuwa na tamasha hilo umeingizwa hivi majuzi baada ya watu kulalamika. Hawa wazungu wanaona waafrika sisi sijui tuko kama vile mabumbuwazi au? Kwanini kwa mfano wanamuziki wa Afrika wanapewa sehemu yao wenyewe ya kutumbuiza na sio kule kwenye matukio makuu yanayopewa kipaumbele na vyombo vya habari? Huko vichochoroni watakapotumbuiza Waafrika sijui atakwenda nani. Sijui wanamuziki wa Afrika hawawezi kutumbuiza kwenye majukwaa makubwa na wanamuziki wakubwa wa Magharibi?

Karibu saa nane na nusu usiku. Nakwenda kulala, tutaonana kesho.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com