7/01/2005

Maandamano makubwa kesho...mji umejaa askari

Tumewasili salama hapa Edinburgh. Usiku wa leo nilikwenda kutembea katikati ya jiji. Katika pitapita zangu nimekutana na Watanzania watatu. Mmoja anatoka kule kijijini kwetu! Dunia ina mambo.

Mji mzima umejaa polisi na walevi. Kila mtu anaelekea kuyumba kwa kulewa. Wako wanaopigana mabusu, kukumbatiana, kugombana, n.k. Polisi wamejazana kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya maandamano makali kuanzia kesho kupinga sera za wezi wakuu duniani. Maduka mtaa ya Princess yamewekewa mbao ili kuzuia mawe toka kwa waandamanaji. Tunaambiwa kuwa hapa usckochi kutakuwa na wanaume wazungu 8 (viongozi wa G8), wapinga mifumo yote ya utawala (anarchists??) 10,000, na wanaharakati 100,000. Kuna kazi. Mabango kila mahali.

Vyombo vya habari hapa Uingereza vina picha kubwa ya "watakatifu" wawili, Tony Blair na Bob Geldof. Geldof anaamini kuwa juhudi za wapinga mfumo wa kibepari zimefanikiwa kwani mabepari hao wanapokutana wiki ijayo watakubali kusaidia masikini. Geldof sijui anatumia kitu gani kufikiria. Hivi unawezaje kukaa kikao na shetani kupanga jinsi ya kumpindua huyo shetani? Ndio anavyotaka Bob Geldof. Kaandaa tamasha la muziki la LIVE 8 maeneo mbalimbali duniani. Tamasha linahusu Afrika ila wanamuzki wa afrika hawapo. Wanamuziki wa Afrika wamepewa ukumbi maalum kwa ajili yao peke yao. Tena baada ya kutokea malalamiko. Mwanzoni waafrika hawakuwa kwenye ratiba yake, hata mji wa Johannersburg ambao ndio mji pekee wa Afrika utakaokuwa na tamasha hilo umeingizwa hivi majuzi baada ya watu kulalamika. Hawa wazungu wanaona waafrika sisi sijui tuko kama vile mabumbuwazi au? Kwanini kwa mfano wanamuziki wa Afrika wanapewa sehemu yao wenyewe ya kutumbuiza na sio kule kwenye matukio makuu yanayopewa kipaumbele na vyombo vya habari? Huko vichochoroni watakapotumbuiza Waafrika sijui atakwenda nani. Sijui wanamuziki wa Afrika hawawezi kutumbuiza kwenye majukwaa makubwa na wanamuziki wakubwa wa Magharibi?

Karibu saa nane na nusu usiku. Nakwenda kulala, tutaonana kesho.

3 Maoni Yako:

At 7/01/2005 07:46:00 PM, Anonymous Anonymous said...

Polisi wa nini huko nchi za kidemokrasia?

 
At 7/02/2005 12:08:00 AM, Blogger msangimdogo said...

Uwakilishi wako huko ni muhimu sana kaka, wengi tunataka kujua hivi hawa jamaa huwa wakikaa kutujadili ni kweli hata sura zao zinaonyesha kuwa zina uchungu na sisi au ni porojo tu za kwenye vyombo vya habari lakini wanakuwa wakitukejeli?

 
At 7/02/2005 02:25:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

Nadhani hatushirikishwi kwa sababu ya ujinga wa baadhi ya wasomi na wanasiasa wetu. Hivi jitu zima na akili yake lililotumia fedha za umma kusomshwa linaamini kabisa kwamba maendeleao ya Afrika yataletwa na Blair na Gedof sijuhi nani? Kwa nini wakushirikishe wakti wewe umeshindwa kuwa na ajenda yoyote ya kujikwamua? Ndicho tunachostahili hicho.

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com