2/11/2006

KWAHERINI...

Kwaherini ndugu zanguni.

Kwaheri hii sio ya kuacha kublogu. Sio kama ile ambayo Michuzi aliyotupa hivi majuzi.
Kwaheri hii ni ya kuhama nyumba. Sio kuacha kublogu. Naamini mnafahamu kuwa sitakaa niache kublogu hata kwa mtutu. Nimekuwa siandiki sana na pia hata barua pepe nyingi (za wasomaji na marafiki) sijazijibu. Nilikuwa katika ujenzi wa nyumba mpya. Ujenzi wenyewe bado unaendelea. Unajua ukihamia kwako hata kama madirisha hayana vioo huwa hakuna noma. Hata gunia au bati utaweka maana ni kwako.

Wakati huo huo nimeendelea kuandika ule mwongozo wa wanablogu. Mwongozo huu daima utakuwa unaendelea kuandikwa kutokana na mabadiliko ya haraka ya teknolojia na kutokea kwa mambo mapya. Mwongozo huu umerekebishwa kwani ule wa mwanzo ulikuwa na makosa mengi hasa katika kodi za "HTML." Niliuandika wakati naanza kujihusisha na haya mambo. Baadhi yenu mlinishtua juu ya makosa yaliyokuwepo. Nimesahihisha na kuongeza mambo kadhaa. Kazi yenyewe bado sana. Niliyoandika hivi sasa ni kama asilimia tano.

Ingawa mwongozo huu unalenga hasa wale ambao wana nia ya kuanza kublogu, kuna mambo kadhaa ambayo yanaweza kusaidia hata wale waliobobea. Kama sio mambo yaliyoko hivi sasa basi baadaye kutakuwa na mambo ambayo unaweza kufaidika. Bonyeza hapa usome mwongozo huo.

Haya, sasa nachukua nafasi hii kuwataka mkaribie kwenye makazi yangu mapya kwa chai. Makazi hayo ni.....

Bonyeza hapa uyaone mwenyewe.

2/07/2006

Mchezo wa kuigiza: Watanzania na Utanzania Wetu

Mti Mkubwa (ambaye Michuzi anamuiita Mti Mkubwa Mkavu) ni mwanablogu ingawa sio mwanablogu. Suala la Mti Mkubwa kuwa mwanablogu ingawa sio mwanablogu ni moja ya mifano ambayo mimi huitazama kama ni faida za teknolojia ya blogu. Je ni mara ngapi umeona maoni ya wasomaji kwenye magazeti yamewekwa ukurasa wa mbele? Mti Mkubwa ni msomaji mzuri sana wa blogu na mtoa maoni changamoto. Mara nyingi maoni yake huwa yanakuwa mazito sana kiasi ambacho wanablogu huyaweka ukurasa wa mbele badala ya kuyaacha kwenye kidirisha cha maoni. Hii ni sawa na mhariri wa gazeti kuchukua maoni ya msomaji na kuyaweka kwenye ukurasa wa mbele. Kwahiyo utaona kuwa kutokana na maoni na taarifa mbalimbali anazotoa Mti Mkubwa kuweka ukurasa wa mbele za blogu zetu, unaweza kusema kuwa Mti Mkavu ni mwanablogu (ingawa sio moja kwa moja, kwa maana ya yeye kufungua blogu yake mwenyewe).
Read more ยป

Michuzi...kisa ni nini hasa?

Matukio mengi yanayotokea duniani hii leo hii. Michuzi anataka kuacha kublogu katika blogu yake tuipendayo ya picha. Nakuomba umsihi abadili uamuzi wake. Ingawa kuamua kublogu au kutoblogu ni uamuzi wa mtu binafsi, unaweza kublogu ikafika wakati ambapo uamuzi wa kuendelea au kuacha unakuwa sio wako binafsi. Hasa inapokuwa ni mtu ambaye blogu yake ni sawa na jumba pepe la makumbusho ya taifa kwa picha. Ina maana kuwa tuna haki na kumhoji atupe sababu za msingi. Sababu aliyotoa kwenye blogu yake haijaniridhisha. Labda atufafanulie zaidi. Bonyeza hapa umsome. Iwapo kuna mtu anamuunga mkono uamuzi wake, mtu huyo ana haki pia ya kutoa maoni yake kwenye kidirisha cha maoni hapo kwenye blogu ya Michuzi. Mimi binafsi simuungi mkono na unaweza kusoma maoni yangu hapo kwenye blogu yake.

2/04/2006

Blogu Hadi Kasulu..

Kama mapinduzi ya uandishi pepe unaona kuwa ni utani, fikiria tena. Kasulu nako kuna blogu. Ndugu yetu Njili Mwakoba amekata shauri. Ameanza kublogu. Mtembelee umkaribishe. Bonyeza hapa.

2/01/2006

Natangaza Kuzaliwa Kwa....

Je una habari za kuzaliwa kwa blogu hizi? Nitaandika machache kutokana na ujio wa wanablogu hawa wapya (ukiacha blogu ya watoto ambao ni ukurasa wa pili wa Da Mija). Watembeeleeni tafadhali na kuwaunga mkono. Kuna ndugu Lubuva, bonyeza hapa. Halafu Kisima cha Weledi, bonyeza hapa. Kutana na Jungu Kuu (lina ukoko au halina?), bonyeza hapa. Na masuala ya watoto kupitia Da Mija, bonyeza hapa.

Kasri halali akitafuta kila mbinu za kuleta wanablogu wapya. Msome mwenyewe kwa kubonyeza hapa kuhusu juhudi zake hizo na matunda yake.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com