3/04/2005

WATANZANIA WALAANIWA MICHANGO?

Rafiki yangu wa karibu kanitumia waraka huu mzuri sana unaotembea katika mtandao wa kompyuta. Nadhani umeandikwa na mtu aitwaye Phillemon S. Mutashubirwa. Nimependa sana uchambuzi na malalamiko yake. Ukisoma utacheka ila jambo lenyewe sio mzaha. Nimeweka hapa bila idhini yake, ila naamini kuwa hatanipeleka mahakamani kwa hilo. Haya usome na utafakari:
WATANZANIA NA MICHANGO:
MICHANGO ah! Mungu wani. Naigwa go!
Nchi gani hii kila ukiamka, kila ukiwa njiani, ofisini au ukilala ni kusakamwa na michango tu?
Michangooo, michangooo na michangoo! Twatolewa genii mpaka tumepata
pancha.

Hapana naapa! Kwa sasa mmezidi. Amka asubuhi utasikia hodi,
ukifungua kuna mtoto na kikadi kilichoburuzwa kwenye kompyuta kikiomba
mchango wa "kitchen party." Yarabi!
Unamwambia utawasiliana na baba yake anaondoka. Upo kwenye daladala unawahi Pugu Road kazini, unaombwa samahani na mtu akidai alikuwa na barua yako na anakupatia bila hiana. Mtumeee! Unafungua unakuta ni kakadi kengine ka mchango. Safari hii ni ka "chicken party na kameonyesha kiwango kabisaa. Kwa fasheni ya sasa ni 7,000/-. Huyu ni wa aibu, hivyo unampa tano ukidai mbili utamtuma mtoto.

Unatoka kazini hujala chochote kwa vile 5,OOO/= ulitoa kwenye "chicken party" ambayo hata maana ya neno lenyewe hujui. Unakuta kengine nyumbani. Hako ni ka mchango wa "send off'. Jamani wanitakani?
Unaoga, ghafla aja mtu na kadi tena safari hii ni mchango wa harusi ya shemejiyo. Unajikamuakamua ili usiadhirike ukweni, unampatia kiasi kilichokuwa ada ya Sikujua shuleni.
Hayo bado kuhudhuria vikao vya shemejio vya harusi nako kuna kamchango ka kila mkutanapo kanaitwa uchache au chakaza. Shemeji mtu tena si ni lazima wakukamue kamasi mwanangu?
Haiishii hapo, unakuja ujumbe kuwa dada yake dada wa mama yako mzazi kafia Muhimbii yuko mochwari. Hapo achilla mbali bakuli la mchango utakalokuta, patakuwepo pia kitabu cha kujiorodhesha na kiasi mtakachotoa. Michango haitoshi, sasa yabidi wale wa karibu yake mjazie ili iwezekane kukodisha "Fuso" ya kumpleka. Na huko nyumbanl ni lazima mkamuliwe tena hela ya kununulia mboga.
Unasema walau sasa napumua, Inatoka barua kwa wajomba zako kuwa ile arobaini ya babu ni mwezi ujao, Hapo yataka mchango wa kununulia ng'ombe na mchele kwa ulaji wa siku hiyo.
Kwani utakimbia jamii yenu kwa vile imekuwa ya michango? Kazini wameanza kukukata mshahara kwa madeni uliyo nayo SACCOS. Mtoto wa jirani ambaye umemdhamini ubatizo naye aja akidai mchango wa kunuunulia gauni la "birthday". Ebo! Sasa mwanangu? Utasahau mdogo wenu wa mwisho alipigwa retrenchi na sasa ana mtoto mchanga wa kubatiza. Utakwepa vipi
usimchangie kitu kidogo atakapowahi kwako majogoo?
Afadhali usingezaliwa Kipatimu mwanangu. Mwezi huu ni wa kuwacheza watoto. Utawaambla nini huko kwenu wakuelewe kama hukutuma mchango wa hilo tamasha? Bado wana wewe kaka! Mtoto wa kaka yako anapata komunio utamkwepaje mbele ya jamii iliyokuzunguka? Afadhali tajiri yako asingekuwa na mtoto Chuo Kikuu anayegradueti na keshakuletea kadi ya
mchango.
Utachanga sana graduesheni ya sekondari, chekechea hata na darasa la sab aachilia mbali VETA. Mtajiju wenyewe, nani aliyewatuma kuzaliwa Bongo, Afadhali wanajeshi hawana sherehe hata wapatapo umeja. Utadhani sasa utapumua uendapo nyumba za ibada, Yallaaah!
Utakutana na michango ya ofisi ya paroko, mchango wa jengo na pikipiki ya shemasi. Mpo hapo?
Kijijini ndo usiseme tena. Kuna barabara, shule, maji, zahanati, ugeni wa DC, vyote vyadai mchango na mara nyingi hakuna risiti. Si ni jamaa zako una wasiwasi gani? Umesahau mfereji wa kijiji, trekta la mshikamano vyote vyataka michango achilia mbali mchango wa damu Muhimbili! Afadhali huu wa damu kwa vile hauhusu fedha. Unafikia mahali unasema utapanchi hiyo michango. Ukiwaza hayo, mara anapita Katibu kata mwenyewe. Huyu anadai mchango wa mapokezi ya Waziri Mkuu au ya Mwenge utasemaje?
Hakuna huruma na mtu wala hakuna wa kutaka kujua kipato chako kabla hajakupa kadi ya mchango. Shuleni watatuma barua kuhusu mchango wa kumwaga mwalimu mkuu. Bado michango ya tuisheni, uji wa saa nne, safari, Serengeti na T-shirt za shule. Mmesahau redio ya shule ikikosa betri wazazi shurti,wachangishwe? Mwashangaa nini hospitalini hamchangii?
Michango hii! Sasa mtatukamua damu.
Ipo ya kwaya, Saidia Simba Ishinde, usafi wa makaburi, basi la kijiji. Bado sijasema michango ya SACCOS na upatu kazini kwenu
HAYAA !!!

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com