2/06/2005

TOVUTI YA WAZIRI MKUU...WALE WALE! TUFANYE NINI?

Rafiki yangu kanitaarifu kuwa ile vita nilioivalia njuga ya kutaka tovuti zote za umma (bunge, sirikali, ikulu, n.k.) kuwa katika lugha inayoeleweka na walalanjaa, wakeshahoi, walalahoi, makabwela, n.k. ambao ndio huamka asubuhi kuwapigia kura, ni vita nzito sana. Kumbe waziri mkuu naye kalewa ule mvinyo ulioletwa toka akina Mangungo waliposaini ile mikataba ya hadaa. Tovuti ya waziri mkuu ukiifungua huwezi amini kuwa huyu ni waziri mkuu wa sirikali ya akina Mawazo, Abuu, Magoti, Kulusumu, Mariamu, mama Zuberi, Mateso, n.k. ambao walimaliza darasa la saba katika shule ambazo hata mbao za kufundishia au chaki za kuandikia hakuna. Tembelea tovuti hii mwenyewe uniambie. Wanawaundia tovuti hizi "wafadhili" wakijifanya kuwa ni tovuti zetu. Utumbo na uongo huu tutaukomesha. Watanzania tuna mwisho wa kukubali michezo michafu kama hii ya ukoloni mamboleo, utumwa wa kimawazo, utegemezi, n.k.
Rafiki yangu aliyenikumbusha kuhusu tovuti hii ambayo ilizinduliwa rasmi pale Dodoma tarehe 19/06/2004 kauliza kama watawala wa Tanzania wanaopenda kujiita viongozi (na kujifanya eti wanamuenzi Nyerere...waache kabisa dhihaka na jina na falsafa za Mwalimu) wanafikiri kuwa tarakilishi haziwezi kuelewa kiswahili ndio maana tovuti zao ni za kiingereza.
Ukifungua tovuti hii unakutana na picha ya Sumaye amekaa akijifanya yuko bize. Sijui alikuwa anasaini mkataba gani (ambao nahisi utakuwa wa kilaghai) siku hiyo. Kumbuka kuwa huyu ndiye yule anayependa kusema kuwa sirikali yetu hufanya kazi usiku na mchana. Na labda hii picha ilipigwa usiku wa manane!
Utasikia wakati huo huo (narudi kwenye tovuti na lugha) sirikali yetu ikikaa kwenye mikutano na "wafadhili" wakiongelea hili neno jipya la kuchukulia fedha toka Ulaya na Marekani. Neno hilo ni "digital divide." Hili neno linaelezea pengo lililopo kati ya wale watu wachache wenye uwezo wa kutumia, kuelewa, kumiliki, n.k. teknolojia ya zana mpya za mawasiliano na habari na wale wengi wasio na uwezo wowote. Kumbe kipengele kimojawapo cha hiyo "digital divide" yao wanayoifanyia mikutano, warsha, na makongamano ni lugha. Ukiachia mbali uwezo mdogo wa kifedha unaofanya wengi kutokuwa na uwezo wa kutumia teknolojia/zana hizi, kuna suala la lugha. Lugha inayotumika zaidi katika intaneti na katika programu zake ni kiingereza, hii inafanya elimu na maarifa yaliyomo katika mtandao kufikiwa na tabaka dogo la wale wanaoijua lugha hii. Sasa sirikali yetu badala ya kujaribu kupunguza ukubwa wa hili pengo la wale wanaofaidika na wasiofaidika na teknolojia hii kwa kuweka masuala ya sirikali yao katika lugha rahisi kwao kuelewa wanachukua ndege hadi Uingereza kuazima lugha ya kuongea na Watanzania wenzao. Au inawezakana hawataki kuongea nasi? Majirani za Rais na waziri mkuu (wavuvi na wauza samaki pale kigamboni) wanaweza kuelewa chochote katika tovuti ya waziri mkuu na ile ya ikulu? Je, nikisema kuwa sirikali ya Tanzania sio ya Watanzania kuna atakayebisha? Kama ni ya Watanzania inawezaje kuongea nao kwa lugha ngeni kwao? HAKUNA SABABU YOYOTE YA MSINGI ZAIDI YA UONGO, DHARAU, UTUMWA NA UTEGEMEZI. Tazama tovuti hiyo hapa.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com