6/16/2004

Kichaka

Vyombo vya habari hapa vinazungumzia sana juu ya madai kuwa Rais Mugabe wa Zimbabwe aliiba kura. Nashangaa kwanini hawasemi pia kuwa huyu rais Kichaka (jina lake kwa kiswahili) aliiba kura! Sasa wizi wa kura utaanzwa kufanywa kwa kutumia teknolojia. Kampuni ya Diebold imetengeneza mfumo wa kupiga kura kwa njia ya electroniki (kwa kutumia mdahalishi). Kampuni hii huwa inatoa fedha nyingi kukiunga mkono chama cha Rais Kichaka cha kihafidhina. Na kampuni hii itakuwa inajua siri ya kuweza kubadili mahesabu na hakuna mtu atakayeweza kuthibitisha. Pia kama kuna utata juu ya idadi ya kura kama ilivyokuwa kule California, hakuna namna ambayo watu wanaweza kuthibitisha kuwa walipiga kura.

Kuna wizi mwingine wa kura wa kijanja sana. Ukiwa jela au ukiwa uliwahi kufungwa huna haki ya kupiga kura. Kwakuwa wafungwa wengi ni wanaume weusi. Na watu wengi walioko jela ni masikini maana matajiri huwa hawaendi jela. Kwanza wana uwezo wa kupata mawakili wa hali ya juu kabisa. Pili, wanakutana na viongozi wa nchi, majaji, na wanasiasa katika viwanja vya gofu, majumba ya kufanyia mazoezi, kwenye sherehe, baharini wakivua samaki, klabu za kucheza mchezo wa darts . Wanaishi katika dunia moja na watunga sheria, watafsiri sheria, na wakamataji wahalifu.

Kwakuwa basi watu wengi wenye rekodi za kufungwa ni weusi na wazungu wachache masikini. Na kwakuwa masikini wengi hawakipendi chama cha Conservative kutokana na rekodi yake ya upendeleo zaidi kwa matajiri. Chama hiki kinaunga mkono sheria hii ya kuwa wafungwa wasipige kura maana wanajua kuwa masikini hawa walioko jela au waliokuwa jela wakiruhusiwa itakuwa ni sawa na kuwapa chama cha Democrat kura zaidi. Ukienda California, katika kila watu weusi watano, watatu hawaruhusiwi kupiga kura. Yaani kuna binadamu hawana haki ya kupiga kura kabisa hapa duniani. Kura ni kati ya haki ambazo ukinyima mtu unakuwa umefika hatua ya juu sana katika udikteta. Udikteta huu ni mbaya kweli, ila hauonekani kwa urahisi. Ndio maana watu wengi tukiongelea viongozi wala rushwa tunataja viongozi wa nchi masikini, kumbe nchi tajiri rushwa imefichwa sana. Huioni kwa urahisi. Kwanini? Sababu kubwa ni kuwa rushwa katika nchi kama ni kubwa sana. Kwahiyo ukiona mtu anasema hapa hakuna rushwa ujue huyo mtu ni masikini. Masikini hawahusiki na rushwa kwa wingi kama matajiri. Lakini hata hapo Tanzania tunajua kuwa sisi masikini tunaweza kudhani kuwa viongozi wetu hawachukui rushwa. Utajuaje wakati hawawezi kuja kuchukua rushwa kwako? Wanachukua kwa wale wenyenazo.

Ninachosema ni kuwa wizi wa kura hapa katika nchi ya KIchaka umehamia kwenye kompyuta na sio masanduku ya kura tena.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com