VITA YANGU NA TOVUTI ZA KIINGEREZA TANZANIA
Sitaki mseme kuwa ninaandama hawa jamaa walioko madarakani kwa kutengeneza tovuti za bunge, ikulu, ofisi ya waziri mkuu kwa lugha ya kiingereza bila sababu za msingi. Nitatoa sababu mbili kuu kwa sasa. Sababu ya kwanza inatokana na kauli mbiu maarufu ya sirikali ya rais Mkapa. Alipoingia tu madarakani alisema, "Hizi ni zama za uwazi na ukweli." Uwazi unapokuwa katika lugha ngeni kwako usiyoijua, lugha ambayo unahitaji kamusi ili kuelewa unakuwa ni uwazi? Ukweli ukiwekwa katika lugha ya kigiriki kisha ukaupeleka kwa wachina ukweli huo utakuwa na faida gani kwao? Ukiweka ukweli kwenye kifaransa kisha ukaupeleka kwa watu wanaoelewa tu kiarabu, ukweli huo utakuwa na faida gani? Ni sawa na kusema kuwa sirikali ya Mkapa inajali uwazi na ukweli wakati ambapo lugha inayotumika katika tovuti zake ni lugha ngeni kwa wapiga kura. Tovuti hizi ni kiunganisha kati ya sirikali na wana wa nchi, sio kiunganishi kati ya sirikali na wafadhili. Uwazi na ukweli utakuwa uwazi na ukweli kwa Mtanzania utakapokuwa katika lugha ya Kiswahili. Unaona ndio maana wengine tunaita serikali "sirikali." Wananikumbusha zile enzi ambazo Biblia ilikuwa hairuhusiwi kutafsiriwa katika lugha inayoeleweka kwa waumini. Inanikumbusha pia kuwa mtu wa kwanza kutafsiri Biblia kwa kiingereza alichomwa moto hadharani. Sirikali kama kanisa vimekuwa ni vyombo vyenye kupenda sana mamlaka na nguvu, njia mojawapo ya kuhakikisha usalama wao ni kuficha ukweli hata pale wanapotamka hilo neno ukweli kila wanapofungua mdomo. Haya, sababu ya pili ninayoitoa ni kauli ambayo aliitoa rais mwenyewe Machi 18, 2003 wakati akifungua kongamano linalohusu uimarishaji wa mawasiliano kati ya sirikali na umma. Haya ndio maneno aliyoyasema (kwa kiingereza!). Soma kwa makini kisha uniambie anamaanisha nini anaposema haya huku tovuti ya ile ofisi tuliyompa, yaani ikulu, haiko kwenye lugha ambayo itaimarisha mawasiliano: "Let me now address the government's duty to communicate. And I use the broader concept of 'communicate', not the narrow one of 'inform'. For, important as the duty to inform is, it is much more important to communicate, creating space for dialogue, and generally conducing to a free flow of thoughts and ideas. Communication, rather than information, builds stronger institutions and processes for good governance. It is about improving interaction between government and the governed, in whose name decisions are made, tax money spent."
0 Maoni Yako:
Post a Comment
<< Home