5/25/2005

MKUTANO WA COMMONS-SENSE

Nimewasili hapa jana baada ya safari ya masaa 17 hivi. Nadhani nilitakiwa kuoga na magadi kabla ya kuondoka ili kuondoa kisirani kwani begi langu la nguo halikufika! Litafika leo usiku na nitalipokea kesho! Niende nikanunue nguo mpya? Nisubiri
Kwa wale wasiofahamu, ninahudhuria mkutano unaoitwa Commons-Sense ulioandaliwa na chuo kikuu cha Wits, Creative Commons (Afrika Kusini), na Links. Mkutano huo unafanyika hapa katika jiji la Egoli ( jina la Kizulu la jiji la Johannersburg). Shughuli rasmi zitaanza leo jioni kwa tafrija ya mkia wa jogoo (kwa kiingereza wanaita "cock tail"). Tayari nimekutana na watu wawili ambao nao wanahudhuria mkutano huu. Dada mmoja toka Kenya na mwingine toka Marekani.
Nenda hapa kwa taarifa zaidi juu ya mkutano huu.
Jana usiku, ingawa nilikuwa nimechoka, sikujisikia kulala. Nilishuka chini (ninakaa hapa) kwenda kuongea na waswahili wenzangu ambao kazi zao ni ulinzi, ufagizi, kufungua milango, n,k. Tsedu ni mlinzi wa usiku hotelini hapa. Anaishi kitongoji cha Alexandra. Tsedu ni rasta: anamuenzi Mfalme wa Wafalme, Simba wa kabila la Yuda Haile Selassie I, Jah! Rastafari!
Tsedu alinivunja mbavu. Baada ya kuniambia kuwa yeye ni rasta na anapenda sana kusikiliza muziki wa hisia na mafunzo, Rege, nilimuuliza kama anampenda Lucky Dube. Akanitazama kwa mshangao na kusema, "Dube hapigi rege. Ile sio rege!" Tsedu anawasikiliza wanamuziki kama Culture, Burning Spear, Bob Marley, Mutabaruka (yule mshairi anayetembea pekupeku), Luciano, n.k. "Rege ni mafunzo, ni tenzi za rohoni, ni mashairi ya kiroho..." Tsedu ananiambia.
Karibu kila wimbo niliomtajia wa wanamuziki anaowasikiliza, alikuwa amekariri maneno yake na hata ufafanuzi wa jinsi ujumbe wa nyimbo hizo unavyoendana na hali ya kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni duniani hivi sasa. Nilipomtajia wimbo wa Burning Spear uitwao "Days of slavery." Alitabasamu huku akitikisa kichwa. Kisha akaanza kuuimba. "Watu wengi wanaposikiliza huu wimbo wanafikiria mambo yaliyotokea miaka mingi iliyopita. Hapa Afrika Kusini utumwa anaozungumzia Burning Spear upo hadi leo."
Tulipiga gumzo na Tsedu kwa masaa kadhaa...nadhani nilienda kulala saa tisa. Nilipomtaja Steve Bantu Biko, Tsedu alitazama chini, uso wake ukajaa huzuni. Alikaa kimya kwa muda kisha akasema, "Black consciousness." Black Consciousness ni jina la falsafa na itikadi aliyokuwa akihubiri mwanamapinduzi Biko. Baada ya muda kidogo alinieleza kwa kina jinsi Biko alivyouawa kinyama. Alivyoburuzwa akiwa amening'inizwa nyuma ya gari katika barabara ya kokoto. Uchi wa myama. Alipomaliza kunieleza kwa undani na hisia kali niligundua kuwa sikuwa ninafahamu kwa kina yaliyotokea siku za mwisho wa uhai wake. Maelezo yake yalinitia hasira na huzuni kwa wakati mmoja. Hadi sasa bado kuna donge limekwama kooni.
Nilipomuuliza Tsedu juu ya kitongoji anachoishi, visa alinieleza visa ambavyo vimenijaza huzuni kubwa. Anasema kuwa maisha wanayoishi Waafrika katika vitongoji mbalimbali nchini humu hayana thamani yoyote. Vifo kutokana na ukimwi, ujambazi wa kutumia silaha vimekuwa ni kitu cha kawaida. "Nikiwa nyumbani nikasikia mlio wa risasi huwa ninaendelea na shughuli zangu. Hata watoto wangu wamezoea. Kila mtu kazoea. Hakuna anayeshtuka. Tumekuwa sugu. Tumekuwa viziwi. Tumekuwa vipofu. Hii ndio njia pekee ya kuendelea kuwa na akili timamu. Bila hivyo utarukwa na akili au utakata tamaa na kujiua. Anasema majambazi katika vitongoji vya weusi wamefika hatua ambayo hakuna kinachowazuia kupora mtu yeyote na saa yeyote. "Majambazi wanampora mtu pembeni yako, unatazama na kuendelea na shughuli zako." Ananiambia.
Anasema kuwa siku moja aliporwa simu ya mkono. Kawaida akiwa vitongojini hapendi kutumia simu yake. Siku hiyo alisahau kuizima. Akiwa anapita mtaani, simu ikalia. Jamaa watatu wakamfuata, mmoja wao akamwambia, "Pokea hiyo simu. Ukishamaliza kuongea tupe simu yetu." Wakati wanamwambia hivyo mmoja wao alikuwa amechomoa bastola.
Nitakutana na Tsedu leo usiku baada ya ufunguzi rasmi wa mkutano na tafrija ya mkia wa jogoo. Usisahau kutembelea tovuti ya mkutano huu. Nitakuwa ninawapa taarifa mbalimbali kadri mkutano unavyoendelea. Ninakwenda kutembea mjini hadi jioni. Sijui nikanunue bastola...maana nataka kwenda ile mitaa ninayoambiwa kuwa nisithubutu kupeleka unyayo. Huko ndio ninataka kwenda. Niombeeni!!!!
Sobonana futhi (tutaonana baadaye kwa Kizulu).

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com