2/28/2005

TANZANIA YAZIDI KUENDELEA

Tanzania inazidi kupiga hatua katika maendeleo ya wananchi wake. Muda sio mrefu daladala zitapigwa marufuku ili mwekezaji anayekula sahani moja na vitofali (sio vigogo tena siku hizi) aweze kuleta mabasi yake!
Hatua nyingine kubwa kimaendeleo inaonekana katika suala la mama lishe, ambao kampeni ya CCM ilidai kuwa ina fungu la fedha la kuwasaidia. Duka la kaburu la Shoprite jijini Dasalama hivi sasa linauza ugali na maharage kwa bei ya chini zaidi ya mama ntilie. Hali hii inatishia kipato cha akina mama hawa, wengi wao wakiwa wana familia kubwa zinawategemea, na hivyo kuimarisha upenzi wa wananchi wa kawaida kwa sirikali yao inayowajali sana sana kiasi cha kuwa na sera, mikakati, na kila mbinu za kuwalinda dhidi ya misukosuko ya soko huria ambayo ndio kwanza wanaionja.
Hatua ya juu kabisa ya maendeleo ambayo itafanya Tanzania kuwa ni moja ya nchi za dunia ya kwanza na pengine kuingia katika kundi la nchi tajiri duniani la G8 na kufanya kundi hilo kuwa G9 ni pale kilio na sala zangu vitakaposikiwa na mungu ambaye aliacha kuongea na wanadamu zamani sana toka alipoongea na manabii na mitume wa kwenye biblia na kurani. Mungu anayetupenda sana kiasi cha kumwacha shetani aje duniani kutushawishi ambapo baadaye tukifa atatuchoma moto wa milele...ingawa pia anasifika sana kwa huruma! Mungu huyu pia anachoma moto watoto wadogo wanaofariki kabla ya kubatizwa kwa mujibu wa teolojia ya kiluteri (msije mkasema nimetunga) kwa kuwa eti wamerithi kitu kinaitwa dhambi ya asili toka kwa Adamu na Hawa. Basi mungu huyu akisikia kilio na sala zangu kuhusu kubinafsishwa kwa ikulu na Tanzania kuwa na rais kaburu, nchi yetu itakuwa imeruka toka ulimwengu wa nne hadi wa kwanza.
Wale wanaotaka kujiunga na kampeni yangu hii tuwasiliane maana hili jambo sio la mchezo. Wenzetu wa Kenya nao ambao wamechoshwa na wazee kama Kibaki wanaweza wakaiga mfano wetu. Waamue kimoja kama sisi. Warudishe wazungu maana hawa jamaa wana akili kweli. Si mnaona nchi zao zilivyoendelea na jinsi zina "demokrasia" ya kweli? Halafu wana upendo sana. Si unaona wameanzisha mashirika kama Benki ya Dunia au Shirika la Fedha Duniani ili kutusaidia? Lazima watakuwa wameshika dini sana. Lazima. Wana upendo wa ajabu kabisa. Yaani wanaanzisha kabisa shirika linaitwa Shirika la Fedha Duniani! Jamani. Upendo ulioje.
Akina Nyerere, Dedan Kimathi, Nkrumah, Kaunda, n.k. walikosea sana walipogombea uhuru. Uhuru kitu gani. Wangeacha hawa jamaa wenye roho njema namna hii waendelee kutawala. Sitaki wala kusherehekea tena sikukuu ya uhuru. Nimegundua uhuru ilikuwa ni kosa kubwa sana. Sasa tunahitaji mashujaa wa kurudisha ukoloni. Tuwatungie nyimbo na kuwajengea masanamu ili tuwasahau kabisa wale waliotupoteza njia.
Mimi namtaka kaburu tu. Sina haja na wengine. Wakenya wanaweza kuwarudia Waingereza. Waganda nadhani wameshamkamata Mmarekani. Mimi nimeshamwahi kaburu. Asije mtu akaniingilia. Bila kumpeleka kaburu ikulu sitalala. Yaani tuwape tu mashirika na machimbo ya madini na mashamba? Hata, sikubali. Tuwape na ikulu kabisa. Ikishindikana nitakwenda hadi mlingotini Bwagamoyo kutafuta kizizi cha kuleta kaburu matata iya!

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com